Cyril Chami: Historia yake na ubunge wa Moshi Vijijini

JokaKuu

Platinum Member
Jul 31, 2006
30,269
54,664
..interview kati ya Cyril Chami na gazeti la Raia Mwema.

..nimewaletea sehemu tu ya mahojiano hayo.

..habari nzima inapatikana hapa.



Raia Mwema: Wewe ni mchumi, mhadhiri, umefanya kazi Ikulu, sasa ni mbunge na naibu waziri uliyepitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na tuzungumzavyo wewe ni Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko, uzoefu wako ni nini huko kote ulikopita?

Dk. Chami: Nakushukuru kwa swali hili. Mwanasiasa ni lazima wakati fulani aeleze ni wapi alikotokea ili watu wajue.

Baada ya kumaliza shahada ya kwanza Chuo Kikuu cha Dar es Salaam nilibaki pale nikiwa nasoma shahada ya pili. Nilipomaliza nikafundisha pale kwa mwaka mmoja.

Kisha nilikwenda Sweden kwa kozi fupi, na baadaye nikaenda Canada kwa kozi ya udaktari wa falsafa katika uchumi. Niliporudi, baada ya miaka sita na nusu, sikufanikiwa kupata kazi pale Chuo Kikuu, badala yake nikaenda REPOA.

REPOA ni shirika linalohusika na utafiti wa masuala ya umasikini. Huko nikawa chini ya Profesa Joseph Semboja, akanipokea vizuri sana na akanisaidia sana.

Ni hapo, kwa mara ya kwanza, nilipoanza kufahamu umuhimu wa kuunganisha kazi za wasomi na za Serikali. REPOA ni sekretariati ya stadi za masuala ya umasikini kwa upande wa Serikali. Nilikuwa mmoja wa wataalamu na nilijifunza mambo mengi pale, ikiwa ni pamoja na ukweli kwamba Serikali haiambiwi kwamba jambo hili ni lazima ilifanye, bali kwamba likiipendeza ione kama inaweza kulifanya.

Kwa mara ya kwanza, nikajua kwamba unapowasiliana na Serikali lazima utumie lugha nzuri. Baada ya miaka miwili nikiwa pale REPOA, Ikulu wakanitafuta, wakataka nikamsaidie Dk. Kimaro aliyekuwa msaidizi wa masuala ya uchumi wa Rais Benjamin Mkapa.

Nilikwenda, na kwa kweli baada ya kufika nilishangaa sana. Nilishangaa kwa sababu Serikali ilikuwa tofauti na jinsi mimi, kama msomi wa chuo kikuu, nilivyokuwa naijua huko nyuma. Na hata nilipokuwa mtafiti pale REPOA sikujua kwamba Serikali ni taasisi yenye nguvu inayofanya kazi namna ile. Na hasa taasisi ya Urais yenyewe.

Nisiseme uongo. Kabla nilikuwa nadhani kuwa Rais ana raha sana. Lakini nimefika pale Ikulu nikamwonea huruma sana Rais. Muda wote Rais anafanya kazi. Ni mateso makubwa. Niseme tu kwamba kwa viongozi wengine pia kama Makamu wa Rais na Waziri Mkuu kazi ni hivyo hivyo. Kazi ni nyingi, unapangiwa kila kitu.

Bila ya shaka timu yetu ile chini ya Dk. Kimaro ilimshauri Rais kama ilivyopasa. Nilikaa pale mpaka mwaka 2004, mwaka 2005 wakanifuata wenzangu wa jimboni. Wakasema jimbo limekuwa katika mikono ya Upinzani kwa miaka 10. Tungependa tulikomboe.

Wakasema wewe ni kijana unaweza kutusaidia pale. Mwanzoni nilisita. Lakini walipozidi kunibana mwisho nikakumbuka usemi ule wa Kauli ya Wengi ni Kauli ya Mungu. Nikaenda, nikagombea na kwa jitihada za wapiga kura nikapata asilimia 78 ya kura zote huku Rais akishinda kwa asilimia 80 na tukapata madiwani katika kata 14 kati ya 16.

Baada ya uchaguzi, nikiwa naenda jimboni kushukuru, ghafla nilipigiwa simu nikiwa pale Mto Wami ikinitaarifu kwamba Rais ameniteua kuwa Naibu Waziri katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. Kusema ukweli nilishangaa sana.

