Chadema Kigamboni wataka kuandamana kumpinga Magufuli

Tumaini Makene

JF-Expert Member
Jan 6, 2012
2,642
6,071

TAARIFA KWA VYOMBO VY A HABARI

TAMKO LA WANACHADEMA KIGAMBONI JUU YA MAANDAMANO KUPINGA UAMUZI NA KAULI ZA WAZIRI JOHN MAGUFULI

WANACHAMA wa CHADEMA Kigamboni na Watanzania wengine kwa ujumla wanaoguswa na maamuzi mabovu ya serikali, kupitia kwetu viongozi wao, wanapenda kueleza umma wa Watanzania kuwa wamedhamiria kufanya maandamano ya amani wakati wowote kuanzia sasa, yatakayofuatiwa na mkutano wa hadhara ikiwa ni njia ya kutoa maoni na hisia zao kupinga amri ya serikali kupitia kwa Waziri John Magufuli ya kupandisha nauli ya abiria, vitu na bidhaa!

Asubuhi ya Januari Mosi, 2012 ilikuwa ni kati ya siku zenye machungu makubwa kwa wananchi wa Dar es Salaam, hususan kwa sisi wakazi wa Kigamboni.

Ndiyo siku ambayo Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa Dkt. John Magufuli alipigilia moja ya misumari mikubwa katika jeneza la maisha magumu linalozidi kutengenezwa na serikali hii ya awamu ya nne, karibu kila siku na kuzidi kuwadidimiza Watanzania katika kaburi la umaskini.

Ndiyo siku ambayo pia, Watanzania kwa ujumla wao, hasa wanaotumia jicho la tatu kuyaangalia na kutafakari masuala mbalimbali yanayoendelea nchini na utendaji kazi wa watawala waliopo, waligundua rangi halisi ya Dkt. John Magufuli, kuwa ni mtawala (si kiongozi) wa aina gani kutokana na lugha ya kejeli, matusi na dhihaka iliyovuka mipaka kutumiwa na mtu wa nafasi kama yake kwa watu wanaotakiwa kuwa mabosi wake, yaani wananchi.

Kama ilivyoripotiwa katika vyombo vya habari mbalimbali siku ya Januari 2, 2012, Dkt. Magufuli alifanya ziara inayosemwa kuwa ilikuwa ya kushtukiza kutembelea Kivuko cha Kigamboni, kwenda kujionea utekelezaji wa agizo lake la kupandisha kiwango cha nauli na baadaye akaweka msisitizo wa matumizi ya nauli hizo mpya, alizozipandisha hivi karibuni.

Ambapo kinyume kabisa na matarajio ya wananchi kuwa waziri huyo angeliamua kuwa kiongozi kwa kusikiliza hoja za wananchi, kujadiliana, kushauriana nao na kufikia makubaliano ya namna bora ya kusimamia utaratibu wa uendeshaji wa Kivuko cha Kigamboni, Dkt. Magufuli aliamua kuonesha wazi gamba lake la ulevi wa madaraka na sifa, ambayo ndiyo hulka ya watawala, kwa kutujibu kwa kejeli Watanzania tunaoishi/kufanya kazi/shughuli zetu Kigamboni.

Waziri kama alivyonukuliwa katika vyombo vya habari, (ambavyo vilimnukuu kwa usahihi kabisa, ndiyo maana hajasikika akiomba samahani au kusema kuwa amenukuliwa vibaya), ametukejeli kwa kiwango kikubwa cha kuudhi na kukasirisha, kuwa kama hatuwezi kulipa ongezeko la nauli mpya basi tujifunze kupiga mbizi, ili tuvuke kwa kuogelea, turudi vijijini ama tuzunguke tupitie Kongowe.

Siku hiyo hiyo katika hiyo ziara yake, Dkt. Magufuli alipingwa vikali na Mbunge wa Kigamboni, Dkt. Faustine Ndugulile ambaye amenukuliwa katika vyombo vya habari akisema kuwa mapato ya kivuko yameendelea kubakia hapo yalipo kutokana na baadhi ya watumishi kukatisha risiti hususan za magari kwa kutumia vitabu bandia, pamoja na kuzirudisha katika mzunguko tiketi zilizotumika.

