Chadema ruksa ibada ya mazishi

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
268
IBADA ya marehemu wawili waliouawa na polisi katika vurugu za maandamano ya Chadema
inatarajiwa kufanyika katika uwanja wa NMC leo, baada ya Polisi kuridhia shughuli hiyo ya mazishi kufanyika.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba, alisema Polisi imekubaliana na ombi la chama hicho na ibada itafanyika kuanzia saa 4 asubuhi.

Mwigamba alisema baadhi ya viongozi wa Polisi walikuwa wakimpotosha Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Thobias Andengenye, juu ya kufanyika kwa ibada hiyo katika uwanja wa NMC kuwa kutasababisha vurugu.

“Kamanda ameshatukubalia na matangazo si unayasikia juu ya watu kuhamasishwa kuhudhuria ibada hiyo kwa wingi katika uwanja huo na hakutakuwa na vurugu, kwani viongozi wa dini ndio watakuwa wakiratibu ibada hiyo,” alisema.

Katibu huyo alisema Chadema haihitaji ulinzi wa polisi kwenye ibada ila imetoa taarifa juu ya mkusanyiko wa watu ambao wana lengo la kufanya ibada na ndiyo azma ya chama na si vinginevyo.

“Nafikiri hata polisi siku hiyo hatuwahitaji … wao wakae huko huko waliko na watuachie sisi
tumalize ibada ya kuwaombea marehemu wakazikwe,’’ alisema.

Kamanda Andengenye alipopigiwa simu kutoa ufafanuzi juu ya hilo, simu yake ya mkononi ilipokewa na msaidizi wake, aliyejibu kuwa Kamanda yuko kwenye kikao cha ulinzi na usalama cha mkoa.

Mwigamba alisema miili ya Denis Mtui na Ismail Omary itapelekwa katika uwanja huo saa 4 asubuhi ili kila mkazi wa Arusha aweze kutoa heshima yake ya mwisho.

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Arusha, Onesmo ole Nangole, amemwomba Waziri Mkuu Mizengo Pinda, atoe tamko kuhusu vurugu zilizotokea hapa na kusababisha uvunjifu wa amani, vifo vya watu watatu na uharibifu wa mali.

Nangole alitoa ombi hilo ofisini kwake kutokana na Ofisi ya Waziri Mkuu kuonekana kukaa kimya juu ya tukio hilo ambalo lilipaswa kufikiwa muafaka, badala ya kuendelea kutolewa kwa matamko siku hadi siku yenye kuleta chuki na uhasama kwa jamii.

Alisema ni vema ofisi ya Waziri Mkuu ikatoa tamko ambalo litazuia mijadala inayoendelezwa sasa na taasisi mbalimbali zikiwamo za dini na vyama vya siasa ambayo mingi inachochea jazba kwa wananchi na kusababisha vurugu kuendelea bila sababu.

Alisema matamko hayo yanasababishwa na ofisi kuu ambazo zina uwezo na mamlaka ya kuzizuia, kukaa kimya, suala ambalo linazidi kutoa mianya ya matamko hayo kuendelea kutolewa na huenda hali hiyo isipodhibitiwa, amani inaweza kutoweka.

Katibu wa CCM wa Mkoa wa Arusha, Mary Chatanda, alisema tukio la jana la madiwani wa Chadema kususia kikao cha serikali za mitaa - ALAT kilichofanyika kutokana na kutomtambua yeye kama mjumbe halali, ni mwendelezo wa lile la umeya kwa kuwa ufafanuzi ulishatolewa juu yake.

Alisema madiwani hao wana lengo la kupotosha wananchi wa hapa, kwa kuwa wao wameshaelewa ila wanashindwa kuwarudia wananchi kuwaeleza kuwa awali hawakuelewa jinsi alivyokuwa mjumbe wa mkutano huo kwa kuwa ni mbunge wa viti maalumu Tanga.

Aliwataka viongozi hao wa Chadema kuacha kufanya matendo hayo ambayo mwisho wake yatazua vurugu na badala yake, waanze kufanya kazi za kuwatumikia wananchi wa kata zao kwa ajili ya maendeleo.

Jana jioni Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe alisema kuwa miili ya marehemu itaongozwa kwa maandamano kupita katika baadhi ya barabara za Jiji la Arusha hadi katika Uwanja wa NMC ambapo ibada ya mazishi itafanyika.

Mbowe ambaye aliitisha mkutano na waandishi wa habari katika Ofisi ya Mbunge wa Arusha mjini, Godbles Lema alisema mbali na Polisi kuruhusu kufanya ibada katika eneo la NMC, pia imeruhusu maandamano.

Maiti hao watapitishwa katika barabara ya Goliondoi na Sokoine hadi Uwanja wa NMC mara tu baada ya kutolewa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru.

Wabunge wote 48 wa Chadema pia watakuwepo na tayari wabunge 18 wameshawasili mjini Arusha kuhudhuria mazishi hayo.

Mwenyekiti huyo alisema mbali ya wabunge hao, viongozi wote wa Chadema Taifa, wakurugenzi wa idara zote za chama hicho na wengine kutoka katika mikoa mbalimbali,
wameshawasili mjini Arusha.

Baada ya kutoa heshima za mwisho, marehemu Omari atazikwa kwanza katika mji wa Usa ulioko wilayani Arumeru mkoani Arusha na baada ya kumalizika kwa maziko hayo, ndio mwili wa Mtui utasafirishwa kwenda wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro.

Mbowe alisema waombolezaji wote watavaa nguo nyeusi na vitambaa vyeusi vilivyofungwa mkononi kuashiria maombolezo.
 
Back
Top Bottom