Baadaye niliapishwa na nikaanza kazi chini ya Dk. Asha Rose Migiro - mama mchapakazi kweli kweli ambaye alinilea vizuri sana. Baada ya yeye kuteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alikuja Waziri Bernard Membe, kazi ikawa ileile hadi ilipompendeza Rais Jakaya Kikwete kuniteua kuwa Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko.

Mara nyingi watu wanaona kwamba waliomo serikalini ni watu wanaofaidi sana, lakini nataka niseme kwamba si kila aliyeko serikalini anakula raha. Kazi kama hii ya kwetu ni kazi kubwa yenye heshima. Ni kazi ya kuaminiwa. Unaaminiwa, unaenziwa, lakini pia majukumu yake ni mazito kwelikweli.

Hii ni kazi ambayo haikupunguzii majukumu yako ya kuwa baba au mama kwenye nyumba. Au kuwa mtoto kwa baba yako au kwa mama yako
Jambo lolote likijiri katika eneo ulilopewa lazima ujieleze. Yote haya yamenipa uzoefu ambao umenifanya nitumie ule ujuzi wa shuleni kuona ni jinsi gani naweza kutumia ujuzi huo kuisaidia Serikali.

Nawashukuru sana Rais Mkapa na sasa Kikwete ambao wamejitahidi sana kutumia wasomi katika serikali zao. Ni jukumu letu sisi kama wasomi kujaribu kuona kwamba ujuzi wetu wa kisomi unashuka kabisa hadi chini katika maeneo ambayo yanamgusa mtu wa kawaida.

Ninafurahi sana kuona wasomi wa kutosha katika Baraza la Mawaziri na katika Bunge. Nawaona wabunge kuwa watu wanaojali sana maslahi ya watu. Sasa huwezi kwenda na muswada ukadhani kuwa utapita hivihivi. Wabunge wanasoma sana, na wewe kama waziri lazima ujiandae vilivyo.

Changamoto nyingine ninayoiona ni wakati wa kujibu maswali bungeni. Mwanzoni nilikuwa naona kuwa inatisha, sasa tumekwisha kuzoea, na hakika wabunge wana haki ya kuuliza maswali kwa niaba ya wapiga kura wao na sisi kama Serikali tunapaswa kuwajibu. Nafurahia maswali yale kwa sababu ni fursa nzuri ya kuifanya Serikali ieleweke vyema kwa jamii.

Pale nilipo - Biashara, Viwanda na Masoko nina Waziri mwingine mwenye uwezo, Dk. Mary Nagu, na tunafanya kazi vizuri. Hii ni wizara yenye taasisi nyingi, ndogondogo, lakini muhimu ambazo zinakufanya kila wakati uwe na kazi ya kufanya. Ni wizara ambayo inakufanya utumie sana akili. Hakuna taasisi hata moja ambako utakwenda upige domo tu.

Nafarijika kwamba wizara hii ina wataalamu wengi sana. Unapokuwa nje huwezi kujua kuwa nchi hii ina hazina kubwa ya watalaamu kiasi hiki.

Raia Mwema: Jimbo lako ni salama kiasi gani tunapoelekea katika Uchaguzi Mkuu mwakani? Taarifa zinaonyesha watu wanapitapita huko.

Dk. Chami: Natoa shukrani kwa wananchi wa Moshi Vijijini. Watu wa pale Moshi wanafikiria sana kuhusu suala la fedha katika siasa na wanadhani kwamba mtu akiwa na fedha ndiye atakuwa mwanasiasa bora. Wakimuona mtu ana magari na magorofa, wanasema safi, huyu anaweza kuwa mbunge. Lakini jambo la ajabu nilipokwenda pale mimi nikiwa kama kijana msomi niliwashawishi wananchi kwamba tunakwenda vibaya kudhani kwamba mwenye fedha yake mfukoni ndiye anaweza kuwa mbunge mzuri.

Niliwaeleza wananchi ya kuwa mbunge ni daraja tu kati ya wananchi na Serikali, kati ya wananchi na wafadhili mbali mbali. Pia mbunge ni daraja kati ya wananchi na wananchi wenyewe, kwa hiyo ni muhimu kuchagua mtu ambaye atakuwa ni daraja kuliko kutafuta mtu ambaye sifa yake kubwa ni fedha yake. Hii ni kwa sababu hakuna mbunge mwenye fedha yake mwenye uwezo wa kujenga daraja au barabara kwa fedha yake mwenyewe. Vile vile hakuna mbunge mwenye uwezo wa kujenga shule wala hospitali kwa fedha yake mwenyewe. Anaweza akatokea mbunge mmoja akajenga daraja au zahanati ili kuonyesha kuwa anaweza, lakini ukweli ni kwamba hatoweza kujenga hospitali ya watu laki mbili na nusu.

