BAK
JF-Expert Member
- Feb 11, 2007
- 124,790
- 288,007
Rushwa inalitafuna Bunge, Spika amebaki mtazamaji |
Thursday, 21 July 2011 21:12 |
Mwananchi JANA tulichapisha habari zilizoonyesha jinsi tuhuma za rushwa zinazowakabili baadhi ya wabunge zinavyoendelea kulitikisa Bunge. Tuhuma hizo siyo tu zinaonekana kulitia doa Bunge letu tukufu, bali pia zinatishia kuzisambaratisha baadhi ya kamati za kudumu za chombo hicho cha kutunga sheria. Wahanga wa tuhuma hizo katika siku za hivi karibuni ni Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) inayoongozwa na Mbunge wa Vunjo, Augustine Mrema na ya Nishati na Madini iliyo chini ya Mbunge wa Bumbuli, Januari Makamba. Mpaka sasa hakuna anayejua lini mzimu huo wa rushwa ulianza kuzitafuna baadhi ya kamati hizo za kudumu hadi kuzifikisha hapo zilipo. Itakumbukwa kuwa, kamati hizo zilipoundwa baada ya Bunge la Kumi kuanza kazi mwishoni mwa mwaka jana, kamati nyeti za Bunge zinazoshughulikia hesabu za Serikali Kuu, Serikali za Mitaa na Mashirika ya umma zilianza kazi kwa kishindo kiasi cha kuwakuna wananchi kwa jinsi zilivyokuwa zinafanya kazi kwa ufanisi. Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa, kwa mfano, ilijizolea sifa kemkemu kwa jinsi ilivyoanza kazi yake kwa mwendo wa kasi na kupambana na ufisadi katika halmashauri ilizokuwa imezikagua. Sote ni mashahidi wa jinsi kamati hiyo ilivyowashukia watendaji katika halmashauri mbalimbali nchini, kiasi cha baadhi yao kukatwa asilimia fulani ya mishahara yao baada ya kushindwa kutoa maelezo ya kuridhisha kuhusu matumizi ya fedha za halmashauri zao. Lakini kamati hiyo sasa inaelekea kusambaratika kutokana na tuhuma za rushwa zinazowakabili wajumbe wengi wa kamati hiyo, kiasi kwamba imeshindwa kukutana licha ya Mwenyekiti Mrema kuitisha vikao mara tatu kwa nyakati tofauti. Mrema mwenyewe amekiri kwamba kutokana na hali hiyo ya wajumbe wengi kutofika kwenye vikao, anakusudia kuwasilisha taarifa hiyo kwa Spika wa Bunge ili kupata mwongozo wa nini la kufanya. Gazeti hili limeona taarifa rasmi za Bunge (Hansard) zinazothibitisha kuwa, Mrema aliitisha vikao hivyo. Kitendawili ambacho sasa kimefumbuliwa ni kwamba, baada ya mjumbe wa kamati hiyo, David Kafulila kuwatuhumu bungeni wajumbe wawili wa kamati hiyo kwa kuomba rushwa kwa uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, mkoani Tanga wakati kamati hiyo ilipokuwa inakagua miradi mbalimbali, wajumbe wengi walipata mfadhaiko na kukacha vikao ambavyo ajenda yake kuu ilikuwa kujadili tuhuma hizo za rushwa ambazo tayari zilikuwa zimemfikia Mrema na Spika mwenyewe. Lakini kumbe mfadhaiko ndani ya kamati hiyo uliongezeka maradufu baada ya baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo waliokwenda mkoani Pwani kukagua miradi ya halmashauri za mkoa huo, pia kudaiwa kuomba rushwa kwa uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiserawe ili wasiuchukulie hatua baada ya kugundua madudu katika mahesabu ya baadhi ya miradi iliyokuwa imetengewa fedha. Hiyo ndiyo siri ya kuwapo mshikemshike na mfadhaiko katika kamati hiyo na hakika, hiyo ndiyo sababu kuu inayowatia hofu wajumbe wengi wa kamati hiyo kiasi cha kuogopa kuhudhuria vikao vya kamati hiyo. Kwa mwenendo huo wa wajumbe wengi wa kamati hiyo, hatuna sababu ya kutoamini kwamba halmashauri nyingine zilizokaguliwa na kamati hiyo ziliombwa rushwa lakini zilikosa ujasiri wa kutoa taarifa kwa mamlaka husika, tofauti na walivyofanya wakurugenzi wa halmashauri za wilaya za Kiserawe na Handeni. Tunapoangalia uozo uliomo ndani ya kamati hiyo na kutathmini kiwango cha uozo katika Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini na Bunge zima kwa jumla ambalo wiki iliyopita lilikumbwa na tuhuma za wabunge wake wengi kupokea rushwa ili lipitishe bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini, hakika tunafadhaika na kupata mashaka juu ya mustakabali wa nchi yetu. Kinachotufadhaisha zaidi ni pale Spika wa Bunge anapokaa kimya pasipo kuamuru kufanyika kwa uchunguzi huru wa Kibunge ili hatua zichukuliwe kwa wabunge waliodai au kupokea rushwa. |