Barua ya Wazi kwa Gen. Mwamunyange: Mkikaa kisiasa, mtalaumiwa kama wanasiasa!

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Mar 10, 2006
33,475
39,991
BARUA YA WAZI KWA GEN. MWAMUNYANGE -
JESHI LINAPOKAA KISIASA ZAIDI LITALAUMIWA KISIASA ZAIDI
Na. M. M. Mwanakijiji


Gen. Mwamunyange, kwanza salaam!


Natanguliza pole zangu na sala zangu kwa wahanga wa mlipuko wa mabomu huko Gongo la Mboto na vile vile pole kwa jeshi letu la Wananchi kwa tukio jingine ambalo limetokea ndani ya miaka miwili tu toka tukio kama hilo limetokea huko Mbagala kilometa chache tu toka Gongo la Mboto. Lakini kinyume na tukio la Mbagala tukio hili limeendana na lawama za wazi juu ya jeshi na hususan hata kilio cha kutaka viongozi wa kijeshi ukiwemo wewe mwenyewe mjiuzulu.


Ninaelewa kabisa hisia za Watanzania wenzangu juu ya suala hili na kwanini wanahisia kuwa katika tukio hili la wiki iliyopita ipo haya ya viongozi wa jeshi kuwajibishwa. Imekuwaje hadi jeshi letu linafikia kulaumiwa na viongozi wake kutaka kuwajibishwa kwa mambo ambayo kisheria hamuwezi kuwajibishwa nayo? Ni kwanini tumefikia mahali ambapo chombo pekee kilichokuwa kimebakia kikibeba heshima ya wananchi kinapotajwa hadharani kuwa kimeonesha uzembe au kutokuwa waangalifu? Gen. Mwamunyange naomba nipendekeze jibu langu.


Jeshi limepoteza Utukufu wake (the military has lost its glory).
Mtu yeyote aliyekuwa anafuatilia matukio ya Misri katika mapinduzi baridi yaliyomuondoa Hosni Mubarak atakuwa amevutiwa na jinsi gani wanajeshi walivyopokelewa mitaani kwa makumbatio na mabusu kutoka kwa wananchi wao. Yaani, wakati wananchi wanapoteza imani na jeshi la polisi, wamepoteza imani na rais wao, wamepoteza imani na chama tawala walijikuta wamebakia na imani juu ya jeshi lao. Hii ni kutokana na rekodi na umahiri wa jeshi hilo kuanzia vita ya 1967 dhidi ya Israeli na jinsi gani limeweza kuonesha umahiri katika vita ya kumuondoa Sadam kule Kuwait. Jeshi la Misri lilikuwa na bado limebakia kuwa na utukufu wake - yaani utukufu wa mashujaa.


Wananchi wa Misri walijua na walitambua toka ndani ya mioyo yao kuwa tumaini la mwisho la ulinzi wa utu wao, huru wao, na haki yao kuwepo kama taifa imebakia mikononi mwa jeshi. Walionesha mapenzi na jeshi lilionesha kwanini linastahilil mapenzi hayo pale ambapo liliamua kukaa nje kabisa ya siasa za wakati huo na kutoa amri kwa wapiganaji wake wote kutokuinua silaha zao dhidi ya wananchi wao. Tukumbuke kuwa jeshi la Misri ndilo kubwa kuliko majeshi yote ya Afrika na majeshi yote ya nchi za Kiarabu na ni miongoni mwa majeshi 10 makubwa duniani. Ni jeshi ambalo limejipatia sifa duniani kwa vifaa vyake na hata uwezo wake - inadaiwa katika Mashariki ya kati linafuatia lile la Israeli tu kwa nguvu. Hivyo jeshi la Misri limejenga utukufu wake mbele ya wananchi wake na utufuku wake umeonekana uking'ara pale taifa hilo lilipopotia saa yake ya giza.


Hayo yote yanajulikana kwako Gen. Mwamunyange; lakini ninachojiuliza na ambalo linaelekea kujibu swali langu hapo juu unafikiri Watanzania wanaliangalia jeshi kwa mapenzi waliyokuwa nayo zamani? Ukiondoa kuliangalia kwa maana ya kuwa linatimiza wajibu - kama wakati wa majanga mbalimbali- unafikiri Watanzania wanamapenzi yale yale wanapowaona wanajeshi wao tena? Ninachouliza hasa ni kuwa unafikiri jeshi letu bado lina utufuku ule ule mbele ya wananchi?


Gen. Mwamunyange, jeshi letu baada ya vita ya kumng'oa nduli Idi Amin na katika majukwaa mbalimbali ya mapambano wakati wa harakati za Ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika jeshi letu lilijengea utukufu. Wengine tunakumbuka jinsi gani tuliwapokea mashujaa wetu walipotoka vitani; na jinsi gani tuliona fahari wakati wanapita mbele pale Uwanja wa Taifa wakihitimisha safari yao huku yale maneno ya fahari kuwa "kazi mliyotutuma tumeimaliza" yakiwa mbele yetu. Kwa wengine wetu hakuna wakati wowote ambapo Watanzania wamewahi kuona fahari ya jeshi lao kama wakati baada ya vita ya Uganda hadi hivi karibuni. Wakati wa aibu ilikuwa pale jeshi lilipoasi, lakini pale lilipoundwa upya na kujitofautisha kuwa ni jeshi "letu" hasa ndipo hapo tuliona utukufu wake.


Gen. Mwamunyange, utukufu huo ulianza kuondolewa miaka michache hii iliyopita na hasa pale ambapo jeshi lilipoanza kuonekana kuwa limekaa kisiasa zaidi. Na naomba nipendekeza kuwa hakuna wakati wowote ambao jeshi letu lilikaa kisiasa sana kama wakati wa Uchaguzi Mkuu mwaka jana. Kabla yake jeshi letu limehusishwa na vitendo vya ufisadi wa Meremeta, jeshi letu limetajwa katika kashfa hizo mbaya na pale ambapo ilionekana kuwa jeshi limeamua kujipanga na kula kiapo cha kuilinda CCM na kufanya lolote lile ili wananchi waichague CCM jeshi lilivunja ule mwiko mkubwa kabisa ambao jeshi la Misri halikuwa tayari kuuvunja - yaani kuweka utii wake kwa kikundi cha watu wachache badala ya utii wake kwa wananchi.


Nimewahi kuandika huko nyuma kuwa labda tuambiwe ni lini jeshi letu lilibadilishwa kutoka kuwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania na kuwa Jeshi la Chama cha Mapinduzi au ni lini liliacha kuwa Jeshi la Wananchi na kuwa Jeshi la Rais wa Jamhuri ya Muungano? Kama bado jeshi letu ni lile la wananchi basi ni wazi mambo kadhaa lazima tuyaweke wazi ili jeshi lirudishe utukufu wake.


Gongo la Mboto mwenye kutakiwa kuwajibika ni Waziri
Nimesema hapo juu nakubaliana na uongozi wa jeshi kuwa hakuna afisa wa jeshi anayepaswa kujiuzulu na Brig. Gen. Meela alisema kweli kabisa kuwa jeshi haliongozwi kisiasa na kuwa linaongozwa na sheria ya Ulinzi ya mwaka 1966 (na mabadiliko yake ya baadaye). Matukio yote mawili (lile la Mbagala na la Gongo la Mboto) yote yanatokana kwa kiasi kikubwa na kukosekana kwa uongozi wa kisiasa wa kuweza kuangalia mahitaji ya jeshi na kuyashughulikia mapema iwezekanavyo.




Kwa mujibu wa sheria hiyo hapo juu Waziri ndiye mwenyewe kuwajibika na na masuala yote ya udhibiti na utawala wa shughuli za jeshi ukiondoa mambo yale ambayo yameachwa mikononi mwa Rais kwa mujibu wa Katiba na sheria hiyo. Waziri tunaambiwa ndiye mwenye wajibu wa kusimamia ujenzi na ukarabati wa mambo yote yanahusiana na jeshi na ulinzi wa nchi (Ibara ya 5). Ni yeye pekee basi ndiye kutokana na sheria anatakiwa kuwajibika kwani baada ya tukio la Mbagala alitakiwa kuonesha uongozi kwa kusimamia lengo la kuhakikisha kuwa jeshi haliwezi kujikuta kwenye tukio kama hilo tena.


