CCM bado hakukaliki

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,268
33,040
Vita ya maneno na kejeli miongoni mwa viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na waliopo serikalini, inaashiria ukosefu wa dira ya pamoja katika kuiongoza nchi na watu wake.

Hali hiyo inatajwa pia kuwa kielelezo cha jinsi watawala wanavyokosa stadi za umoja katika mwelekeo, fikra na malengo ya kufikia utekelezaji wa ahadi walizozitoa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2010.
Wachunguzi wa mambo ya kisiasa, (wengine kwa kutotaka majina yao kutajwa gazetini) wamezungumza na NIPASHE Jumapili kwa

nyakati tofauti, wakikosoa mwelekeo wa CCM na serikali katika kulitumikia taifa.
Hatua hiyo imekuja baada ya wabunge wa mkoa wa Dar es Salaam, hususan waliotokana na CCM, kumshambulia Waziri wa Ujenzi, John Magufuli kwa hatua ya kupandisha nauli kwenye kivuko cha Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Magufuli alitangaza ongezeko hilo wiki iliyopita, hali iliyosababisha hasira za watumiaji wa kivuko cha Kigamboni, kufikia hatua ya kumzomea.

Hata hivyo, Magufuli alisema ongezeko hilo la kutoka Sh. 100 hadi 200 halipo Kigamboni pekee, bali kwa vivuko tofauti nchini.
Alitoa mfano wa vivuko hivyo na nauli zinazotozwa kwenye mabano kuwa ni Chato (Sh. 300), Pangani (Sh. 200), Kisorya (Sh. 300), Lugolora (Sh. 500), Nyakarilo (Sh. 3000), Chato-Bukombo (Sh. 2,000), Kirambo (Sh. 500) na Utete (Sh. 300) na kwamba wanafunzi wanasafiri bure.

Magufuli alisema watumiaji wa kivuko cha Kigamboni watakaoshindwa kulipa Sh. 200, wapige mbizi baharini ili wavuke, kuzunguka kupitia Kongowe mkoani Pwani ama warejee vijijini kulima.
Kauli za Magufuli ziliwaibua wabunge wa mkoa wa Dar es Salaam wakiwemo wa CCM waliosimama kidete kumshambulia Waziri huyo

anayehudumu kwenye serikali ya chama wanachotoka.
Miongoni mwa wabunge hao wa CCM ni Abbas Mtemvu (Temeke) na Dk. Faustine Ndugulile (Kigamboni).
Hata baada ya kuitisha mkutano wa pamoja, wabunge hao wamekaririwa na vyombo vya habari wakiendelea kulumbana na Magufuli kwa utaratibu unaoonyesha tofauti za kimitazamo, msimamo wa kichama na kiitikadi kati yao.

Wakati hali ikiwa hivyo kati ya Magufuli na wabunge hao, Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, alikaririwa akijibu hoja za Waziri Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye, alipozungumzia mambo mbalimbali katika kipindi cha Dakika 45 kinachorushwa na runinga ya ITV.
Moja ya mambo ambayo Sumaye aliyajadili na kutoa changamoto ni ongezeko la posho kwa wabunge, hoja iliyojibiwa na Ndugai, akimtaja (Sumaye) kuhusika na uasisi wake (posho).

Hata hivyo, Ndugai alienda mbali zaidi na ‘kumsuta’ Sumaye kwa changamoto alizotoa, kisha akasema kauli zake (Sumaye) zina mwelekeo wa mbio za urais wa 2015.
Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa na Uongozi wa Umma wa UDSM, Dk.

Benson Bana, anasema mazingira ya malumbano hayo ni kielelezo cha jinsi CCM na serikali yake wanavyokosa fikra na malengo ya pamoja katika kutawala.

