Nani Chaplain wa Bunge Letu?
Je, watanzania tunaelekea wapi kama Taifa? Kinachonisukuma kwenye swali hilo ni mwenendo wetu wa kisiasa, kiuchumi na kijamii ambamo kila tukipiga hatua moja mbele, tunapiga hatua zingine kadhaa nyuma na kutereza. Hili limeendelea kutusumbua watanzania kwa zaidi ya miongo minne na nusu tangu tulipopewa uhuru wa kujitawala.
Leo nimetaka kujua jambo moja: Je, kwenye Bunge, Mahakama au Serikali yetu kuna kiongozi yeyote anayesimamia kutoa ushauri nasaha wa maadili mema na maswala ya kiroho? Kwa nini nauliza hili?
Kwa tafsiri ya afya ya Shirika la Afya Duniani (WHO), afya njema ni kuwa na siha nzuri kimwili, kiakili, na kiroho. Viongozi wetu wana afya nzuri sana kimwili kutokana na lishe na medical check-ups walizo nazo, hatuna shaka na hilo. Na hata kama kuna shida kidogo tumeshuhudia ndege zikipaa mara nyingi kwenda India, Ujerumani, Uingereza, Marekani na sehemu mbalimbali kuwaweka sawa kimwili. Wengi wao wanapata nafasi za mafunzo katika semina na short courses wanazozipata kila wakati, ingawa kwa kweli tuna wasi-wasi na muda wanaojitengea kwa kujisomea wao wenyewe. Haya yote ni katika kuweka sawa maeneo muhimu ya afya ya mwanadamu. Swali ni: je, viongozi hawa wana utaratibu uliowekwa na Bunge wa check-ups za afya zao kiroho ili wakamilike kwa tafsiri ya kuwa na afya njema na hatimaye utendaji bora? Kwa sababu kama mtu asipopata attention kwenye eneo moja kati ya hayo hataweza kudai kukamilika kiafya. Badala yake anaweza kuelemewa kwa namna moja au nyingine. Mtu anapoendelea kunawiri kimwili tu bila kuendelea kukumbushwa kwamba kuna nguvu kuu zaidi zinazompatia uwezo na hekima za mambo muhimu yanayohusiana na maadili na mwenendo mwema na kwamba anawajibika kwazo, kuna athari nyingi na zilizo dhahiri ni zile za kushuka uwezo wake kiutendaji, kushindwa kuutawala mwili na maamuzi yake na hivyo kuelemewa na ulafi, tamaa, uchu, kushindwa kuheshimu sheria na mambo mengi ambayo yanahitaji siha ya kiroho.
Lakini baya zaidi ni kujidanganya kwamba anaweza kutegemea uwezo wake binafsi. Na kama kiumbe huyu akibaki kutegemea uwezo wake binafsi, basi tarajia lolote, kwani ni kiumbe hatari kuliko wanyama wa mwituni.
Ninasema hivyo nikiwa na imani kubwa kwamba mwenendo na maadili aliyonayo mtu yana sehemu kubwa sana kwa utendaji wake kama kiongozi (bora).
Naamini kwamba maoni yangu hayatochukuliwa kama campaign ya kutaka kuwa na serikali ya wachungaji na mashehe. Hii sio hasa nia yangu kwani hata hao wanaweza kuwa na tatizo lile lile. Ninalopendekeza hapa ni kuwa na viongozi wenye msingi mzuri wa uadilifu, wenye elimu ya kutosha kujua tofauti ya baya na jema na kuwa na mfumo maalumu wa kuwawajibisha wale wanaopungukiwa na kiwango cha uadilifu tunachokihitaji.
Kama tukishindwa kulielewa hili na umuhimu wake, mambo kadhaa ni hakika kwetu watanzania:
1.Tutaunda kamati nyingi sana za uchunguzi na bado tusifike mbali.
2.Na tutaendelea kwa muda mrefu kushangaa matendo ya ajabu kabisa yafanywayo na wenzetu kila kukicha.
