CHADEMA Tarime yailiza CCM uchaguzi S/Mitaa

Magezi

JF-Expert Member
Oct 26, 2008
3,359
692
na Sitta Tumma, Tarime


CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Wilaya ya Tarime, kimekichachafya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa kujizolea vitongoji 95 na vijiji 14 katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Ushindi huo umeelezwa kuwa ni salamu na dalili mbaya kwa CCM, kwani awali CHADEMA haikuwa na kitongoji na kijiji hata kimoja, ikiachiliwa mbali mtaa mmoja uliokuwa ukiongozwa na chama hicho cha upinzani.
Wakizungumza na Tanzania Daima, Mbunge wa Tarime, Charles Mwera (CHADEMA), na Diwani wa Tarime Mjini kupitia CHADEMA, John Heche, walisema chama chao kimetoa upinzani mkali kwa chama tawala, kwani kwa baadhi ya maeneo wagombea wa CCM walishindwa kufanya kampeni kutokana na kutokubalika.

“CHADEMA hapa Tarime tumeiharibu CCM, na inawadanganya watu kwamba imepata ushindi wa kishindo nchini...sisi hatukuwa na kitongoji hata kimoja, lakini leo tumeshinda vitongoji 95 kutoka kwa CCM.
“Tunasema CCM imeangukia pua hapa Tarime katika uchaguzi huu wa serikali za mitaa, tunaamini wananchi watazidi kutuunga mkono siku hadi siku, na ninatoa salamu kwa CCM kwa uchaguzi mkuu mwakani,” alitamba Mwera.

Aidha Mwera alisema, katika uchaguzi huo, CHADEMA imeweza kujinyakulia mitaa mitano kutoka kwa CCM, jambo ambalo wanajivunia nalo kwa kuaminiwa zaidi na wananchi wa Wilaya ya Tarime.

Kwa upande wake, Heche alitamba kwa kusema kwamba, ngome ya Chedema wilayani humo itazidi kuimarika siku hadi siku na kwamba katika uchaguzi mkuu ujao, CCM itapoteza maeneo mengi, kwani wananchi wa Tarime siku hizi hawadanganyiki.

Kwa mujibu wa Heche, ushindi wa CHADEMA katika vitongoji, mitaa na vijiji unatokana na ushirikiano mzuri uliopo kati ya viongozi na wananchi wa wilaya hiyo, na kwamba viongozi wa chama hicho wataendelea kupambana na mafisadi pasipo kumwogopa mtu.

Source: T/Daima
 
Back
Top Bottom