Chaguzi ndogo zinavyoiweka CCM uchi

MASEBUNA

JF-Expert Member
Oct 9, 2011
243
54
KAMA kuna kitu kinachokitesa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa sasa basi kitu hicho ni chaguzi ndogo za majimbo. Chaguzi hizo zinaivua CCM nguo na kuiweka uchi. Lakini kwa vile chaguzi hizo kwa namna moja au nyingine zimeushikilia uhai wa chama hicho ndipo kinapojikuta hakina ujanja isipokuwa kukubali kuchagua moja kati ya mawili.

Mosi, kuficha uchi na kukubali kufa kwa kuogopa fedheha au kujiweka uchi ili kila mmoja ayaone maradhi yanayokisumbua chama hicho katika jitihada za kuulinda uhai wake. Imesemwa mpaka na makada wakubwa wa chama hicho, na inajionyesha wazi kwa kila mmoja kwamba makosa yaliyofanyika ndani
ya CCM yamekiondolea chama hicho mvuto kwa wananchi.

Kwa kuukubali ukweli huo mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, akatangaza mkakati aliodhani ungeweza kuurudisha mvuto wa chama kwa wananchi. Akasema ni lazima chama kijivue magamba. Mpaka hapo mwenyekiti alikuwa amekiri kwamba chama chake kilikuwa nayo matatizo makubwa, ambayo yeye aliamua kuyaita magamba kwa lugha ya kisanii. Bila shaka Mwenyekiti Kikwete alikuwa na imani kwamba kauli hiyo ya kuikiri dosari ndani ya chama chake na kuahidi kuishughulikia ilitosha kuwarudishia imani wananchi kwamba chama hicho sasa ni safi hata kabla ya kuuona utekelezaji wa ahadi hiyo. Kwamba wananchi wangekubali kumnunua mbuzi kwenye gunia.

Ila baadhi yetu tuliichukulia kauli ya JK ya kujivua gamba, kama dawa ya kutuliza maumivu tu kwa mgonjwa anayesumbuliwa na saratani bila kukigusa kiini cha tatizo ambacho ni saratani yenyewe. Matatizo yanayotajwa kwenye Chama Cha Mapinduzi ambayo yameshamiri na kuanza kukitenga chama hicho na wananchi, kama vile rushwa, ufisadi wa aina mbalimbali, mmomonyoko wa maadili, myeyuko wa
uzalendo kwa nchi nakadhalina, ni matatizo yaliyokwishageuka saratani.

Kwahiyo si rahisi kuyaondoa matatizo hayo kwa ahadi tu ya kujivua gamba. Maana kawaida ya saratani ni lazima iondoke na baadhi ya viungo kama imewahiwa kugundulika na kuonyesha dalili za kuponyeka
na kuunusuru uhai. Wasiwasi nilio nao ni kwamba kitu hicho hakijapata ujasiri wa kukimudu ndani ya CCM
ya sasa. Kwa sasa ni vigumu kutenganisha rushwa na CCM.

Pamoja na kanuni ya chama hicho isemayo rushwa ni adui wa haki, sitatoa wala kupokea rushwa, ni mwana CCM gani anayeweza kusimama na kujigamba kwamba hajawahi kutoa rushwa katika kuhakikisha usalama wa nafasi yake ndani ya chama? Kama hali iko hivyo unawezaje kuifuta rushwa ndani ya CCM ukabaki na CCM iliyo hai? Hiyo tayari ni saratani ndani ya chama hicho. Chama ambacho kimeikumbatia rushwa na kuifanya ndiyo nyenzo kuu ya mafanikio ya kila kitu kinawezaje kuwahakikishia wananchi ustawi wao huku haki ya kila mmoja ikiwa imezingatiwa?

