CCM inazifuata RTC, Gapex, Hizbu na Imekosa watu kugombea ujumbe wa nyumba kumi na ubalozi

nngu007

JF-Expert Member
Aug 2, 2010
15,862
5,797
[h=1][/h]

picture-73.jpg

Na Nyaronyo Kicheere - Imechapwa 23 May 2012

Waraka wa Wiki


HIVI ni mimi peke yangu ninayesikia na kusoma au nanyi wenzangu mnasikia na kusoma habari hizi? Eti kwamba sasa Chama cha Mapinduzi (CCM) kimekosa watu wa kugombea ujumbe wa nyumba kumi au ubalozi!


Eti chama tawala kinagomewa na mabalozi wake wa zamani ambao sasa hawataki kugombea kwa tiketi ya chama hicho! Na kwamba mashabiki na wanachama wengine wa CCM nao eti hawataki kugombea chini ya CCM! Ama kweli kupanda mchongoma kushuka ndiyo ngoma!

Pia nimesikia na kusoma magazetini eti Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM iliyokutana wiki iliyopita mjini Dodoma imeridhia chama hicho kujadili madaraka ya rais, kuhoji mahakamani matokeo ya uchaguzi wa rais, na mgombea binafsi.


Hayo yote niliyoyasoma na kuyasikia ni dalili za chama kilichochoka, kilichokata tamaa na kinachojiandaa kushindwa na kupokwa madaraka na chama au vyama vingine vya siasa vinavyopanda chati siku hizi.


Nadikiriki kutabiri kwa Kikurya kwamba “umuhiko gohikile”, ninamaanisha mwisho wa CCM umefika na kwamba mwezi Januari 2016 CCM haitakuwapo madarakani na hapo ndipo zitakapotolewa simulizi kwa watoto na wajukuu zetu juu ya CCM na watangulizi wake kama ifuatavyo:


Hapo zamani za kale katika miaka ya sitini hadi sabini palikuwapo na shirika kubwa la umma likiitwa Saidia Tujenge Chetu au kwa Kiingereza State Trading Corporation (STC) na ilienea nchi nzima.


Miaka si mingi STC ilishindwa kutekeleza majumu yake ndipo serikali ya TANU enzi hizo chini ya rais wa kwanza Julius Kambarage Nyerere ilipoivunja na kuunda RTC yaani Regional Trading Corporation au kampuni ya Biashara ya Mkoa kwa kila mkoa wa Tanganyika.


Enzi zake miaka ya sabini na themanini RTC ilitamba sana na ilikuwa na ukiritimba wa karibu kila kitu. Mtu alikuwa hapati kitu katika Tanganyika bila kupitia RTC, si sabuni, si sukari, hata kanga na vitenge vilipatikana kwenye maduka ya RTC pekee.


Yaliundwa maduka ya ushirika na yale ya kaya ambayo ndiyo pekee yaliyopewa bidhaa muhimu kutoka maduka ya RTC. Lakini yote hayo yako wapi siku hizi? Tambo zote za RTC, maduka ya ushirika na yale ya kaya ziliishia kwenye biashara huria au liberalization.


Katika enzi hizo hizo za STC na RTC lilikuwapo shirika moja la umma lililohusika na ununuzi wa mazao mchanganyiko kwa kimombo GAPEX au General Agricultural Export lililonunua kutoka kwa wakulima ufuta, dengu, mbaazi, alizeti na mazao mengine ya aina hiyo na kuyauza nje.


Awali Gapex ilitamba sana; ilivuma sana na ilipata biashara na faida kubwa. Baadaye kukaanza mtindo wa mazao ya Gapex kuharibika mara kwa mara katika mabohari na kila mara yalipoharibika yalinunuliwa na kampuni moja ya kizalendo iitwayo Mohamed Enterprises.


Sababu zilizotolewa wakati ule ni kwamba Mohamed Enterprises ilinunua mazao yale yaliyoharibika kwa nia ya kuyauza kwa wafugaji walishie mifugo yao. Wakati huohuo kukazuka urafiki wa ghafla kati ya Mkurugenzi wa Gapex na Mkurugenzi wa Mohamed Enterprises.


Huku urafiki wa wakurugenzi wa makampuni hayo ukiendelea na Gapex ikipoteza biashara na Mohamed Enterprises ikiendelea kupata biashara Gapex ilikufa na Mohamed Enterprises ikaendelea hadi leo. Wasichokifahamu watanganyika ni kama urafiki wa wakurugenzi wa Mohamed Enterprises na Gapex unaendelea hadi leo. Ipo wpi Gapex jamani?


Kwa waliokuwa wakiishi Morogoro watakumbuka kampuni nyingine mbili mashuhuri sana. Kampuni hizo zilizotamba sana miaka ya themanini ni ya mafuta (Moproco) na ya viatu (Moro Shoe).


Katika miaka hiyo ya themanini nyakati za bei za kuruka na ukosefu wa bidhaa mtu hakupata mafuta ya kula kama hakuwa na cheo fulani katika CCM au serikalini. Pia mtu hakupata kiatu safi enzi hizo kikiitwa “raba mtoni” bila kufika kwenye duka la Moro Shoe.


Watanganyika makumi kwa mamia walijipatia mafanikio na umaarufu wa mapesa kwa kununua viatu vya Moro Shoe na kuviuza Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Dodoma, Mbeya na kwingineko. Lakini baadaye umaarufu wa Moro Shoe na Moproco uliporomoka na leo havisikiki tena.


Kwa maana nyingine STC, RTC, Gapex, Moro Shoe na Moproco vilipoteza umaarufu na kufa kutokana na kupatikana mbadala wao. Maduka ya RTC, maduka ya ushirika na yale ya kaya yalipoteza umaarufu na kufa kutokana na kushamiri biashara huria.


Nayo CCM leo hii imepoteza umaarufu hadi kufikia kukosa watu wa kugombea ubalozi au ujumbe wa nyumba kumi kutokana na sifa zake mbaya kama vile wizi wa kura, wizi na ubadhirifu wa mali ya umma ili kuzitumia katika kununua kura na kuhonga wapiga kura.


Imefikia hatua CCM imeishiwa mbinu za kupata pesa halali za kuhonga na kuwanunua mawakala, wasimamizi wa uchaguzi na wajumbe wa Tume ya Uchaguzi kwa sababu mchezo mchafu kama EPA sasa unafahamika kwa wote, uanzishaji kampuni za kitapeli kama Deep Green nao unajulikana kwa wote.


Sasa wakuu wa CCM hawana hoja, hawana mbinu za kupatia pesa na hawana uongo mwingine wa kujipatia pesa za kutolea takrima, kupikia pilau, kununua kanga, kofia, fulana na skafu za kugawa bure kama hongo kwa wapiga kura ndiyo maana sasa wanaonekana hawafai.


Baada ya kujikuta wapo njiani wakielekea waliko STC, Gapex, RTC, Moproco, Moro Shoe, Mtwara Retco, Moretco na wengineo ndipo sasa wanajikakamua kuanzisha mjadala wa kuweka mazingira mazuri watakapokuwa wapinzani 2015. Kwa ufupi wanajiandaa kuwa wapinzani 2015 period.


Sasa tunasikia eti CCM wanajadili mgombea binafsi, serikali tatu, madaraka ya rais, kuhoji matokeo ya uchaguzi na kadhalika. CCM wanataka sasa waweze kuhoji matokeo ya rais asiyekuwa wa CCM atakayechaguliwa 2015! Ha ha ha ha ha. Sijui kama watalaam wa habari za kiintelejensia akina IGP Said Mwema wanakubaliana nao au la.


Itabaki kuwa simulizi kuwa hapo zamani za kale ilikuwapo CCM, Hizbu, ANC ya Mtemvu, Gapex, na Moro Shoe lakini leo wote hao kwishnei.



 
Back
Top Bottom