Jimbo langu lina vijiji 75, lina kata 16, haiwezekani mtu mwenye fedha yake kujenga kote huko, hawezi peke yake kujenga shule katika eneo lote la kata 16.

Kwa hiyo, inabidi apatikane mbunge ambaye anajua hazina ya taifa iko wapi na namna gani ya kwenda kuileta. Lakini la pili, wabunge waliokuwa wameongoza pale, wa Upinzani, kwa miaka 10, walikuwa wamefundisha watu wasichangie miradi ya maendeleo kama vile ujenzi wa shule au zahanati eti kwa sababu hiyo ni kazi ya Serikali.

Lakini mimi nilipoenda nilisema haiwezekani Serikali kuchangia kila kitu, ni lazima na sisi tujizatiti. Tukijizatiti na Serikali itaona umuhimu. Nafurahi kusema kwamba wananchi wameelewa, na wanachangia katika mambo yote ya maendeleo.

Pili, nafurahi kuona wananchi wameelewa kuwa mbunge hapatikani kwa kuwa ana pesa nyingi. Mbunge anapatikana kwa kuwa ana uwezo wa kushawishi mamlaka mbalimbali zikatoa ile keki ya taifa ambayo watu wamechangia, ikarudi katika jimbo lake. Hilo tumelifanya kwa kiwango kikubwa.

Tukizungumzia sekta ya elimu, wakati wabunge wenzangu wanajisifu pale bungeni kwamba wamejenga shule kila kata bado kata moja tu. Sisi kule Moshi Vijijini tumejenga shule kila kata. Tuna kata 16 na kila kata ina shule moja, kata 13 zina shule mbili mbili. Kwa hiyo tumejenga shule 13 za ziada kwa kipindi hiki ambacho nimekuwa mbunge kwa jitihada mbalimbali ambazo wanajimbo wameshiriki.

Mimi mwenyewe nimechangia shilingi milioni 424 ambazo ni za kutoka kwa wafadhili mbalimbali. Kama ambavyo nimesema, mbunge ni daraja, fedha hizi si zangu, watu mbalimbali pamoja na mimi tumechangia pale. Nimechangia simenti mifuko 3400 ili kuwasaidia wananchi katika kujenga shule, lakini pia nimepata misaada mbalimbali katika maeneo ambayo nimejenga madarasa, nimetoa matofali ambayo nimepata kwa wafadhili mbalimbali na nimepeleka katika maeneo mbalimbali na yanafahamika.

Lakini vilevile nimepata misaada mbalimbali kutoka sehemu mbalimbali na nikaitumia hiyo kujenga shule katika maeneo mbalimbali.

Kilio changu jimboni kimekuwa ni kwamba elimu ndiyo urithi pekee wa hakika tunaoweza kumwachia mtoto. Hakuna mtu mwenye shamba wala ng'ombe au madini Moshi, kitu pekee cha kumwachia mtoto ni elimu.

Mimi nimekwenda mbele zaidi, kwamba elimu bila ubora si elimu. Kuwa na wanafunzi wasio na vifaa au walimu wasioweza kufundisha vyema kwa kuwa hakuna vifaa, ni kazi bure. Kwa kuona hayo nimehangaika nikapata vitabu. Hivi tunavyozungumza nimegawa jimboni vitabu vya thamani ya shilingi milioni 800. Mgao huu haukubagua, nimegawa vitabu hivyo katika shule za Serikali na hata za makanisa na awamu nyingine inakuja.

Baadhi ya vitabu hivyo vimetoka Marekani, sasa kama kawaida, wapo wanaohoji eti kwamba hivi haviko kwenye mtaala wa kwetu, lakini mimi nawaambia kwamba hivyo ndivyo alivyosoma Rais wa Marekani, Barak Obama. Hivi ni vitabu ambavyo mtoto anatumia kujazia pale mwalimu alipofikia. Nimetoa pia jimboni kompyuta 50 na mambo mengine yanaendelea.

Jimboni tuna shida kubwa ya kilimo, kwanza, kwa sababu mashamba hakuna. Yamegawanywa katika vipande vidogo kwa wanafamilia kiasi kwamba kila mmoja akijenga nyumba yake unakuta vishamba vinavyobaki vya kahawa na vanilla ni vidogo.

Sisi tumewaambia watu kwamba wanaweza kuanza kujiandaa kwenda katika sehemu nyingine za Tanzania ambako kuna ardhi safi na kubwa ya kutosha. Tutafanya utaratibu wapate maeneo ya kulima katika sehemu nyingine nchini.