Vilevile inaonekana jinsi chama hicho, ambacho mwanzoni kilikuwa cha wakulima na wafanyakazi tena kikiwategemea haohao kujiendesha, kilivyojigeuza mithili ya jini na kuwakumbatia mabwanyenye ambao kwa sasa ndio nguzo kuu za chama hicho. Sasa unawezaje kuzitishia nguzo hizo halafu udai unakitakia mema chama hicho na mtu akuelewe? Hiyo ndiyo inayoonyesha kwamba kauli ya kujivua gamba ilitolewa kimzaha bila kuupima uzito wa ukweli uliokuwa umebebwa ndani yake.

Kauli kama hiyo ya kujivua gamba ingeweza isihojiwe na wananchi kwa kudhani kwamba ingeweza kutekelezeka kama dhamira ilivyosikika bila kuonekana na ikizingatiwa kwamba aliyetoa kauli hiyo ndiye kinara wa chama. Lakini bahati mbaya sasa kauli hiyo imeanza kuchokonolewa na hizi chaguzi ndogo na
hivyo kuonekana kwamba kumbe haikuwa na uzito wowote. Uchokonozi huo ulianzia Igunga ambako
mhimili mmoja wa CCM, Rostam Aziz, baada ya kusakamwa sana ndani ya chama chake hicho akidaiwa kwamba yeye ni gamba lililohitajika kuvuliwa, akaamua kujivua mwenyewe bila kusubiri kuvuliwa. Wenzake ndani ya chama wakadhani ni masihara kwa vile kauli hiyo ililengwa kuyatuliza maumivu bila kutibu ugonjwa, lakini walikuwa wamechelewa maana mhimili huo ulishauvua hata ubunge uliopatikana kwa
tiketi ya CCM.

Hapo ndipo CCM ikalazimika kubaki uchi kwa mara ya kwanza, ikayaweka hadharani maradhi yanayoisumbua ikiwa imeutilia maanani wimbo ulioimbwa na kada maarufu
wa chama hicho, John Komba, usemao kwamba mwenye kuficha maradhi kwa aibu au kwa kuogopa fedheha ni lazima kilio kitamfichua.

Badala ya CCM kufanya sherehe kushangiliakwamba gamba moja limeondoka vikaanza
kufanyika vikao vya kutafuta namna ya kumwangukia Rostam ili akubali kuibeba CCM ili iweze kulirudisha jimbo hilo kwenye himaya yake. Hebu tujiulize, mpaka hapo tunaonaje? Rostam alikuwa gamba kwa chama au mhimili wa chama?

Badala yake msemaji wa chama ambaye muda wote alikuwa amebeba bango la magamba ndiye akaonekana mchafu kwa chama na kupigwa marufuku asikanyage Igunga kukichafua chama katika harakati za kulirudisha jimbo hilo kwenye himaya kikiwa mabegani mwa mhimili wake. Kama nilivyosema awali, chaguzi ndogo zinaitesa sana CCM kwa kukilazimisha kubaki uchi na kuyaanika maradhi yake. Kwa sasa kuna uchaguzi mdogo katika jimbo la Arumeru Mashariki kufuatia kifo cha mbunge wa jimbo
hilo, Jeremiah Sumari (CCM).

Tumeona mnyukano ulivyokuwa ndani ya chama hicho katika kumpata mgombea wake.Hapo kuna mambo kadhaa ya kuyaangalia kwa makini ili kuona namna uchaguzi mdogo unavyoisulubu CCM. Mpambano mkubwa wa kumpata mgombea wa CCM ulikuwa kati ya CCM ikiongozwa na
mwenyekiti, upande mmoja, na Sioi Sumari anayesemekana kusimamiwa na kambi ya Lowassa kwa upande mwingine. Ikumbukwe Lowassa ni mmoja wa makada wa CCM wanaodaiwa kuwa ni magamba. Kwa hiyo kilichofanyika ni Lowassa kutaka kuwaonyesha CCM uwezo wake kwa kumpitisha mgombea anayemtaka yeye huku chama nacho kikiwa kimejipanga kuizuia nguvu ya Lowassa.

