Chadema, Polisi wabishania eneo la kuombea marehemu

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
268
Mgogoro mwingine umeibuka kati ya Jeshi la Polisi mkoani Arusha na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kufuatia hatua ya polisi kukataa kuruhusu uwanja wa NMC kutumika kuwaaga marehemu waliouawa na polisi katika vurugu zilizotokea Jumatano iliyopita.
Hatua hiyo inakuja wakati chama hicho kikiwa tayari kimefanya maandalizi ya ibada ya kuwaaga marehemu kesho kama mashujaa waliofia katika vuguvugu la kutafuta haki.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Chadema mkoani Arusha, Samson Mwigamba, alisema hadi kufikia jana saa 8:00 mchana, walikuwa bado hawajapewa kibali cha kufanyia ibada katika uwanja huo maarufu kwa mikutano ya hadhara.
Alisema Polisi wanasita kutoa kibali kuruhusu kufanya ibada za mazishi kwenye viwanja vya NMC kwa madai kuwa eneo hilo ndilo lilikuwa chanzo cha vurugu zilizosababisha maafa na kwamba huenda watu watapandwa na hasira na kuzua vurugu nyingine kati yao na polisi.
“Mimi bado naendelea kumwelewesha Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, atoe kibali hicho cha kuruhusu ibada yetu tufanye NMC, kwa sababu ndio mahali tulipokutana na marehemu kabla ya kuuawa na polisi, pia nimemhakikishia kuwa hakuna tatizo litakalotokea,” alisema Mwigamba.
Alieleza kwamba waliambiwa na polisi kuwa eneo mbadala la kufanyia ibada ya mazishi ni viwanja vya Suye au Shule ya Msingi Sinoni, ambako ni nje ya Jiji.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Thobias Andengenye, alipotafutwa ofisini kwake na waandishi wa habari, katibu muhtasi wake alieleza kwamba alikuwa katika kikao na viongozi wa juu wa jeshi hilo.
“Kamanda hayupo ofisini, leo yuko katika mkutano labda mrudi baadaye au muwasiliane naye kwa njia ya simu,” alisema katibu muhtasi huyo ambaye hakutaka kutajwa jina.
Hata hivyo, waandishi wa habari walimpigia simu yake ya kiganjani kwa muda mrefu na ilikuwa ikiita bila kupokelewa.
Naye Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema, alisema polisi hawana haja ya kupata wasiwasi, wao watoe kibali na kama wanahofia usalama wao, basi wenyewe Chadema watalinda amani eneo hilo la msiba.
“Kwani hapo patakuwa na ibada na hakutakuwa na vurugu zozote, wao wasiwasi wao kwa kile kibaya walichowafanyia wananchi, kuwapiga risasi kama wanyama,” alisema Lema.
Aidha, Lema alisema tayari wagonjwa wawili ambao ni Frederick Elia na Franck Joseph, wamewahamishia katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC, mkoani Kilimanjaro kwa matibabu zaidi baada ya hali zao kuwa mbaya.
Lema alisema chama chake kuanzia ngazi ya mkoa hadi taifa, kinaendelea kushirikiana na watu wenye mapenzi mema katika kutoa misaada ya hali na mali kwa familia za marehemu hao.
Marehemu waliopoteza maisha katika vurugu hizo ni Ismail Omary, mkazi wa Mbauda na Denis Michael, mkazi wa Sakina.
Ibada maalum ya kuagwa narehemu hao itafanyika kesho na kuwashirikisha viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa, madhehebu ya dini na wananchi kwa ujumla.
CHADEMA YASHINDA UENYEKITI HAI
Katika hatua nyingine, Chadema kimefanikiwa kupata nafasi ya kuongoza Halmashauri ya Wilaya ya Hai baada ya Diwani wa Kata ya Machame Kaskazini, Clement Kwayu, kuibuka mshindi wa nafasi ya Mwenyekiti.
Kwayu alipata kura 12 dhidi ya Ally Mwanga (CCM), Diwani wa Kata ya Masama Mashariki aliyepata kura 10.
Akitangaza matokeo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Melckzedeck Humbe, alimtangaza Kwayu kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo kwa miaka mitano ijayo.
Hata hivyo, nafasi ya Makamu Mwenyekiti ilipigiwa kura mara mbili baada ya wagombea Adrsi Manrai, Diwani wa Kata ya Weruweru (CCM) na Deogratias Kimaro, Diwani wa Kata ya Masama Kati (Chadema), kufungana hadi mgombea wa Chadema alipoamua kujitoa.
Akitangaza uamuzi wa kujitoa, Kimaro alisema kutokana na
Mwenyekiti kutoka Chadema, ni vyema akamuachia mwenzake kwa kuwa lengo si kuendeleza itikadi za vyama vyao, bali kuhakikisha maendeleo ya dhati yanapatikana kwa wananchi wa Jimbo la Hai.

MARY CHATANDA ACHAFUA TENA HALI YA HEWA
Wakati huohuo, Mbunge wa Viti Maalum Tanga na Katibu wa CCM Mkoani Arusha, Mary Chatanda, anaendelea kusababisha mgogoro wa kisiasa mkoani Arusha, baada ya kulazimisha kuwa mjumbe halali wa kikao cha Jumuiya za Serikali za Mitaa Tanzania (ALAT) mkoani Arusha na kususia kikao cha uchaguzi.
Kikao hicho kikiwa kinaendeshwa na Mwenyekiti wa muda, Ismail Katamboi, Diwani wa Kata ya Kisongo, kilisababisha wajumbe sita wa Chadema kutoka nje ya ukumbi huo kwa madai ya kuwa kimeingiliwa na mjumbe haramu, Chatanda.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutoka ndani ya kikao hicho, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbles Lema, alisema yeye na wenzake watano Cesilia Paleso, Diwani Viti Maalum Karatu; Lazaro Maasai, Mwenyekiti Halmashauri Karatu; Joyce Mukya, Mbunge Viti Maalum Arusha; Winner Kitembe, Diwani wa Karatu na Mchungaji Israel Natse, Mbunge Karatu, wamelazimika kutoka nje ya kikao hicho.
“Sisi tumetoka ndani ya kikao hiki kwa sababu Chatanda ambaye ni Mbunge wa Tanga iweje leo apige kura kuchagua wawakilishi wa mkoa Arusha," Alihoji Lema.
Wakati hayo yakijiri, wajumbe halali wa kikao hicho walitakiwa kuwa 40, lakini baada ya wajumbe sita wa Chadema kutoka nje walibaki wajumbe 28 wa CCM wakiendelea na uchaguzi.
Hata hivyo, wabunge kadhaa wa CCM hawakuhudhuria, wakiwemo Edward Lowassa (Monduli); Lekule Laizer (Longido; Goodluck Ole Medeye (Arumeru Magharibi); Jeremiah Sumari (Arumeru Mashariki) na wajumbe wawili wa Halmashauri ya Jiji ambao hawajachaguliwa.
Aidha, Gaudence Lyimo, ambaye ushindi wake wa Umeya ni wa utata hakuhudhuria.
Chatanda ndiye aliyesababisha mgogoro wa Umeya katika Jiji la Arusha.
Imeandikwa na Charles Ole Ngereza na Cynthia Mwilolezi (Arusha na Salome Kitomari (Moshi).


CHANZO: NIPASHE
 
Huko mbeleni kila kusanyiko la watu litahitaji kibali cha polisi. Sijui nchi inapelekwa wapi na hizi hofu za kijinga zinazotokana na "taarifa za kiintelejesia". Itabidi mkitaka kwenda mpirani, kwenye mazishi, harusi, kitchen party nk mpate kibali cha polisi
 
Huko mbeleni kila kusanyiko la watu litahitaji kibali cha polisi. Sijui nchi inapelekwa wapi na hizi hofu za kijinga zinazotokana na "taarifa za kiintelejesia". Itabidi mkitaka kwenda mpirani, kwenye mazishi, harusi, kitchen party nk mpate kibali cha polisi

Kiswahili kimekuwa watu watakuelewa vibaya, tumia kiswahili kilekile cha zamni (fasaha)
 
Ujinga mtupu wa polisi. Watoe kibali halafu wao wakae pembeni waone kama kutatokea vurugu!
Ila wakizuia nawaomba viongozi wa CDM wasirudi nyuma, pakia miili ya marehemu halafu elekeeni uwanjani kuwaaga, hata polisi wataona aibu kuzuia, na kama wakizuia waachieni miili ya marehemu waamue wapi pa kuipeleka wenyewe.
Tusipokuwa makini tutafikishwa mahali pa kuomba vibali polisi hata kufanya kikao cha familia!
 
Back
Top Bottom