Kuna eneo hili la Lower Moshi. Watu wanaonyemelea jimbo wanapita pita wakisema kwamba hakuna maji na kwamba hiyo ni kero. Nataka kusema kwa msisitizo kwamba huu ulikuwa ni mradi mkubwa wa kilimo cha mpunga uliokuwa unafadhiliwa na Japan. Ulikuwa ukizalisha kwa mahitaji ya eneo lote la Kaskazini mwa Tanzania na sehemu kadhaa Kenya.

Lakini baada ya muda maji ya mto Rau yakakauka. Haya ni maji yaliyokuwa yakitoka katika vyanzo vya maji vya Mlima Kilimanjaro ambavyo vimeharibika baada ya ukataji miti wa zaidi ya miaka 40. Baada ya maji kukauka tumekwenda kwa Wajapan ili tuweze kupata chanzo kingine cha maji kutoka mto Kikuletwa ulioko kilometa 13 kutoka eneo la Mabogini iliko Lower Moshi.

Wakasema hakuna shida mradi wapate uhakika wa meta tisa za ujazo kwa sekunde ndipo tunaweza kuyachukua maji hayo. Tukasema tukifanya hivyo watu wanaoishi kusini mwa Mabogini watakumbwa na ukame kwa sababu maji yatakauka huko.

Tukawa tupo tayari kuwapa maji ya mita 3. 67 za ujazo kwa sekunde. Wazo hilo wakalikataa. Alipokuja balozi mwingine tukauza tena wazo hilo na huyu akaelekea kuelewa. Akasema kama Serikali itakuwa tayari kuchangia watasaidia. Nikaja kumwomba Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambaye alikuja mwenyewe mwaka huu kuangalia na akasema Serikali itauchukua mradi huo. Akasema zitatengwa fedha za kukarabati miundombinu kwanza ili kuzuia maji ya kiasi cha asilimia 30 yanayopotea kutokana na kuchakaa kwa miundombinu.

Tunavyozungumza sasa bajeti imepita Wizara ya Maji na Umwagiliaji itaweka fedha pale. Kwa hiyo watu wanaposema mbunge hajafanya kazi, hizi ni kelele tu, kazi imefanyika pale.

Nikueleze kidogo kuhusu barabara. Tangu dunia iumbwe yapo maeneo ambayo katika jimbo langu hayakupata kuwa na barabara ya lami. Najua kuna maeneo mengine nchini na mengine ni makao makuu ya mikoa au wilaya hayana lami. Lakini mimi nimejenga hoja juu ya ukweli kwamba aina ya udongo wa jimboni kwetu ni wa utelezi sana. Bila kuwa na lami pale watu hawawezi kufanya shughuli za maendeleo.

Pili, barabara nilizoomba zijengwe ni za kwenda Mlima Kilimanjaro kwa nia ya kuboresha utalii. Mlima huu ndio unaoingiza mapato makubwa kuliko maeneo mengine ya aina yake ya utalii nchini. Unaingiza zaidi ya asilimia 50.

Ukiboresha barabara hizi utaboresha mapato ya KINAPA (Kilimanjaro National Park) na hivyo ya nchi nzima. Nafurahi Rais Kikwete aliliona hilo na akaahidi kunijengea barabara mbili ya Kibosho na ya Uru. Sasa mkandarasi yuko kwenye eneo.

Tumefanya shughuli nyingi zikiwamo za uwezeshaji. Baada ya kushuka kwa soko la kahawa, wengi waliachwa na hali mbaya. Sasa tumehamasisha sana uanzishwaji wa saccos. Watu wanaotuunga mkono na mimi tumeamua tutaanzisha Benki ya Maendeleo ya Watu wa Moshi Vijijini.

Mchakato unaendelea. Mchakato wa kuanzisha benki unakutaka uwe makini sana ili ikianza isife. Kinachoendelea sasa ni kupata wadau watakaojifunga na benki hiyo kama wanahisa. Kazi ya benki hii itakuwa ni kukopesha saccos, na zenyewe zitakopesha wananchi. Hii itakwenda sawa na kauli ya Rais Kikwete kwamba mafanikio si rahisi bila mikopo.

Jingine nililolikazania sana jimboni ni mshikamano wa jamii. Kwa taarifa yako, mimi na Mbunge wa Vunjo, Aloys Kimaro, ndio wabunge wa kwanza kutoka eneo letu kuleta timu ya madiwani jimboni hapa bungeni kujionea mambo mengi ambayo hawakuwa wakiyafahamu. Baada ya pale tumekwenda mbele zaidi, sasa tunaalika viongozi wa chama chetu, Chama cha Mapinduzi (CCM). Tutaita watendaji wengine pia nao waje uwezo ukipatikana.

Tunataka ionekane kwamba mambo tunayofanya jimboni hayapishani na yale ambayo Taifa linaelekeza kutoka bungeni. Niko mbioni pia kuanzisha Baraza la Wazee kwa jimbo zima. Mchakato unaendelea na likishaanza tutakuwa na mshikamano zaidi.

Mambo ni mazuri hata katika afya. Kuna uamuzi wa Serikali kwamba kila kijiji kiwe na zahanati na kila kata iwe na kituo cha afya. Tunawaandaa wananchi kwa ajili hiyo na tumewaambia kwamba pamoja na hatua hiyo ya Serikali wao pia wawe tayari kuchangia katika nguvu za Serikali, na tumeboresha na kukarabati zilizokuwapo.

Baada ya yote haya, niseme kwamba changamoto bado ni kubwa jimboni. Wapo watu ambao hawaridhiki na hawaamini kwamba mambo huenda kwa kupangwa, hayaendi kwa kasi hiyo wanayoitarajia. Lakini Roma haikujengwa siku moja. Dhana ya kwamba mbunge atafanya kila kitu haiwezekani na wala kwamba mbunge atawapa fedha si jambo la kweli.

Kama nilivyosema mbunge ni daraja. Mimi nitajihidi kusimamia mambo ya muhimu katika sekta zote. Najua ndani ya chama kuna watu ambao wanasema wanataka kuja tupambane mwakani.

Labda kinachoendelea. Huwezi kutaka kumwondoa mbunge ambaye kishafungua njia.

Niseme pia kwa ndugu zangu wa Kilimanjaro, hasa wa ukanda wa Uchagani tusitukuze mno fedha. Ukipewa pikipiki au baisikeli na mtu, haina maana kwamba hivyo ndivyo vya mwisho katika maendeleo. Tulipoteza jimbo kwa miaka 10, sasa ni wakati wa kujijenga upya.
 
Hii kauli ya 'kupoteza jimbo kwa miaka 10' ni kudharau demokrasia na haki ya wananchi kujiamulia ni nani awaongoze. Angeweza tu kuzungumza bila kudai kuwa jimbo lilipotea kwa miaka 10.
 
Kaizer,

..inawezekana Cyril Chami anazungumza kama mwana CCM.

..nadhani interview nzima ni nzuri except for a few partisan statements.

NB:

..maelezo yake kuhusu majukumu ya mbunge on the paper na hali halisi on the ground nadhani ni mambo ya kuzingatiwa sana.
 
1. Chami.. Waziri Msomi anayejitatahidi! Uwezekano Mkubwa akapata tena mara ya pili! Nadhani akipata tena Ubunge hata Uwaziri kamili anaweza kupewa!

2. Ila Kimaro wa Vunjo wananchi hawampendi..anafulia taratibu..uwezekano mkubwa akapigwa chini 2010!
 
Mzalendohalisi,

..nasikia Prof.Jumanne Maghembe naye ameanza kupewa mchecheto.

..sijui kama Prof atarudi maana habari zenyewe ni kwamba kuna "mzee maarufu wa Mwanga" ameamua kutupa karata yake kwa mwana Mwanga mwingine.
 
Kaizer,

..inawezekana Cyril Chami anazungumza kama mwana CCM.

..nadhani interview nzima ni nzuri except for a few partisan statements.

NB:

..maelezo yake kuhusu majukumu ya mbunge on the paper na hali halisi on the ground nadhani ni mambo ya kuzingatiwa sana.


yeah mi nimesoma the whole text, nimeona 'ameteleza' hapo kwenye partisan politics tu, otherwise iko safi.
Ni vema alivokuwa wazi kuwa 'misaada' hiyo si ya kwake binafsi, ila aende mbele zaidi kusema anasaidiwa na kina nani kuanzia watu binafsi, mashirika nk na ni nini dhamira yao wanapotoa misaada hiyo.
 
Mzalendohalisi,

..nasikia Prof.Jumanne Maghembe naye ameanza kupewa mchecheto.

..sijui kama Prof atarudi maana habari zenyewe ni kwamba kuna "mzee maarufu wa Mwanga" ameamua kutupa karata yake kwa mwana Mwanga mwingine.

hehehe, hivi huyu mzee hajastaafu tu wajameni, bado anaweza kutingisha viberiti> manake nasikia wanamwanga hawasikii hawaambiwi kwa huyu na kama ni kweli katia fitna basi Maghembe ajiandae kurudi kufundisha!
 
Mheshimiwa Chami amejitahidi kujieleza

Ila mimi sijaona jitihada zake akiwa mchumi kujaribu "microfinance" kwa mapana yake ikiwa na kuwahimiza wananchi wa jimbo lake wafanye biashara zao binafsi au waungane.

Halafu anaongelea kuhusu kujengwa barabara kuelekea kwenye mlima kilimanjaro ambayo yeye anaona kama ndio kitega uchumi pekee, mheshimiwa mbunge si ametembea nchi mbalimbali duniani ni kwanini asijifunze kwamba hata humo barabarani wananchi wanaweza kuweka vitega uchumi vyao kama vile migahawa, maduka mazuri na hata mahoteli?

Mwisho anaongelea kuhusu saccos ambayo ufanisi wake unategemea fwedha za kukopeshana ni kwanini asizungumze na mabenki yakawasogelea wananchi humo majimboni?

Lakini anaonekana ni mtu anaejitahidi kufanya mambo.
 
Kaizer,

..unajua Mwanga sasa hivi kuna wazee wawili maarufu. kuna mmoja ambaye ni wa siku zote, na mwingine ambaye ameibuka upya mwaka 2005.

..niliwahi kuambiwa kwamba uchaguzi wa 2000 mzee maarufu alikuwa na mgombea wake, lakini akashindwa ktk kura za maoni na Prof.Maghembe.

..uzuri ni kwamba in 2000 Prof.Maghembe alikuwa hana record, kwa hiyo ilikuwa rahisi kubabaisha kwa kupiga domo tu. but now he has a record, kwa msingi huo ni rahisi kumpiga chini kama hana alilolifanya.

Richard,

.Dr.Chami ameeleza kwamba wako ktk process ya kuanzisha benki ya wananchi.
 
Alisoma Uru Seminary. Ni brite hapo juu penye oblongata
jamaa alikuwa rais wa wanafunzi akiwa uru seminary na alilteua nchimbi kuwa waziri wa serikali yake akiwa form one......aidha alikuwa rais wa serikali ya wanafunzi ule mwaka waliogoma chuo kikuu mpaka Matiko Matare akafukuzwa.yeye alikuwa rais upande wa mlimani na matiko alikuwa overall ya mlimani na muhimbili
 
Sina Upenzi sana na Viongozi wengi waliomo ndani ya CCM kwa sababu wengi wamejawa na Umimi na Ufisadi wa kupindukia...Lakini kwa huyu Muungwana Dr.Chami sina wasiwasi nae..ni mmoja kati ya Viongozi wachache Vijana wa CCM wenye uchungu na maendeleo ya Majimbo yao na Nchi kwa Ujumla....Dr Chami hana makuu na anazungumza na watu wa kariba yote.Nimekwishakutana na Chami mara nyingi akiwa Nje ya Nchi na mara zote anasisitiza nini tufanye ili tujenge kwetu (Tanzania).Dr.Chami ni Mmoja kati ya Viongozi wachache anayezungumzia uzuri wa Dual Citizen na nini tutafaidika ikiwa kama tutaipitisha sheria hiyo.

Katika Mahojianao yake na Gazeti la Raia mwema ameonyesha ni kwa kiwango gani amekomaa kisiasa.Ni wazi kuwa kuna watu wananyemelea Jimbo hilo.DC Betty Machangu ni mmoja wapo, Watu hao wawe makini kupambana kwa Hoja,kwa Sababu Jimbo la Dr Chami ni moja kati ya Majimbo machache yenye viongozi wanaokubalika!
 
Hatari kubwa kwa Jimbo la Cyril alikua Ngawaiya, lakini inaonekana wamekwisha strike a deal na Ngawiya ameamishia Taliban wake jimbo la Moshi mjini linalodhibutiwa na Ndesamburo, lakini kinyang'anyiro kipo kwa kuwa mtoto wa Mangi Marialle na yeye analimezea mate Jimbo la Moshi Mjini! Ila kwa namna Kimaro Aloyce alivyojitengenezea maadui na shemeji yake Che Nkapa ni wazi kuwa atalipoteza katika kura za uteuzi kwa Marialle ambaye sasa ameshauriwa ahamishie vita jimbo la Vunjo.

