Daniel Naftali, historia yake inamtetea katika utetezi wa vijana

Bubona

JF-Expert Member
Aug 31, 2011
448
93
Wakuu ninawasalimu,


Juzi, kama ilivyo kawaida yangu, nilinunua gazeti la Mwananchi. Wakati nikiendelea kuzipitia kurasa za gazeti hili, nilikutana na makala iliyonivutia sana. Ilikuwa inamhusu kijana Daniel Naftali na uchaguzi wa BAVICHA ngazi ya taifa. Kijana huyu ninamfahamu vizuri kwa umahri wake katika uongozi na uchapa kazi.


Katika makala ile, kijana huyu anaelezea ndoto yake ya kuwa mtetezi wa vijana. Ameulizwa maswali mengi na kuyajibu kwa ufasaha kwa lugha iliyojaa busara na hekima ya uongozi. Kwa kadri ninavyomfahamu kijana huyu, ndoto yake hii haijaanza juzi - ilianza siku nyingi na alianza kuitekeleza siku nyingi. Historia yake inayathibitisha hivyo.


Kwa mfano, alipokuwa Waziri wa Mikopo katika chuo kikuu cha Dar es Salaam, aliwatetea zaidi ya wanafunzi 2000 waliokuwa katika hatari ya kukosa elimu kwa kukosa mkopo, wakapata mkopo na kupata elimu. Aliyafanya haya bila kujali misukosuko inayowakuta watu wengi wanaotetea haki vyuoni. Alifanya hesabu za kiuongozi na kizalendo, zinazoweza kufanywa tu na watu waliojitoa kutetea wenzao. Aliona heri afukuzwe chuo yeye peke yake, kuliko wanafunzi zaidi ya 2000 kufukuzwa chuo kwa kukosa mikopo. Lakini pia, kijana huyu aliamini hakuna haki ya kudumu katika jamii ya watu ambao nusu wanapata haki na nusu wananyimwa haki. Alipigana kuhakikisha vijana wote waliokuwa wamepata udahili chuoni hapo wanapata haki ya kusoma bila kukwamishwa kwa kunyimwa mikopo. Alifanikiwa sana, madai aliyoyasimamia yalifanyiwa kazi, vijana wakasoma.


Daniel Naftali ametangaza rasmi kuchukua fomu ili aombe kuwa Mwenyekiti wa BAVICHA. Ninamuunga mkono kwa uamuzi huo nikiamini ataendelea kuwa mtetezi wa vijana wote kama ambavyo amekuwa akithibitisha siku zote. Chini ya uongozi wa kijana huyu, BAVICHA itaendelea kuwa kimbilio la vijana wote. Historia ya kijana huyu katika utetezi wa vijana inamtetea sana, akichaguliwa ataifaa BAVICHA.


Haya ni maoni yangu. Wengine mnasemaje kuhusu kijana huyu na ndoto yake ya kuwa mtetezi wa vijana?


Kwa unyenyekevu, ninawasilisha.
 
Niliaza Kumjua Naftal Pale UDSM Nikiwa Nafanya Kazi Kitengo CoEt Ni Moja Ya Vijana Wenye Sifa Za Uongozi ...Maana Anaweza Kujenga Hoja Na Kuzisimamia Ipasavyo ...NAUNGA MKONO DANIEL NAFTAL KUWA MWENYEKITI WA KUONGOZA TAHASISI YETU YA BAVICHA ... DANIEL NAFTAL Tumaini Jipya La Vijana.
 
Back
Top Bottom