CHADEMA Iringa yamshukia Mwakalebela

Serayamajimbo

Senior Member
Apr 15, 2009
191
38
MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), wilaya ya Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa amesema Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Fredrick Mwakalebela, amepotea njia kugombea ubunge jimbo la Iringa mjini kwa kutumia michezo kwani mahitaji ya wakazi wa jimbo hilo si michezo.
Alisema Mwakalebela ameshindwa ubunge jimbo la Iringa Mjini hata kabla ya uchaguzi wala kuchukua fomu hivyo anapaswa kujipanga upya kwa mwaka 2015 sio 2010 tena.
Kauli hiyo ya CHADEMA imekuja huku zikiwa zimepita siku mbili toka Mwakalebela kupitia kampuni yake ya michezo Vannedrick (T) Ltd kudhamini mashindano ya Kombe la Krismasi na mwaka mpya katika jimbo la Iringa mjini kwa asilimia 100 huku akieleza kusudio lake la kugombea ubunge jimbo hilo mwaka 2010.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, mwenyekiti huyo wa CHADEMA alisema, kwa upande wake yeye na Mwakalebela ni marafiki ila katika suala hilo la kudhamini michezo kama njia ya kuwahadaa wakazi wa jimbo la Iringa Mjini haungi mkono na anachofanya Mwakalebela ni kuwachanganya wakazi wa jimbo hilo wanaohitaji kumpata mbunge atakayewatumikia kwa kufuata matakwa yao.
“Naomba mnielewe …sio ugomvi na Mwakalebela ila napenda kumweleza ukweli kuwa hawezi kupata ubunge jimbo la Iringa mjini kwa staili hiyo ambayo amekuja nayo ya michezo kwani mahitaji makubwa ya wana Iringa sio michezo; michezo ni sehemu ya burudani kwao….Iringa wanahitaji kuelimishwa juu ya kilimo, utunzaji mazingira kwa kupanda miti, afya na maendeleo yao mengine nje ya michezo,” alisema Msigwa.
Msigwa alisema kwa upande wake bado anampongeza mbunge wa jimbo la Iringa Mjini, Monica Mbega (CCM), kwani ameweza kufanya kazi nzuri katika kuwatumikia wana Iringa, japo kwa sasa anapaswa kupokelewa na CHADEMA.
 
Back
Top Bottom