CUF, NCCR wajipakaza uozo wa CCM

KAMA viongozi wa NCCR-Mageuzi, Chama cha Wananchi (CUF), Tanzania Labour Party (TLP) na United Democratic Party (UDP) wangekaa chini na kupima sababu za kuporomoka kisiasa kwa Mchungaji Christopher Mtikila wa DP, wasingekubali mwaliko wa ikulu kunywa sifongo.

Prof. Ibrahim Lipumba (CUF), James Mbatia (NCCR-Mageuzi), Augustine Mrema (TLP), na John Cheyo (UDP) wametia saini kujimaliza kisiasa wao na vyama vyao ili kunusuru hadhi ya Rais Jakaya Kikwete pamoja na chama chake – Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Taratibu wameamua kufuata nyayo za Mtikila kuporomoka wao na vyama vyao. Katika miaka ya mwanzoni mwa 1990, mara baada ya mfumo wa vyama vingi kuruhusiwa, Mtikila alikuwa miongoni mwa wanasiasa waliotikisa nchi na kuvutia wananchi.

Mwaka 1993 alitinga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na kuwasha moto wa mageuzi nchini. Alipotaka kuanza kuhutubia kwa Kiswahili wanafunzi wakamwambia “English please.” Mtikila alitii agizo hilo na alipomaliza “kumwaga sumu” akajikuta mamia ya wanachuo wamemzunguka kwenye gari lake na kuanza kulisukuma. Walikuwa wanamfurahia.

Siku nyingine akiwa katika viwanja vya Jangwani, jijini Dar es Salaam, Mtikila alitoa hotuba iliyohamasisha mamia ya watu kwenda kuvunja vioo vya magari ya watu aliowaita ‘ma*********’ yaani matajiri wa Kiasia. Kila mahali alipokwenda kuhutubia alifuatwa na maelfu ya watu kumsikiliza na kujiunga na chama chake. Mtikila wa leo si wa miaka ya 1990; amebaki yeye na wanachama wake kiduchu sana. Mambo kadhaa makubwa yalichangia kuporomoka na kumaliza umaarufu wake. Kwanza ni nguvu ya upepo wa mageuzi aliyoingia nayo Mrema kutoka CCM na kuibukia NCCR.

Mrema aliyejitoa CCM kupinga hatua ya serikali kuratibu wizi wa mamilioni ya shilingi yaliyotengwa kwa ajili ya uendelezaji mashamba ya mkonge; alikuwa kivutio kikubwa. Alizunguka nchi nzima kuishtaki serikali ya CCM kwa wananchi, kwamba imeshindwa kuwaletea watu maisha bora.

Pili, ili kurejesha mvuto wake, katika kipindi ambacho NCCR ilikuwa madhubuti na kutishia mustakbali wa CCM kuunda tena serikali, Mtikila akajiingiza katika mradi mchafu wa kuisaidia CCM kumponda Mrema na NCCR yake. Mtikila alikerwa na umaarufu wa Mrema kuliko ufisadi wa serikali iliyopo. Mtikila ameendelea na mradi huo hadi katika miaka ya hivi karibuni. Mfano katika uchaguzi mdogo wa ubunge jimboni Tarime, alijitokeza kuwaponda wapinzani wenzake hadi akapigwa jiwe.

Tatu, Mtikila amejitokeza kuwa mtu aliyepoteza dira. Anachokipinga hadharani ndicho anakifanya kwa siri. Mathalani amekuwa akiwaponda mafisadi mchana, lakini usiku anapokea misaada ya fedha kutoka kwao. Wengi ameridhiana nao na kunyamaza.

Ugonjwa huu uliomkumba Mtikila hadi kupotea katika siasa za mageuzi ndio unawanyemelea kwa kasi Mbatia, Mrema, Cheyo na katika hali ya kushangaza Prof. Lipumba. Viongozi hawa wote wanajua ‘rafu’ za CCM; wanajua jinsi serikali ya CCM inavyotumia wapinzani kupunguza au kuzima kasi ya upinzani kwa kuchonganisha vyama, kuvilipa fedha, kutumia polisi kutwanga virungu vyama machachari na kuzushia udini, ukabila, fitina na chuki.

Viongozi hawa wanajua jinsi Mrema alivyoshuka daraja alipofuata nyayo za Mtikila kuponda vyama vingine vya upinzani. Baada ya kukataa kuungana na vyama vingine mwaka 1995, Mrema ‘aliugua ugonjwa’ wa kuwaponda wapinzani huku akijitukuza yeye tu. Mrema hakusalimika, katika uchaguzi wa mwaka 2000 akiwa amehamia TLP, akaporomoka.

Vilvile viongozi hawa wanajua polisi, usalama wa taifa walivyotumika kumvuruga Mrema hadi akakimbia NCCR na kuhamia TLP ambako uliibuka mgogoro mwingine usio kichwa wala miguu uliomtoa mwasisi wake, Leo Lekwama aliyejipatia umaarufu kwa kusigina katiba katika viwanja vya Jangwani. Hatimaye Lekwama kwa kuchoshwa na visa vya Mrema, akaamua kurejea CCM.

Naye Cheyo anajua umafia wa CCM ulivyomkosesha kura hata katika kituo alichopigia; akaambulia kura yake, mkewe na ndugu zake wawili. Prof. Lipumba, msomi aliyekubalika zaidi uchaguzi wa mwaka 2000 na 2005, yeye na chama chake, muda wote wamewaaminisha wananchi kwamba kura zao katika uchaguzi wa 2005 ziliibwa kwa teknolojia ya kisasa. Kwamba watu wakimpigia kura Profesa Lipumba wino ulikuwa unafutika katika karatasi zile za kura kutoka Afrika Kusini.

Katika kampeni mwaka jana alijibainisha kuwa ni Mlima Kilimanjaro huku mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa akimwita kichuguu. Baada ya uchaguzi, Profesa akaungana rasmi na kina Mrema, Cheyo na Mbatia kushambulia CHADEMA eti kina mikakati ya kuvunja amani ya nchi.

Hao wote wanaimba wimbo “heri shetani umjuaye CCM kuliko CHADEMA usiyemjua.” Kama CCM hawako salama, wamepoteza umaarufu, kitu gani kimewavutia Mrema, Mbatia, Cheyo, Profesa kuingia katika jahazi linalozama?Viongozi wa vyama hivyo wanaweza kujibu hoja hizi kwa mstari mmoja tu au wakapuuza, lakini ukweli historia itawahukumu. Maana hawawezi kushirikiana na adui yao CCM na wakabaki wanaaminiwa na wananchi kuwa ni wapinzani makini wenye nia ya kuingia ikulu. Maana wote; Mrema, Cheyo, Mbatia na Profesa wamenyanyua bango linalosomeka ‘On ne change pas l’equipe qui gangne’ yaani Hakuna Kubadili Timu ya Ushindi (CCM).’

Mrema anajua CCM wanavyotapatapa wakibanwa vilivyo na njia wanayotumia ni uzushi. Alidaiwa kuchota mamilioni ya shilingi alipoondoka serikalini; alidaiwa kuendesha siasa za ukabila; baadaye akaambiwa ana udini. Leo ameungana na wazushi CCM wanaotapatapa kuzushia CHADEMA kuwa kinataka kuvunja amani.

Profesa anakumbuka CCM ilivyomtumia Balozi wa Marekani, Charles Stith hadi kuanza kutoa taarifa za tishio la ugaidi katika visiwa vya Unguja na Pemba; haukuonekana. Mwaka 2001 wakati anaaga Balozi Stiith alifafanua kile alichoita ugaidi akisema siasa kali hazitasaidia Zanzibar kutatua matatizo yake ya kiuchumi. Profesa ndiye alikuwa wa kwanza kumjibu Balozi Stith kwamba ni mzushi.

Lipumba ambaye alifikia kuvunjwa mkono na Polisi wa CCM wakati wa kampeni za uchaguzi, anajua uzushi ule ulivyochangia kuiathiri CUF kwamba ni cha kidini na kimejaa Wapemba. Hoja hizo zilitumiwa tena na Fatma Maghimbi alipojiondoa na kurudi CCM.

Lipumba bado anakumbuka jinsi CCM ilivyomtumia aliyekuwa mkuu wa jeshi la polisi, Omari Mahita kuangamiza chama chake kwa kukizushia kuwa kimeleta majambia wakati haikuwa kweli.

Hivyo basi, kama Mtikila aliporomoka kwa kunanga wapinzani wenzake, Mrema akakanyaga kaa la moto alipojiona bora kuliko wapinzani wengine, Mbatia na Prof. Lipumba hawawezi kupata umaarufu kwa kuwachafua wapinzani wenzao. Hapana shaka wataporomoka tu maana historia ina tabia ya kujirudia.

Source: Mwanahalisi
 
Back
Top Bottom