Ni kwa sababu hiyo Gen. Mwamunyange nashangazwa na ujasiri wa Dr. Hussein Mwinyi kuweza kutangaza kuwa ati yeye hawezi kuwajibika kwa yaliyotukia na ninashangazwa zaidi na uongozi wa juu yake kumuacha aendelee kuwa madarakani. Kama katika tukio hili la Gongo la Mboto Dr. Mwinyi amegoma kujiuzulu kwa sababu haamini kuwa yeye ndiye mwajibikaji mkuu basi kuanzia sasa katika Tanzania tupige marufuku watu kujiuzulu kutokana na matukio yanayotokea chini yao. Kama yeye hatojiuzulu nani ajiuzulu?


Wanajeshi hawawezi kujiuzulu kiholela. Wanajeshi wanatakiwa kujiuzulu pale wanapo "challenge" madaraka ya kiraia au kwa mujibu wa taratibu za kijeshi. Hili ndilo lililomsababisha Gen. McChrystal wa Marekani ambaye katika mahojiano na gazeti moja la nchi hiyo alionekana kuonesha dharau ya wazi dhidi ya Rais Obama na Waziri wa Ulinzi; kwa kufanya hivyo alivunja nidhamu ya kijeshi ambayo imeweka jeshi mikononi mwa raia. Mfumo huo upo hata kwetu. Kiongozi wa Jeshi hawezi kumdharau Rais au Waziri wetu na akabakia kwenye amri yake kwani atakuwa ameweka changamoto ya utawala wa kiraia.


Sasa kama hilo ni kweli, kwanini Dr. Mwinyi aendelee na uongozi wake? Kwanini Katibu Mkuu wa Wizara ambaye ni mtendaji wa mkuu wa wizara na yeye asiwajibike kwani wao pekee ndio ambao wanatakiwa kuleta mbele ya viongozi wa kisiasa mahitaji ya jeshi na kuhakikisha yanapangiwa bajeti na kusimamiwa. Ni wao ndio ambao wangeweza kuamua kwa kutekeleza sera ya chama kilichoko madarakani nini kifanyike kuhusu kambi za jeshi, ziwe wapi, n.k Ndio maana narudia wito ambao umeshasemwa na wengine kuwa viongozi hawa wajuu wa Wizara ya Ulinzi ni LAZIMA wawajibike kwani kisheria na kiutaratibu ni wao pekee ambao wanawapaswa kuwajibika na itakuwa kutamalaki kwa kuvumilia uzembe kama Rais Kikwete hawezi kuona haja ya kuwawajibisha.


Janga kuu zaidi naamini ni kwa viongozi hawa kuendelea kuwa madarakani; itabidi tujiulize hadi nani afe au nini kilipuke ndio tutawawajibisha watu?


Gen. Mwamunyange, pamoja na ukweli huo bado kuna jukumu ambalo liko mikononi mwao kama mkuu wa majeshi. Umeonesha kushindwa kujali hisia za Watanzania ambao wameumizwa na tukio hili na tulitarajia kuwa ungekuwa mstari wa mbele wewe mwenyewe kuzungumza na Watanzania badala ya kupiga picha na wanasiasa. Baada ya tukio la Mbagala na sasa tukio la Gongo la Mboto tulitarajia ungekaa na waandishi wa habari na kutoa maelezo na kujibu maswali yao mbalimbali; tulitarajia kuona uongozi wetu wa kijeshi ukijenga utukufu.


Ipo haja ya haraka na ya lazima ya jeshi kuanza kujenga taswira yake upya mbele ya wananchi hasa baada ya kuiboronga kwenye siasa za uchaguzi. Ni lazima jeshi lirudishe utukufu wake kwani wananchi wasijikute wanapoteza imani na vyombo vyote vya serikali. Katika upande huu jukumu hilo linakuangukia na wewe na uongozi wa juu wa jeshi letu. Hili hata hivyo ni gumu kwa sababu kabla hamjaweza kurudi na kukaa kijeshi zaidi itabidi muachane na kukaa kisiasa. Ipo haja ya jeshi kuandaa mwongozo wa mahusiano kati ya wanajeshi na wanasiasa bila ya kuathiri sheria ya ulinzi. Yaani, uhusiano wa jeshi na viongozi raia uwe ni wa kikazi na si wa kiurafiki wa kisiasa. Jeshi ni lazima lirudishe utukufu wake kwani ukaribu uliopo sasa hivi unalifanya jeshi lishindwe kukaa pembeni pale "wanasiasa rafiki" wanapokuwa kwenye matatizo ya kisiasa.