Dk. Bana alisema tukio la kati ya wabunge na uongozi wa CCM mkoa wa Dar es Salaam kwa upande mmoja na Magufuli upande mwingine, ama Ndugai na Sumaye, linaonyesha kile alichokiita mparaganyiko na ukubwa wa tofauti ndani ya watawala.
Alisema kauli ya Magufuli akiwa katika wadhifa wa uwaziri, ni kauli ya serikali ya CCM, hivyo inapotokea kukosoana kati yao, linakuwa tatizo linalohitaji kushughulikiwa.

“Hapa inavyoonekana kinachotafutwa si suluhu ya tofauti za fikra, msimamo na malengo kuhusu ongezeko la nauli za vivuko ikiwemo Kigamboni, bali ni kama anayetafutwa hapa ni Magufuli,” alisema.
Kuhusu hoja ya Ndugai kwa Sumaye, Dk. Bana alisema kitendo cha (Sumaye) kupinga ongezeko la posho kwa wabunge kilikuwa

sahihi kwa vile suala hilo (ongezeko la posho) limepata upinzani kutoka kwa umma mpana.
“Hata kama mtu aliasisi posho akiwa madarakani, halafu akaona kasoro yake na kushauri kuwa jambo hilo si jema na halipaswi kuendelea, ni hoja nzuri yenye tija,” alisema.

Hata hivyo, Dk. Bana alisema ingefaa sana kwa Sumaye ambaye alimsifia kwa majibu yake wakati wa kipindi cha Dakika 45, kutumia njia nyingine katika uwasilishaji wa baadhi ya hoja ikiwemo kuonana moja kwa moja na Rais Jakaya Kikwete.
“Unajua huyu bwana (Sumaye) anaheshimika na kwa vile aligombea kupata tiketi ya CCM kuwania urais mwaka 2005 akashindwa na Kikwete, watu wanaweza kufikiri kuwa bado ana usongo wa mbio zile,” alisema.

Dk. Bana alisema Sekretarieti ya CCM inayoongozwa na Katibu Mkuu, Wilson Mukama, inaonekana kushindwa kuyaunganisha makundi hayo yaliyoibua malumbano hadharani.

Alisema kuyakutanisha makundi hayo kutasaidia kurejesha uhusiano mzuri kati ya Ndugai na Sumaye kwa upande mmoja na wabunge wa CCM, watendaji na wanachama wa chama hicho mkoani Dar es Salaam na serikali kupitia kwa Magufuli.
Lakini Waziri Mkuu mstaafu, Joseph Sinde Warioba, anapuuzia malumbalo kati ya Magufuli na wabunge wa CCM wanaoungwa mkono na uongozi wa CCM mkoa wa Dar es Salaam.

Warioba alisema malumbano hayo ni sehemu ya ‘matukio’ ambayo kwa hadhi yake hapaswi kutoa maoni ya kina.
Baada ya kutambua umuhimu alionao kutoa maoni yake kwa umma, Warioba alisema, “hayo ni mambo ya matukio tu, mtutafute kwa issue (masuala) ya kitaifa,” alisema Warioba, mmoja wa viongozi wastaafu wanaoheshima ndani na nje ya nchi.

Naye Dk. Salim Ahmed Salim ambaye pia ni Waziri Mkuu mstaafu, alipopigiwa simu ya mkononi alisema hawezi kutoa maoni yake kwa sasa kwa vile hadi kufikia jana, alikuwa anahudhuria mkutano unaofanyika jijini London, Uingereza.

Mwenyekiti wa Chama cha Democratic (DP), Christopher Mtikila, ameipuuzia kauli ya Ndugai na kusema inaonyesha jinsi anavyoshiriki mkakati wa kuwafunga midomo watu wanaosema kweli.

Mtikila alienda mbele zaidi na kudai kuwa, Ndugai anastahili apime majibu yake kwa Sumaye na achukue uamuzi kwa maslahi ya umma.
Mbali na kumuita Sumaye kuwa muasisi wa posho kwa wabunge, Ndugai alikaririwa akisema Waziri Mkuu mstaafu huyo si muadilifu kwa vile alisaidia kupitisha kwa sheria ya malipo kwa viongozi wakuu wastaafu wakati akikaribia kustaafu.



CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom