CCM wajikaanga; Sofia Simba amrarua Kigwangala baada ya jina la Bashe kufyekwa

nngu007

JF-Expert Member
Aug 2, 2010
15,862
5,797
Waandishi Wetu

Toleo la 260
26 Sep 2012



  • Wabunge kibao wafyekwa, wamo waliosaini Pinda ang'oke bungeni
  • Kamati Kuu, NEC mpya kubakiziwa viraka vya wabunge, mawaziri



MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Mrisho Kikwete, ameuvuruga mtandao wa Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, anyetajwa kuwa anakusudia kuwania urais mwaka 2015.


Kikwete, kupitia Kamati ya Usalama na Maadili ya chama hicho kikongwe chenye umri wa miaka 35 sasa, amefyeka takriban robo tatu ya mtandao wa ‘urais-2015' unaodaiwa kusukwa na Lowassa kwa kusaidiana na swahiba wake kisiasa, Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, kupitia Uchaguzi Mkuu wa ndani ya CCM, Raia Mwema, limeelezwa.
Kikwete anadaiwa kuchukua hatua hiyo kwa kusaidiwa na taarifa za kiusalama kuhusu wagombea ambao kwa sehemu kubwa walipachikwa kuandaa mtandao wa kupata mgombea urais 2015.


Kwa miaka mingi sasa, CCM imekuwa na kitengo chake cha usalama na maadili ambacho hata hivyo, kimekuwa wakati fulani kikiyumba kutimiza wajibu wake ipasavyo.


"Kamati Kuu pamoja na Halmashauri Kuu (NEC) ya chama ni vyombo ambavyo vimerahisishiwa kazi zake, Kamati ya Usalama na Maadili ambayo awali ilipangwa kufanyika kwa siku mbili lakini ikabainika muda huo hautoshi, ilifanya kazi kwa weledi mkubwa, ikitumia taarifa za kiintelijensia kupitia jina moja hadi jingine. Vibaraka, makapi na mitandao ya wapambe wa urais imevunjwa.


"Ingawa unaweza kuona mwisho wa vikao majina ya Lowassa na Andrew Chenge yamepitishwa lakini wamebaki wenyewe, mitandao wanayodaiwa kuiandaa imevunjwa kabisa. Wamebaki wenyewe bila mizizi," kinaeleza chanzo chetu cha habari kikikariri taarifa za Kamati ya Usalama na Maadili ya CCM ambayo, imepitia jina kwa jina, wilaya kwa wilaya kuhusu waliojitokeza kuwania nafasi hizo za uongozi ndani ya chama hicho kilichotokana na muungano wa vyama vya Tanganyika African National Union (TANU) na Afro Shiraz Party (ASP).


Sofia Simba dhidi ya Kigwangala

Taarifa za ndani ya kikao cha Kamati Kuu ya CCM kilichoanza kuketi Jumatatu wiki hii, kikiwa kimetanguliwa na vikao vya siku tatu mfululizo vya Kamati ya Usalama na Maadili ya CCM, zinaeleza kuwa Mwenyekiti anayemaliza muda wa Umoja wa Wanawake wa chama hicho (UWT), Sofia Simba, alikuwa kidedea kumtetea mgombea ujumbe wa NEC kutokea Wilaya ya Nzega, Hussein Bashe anayeaminika kuwamo katika mtandao wa Lowassa na awali, mtandao wa aliyekuwa Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz.

Mara kwa mara, Sofia alikuwa akimtetea Bashe lakini Mwenyekiti wa kikao cha Kamati Kuu ya CCM, Kikwete alikuwa ‘akizima' baadhi ya hoja zake zilizojiegemeza katika utetezi wa kundi lake badala ya utetezi wa chama.


Katika hali inayodaiwa kuwa ni Sofia kuzidiwa na changamoto za Kikwete akiwa kama Mwenyekiti wa kikao hicho, mwanamama huyo mwenye msimamo wa kutaka wabunge wa Viti Maalumu kuwekewa kikomo, alihoji ni kwa nini sababu zilizotumika kumwengua Bashe zisitumike kumng'oa Mbunge wa Nzega, Dk. Khamis Kigwangala.


"Kama suala la utovu wa maadili ya chama, wote wamehusika ni kwa nini basi mmoja ang'olewe na mwingine aachwe," anakaririwa Sofia Simba akipinga Kigwangala kubaki na kutokana na msimamo wake huo, Kikwete alikishawishi kikao kuondoa majina yote ya Bashe na Kigwangala.