Lakini mwisho wa yote kambi ya Lowassa ikaibuka kidedea kuashiria kuwa yeye bado ni mhimili ndani ya CCM na wanaomuita gamba wakome. Akaibwaga kambi ya CCM ikiongozwa na mwenyekiti! Pamoja na ushahidi wa wazi wa kwamba ulichezwa mchezo mchafu wa rushwa katika kumpitisha Sioi Sumari kwenye kura za maoni, bado vikao vya juu vya CCM vimeshindwa kuyabatilisha matokeo hayo, kama ilivyokuwa ikifanyika miaka ya nyuma. Vimeamua kuyabariki matokeo ya kura za maoni licha ya uchafu ulioambatana nayo.

Hofu ya CCM ni kwamba uamuzi wowote ambao ungekwenda kinyume na matokeo hayo machafu ungeweza kukionyesha chama njia ya kwendea kuzimu. Hayo ni mateso mengine yanayokikabili chama hicho katika hizi chaguzi ndogo. Fikiria, kama chama kinaletewa ushahidi wa waziwazi kwamba mmoja wa makada wake amekiuka maadili ya chama kwa lengo la kujinufaisha yeye binafsi huku akiwa
amekipaka chama matope, lakini chama kikashindwa kumchukulia hatua yoyote kwa kuhofia nguvu iliyo nyuma ya mtu husika. Huo utakosaje kuwa uthibitisho kuwa chama hakiko tena kwenye misingi ya maadili yake bali kimesimama juu ya nguvu za watu fulani waliojigeuza mihimili ya chama hicho hata
kama watu hao ni wachafu kiasi gani?

Jambo jingine linaloshangaza ndani ya CCM, kama ambavyo tumekuwa tukionyesha mara kwa mara, ni la chama hicho kujiendesha kifamilia na kikoo mithili ya ufalme badala ya kujiendesha kitaasisi. Mbunge aliyekufa wa Arumeru Mashariki ni Jeremiah Sumari. Kabla hata maiti yake haijaoza kaburini chama kinamteua mtoto wake kuirithi nafasi ya baba yake! Nani kasema kwamba ukoo wa Sumari ndio pekee
unaopaswa kutoa mbunge wa Arumeru Mashariki? Mimi naamini kwamba Sumari kaacha mali nyingi alizowarithisha wanae, lakini ubunge si kati ya mali hizo.

Ubunge ni mali ya wana jimbo wala haikuwa mali yake. Kwa hiyo wana Arumeru Mashariki ndio wanaotakiwa kuelewa mali hiyo wampatie nani bila kuangalia anatoka ukoo gani. Ila niwatahadharishe wana Arumeru Mashariki kwamba kutoa nafasi hiyo kwa zaidi ya mtu mmoja ndani ya familia moja ni kutengeneza aina fulani ya ufalme ambapo wananchi wengine watakuwa wamejitenga kabisa na
nafasi hiyo ya uwakilishi wa wananchi.

Tukirudi kwenye utata wa maamuzi ya CCM tunapata tetesi kwamba mwenyekiti mstaafu, Benjamin Mkapa, ndiye kapewa jukumu la kuhakikisha chama hicho kinaibuka mshindi katika uchaguzi huo mdogo. Lakini ni CCM hiyohiyo ambayo katika mkutano wake wa Halmashauri Kuu uliofanyika majuzi kule Dodoma, imefikia uamuzi wa kuibadili katiba yake ili kuwaondoa viongozi wastaafu katika NEC na badala yake
kuwaundia chombo kingine ambacho bilashaka kitakuwa hakileti vikwazo katika maamuzi ambayo wazee hao wasingeyaafiki.

Wastaafu wameenguliwa kwenye maamuzi na kufanywa washauri. Lakini walio katika maamuzi wakisha boronga wazee walio katika ushauri waitwe haraka kuokoa jahazi! Pamoja na hiyo ikumbukwe kwamba mngao wa CCM ulianza kufifia wakati wa uenyekiti wa Mkapa. Mkapa ni kiongozi aliyepigiwa debe na Baba wa Taifa, Julius Nyerere huku akiwashangaa waliokuwa wakiitamani Ikulu kiasi cha kutoa hata fedha ili wafanikiwe kuingia.