Pia imeripotiwa katika baadhi ya vyombo vya habari kuwa, Dkt. Magufuli alionekana kukerwa na msimamo wa Dk. Ndugulile wa kubainisha mianya ya ubadhirifu unaofanyika katika kivuko hicho. Bila shaka hii inatokana na ukweli kuwa hoja za mbunge huyo zilikuwa zinaharamisha hoja za waziri kuwa eti mapato kidogo yanayopatikana katika kivuko hicho ndiyo moja ya sababu ya kupandisha kiwango cha nauli!

Siku iliyofuata yaani Januari 3, 2012, wabunge wa Dar es Salaam kwa kuona unyeti wa suala hilo, kwa umoja wao, waliamua kutoa kauli, wakimtaka Waziri Magufuli abatilishe uamuzi wake huo wa kupandisha nauli kutokana na ukweli kuwa haukufuata misingi ya michakato iliyo sahihi katika kuwatendea haki wananchi lakini pia wakamtaka atuombe radhi sisi wananchi aliotukosea kwa kututamkia lugha isiyo ya staha.

Kw akiburi chake cha majivuno, kulewa sifa na madaraka ambayo ni hulka ya watu wanaoamua kuwa watawala na si viongozi wa watu, Waziri Magufuli hajatekeleza ushauri na maagizo ya wabunge hao wa Dar es Salaam, ambayo kimantiki ndiyo wawakilishi wa wananchi.

Katika tamko letu hili, Chama cha Demokrasia na Maendeleo Wilaya ya Kigamboni, tunataka kuhoji na kufafanua masuala kadhaa katika kadhia hii iliyosababishwa na Waziri Magufuli! Tunataka Watanzania kwa pamoja, wajielekeze katika kutafakari masuala ya msingi kwa kina na kwa nguvu za hoja, si kupapasa juu juu, huku wakisukumwa na propaganda zinazoonekana kumbeba Waziri Magufuli kwa kitendo chake hicho cha hovyo na kauli zake mbovu zisizo chembe ya uungwana.

Hivi Kivuko ni huduma ama biashara?

Hapa tunaomba Watanzania wajadili kwa mapana mantiki ya kuwepo kwa vivuko vya namna ya hiki cha Kigamboni ambavyo viko sehemu kadhaa mbalimbali hapa nchini. Tunataka Watanzania pia ikiwezekana wajadili utofauti uliopo baina ya matumizi ya vivuko (ferries) na meli, ambapo mantiki ya haraka kutupatia moja ya majibu inapatikana katika utofauti wa usimamizi wa vitu hivi viwili, ambapo vivuko viko chini ya Wizara ya Ujenzi na usafiri wa meli uko chini ya Wizara ya Uchukuzi.

CHADEMA Wilaya ya Kigamboni, tunavyoona sisi, vivuko ni/vinapaswa kuwa huduma na si biashara. Hitimisho la kimantiki kuwa vivuko ni huduma na si biashara linafikiwa kutokana na mifano kadhaa hapa hapa nchini na nje ya nchi, ambapo imedhihirika mahala pengi tu kuwa vivuko ni mbadala wa daraja, ambapo kutokana na uzembe na upungufu wa umakini, serikali imeshindwa kujenga daraja/madaraja katika eneo/maeneo husika ili kuondoa haja ya kutumia kivuko!

Upo mfano sahihi huko Kusini mwa Tanzania. Kabla ya kujengwa kwa Daraja la Mkapa katika Bonde la Mto Rufiji, wananchi walikuwa wakivushwa kwa kivuko/vivuko huku wakilipishwa nauli! Kama ilivyo hapa Dar es Salaam, kwenye kivuko chetu hapa cha Kigamboni.

Tangu baada ya kujengwa kwa Daraja la Mkapa, ambalo linasemekana kuwa moja ya madaraja bora hapa nchini, wananchi Watanzania wenzetu waliokuwa wakisafiri kutoka au kwenda, Kusini, hususan mikoa ya Lindi na Mtwara, walipata ahueni na kuondokana KABISA na kadhia ya kulipa nauli kuvuka eneo la kilometa 1, kutoka ng'ambo moja kwenda nyingine.