Kama elimu na uzoefu wa kisiasa vinatosha kumfanya mtu awe mwadilifu, basi tusingefikia hatua ya kuiona rushwa kama ni jambo la kawaida kiasi cha kulinganishwa rushwa ya mtu mmoja na mwingine ili tujue nani tumpigie kura, na tusingeifanya kigezo cha kupata huduma kwenye taasisi za serikali. Kama elimu na lishe tu vinatosha basi tusingesikia wale wenye shahada za udaktari wa falsafa za sheria wakighushi fedha nyingi za serikali ili waendelee kula. Hawa ndio ambao wangeweza kuwa wa kwanza kupinga jambo ambalo ni kinyume na sheria. Lakini si hivyo. Kama ni elimu na lishe tu tusingesikia wachumi wakilifirisi taifa lao wenyewe. Kama ni elimu na lishe tu basi tusingesikia viongozi wetu wakuu wa nchi wakiwa wao ndio nyota ya mchezo katika rushwa na ubadhirifu na kuwa na mabenki, mkampuni, nyumba za kifahari ndani na nje ya nchi, n.k na wala tusingesikia wake zao wakijihusisha na biashara haramu ili mradi tu wasipwaye kwenye tafsiri ya cheo chao cha First Lady. Kama elimu na lishe tu vinatosha tusingesikia viongozi wakiwafyatulia risasi wafuasi wao eti kwa sababu wameudhiwa. Lishe na elimu havitoshi. Tunahitaji viongozi waadilifu.
Nimeuliza swali hili hali nikijua fika kwamba Serikali yetu haina dini na yumkini vivyo hivyo kwa Bunge letu tukufu na Mahakama pia. Lakini ni imani yangu kwamba viongozi wengi na kiasi kikubwa cha wananchi wa Tanzania wana dini.
Kwa sababu kila kabla ya kuanza kwa vikao vya Bunge tukufu husomwa sala kwa dini kuu za Tanzania. Viongozi wa serikali yetu wanapoteuliwa kwa nyadhifa mbali-mbali za juu hulazimika kuapa wakiwa na vitabu vitakatifu kabla kuanza majukumu yao. Mashahidi wanapotaka kutoa ushahidi mahakamani hufanya vivyo hivyo pia. Na mara kadhaa tunapokumbwa na majanga tusiyoweza kuyatatua au kuyaelewa kwa busara zetu, viongozi wa serikali yetu isiyo na dini huwaomba wananchi kwa umoja wao na tofauti za dini zao kumwomba Mungu atusaidie. Mara zote tumelifanya hili kwa uaminifu mkubwa bila ushuru wala rushwa yoyote. Kwa mfano, mwezi wa Oktoba mwaka 1999 tuliombwa sana kumuombea Baba wa Taifa na tukaitikia kwa moyo mmoja.
Katika majanga makubwa kama ajali, ukame, mafuriko, njaa, magonjwa ya kutisha, n.k tumelazimika kutumia dini zetu kuisaidia serikali yetu isiyokuwa na dini yake.
Sasa kuna janga kubwa ambalo linahitaji maombezi ya wananchi wenye dini kuisaidia serikali ingawa viongozi wetu hawajaliona kabisa. Janga hili ni janga la ufisadi lililovikumba vyombo vya uongozi kama Serikali, Bunge, na Mahakama.
Tatizo hili ni kubwa kuliko tunavyodhani. Ni kubwa kwa sababu janga hili halikuanza jana na nasikitika kusema kwamba halitaisha kesho! Sisemi hivyo kwa sababu siipendi nchi yetu, la hasha! Ninaipenda sana Tanzania. Ninasema hivyo kwa sababu sioni nuru yoyote mwisho wa shimo hili tulilomo.
Sioni nuru kwa kuwa viongozi wetu ni wale wale jana, leo na hata kesho ambao waliotusababishia janga hili wanabadilishana na kupumzishana tu kama wachezaji wa timu ya mpira wa kikapu. Tangu miaka ya 1980 viongozi wa juu wamekuwa wakijigamba kuandaa mazingira mazuri ya kiuchumi lakini hili limebaki kama swala la kujitafutia kura na umaarufu wa kisiasa na kuwaacha wananchi wapiga kura hao wakitaabika na kunyanyasika kila siku hali wakishuhudia miondoko ya ajabu ya viongozi waliowachagua.
Kila mwanadamu ameumbwa na utashi wa asili wa kuabudu hata kama ni kwa mapungufu ya hapa na pale katika imani hiyo. Na ndio maana wale wasioamini Mungu hukidhi utashi huu kwa kuabudu viumbe wengine kama Ngombe, Mbuzi, Kondoo, Miamba, Jua, n.k. Hii ni kwa sababu mwanadamu ameumbwa kama kiumbe tegemezi anategemea uwezo wa asili mkubwa zaidi ya ule alionao na kapewa kiu ya asili ya kutaka kuwa na kiumbe wa kuabudu.