Hatua hii ni mara ya pili kwa Sofia Simba kuwahi kugeuka mtetezi wa moja kwa moja wa mtandao unaoaminika kuwa ni wa Lowassa ndani ya CCM. Ni Sofia huyo huyo aliyepata kunukuliwa kutetea kundi la Lowassa, kiasi cha kutamka Lowassa ndiye mwanamume wa shoka, wakati alipokuwa akirushiwa ‘madongo' na baadhi ya wabunge waliokuwa wakisikilizwa hoja zao na iliyokuwa Kamati Maalumu ya CCM kunusuru kile kilichoitwa mpasuko wa wabunge wa CCM, ambao kwa mujibu wa kauli ya Mwenyekiti wa chama hicho, Kikwete, wabunge hao walifikia hatua ya kutoaminiana kiasi cha kutiliana shaka kuwekeana sumu.


Kamati hiyo maalumu, Mwenyekiti wake alikuwa Mzee Ali Hassan Mwinyi na Katibu wake akiwa Mzee Pius Msekwa, Makamu Mwenyekiti CCM-Tanzania Bara, wajumbe katika kamati hiyo walikuwa ni pamoja na Abdulrahman Kinana, ambaye ametangaza kujing'atua nafasi zote za uongozi alizokuwa akishikilia CCM.


Mgeja, Lembeli hoi, Diallo, Mabina warudi

Washindani wakuu wa siasa za Mkoa wa Shinyanga, ambao hata katika mchakato wa kura za maoni kupata wagombea ubunge kwa tiketi ya CCM, katika Uchaguzi Mkuu wa 2010 walionyesha tofauti zao za kisiasa ikiwamo kuwa katika makundi hasimu ya kisiasa ndani ya chama hicho, Khamis Mgeja ambaye anaelekea kutimiza ungwe yake ya uenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga na James Lembeli, ambaye ni Mbunge wa Kahama wamependekezwa kuengulia na kikao cha Kamati Kuu, ambacho hata hivyo ni nadra sana uamuzi wake kutenguliwa na Halmashauri Kuu.

Mgeja kwa miaka kadhaa sasa amekuwa mpambanaji mtiifu kwa mtandao wa Lowassa kuelekea 2015. Mgeja ameangushwa kama ilivyo kwa Lembeli anayeaminika kuwa mpambanaji mtiifu kwa Mbunge wa Urambo Mashariki, Samuel Sitta, Spika wa Bunge la tisa ambalo lilimng'oa katika wadhifa wa Waziri Mkuu Lowassa.


Kamati Kuu pia imegusa siasa za Jiji la Mwanza ambalo kwa namna fulani mahasimu
wa kisiasa wa CCM, yaani Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) nao wameanza kuyumba kisiasa wakiripotiwa kuchapana makonde baada ya uamuzi wa Kamati Kuu ya CHADEMA kuwavua madaraka madiwani wawili, Henry Matata ambaye ni Diwani wa Kata ya Kitangiri na Adam Chagulani, ambaye ni Diwani wa Kata ya Igoma, jijini Mwanza.


Kwa mujibu wa vyanzo vyetu vya habari, Diallo aliyepata kuwa Mbunge wa Ilemela na naibu waziri na waziri, jina lake limerudishwa kama ilivyo kwa Mwenyekiti wa sasa wa CCM, Clement Mabina, ambaye anatetea nafasi hiyo inayoviziwa na Diallo.


Wapo wagombea wengine wachache ambao majina yao yamerudi kuchuana na vigogo hao wa siasa za Jiji la Mwanza, ambalo ni maarufu kwa uvuvi wa samaki, hususan aina ya Sangara, jina ambalo limepachikwa operesheni za kisiasa za CHADEMA.


Wabaya wa Pinda wafyekwa

Taarifa zaidi zinaeleza kuwa, Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe ambaye ameomba kupitishwa na chama chake ili agombee nafasi ya ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, kutokea wilayani kwao Ludewa, amegonga mwamba.

Mbali na Filikunjombe, Mbunge wa Kisesa ambaye ameanza kujitambulisha kama mwanasiasa mwenye kufuata mkondo wa kupinga ufisadi kama ilivyopata kuwa kwa aliyekuwa Mbunge wa Nzega, Lucas Selelii, Mbunge wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka na Lembeli wa Kahama, naye amefyekwa jina lake. Mpina alikuwa akigombea nafasi ya uenyekiti wa CCM katika Mkoa wa Simiyu lilipo Jimbo lake la ubunge la Kisesa.


Wabunge wengine waliokumbwa na mkasa huo wa kufyekwa majina yao ni pamoja na Mbunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi na mwenzake wa Lupa, Victor Mwambalaswa.


Lowassa, Chenge warudi majeruhi 2015

Kati ya kazi kubwa ambayo imefanywa ni kurudishwa kwa majina ya Lowassa na Chenge bila nguvu zao walizoziandaa ili kutwaa usukani wa uongozi wa chama hicho kikongwe nchini na hatimaye 2015 iwe rahisi kwa mgombea wanayemuunga mkono kupita katika urais. Mikakati yao ni kama vile imekwama, na hasa baada ya kikosi maalumu kufanya kazi kubwa ya upelelezi, kujua mienendo ya wagombea kadhaa waliojitokeza kutaka kuteuliwa katika nyadhifa mbalimbali za uongozi wa ndani wa CCM ambao utadumu hadi baada ya Uchaguzi Mkuu wa kitaifa wa 2015.

"Wao wamerudishwa majina yao kwa ajili ya kushiriki kinyang'anyiro cha kupigiwa kura na wajumbe wa CCM ngazi ya wilaya walikoomba kuchaguliwa, lakini bahati mbaya kwao ni kwamba wanaweza kuchaguliwa na kurudi katika vikao vya uamuzi lakini tofauti na awali, safari hii wakiwa hawama mitandao ya kuwatetea na hata kuwaandalia mapito yao ya kisiasa," kinaeleza chanzo chetu cha habari.


CCM kushindwa kujisimamia

Pamoja na hayo yote, kwa namna fulani, CCM licha ya mbwembwe za Mwenyekiti wake, Kikwete kudai wanaokitabiria kifo chama hicho watakufa wao na kukiacha, hali ya chama hicho kikongwe nchini inaashiria kwamba kwa mara ya pili, kimeshindwa kusimamia uamuzi wake.

Kwa mara ya kwanza, CCM kupitia Sekretariati yake chini ya Katibu Mkuu, Wilson Mukama, kilishindwa kusimamia kile kilichoamuliwa na vikao vyake, hususana suala la kujivua gamba.


Katika kujivua gamba, CCM ilitaka viongozi wake wanaotuhumiwa kuhusika katika rushwa na ubadhirifu wajiengue, ikinadiwa kwa kuzingatia msemo wa Mwalimu Julius Nyerere kwamba; "Mke wa Kaisari hapaswi kutuhumiwa."


CCM, licha ya kupitia kwa viongozi wake, Nape Nnauye ambaye ni Katibu wa Itikadi na Uenezi na John Chiligati ambaye ni Naibu Katibu Mkuu-Tanzania Bara, kunadi uamuzi wa kujivua gamba, uamuzi huo ulishindwa kutekelezwa kama ilivyo hivi sasa, uamuzi wa kutoruhusu mrundikano wa madaraka.


Katika kudhibiti mrundikano wa madaraka, CCM ilielekeza kuwapo kwa kanuni inayotaka nafasi ya ujumbe wa Halmashauri Kuu iwe ngazi ya wilaya badala ya ngazi ya mkoa kama ilivyokuwa awali.


Lakini, pamoja na kuwa ngazi hiyo ianzie wilayani, ilielekezwa kwamba kazi hiyo iwe ya kila siku (full time job) na kwamba mwenye majukumu mengine kama ubunge na uwaziri asigombee.


Hata hivyo, uamuzi huo licha ya kuwa na nia nzuri ya kujenga uwajibikaji na utumishi makini kwa chama hicho, usimamizi imekuwa jambo adimu kwa chama hicho, wabunge na mawaziri wameruhusiwa kugombea na hata kuingia katika Kamati Kuu na Halmashauri Kuu.


Hata hivyo, wachambuzi wa masuala ya kisasa wanaeleza kuwa kama CCM itakuwa na kamati kuu au halmashauri kuu yenye mawaziri na wabunge, vikao hivyo vya Kamati Kuu na NEC vitakuwa na viraka vya mawaziri na wabunge na hivyo mwendelezo wa mgongano wa kimaslahi utadumu.


"Mwingiliano wa vikao vya chama na viongozi wa kiserikali, zamani wajumbe wengi wa kamati kuu na halmashauri kuu tulikuwa tukitokea mitaani na kuingia kwenye chama na kufanya ukosoaji wa kujenga, bila hofu.


"Kuna dalili za Kamati Kuu kugeuka kuwa Baraza la Mawaziri, kipande cha Baraza la Mawaziri au kipande cha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Yaani tutakuwa na CC au NEC yenye viraka vya wabunge na mawaziri, badala ya kuwa Kamati Kuu yenye mikakati na mbinu za kisiasa kwa kuzingatia mazingira halisi ya mitaani, imekuwa ikizingatia mazingira halisi ya ama ndani ya serikali au bungeni," kilieleza chanzo chetu cha habari.


Kinana kujiondoa

Wakati hayo yakiendelea, uamuzi wa aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi kung'atuka katika nafasi za uongozi wa chama hicho umepokewa kwa hisia tofauti, baadhi ya wanaCCM wakiamini anaweza kurudi kwenye uongozi wa chama kwa mlango wa nyuma, yaani kwa kuteuliwa na Mwenyekiti katika wadhifa unaoruhusiwa kiuteuzi kwa mujibu wa katiba ya chama hicho.










 

Interesting inside scoop news... So the incoming President is going to be Prof. Mwandosya ?

LOWASSA ni kafara la KIKWETE kwenye URAIS wa 2005...
 
Back
Top Bottom