Nchini Zambia pia, katika baadhi ya maeneo, wananchi wanavuka katika vivuko kama hiki cha Kigamboni, bure. Maana serikali inajua kuwa ni wajibu wake kuhakikisha eneo kama hilo linakuwa ni sehemu ya barabara, kwa kuunganishwa na daraja.

Hoja tunayoijenga hapa ni kuonesha kuwa kamwe serikali haiwezi kufanya kivuko/vivuko kuwa ni maeneo ya kufanya biashara na kujipatia faida eti kwa kisingizio cha uendeshaji wa mahali husika! Vivuko vitofautishwe na meli! Ndiyo maana hata usimamizi wa vivuko uko chini ya Wizara ya Ujenzi na ule wa meli chini ya Wizara ya Uchukuzi.

Upotoshaji mkubwa; suala si nauli ya shilingi 100 bali ni rationality ya uamuzi huo

Kuna upotoshwaji mkubwa katika suala hili, ambapo inachangiwa sana na vitu kadhaa, ikiwemo propaganda za wanaotaka Waziri Magufuli aendelee kuonekana shujaa hata anapofanya uamuzi wa hovyo na wa kibabe kama huu. Suala jingine linalochangia upotoshaji ni wachangiaji wa mjadala wa suala hili kutoelewa implications za uamuzi wa Magufuli, lakini pia kujikita kuzungumzia matokeo ya kitu badala ya principles.

Mathalani suala sasa linaloonekana kuteka mjadala ni nauli ya shilingi 200, iliyopandishwa kwa asilimia 100, kutoka shilingi 100 ya awali. Sasa inaonekana eti watu wa Dar es Salaam na hasa watumiaji wa Kivuko cha Kigamboni, kuwa tunalilia na kulalamikia shilingi 100 tu, wakati mahali pengine kama Busisi (Mwanza-Sengerema), Kamanga (Mwanza-Sengerema), Chato (Jimboni kwa Magufuli) Watanzania wenzetu wanalipa kati ya shilingi 300/= hadi shilingi 3,000/=

Taswira na propaganda inayojengwa hapa ni kwamba sisi ni walalamishi, tena tunalalamikia kitu kidogo sana, wakati Watanzania wengine wanalipa kitu kikubwa na wala hawajawahi kulalamika! Hoja ya ajabu sana hii.

Wakati tukielewa uhalisia kuwa upandaji wa gharama hizi utaongeza ukali wa maisha kwa watumiaji wa kivuko hicho ambacho ni kiunganisho muhimu kwa wananchi wa rika zote, tunaombwa serikali itueleze, mafanikio yanayojitokeza kwenye mataifa mengine ambayo huduma za kivuko zinatolewa bure lakini kwa Tanzania bei inaongezeka kila mara.

Suala hapa ni rationality ya upandaji wa gharama hizo za nauli, ikihusishwa na namna gani zitakavyopandisha gharama za maisha kwa kiasi kisichoweza kuelezeka kwa wakazi wa Dar es Salaam, hususan sisi wakazi wa Kigamboni.

Uamuzi huo wa kupandisha nauli kama ifuatavyo; watu wazima (sh. 200), watoto chini ya miaka 14 (sh. 50), baiskeli (sh. 300), pikipiki (500), mzigo chini kg 50 (200), mkokoteni (1,500) Guta (1,800) Bajaj (1,300), wanyama (2,000), wanyama wadogo (1,000), gari dogo (1,500), gari dogo pick up (2,000), station wagon (2,000), basi dogo Hiace (3,500) gari zaidi ya tani (7,500) basi kubwa (7,500) na trekta (7,500).

Uamuzi huo una maana kadhaa, ikiwemo kadhia ya kuongeza gharama za uchukuzi, kwa sababu vyombo hivyo ndivyo vinavyotumiwa na wananchi kusafirisha bidhaa, kutoka ama kwenda Kigamboni. Ukishapandisha gharama za uchukuzi maana yake pia unapandisha gharama za vitu/ bidhaa matokeo yake ni kupanda kwa gharama za maisha. Hili ndilo suala, suala si nauli ya shilingi 200.

