CHADEMA kukumbuka waliouawa

Imany John

JF-Expert Member
Jul 30, 2011
2,930
1,165
na Grace Macha, Arusha

VIONGOZI wakuu wa kitaifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), leo watawaongoza maelfu wa wakazi wa Jiji la Arusha katika kumbukumbu ya mwaka mmoja ya watu waliouawa kikatili na askari polisi, Januari 5, mwaka jana.

Taarifa ya Katibu wa CHADEMA Mkoa wa Arusha, Amani Golugwa, ilisema jana kuwa viongozi karibu wote ngazi ya taifa, wabunge, wajumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya chama hicho walikuwa wamewasili mkoani hapa tayari kushiriki kumbukumbu hiyo, huku mamia ya wanachama wakifanya maandalizi muhimu na mazito ya maadhimisho hayo.

Habari za kuaminika zinasema kuwa viongozi hao watafanya makubwa katika viwanja vya NMC, Unga Ltd ambako watawataja waliouawa katika maandamano ya mwaka jana kama mashujaa wa demokrasia nchini.

Imeelezwa kuwa Jeshi la Polisi limetoa baraka zote za mkutano huo, baada ya kile kilichoelezwa kuwa kuzuia maadhimisho hayo kungeweza kuleta hatari nyingine ya machafuko.

Golugwa alisema wamewasiliana na Jeshi la Polisi ili kupata kibali cha mkutano huo wa hadhara ambapo Januari 3, mwaka huu waliandika barua yenye kumbukumbu namba CDM/WLY/PL/11/015 kwenda kwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD) ya Arusha kumtaarifu juu ya mkutano huo.

Katibu huyo alisema baada ya Jeshi la Polisi kupokea barua yao, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Thobias Andengenye, alimpigia simu kumtaka wakutane ofisini kwake jana saa 4:00 asubuhi kujadili suala hilo lakini alipofika hakumwona kwa madai kuwa RPC alikuwa ameitwa kwenye kikao cha dharura ofisini kwa mkuu wa mkoa.

"Kupitia kwa mmoja wa wasaidizi wake, RPC ameniahidi kunipigia ili tukutane mara baada ya kumaliza kikao chake na RC na kulingana na mahitaji ya kisheria, sisi tunaendelea na maandalizi ya mkutano na shughuli zote tulizopanga kufanya kesho (leo) kwani tayari tumewaarifu polisi kama sheria inavyoagiza," alisema Golugwa.

Hata hivyo, uchunguzi umebainisha kuwa jeshi hilo limejiweka tayari kukabiliana na lolote litakalotokea, kwani huenda hotuba za viongozi zitaweza kukumbusha machungu kwa ndugu wa marehemu na wale walioachwa vilema. Mbali na mkutano huo, viongozi waandamizi wa CHADEMA watawatembelea wajane wawili wa marehemu Ismail Oma na Dennis Shirima waliouawa kwa kupigwa risasi na polisi Januari 5, mwaka jana.

Aidha, watawatembelea majeruhi 20 ambao chama kina taarifa zao sahihi na wale waliogharamiwa matibabu kwa msaada wa chama hicho kwa nia ya kuwajulia hali na kuzidi kuwatia moyo kuwa wako pamoja katika harakati za kudai mabadiliko.

"Mwaka wa 2012 tunataka uwe mwaka wa kuifanya Arusha yetu iweze kufikia mabadiliko chanya ya kiuchumi, kisiasa na kijamii na zaidi sana kushughulikia kwa dhati suala la ajira kwa wasio na ajira," alisema katibu huyo.


Chanzo: TANZANIA DAIMA
 
Kibali hakitatoka na watapigwa risasi kwa kufanya mkutano bila kibali......lol
 
Back
Top Bottom