Back to Cyril, Kwa hili la benki ya maendeleo ya watu wa Moshi Vijijini ni politcal na kuwabebesha watu mzigo usiowalazima. Watu wa Moshi Vijiji wanamiliki kwa kiwango kikubwa shares katika benki KNCU amabyo mpaka sasa inajikongoja sana pamoja na kukithiri kwa ufisadi! Je Cyril haoni nimuhimu kupambana na ufisadi KNCU ambao utafanya Benki yake kuwahudumia watu wa Moshi Vijijini badala ya kuiacha ife kwa ufisadi na kuanzisha ingine? Nayo itakufa tu! Hapo ndio wanaponishangaza wanasiasa wetu!!
 
Chami anasema Moshi (V) wawe na Benki nyingine ya Nini???

Mji wa Moshi una benki 13..ni mji mdogo wenye watu 150,000 unaoongoza kwa kuwa na Benki Tanzania. Je kwani wananchi wameshindwa kukopa ktk hizi benki!

Na kuna Saccos kibao kila kona!

1. NBC
2. NMB (2 branches)
3. CRDB (Wamefanya renovation na kupanua sana shughuli pale Kahawa House)
4. Standard charterd
5. ACB
6. Exim
7. KNCU Bank
8. Uchumi Com. Bank (KKKT)
9. Baclays
10. n.k
11.n.k
12. n.k
13. n.k

Sasa kuna haja gani Benki nyingine?
 
hehehe, hivi huyu mzee hajastaafu tu wajameni, bado anaweza kutingisha viberiti> manake nasikia wanamwanga hawasikii hawaambiwi kwa huyu na kama ni kweli katia fitna basi Maghembe ajiandae kurudi kufundisha!


Arudi tu kufundisha.Hawa wanahitajika sana huko vyuoni.Arudi kuungana na Mgombelo kushika chaki.
 
Ukisoma maelezo ya Naibu Waziri na Mbunge utaona adhari za kuwachukua wasomi wataalam na kuwafanya wanasiasa. Ni kweli kuwa kajieleza vizuri, lakini kisiasa zaidi. Yaani kugusia gusia vitu juu juu na kufunika funika vingine bila kuvifikisha mahali stahili. Hii inafanana sana na timu iliyofungwa ikajisifu lakini tuliwala chenga japo wametufunga.
Amezungumzia athari za deforestation Kilimanjaro kuwa ni kukosekana maji mto Rau. Badala ya serikali kuchukua hatua stahili na za muda mrefu kurekebisha jambo hilo hata kama litachukua mika mia moja, kwa kuanzisha miradi ya "reforestation" pamoja na kuelezea hatua zinazochukuliwa kuzuia kabisa ukataji miti na zaidi ya hapo na kuelimisha wananchi wa jimbo lake njia mbadala za kupata gesi au umeme zaidi solar power nk. kwa ajili ya kutumika majumbani kuzuia utumiaji wa mkaa na kuni ameonyesha kukwepa hilo maana hakuna kabisa kinachofanyika. Ningetegemea waziri msomi kama Dr Chami aligusie maana ile snow pale juu ya mlima ilikuwa kilometa 4 sasa haifikii hata mbili.
Ujenzi wa shule ni vyema Kilimanjaro wapepiga hatua sana, lakini nashindwa kuelewa kuwa ameona kuleta tu vitabu kutoka Marekani eti alivyotumia Obama inatosha. Inasikitisha kuona kuwa Waziri msomi kama yeye amesindwa kuona kuwa tunahitaji sana kupata walimu bora kwenye hizi shule tunazojenga. Waliopo wanatakiwa kupelekwa nje wakapate "exposure" zaidi. Na zaidi ya hapo vifaa vya kufundishia havitoshi kabisa. Vijana hawana hata vifaa vya michezo siku hizi. Wakati yeye akiwa shule michezo ni kitu kilikuwa kinazingatiwa sana na umuhimu wake hauna haja ya kujadiliwa.Nakumbuka tulikuwa na waalimu wa michezo, waliosomea kufundisha kipindi hicho tu. Na ilikuwa ni jitihada ya serikali kuhakikisha kila shule inaye angalau mmoja.
Amezungumzia swala la viwanda kidhaifu kabisaa. Mwenyewe ametaja Urafiki Tex. Sungura Tex, hakuweza kueleza nini serikali inafikiria licha ya nini inafanya kuhusu viwanda mama kama hivi pamoja na kwamba amegusia kuwa serikali inaangalia vile vinavyotumia mali ghafi ya hapa hapa nchini. Nimeshindwa kuamini kuwa hakuweza kugusia viwanda muhimu kama General Tyre kuwa Serikali ina mpango gani, na kwanini wanasubiri mpaka vinateketea kabisa badala ya kufanya kila juhudi kuhakikisha angalau wale wataalam wazawa "and the skilled manpower doesn't just get wasted as it is happening now"!
Mkoa wa Kilimanjaro umedorora sana tangu nchi iingie kwenye mfumo wa vyama vingi, ilionekana wazi kuwa ni mkoa ulioadhibiwa kwa kuwa ulitoa wabunge wengi sana wa Vyama vya upinzani, miradi mingi ilikabwa koo. Kabla ya mfumo wa nyama vingi mji wa Moshi ulikuwa unaweza kulinganishwa na mji wa Arusha lakini sasa hivi hakuna tena cha kulinganisha pale. Ameshindwa kukiri hilo kwa sababu ya uchama.