Pia suala jingine la muhimu sana kujua na kujadili ni namna ya udhibiti wa vivuko ambao daima umekuwa chini ya serikali. Watanzania tujadili kwa mapana hii hoja, kama udhibiti wa masuala mengine kama vile gesi, mafuta, maji na usafiri wa majini na nchi kavu, ambako sekta binafsi inashiriki katika kuendesha, tumeweka vyombo vya kudhibiti kama vile TPDC, EWURA, SUMATRA, tukiwadhibiti na kuwasimamia watu binafsi, kwa nini hali haiko hivyo hivyo kwa sekta hii ya vivuko ambayo inaendeshwa na serikali?

Kwa nini tunaendelea kuruhusu matumizi ya sheria mbovu inayoweza kumruhusu mtu mmoja kama waziri kuamua mstakabali wa jamii nzima kama alivyofanya Waziri Magufuli bila hata kuwajibika/kulazimika kushauriana na wadau mbalimbali na kupata ruksa (approval). Huu ni ukiritimba usioweza kukubalika na ndiyo watu wa Kigamboni tunaoupinga.

Kupitia uamuzi huu wa kukurupuka wa Waziri Magufuli, wananchi tujadili na kupinga kwa njia zozote sahihi maamuzi ya namna hii.

Kama katika sekta binafsi na sekta zingine kama umeme tumeweka utaratibu wa kuwashirikisha wadau, kama wafanyavyo TANESCO wakitaka kupandisha bei ya umeme, ambapo EWURA hushirikisha wadau au usafiri wa meli na nchi kavu ambapo SUMATRA hushirikisha wadau wote au TPDC inavyoshirikisha wadau katika masuala ya gesi, kwa nini isiwe katika masuala ya vivuko ambapo Sheria ya Vivuko (Ferry Act) inampatia mamlaka makubwa ya kidikteta waziri husika.

Dhamira ya CHADEMA Kigamboni kuandamana

Wanachama wa CHADEMA Kigamboni tumedhamiria kuandamana kupinga hatua ya serikali kupitia kwa Waziri Magufuli, ya kutupandishia wananchi wa Kigamboni na kutuongezea ukali wa maisha.

Tumefuata utaratibu wa kisheria kama tunavyotakiwa. Januari 2, 2012, CHADEMA Kigamboni, tuliandika barua yenye Kumbukumbu Na. CH/KG/J1/2012, kutoa taarifa ya maandamano ya amani ambayo ilikuwa yafanyike kesho Ijumaa (Januari 6, 2012), ambayo yangeanzia Feri Kituo cha Daladala na kuishia kwa mkutano wa hadhara kwenye viwanja vya Machava.

Katika majibu yake Jeshi la Polisi Wilaya ya Temeke lilisema katika barua yake ya Januari 2, 2012, yenye Kumbukumbu Na. KGD/SO.7/2/A/102, yeye hahusiki. Iliandikwa "napenda kukujulisha kuwa utaratibu wa kutoa taarifa au kuomba kibali cha kufanya maandamano huelekezwa kwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalum. Tafadhali peleka maombi yako pale, nakala kwa RPC Temeke na OCD Kigamboni."

Viongozi wa CHADEMA Kigamboni tulipokwenda kwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalum kama tulivyoelekezwa, alionekana kushangazwa sana na utaratibu huo wa Polisi Temeke, akawamuru watusikilize na watoe maamuzi wao kama taratibu zinavyosema.

Tulivyorudi Polisi Kigamboni, wakatuambia turudi mapema asubuhi Januari 4, 2012 kupata majibu. Kweli OCD wa Kigamboni alitupigia simu asubuhi. Tulipofika pale akatuambia twende ofisi ya RPC Mkoa wa Kipolisi Temeke, ambaye alitukatalia maandamano yetu kwa barua ya Januari 3, 2012, yenye Kumbukumbu Na. TEMEKE/SO.7/2A/223, akisema;

"Hivyo basi tunaona njia ambayo waheshimiwa wameamua kuchukua waheshimiwa wabunge ni njia muafaka ambayo kila mtu anasubiri jibu la serikali. Hii inaonyesha binadamu wanaopenda mashauriano na makubaliano hudumisha amani na utulibu na ndilo somo tunalopata kutokana na sababu hizo, chini ya kifungu Namba 43 (1)(6) cha sheria za Polisi na Polisi Wasaidizi sura 322 kama ilivyorekebishwa mwaka 2002 nasitisha maandamano na mkutano huo mliopanga kufanya tarehe 6.1.2102."