Swala hili la kuamini Mungu na viumbe wengine si swala la imani tupu. Ni swala linaoendana pia na mkusanyiko wa taratibu (maadili) mbali-mbali ambazo kwa kawaida huwa kanuni za maisha ya yule anayeamini. Kwa hivyo imani na maadili haya huwa msingi mkuu wa tabia na chaguzi za mtu na hatimaye mwenendo na matendo yake. Na kwa mantiki hii iliyo wazi kwa wengi ni dhahiri kwamba kuna uhusiano wa karibu sana kati ya imani ya mtu na mwenendo na utendaji wake. Kwa maana nyingine utu wa mtu unategemea sana kile anachokiamini na kukiabudu. Katika hali ya kawaida mtu asiyeamini Mungu utategema atende kama mtu asiyemuamini Mungu na vivyo hivyo kinyume chake.
Tusemapo kwamba serikali haina dini tulielewa hili vema katika mazingira ya kisiasa ambayo Baba wa Taifa alitaka kuyatumia katika kujenga msingi wa umoja usio na ubaguzi wa dini ambao kwake (na baadaye wengi wetu) ulikuwa muhimu sana. Wasi-wasi wangu leo ni pale falsafa hii inapowaingia baadhi yetu kinyume na maana tarajiwa na hivyo kuanza kujiona na kutenda kana kwamba na wao pia, kama watu binafsi, hawana dini.
Baba wa Taifa aliwahi kukemea swala la rushwa lililokithiri kwenye uongozi wa serikali wa awamu ya pili. Uongozi wa serikali ya awamu ya tatu ukaingia kwa staili ya kubweka bila kungata. Ikaendeleza rushwa zaidi kuliko awamu ya pili japo kwa staili tofauti. Uongozi wa awamu ya nne ukaamua kuendeleza yale ya awamu ya tatu. Watu wale wale. Leo hali ya rushwa ni mara dufu. Viongozi wa serikali hubadili tu staili ya ufisadi bila kupunguza makali.
Ninapoyatafakari haya yote ninajaribiwa kuamini kwamba matatizo yaliyopo katika taifa hili kamwe hayatatuliwa na serikali iliyopo madarakani. Ni kumtwisha mzigo asiouweza Rais wetu kama tutadhani kwamba umaarufu uliomuweka kwenye nafasi hiyo unaweza kututalia matatizo haya makubwa tuliyojiingiza kwa miaka yote huku tukichekeana na kupeana vizawadi vya uongo na kweli ili kuzibana midomo kwenye uhalifu wetu.
Taifa letu linahitaji wito kwa wale wenye dini za kweli kutuombea ili Mungu atupe viongozi wa kweli na wasio wafisadi.
Tunahitaji kukumbushana maadili mema na kuogopa ufisadi. Tunahitaji kuheshimiana .
Tunahitaji kuheshimu haki za kila mmoja wetu na sheria ya nchi.
Tunahitaji kutumia utawala wa sheria badala ya ushoga.
Tunahitaji kudumisha amani. Tunahitaji kuomba maadili yafufuke Tanzania.
Tunahitaji kuomba viongozi wapya Tanzania.
Ukweli ni kwamba akina Mkullo na akina Wassira hawana jipya la kutupatia watanzania, wangekuwa nalo Tanzania ingekuwa ni taifa bora zaidi. Akina Balali bado wapo wengi sana. Akina Mahalu tunazunguka nao humu-humu kila siku.
Akina Ditopile wamejaa kila mahala. Wameruhusiwa kununua silaha, na wanazo fedha za kuweka wanasheria. Na hawa watu tusiwakandamize sana kwani wamejikuta katika jamii iliyotoka kwenye msiba msiba wa maadili. Taifa ambalo limesahau tofauti ya mema na mabaya. Likitendwa baya tunacheka na magazeti yetu yananunuliwa zaidi. Likifanywa zuri tunashangaa! Hivyo walijioona kama wako sawa.
Tunachohitaji sasa ni kujenga Taifa jipya. Tunahitaji mabadiliko makubwa zaidi. Mpaka wakati huo utakapotimu watanzania tukae tayari kusikia vituko vingi zaidi.
Raia Mpenda Mema,