Tukirudi tena kwenye swala la Tanzania kutokuwa na viwanda kilinganisha na majirani zetu, hili halifichiki hata kidogo na Tanzania tukijiingiza kwenye jumuiya ya Africa Mashariki bila kujielewa wapi tuko dhaifu na bila kutengeneza takwimu sahihi za nchi husika zitakazoonyesha tofauti zetu kiuchumu na kuwepo makubaliano ya dhati kuwa nia ya kujiunga ni ili katika kipindi maalum tuwe tumefaidika na nini kwenye huo muungano, basi tutaishia kuona sehemu kubwa ya wananchi wa Tanzania kuwa mithili ya watumwa wa jirani zetu. Hili liko wazi kabisa linaonekana kwenye mazao amabayo yanatolewa hapa yanakwenda kuwa repacked Nairobi yanabandikwa product ya Kenya, hata watalii anayekuja kuuona Mlima Kilimanjaro hadi leo wapo wanaokuja wakijua uko Kenya. Watalii wengi wanaokuja nchini wanatua kwanza Nairobi ndipo waendelee na safari za Zanzibar, Ngorongoro na Ml. Kilimanjaro. Mtalii akikaa East Africa kwa wiki tatu anapumzika Kenya wiki mbili na siku tano tu anaingia Tz. Hata huduma kwa Watalii hatujajiweza.
Wanasiasa wetu wanatakiwa kukiri kuwa hawajui sawasawa wanatupeleka kwenye hilo shirikisho tufaidi nini. Na punde litakapotimia wasubiri kuulizwa hilo swali na wananchi, kwa maana haitatuchukua miaka mitano tutakuwa tayari tunachechemea.
 
Mpenda Tz,

1. Chami yupo CCM..na nadhani alipata Uwaziri ili kuwatuliza Kilimajaro kama unavyosema kupunguza hisia kuwa watu wa huu Mkoa wameadhibiwa kwa kuwa na mawazo ya kuikosoa serikali kupitia upinzani!

2. Sijui kama Chami ni member hapa JF kama Zitto. Mimi nitambana aeleze serikali ina mpango/mikakati gani kufufua viwanda Moshi kama zamani?? Au ndo watu wa huu Mkoa wataendelea kuadhibiwa na serikali kwa vile
wana mawazo ya kuunga mkono upinzani??

Je adhabu hii itaisha lini?
 
Mpenda Tz,

1. Chami yupo CCM..na nadhani alipata Uwaziri ili kuwatuliza Kilimajaro kama unavyosema kupunguza hisia kuwa watu wa huu Mkoa wameadhibiwa kwa kuwa na mawazo ya kuikosoa serikali kupitia upinzani!

2. Sijui kama Chami ni member hapa JF kama Zitto. Mimi nitambana aeleze serikali ina mpango/mikakati gani kufufua viwanda Moshi kama zamani?? Au ndo watu wa huu Mkoa wataendelea kuadhibiwa na serikali kwa vile
wana mawazo ya kuunga mkono upinzani??

Je adhabu hii itaisha lini?
Ni kweli kabisa hata wananchi waliomwita na kumwomba agombee waliona mambo yamezidi kuwa mabaya wakaona afadhali wamwite mtu ambaye angalau anatokea pale na anauhusiano mzuri na CCM, hilo ukisoma maelezo yake linajionyesha wazi.

Kuna viwanda vingi sana Msohi ambavyo vimekufa na visingestahili kabisa kufa, ie. Moshi Machine tools, Kibo Match, Vya mbao, kulikuwa na chipboard sijui kama nakumbuka sawa sawa, Kivuki nk. Its a shame!!
 

Similar Discussions

0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom