CCM yataka Waziri Zanzibar ajiuzulu

BabuK

JF-Expert Member
Jul 30, 2008
1,845
329
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimemtaka Waziri wa Sheria na Katiba wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Abubakar Khamis Bakari ajiuzulu, kwa maelezo kuwa ameshindwa kuishauri vizuri Serikali kuhusu sheria na mwenendo wa vyama vya hiari nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari katika makao makuu ya CCM Kisiwandui, Unguja jana, Vuai Ali Vuai alisema kikundi cha kutoa mihadhara ya dini ya Kiislamu cha Jumuiya ya Uamsho, kimesajiliwa kutoa mihadhara ya dini na si kujishughulisha na siasa majukwaani.

Alisema kitendo cha Abubakar kushindwa kuishauri vizuri Serikali kuhusu mwenendo wa kikundi hicho, kimesababisha maafa na kuiingiza nchi katika wasiwasi mkubwa kiasi cha kuvurugika kwa biashara na utalii.

“CCM inamtaka Waziri wa Sheria na Katiba ajiuzulu mara moja, kwa sababu ameshindwa kumshauri vizuri Rais na Serikali kuhusu mwenendo wa kikundi cha Uamsho ambacho kinafahamika kazi yake ni kutoa mihadhara ya dini na si siasa,” alisema Vuai.

Alisema vyama vya hiari vilivyopata usajili wa kudumu wa kufanya shughuli zao, vinasajiliwa na Ofisi ya Katiba na Sheria ambayo ipo katika wizara yake.

Mawaziri walijua Kwa mujibu wa Vuai, mawaziri wa SMZ walikutana na viongozi wa vyama vya siasa na wa jumuiya hiyo Aprili 25 na kuitaka kuacha mihadhara ya siasa, la sivyo ichukuliwe hatua kali za kinidhamu.

“Tulimtaka Waziri wa Katiba na Sheria kulifanyia kazi suala hilo na kuona kwamba kikundi hicho hakifanyi mihadhara ya siasa, ikiwamo kukashifu viongozi na kuhoji uhalali wa Muungano, lakini hakufanya kazi hiyo,” alisema Vuai

Kinalindwa, kifutwe Vuai alisema hivi sasa CCM imetambua kwamba jumuiya ya Uamsho ipo katika kivuli cha chama cha siasa na ndiyo maana imekuwa ikifanya kiburi na jeuri kiasi cha kutamka kwamba hakuna mtu wa kuifuta.

Alisisitiza na kuitaka Serikali kuifuta jumuiya hiyo mara moja kwa sababu imekwenda kinyume na dhamira ya kuanzishwa kwake.

“Tunaitaka Serikali iifute mara moja taasisi ya Uamsho kwa sababu imekwenda kinyume na malengo ya kuanzishwa kwake kama vile Serikali ya Muungano ilipoifuta taasisi ya BAMITA (Baraza la Misikiti Tanzania),” alisema Vuai.

Vuai aliwataka wafuasi wa CCM kuwa watulivu katika kipindi chote na kuacha vurugu hizo ambazo zinahatarisha amani na utulivu.

Kwa mujibu wa Katiba ya Jumuiya ya Uamsho, taasisi hiyo ina kazi ya kutoa mihadhara ya kidini kwa waumini na wafuasi wake na kulinda haki za binadamu kwa makundi ya Waislamu.

Katiba ya chama hicho haitamki kufanya mihadhara ya siasa, ikiwamo ya kuwahamasisha wananchi kuhusu mambo ya siasa.

Serikali yakiri kukosea
Wakati huo huo, SMZ imekiri kufanya makosa kwa kuviachia vikundi vya dini kuhubiri siasa kiasi cha kuleta uchochezi na kusababisha fujo na vurugu.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud alisema hayo jana akiwa kwenye ziara ya kukagua baadhi ya maeneo yaliyokumbwa na fujo na kusababisha hasara kubwa hata makanisani.

Alisema ni kweli vipo vikundi vya kidini ambavyo kazi yao kubwa ni kutoa mihadhara ya kuelimisha jamii ya Kiislamu ambavyo vimejikita katika siasa.

“Tunakubali Serikali imefanya makosa ... hili tatizo lipo, tumeliona kuanzia sasa vikundi vya kutoa elimu kuhusu masuala ya dini ni marufuku kuhubiri siasa,” alisema Aboud.

Alisema Serikali imeunda kamati kuchunguza fujo na vurugu zilizofanywa na jumuiya hiyo. Aliwataka wazazi kuzuia watoto wao kujihusisha na fujo hizo kwani sheria itachukua mkondo wake.

“Tumegundua kwamba watoto wanashiriki fujo hizo ikiwamo kurusha mawe na kuchoma matairi ya gari ... tukimkamata mtoto hakuna masamaha kutoka kwa mzazi yeyote,” alisema Aboud.

Makanisa kulindwa
Awali Mkuu wa Polisi nchini Inspekta Jenerali Said Mwema alisema watatoa ulinzi kwa nyumba za ibada kwa lengo la kukomesha uhalifu huo.

“Tutaweka ulinzi katika nyumba zote za ibada hasa makanisa, ili kusiwe na mipango mengine ya kufanya uhalifu wa hujuma za kuchoma moto makanisa,” alisema Mwema.

Alisema Jeshi la Polisi limegundua, kwamba katika mikakati hii ya vitendo vya uhalifu baadhi ya maeneo yanayolengwa na vikundi hivyo ni makanisa.

Watu 46 mbaroni Mwema alisema watu 46 wamekamatwa kwa tuhuma za kufanya fujo ikiwamo kushambulia polisi kwa mawe na kuchoma moto matairi na kuyaweka barabarani.

Alisema kazi ya kukamata watuhumiwa zaidi wa fujo inaendelea katika mitaa.

Viongozi wa dini
Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Bukoba, Method Kilaini alisema hali ya Zanzibar inatisha na wanaofanya vurugu na uchomaji nyumba za ibada ni wachache na anaamini wengine wengi ni watu wema.

Kilaini aliwataka Wazanzibari wasiokubaliana na hali hiyo na Serikali wahakikishe wanakomesha hali hiyo na kuwataka Wakristo wa Zanzibar na wa Tanzania Bara watulie kwani Kristu haruhusu vitendo vibaya.

“Changamoto ni kubwa, waumini na Wakristo walioko Zanzibar wawe wavumilivu sana kwa wakati huu na wao ni mashahidi katika kutetea imani yao na kumtetea Kristu,” alisema.

Mufti Shaaban Simba wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), alisema watatoa tamko kuhusu matukio hayo baada ya kukutana.

Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana, Valentino Mokiwa ambaye alitaka maoni yake yanukuliwe kama Mkristo na raia wa Tanzania, alisema, “kama hawataki Muungano walitakiwa kutumia busara, badala ya kuchoma moto makanisa.

Je, makanisa ni Muungano?
Wakristu Zanzibar ni kama asilimia tatu hivi,” alisema. Mokiwa alisema haamini kuwa waliofanya hivyo wanafuata maandiko ya vitabu vyao vya dini au wanashindwa kutafsiri maandiko yanavyosema.

“Wangepeleka malalamiko yao katika Baraza la Wawakilishi ambalo lingeyawasilisha kwenye tume inayoshughulikia kero za Muungano na wahusika wangemshauri Rais Jakaya Kikwete kuwa ndoa hii haiwezekani tena, mbona Rais ametoa fursa nyingi tu,” alisema.
Source: Habarileo
 
Back
Top Bottom