Mwalimu Nyerere aliuliza Ikulu kuna biashara gani? Kwamba mtu anayetoa pesa kuingia Ikulu atazirudishaje? Ndipo Mwalimu alipoonya kwamba Ikulu ni sehemu takatifu, si mahali pa kufanyia biashara. Lakini haukupita muda mrefu tangu Mwalimu alipotutoka tukapata habari kwamba Rais Mkapa kasajili kampuni ya biashara kama mjasiriamali aliyekuwa akiishi Ikulu! Mkapa akaigeuza Ikulu yetu sehemu ya biashara akiwa ameisaliti imani aliyokuwa nayo Baba wa Taifa kwake. Baada ya hapo nguvu ya ushawishi iliyokuwa nayo CCM kama ile aliyoitumia Mwalimu kuwashawishi wananchi ili wamkubali Mkapa, ikaporomoka kwa kishindo na kukiacha chama hicho kikitegemea mabavu na shinikizo kwa
msaada wa vyombo vya dola kufanikisha matakwa yake.

Ni katika kipindi hicho cha Mkapa, Tanzania kwa mara ya kwanza katika historia ya ulimwengu, ikazalisha wakimbizi kufuatia mauaji yaliyofanywa na vyombo vya dola. Unguja na Pemba katika CCM kutafuta ushindi kwa mabavu. Kwahiyo ikiwa Mkapa atajitokeza kuifanyia kampeni CCM Arumeru Mashariki itabidi
wananchi wamuulize maswali hayo. Hata kama hakutatolewa fursa ya kumuuliza moja kwa moja, nina imani hakuna atakayeweza kuyazuia maswali hayo yasiulizwe kimoyomoyo. Mkapa aulizwe ni kitu gani kilichosababisha uadilifu ndani ya chama chake kumomonyoka kiasi cha kumfanya yeye akiwa kiongozi
mkuu wa chama na kiongozi wa nchi kuamua kuigeuza Ikulu yetu, ambayo aliambiwa na
Mwalimu wake kuwa ni sehemu takatifu, pango la ulanguzi?

Aulizwe ulikokwenda ushawishi wa CCM ambao nafasi yake imechukuliwa na shinikizo la kutumia mabavu kwa vitisho. Maana ni katika kipindi cha Mkapa tulipoanza kushuhudia kampeni kama hizo za uchaguzi zikiendeshwa kwa mtindo wa kivita kwa kutumia vyombo vya dola badala ya kuwashindanisha makada wa vyama kumwaga sera kwa wananchi. Mkapa pia aulizwe CCM kina uhalali gani wa kuendelea kuaminiwa na Watanzania katika ujumla wao iwapo wanachama wake hawaaminiani tena wala kukiamini chama chao?

Suala la wana CCM kutishiana maisha kiasi cha makada wake wa ngazi za juu kutoleana shutuma za kulishana sumu na mambo mengine machafu na ya hatari linawezaje kukifanya chama hicho kiendelee kuonekana ni tegemeo la Watanzania? Aulizwe kwamba CCM imegeuka chama cha kifalme? Vinginevyo aeleze inakuwaje chama kinajishughulisha na namna mtu atakavyorithi nafasi ya baba yake, kitu kinachohamisha shughuli za chama, kama taasisi ya ki-nchi, na kukifanya chama kionekane kinashughulikia mirathi ambayo inapaswa kuwa shughuli ya kifamilia.
 
Ilipofika CCM ni point of no return, inakwenda kuzama na makundi yake na siku yakizama makundi hayo yatabaki kulaumiana tu maana hawajui mchezo wanaoufanya hatma yake ni nini.
 
Masebuna umechambua vizuri sana! wakisoma robo yao watapata shinikizo la damu, chapisho linaweza kutengeneza by election kadhaa!!!
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom