CHADEMA mwendo mdundo

Kujua kama CHADEMA ni mwendo mdundo au la! hakuitaji kunakshiwa kwa nakala ndefu...hii inaonyesha hali si shwari ndani ya chama. "Mwendo mdundo wa chama" uonesheni kwa vitendo, itasaidia ku-save time ya kuandika nakala ndefu za utetezi.
 
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema propaganda na shutuma mbalimbali zinazoendelea katika chama hicho wamezizoea na haziwatingishi kwani watazimaliza katika vikao vya chama.

Kimedai kwamba hali kama hiyo imekuwa ikitokea mara kwa mara kunapokaribia uchaguzi mkuu, kwani Chadema ni ya wanachama na si Mwenyekiti wake Freeman Mbowe au Katibu Mkuu, Wilbroad Slaa.

Akifungua Kongamano la Baraza Kuu la Vijana wa Chadema(BAVICHA) Kanda ya Dar es Salaam, Kaimu Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika alisema kuanzia mwaka 2004 kwa nyakati tofauti wamekuwa wakikumbana na masuala kama hayo lakini yamekuwa yakimalizika bila kukiathiri chama.

Alisema hata kuondolewa kwa maofisa katika chama hicho si jambo la ajabu la kusababisha shutuma mbalimbali ambazo hawakuwahi kuzitoa awali wakiwa ndani ya chama.

“Hata Mzee Halimoja aliondolewa na hapakutokea malumbano ya aina hiyo hivyo kuna msukumo fulani ili kuyumbisha chama, jambo ambalo wanachama hatudanganyiki kukigawa chama.

“Propaganda zinazoendeshwa baina ya chama chetu kudaiwa kutaka kuwaondoa vijana katika ngazi za uongozi si za kweli hivyo tunawataka wale wanaotoa shutuma mbalimbali kwa chama hicho kuwasilisha vielelezo na siyo kuropoka kama vichaa,” alisema.

Alidai kwamba chama hicho kimekuwa kikitoa nafasi mbalimbali kwa vijana na hakuna mpango wa kuwaondoa vijana kwani waanzilishi wake walistaafu ili kuwaachia vijana nafasi.

Hivi karibuni wanachama wawili wa chama hicho, David Kafulila na Danda Juju, walijivua uanachama wa Chadema.

Kafulila ambaye alikuwa Ofisa Habari wa Chadema, amejiunga na NCCR-Mageuzi.

Juju hajasema chama anachohamia. Alisema fedha zinazopatikana kwa njia ya ujumbe mfupi (SMS) zinaingia katika akaunti za kawaida za chama na hazina usiri wa aina yoyote.

Aliendelea kusisitiza kwamba wako tayari kukaguliwa mapato yake na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwani chama hicho kimekuwa kikikaguliwa hesabu zake kila mwaka na kupata hati safi.

Katika hatua nyingine, Chadema kimemuomba Rais Jakaya Kikwete iwapo atashinda uchaguzi ujao, ateue vijana wenye sifa za uongozi .

Aliwataka vijana kutumia kongamano hilo kukosoa na kujadili masuala mbalimbali yahusuyo mwelekeo wa chama kwa kufuata maadili kwani wao ni walinzi wa chama na yeyote atakayeenda kinyume cha Chama achukuliwe hatua kwani bila kufanya hivyo chama kitakuwa kimefilisika kimaadili.

Aliwasihi kujadili mustakabali wa chama hicho hasa katika kipindi hili ambacho taifa linatarajia kuadhimisha miaka 48 ya uhuru.

Aliwapongeza viongozi wa jimbo la Dar es Salaam kichama kwa kufanikiwa kupata viti 14 katika uchaguzi wa serikali za mitaa tofauti na viwili walivyokuwa navyo.

Awali, Ofisa wa VIjana Taifa, Ali Chitanda alisema kongamano hilo la siku moja linawashirikisha wajumbe kutoka kata 50 katika jimbo la Dar es Salaam.

Watapata fursa ya kujadili kuhusu matokeo ya uchaguzi wa serikali za mitaa na ushirikishwaji wa vijana katika uchaguzi mkuu ujao.

Hakika CHADEMA mwendo mdundo fichua mafisadi.....
 
Back
Top Bottom