CHADEMA Kigamboni kweli tuliamua kuskiliza ushauri wa Jeshi la Polisi wa kusubiri jibu la serikali kwa hoja za wabunge wa Dar es Salaam. Jana, Januari 4, 2012, jibu la serikali lilipatikana kutoka kwa Waziri Magufuli ambaye kwa kiburi, bado amewadharau wawakilishi wetu na kuamua kuendelea na msimamo wa kupandisha nauli akisema kuwa hatabadili chochote.

Anasema tena kwa kujigamba kama ilivyo kawaida yake, kuwa amefuata sheria na utaratibu, kama unavyomruhusu, lakini sisi leo tunataka kumuuliza kitu kimoja tu! Amekuwa akijigamba kuwa anafuata utawala wa sheria, lakini je sheria hizo zote zinatenda haki. Maana msisitizo wa wanasheria siku hizi ni kwamba sheria zinapaswa kuwa zinatenda au zinatoa haki.

Kama ni suala la kufuata sheria pekee, hata Makaburu wa Afrika Kusini walikuwa wakiwanyanyasa Waafrika Weusi, kuwabagua kwa rangi ya ngozi yao hata kutunga sheria ya kuhalalisha ubaguzi wa rangi, ambazo alizitumia kuwatia kizuizini na kuwafunga jela wapiganaji kama akina Mzee Nelson Mandela. Je Magufuli naye anataka kujitapa na kujigamba kama wao kwa kufuata sheria zisizotenda wala zisizotoa haki?

Sasa madam jibu la serikali ambalo polisi walisema tusubiri limeshatoka, tunaomba Jeshi la Polisi eneo husika watuambie lini tutaweza kutimiza haki na wajibu wetu wa kikatiba wa kutoa maoni na hisia zetu juu ya jambo hili. Maana maandamano na mikusanyiko (mikutano) ni moja ya njia za kutoa na kueleeza hisia ama za kukubaliana au kupinga jambo Fulani. Tunaomba sasa watuambie siku, tarehe na muda wa kufanya maandamano yetu huko Kigamboni.

Tunatumaini Jeshi la Polisi watatusikiliza kama sisi tulivyowasikiliza wao kwa majadiliano na makubaliano ya heri, lakini kama hatutapewa fursa na Polisi kushindwa kutuambia hasa lini tufanye maandamano yetu, tutatoa taarifa ya kufanya maandamano hayo wakati wowote ama kwa kibali au bila kibali cha polisi, maana tunatimiza wajibu na haki ya kikatiba.

Imetolewa leo Januari 5, 2012 na CHADEMA Kigamboni

Rose Wilberd, Mwenyekiti Wilaya ya Kichama Kigamboni
 

Attachments

  • KIGAMBONI MAGUFULI.docx
    18.7 KB · Views: 110
CHADEMA kuweni makini kwenye haya malumbano ya kivuko, vinginevyo mtajikuta mnacheza ngoma ya moja ya mtandao wa CCM! Itakula kwenu.
 
Chadema bana kila siku wao matamko tu..

Mkimaliza kuandamana Kigamboni itabidi muende na Mwanza, Bukoba, Kigoma, kote huko serikali wamepandisha bei.

Mwanza itabidi maandamano yafanyike pale Busisi kivukoni na Kamanga
 
Nafikili huu ni mwanzo mzuri, sasa rose wilbert kama m/ kiti wa cdm upande wa temeke ujue mawasiliano na w/chama ni muhimu sana ivyo tunakuomba ulisimamie ili na uwe unatujulisha kila hatua inayofikiwa kwani nasi tuko nyuma yako km kiongozi kwa lolote litakalo amuliwa, tunashukuru sana for your initiatives
 
Msitegemee polisi watabariki hayo maandamano.
Wakikosa sababu watasingizia Alshabab au taarifa za kiintelijensia.
 
Back
Top Bottom