Gen. Mwamunyange, changamoto hii ya kulirudisha jeshi kuwa ni jeshi la wananchi inahitaji maono mapya, fikra mpya na uwezo mpya wa kuthubutu. Unahitaji kulifanya jeshi letu liweze kuaminiwa na wananchi wa vyama vyote na siyo wale wa chama tawala tu. Kwa mfano, hadi hivi sasa jeshi linaonekana halina mahusiano yoyote na uongozi wa vyama vya upinzani. Kwa mfano, kutakuwa na ubaya gani kwa kualika kambi ya upinzani kukutana nao na kufungua mahusiano mapya ya kisiasa? Au mtajiona kana kwamba mnawasaliti CCM? Hili ni muhimu sana kwa sababu jeshi limekuwa lilikutana mara nyingi na viongozi wa CCM ambao pia wana nafasi za uongozi serikalini na halioni shida kufanya hivyo.


Gen. Mwamunyange, ni katika kufanya hivyo na ni katika kuanza mwelekeo mpya wa kulijenga jeshi la kisasa ndivyo hivyo hivyo wananchi wataacha kulilaumu jeshi kwa mambo ya kisiasa na watakuwa tayari kuelewa pale ambapo matukio yaliyo nje ya uwezo wa jeshi kuyazuia yanapotokea. Lakini jeshi likiendelea na mtindo wake wa sasa wa kukumbatiana na wanasiasa wa chama tawala katika misingi ya kuwalinda kisiasa basi linasababisha chuki, na hasira kwa wananchi. Jeshi letu halistahili kuchukiwa kabisa na wananchi wake.


Swali kubwa ambalo liko mikononi mwako na kwa uongozi wa jeshi ni je, jeshi linaweza kuwa jeshi tu na kukaa kijeshi zaidi pasipo kuvurugana na wanasiasa? Je, ipo haja ya kuangalia jinsi gani waliowahi kuwa wanajeshi hasa maafisa wa ngazi fulani kusubiri muda fulani kabla hawajajiingiza kwenye siasa baada ya kutoka jeshini? Maana tumewaona waliokuwa wakuu wa Polisi na wakuu wa Jeshi wakikimbilia CCM mara tu wanapotoka Jeshini na ndipo tunajua kumbe wenzetu walikuwa ni wanachama wa imani wa chama hicho!


Isije kuwa haya yote niliyokuandikia hayana maana kwani tayari umeshaamua kufa na CCM na kuwa una nafasi inakusubiria huko mbele ya safari na hivyo huwezi kuwa mkali sana kwani unaweza ukakosa nafasi huko mbeleni. Wazo hili linatisha. Hata hivyo, ninaamini nyote mnaolitumikia jeshi sasa mnajua wajibu kwa nchi yetu na watu wake na siasa hazitakuwa na nafasi. Vinginevyo, baada ya pigo la uongozi wa CCM ulioshindwa kuliinua taifa, Watanzania watakuwa wamepata pigo jingine -jeshi lililokaa kisiasa.


Ni matumaini yangu, Gen. Mwamunyange, tukio la Gongo la Mboto linatoa nafasi mpya kwa jeshi kujenga taswira yake kwa wananchi. Lakini hilo halitawezekana isipokuwa kama uongozi wa sasa wa kisiasa katika Wizara ya Ulinzi na JKT ukiongozwa na Dr. Mwinyi na Katibu Mkuu Andrew utajiuzulu mara moja na kuwajibika kwa tukio hilo la uchungu. Nje ya hapo, utukufu wa jeshi letu utapotea daima.


Wasalaam!
 
Nakupongeza sana MKJJ kuwakumbusha wajibu wao na nafasi ya jeshi kwa jamii na raia wote...wamejawa na woga wa kutolewa kwenye ulaji kuogopa kufuata viapo vyao vya jeshi na wajibu wa jeshi kwa wananchi na nchi kwa ujumla....wanafanya mazoea badala kufuata kanuni na sheria pamoja nidhamu ya jeshi....

Aibu sana sana siasa zilitolewa jeshini muda mrefu sasa acheni siasa wajibikeni kwa wananchi.....sio kwa mafisadi wachache
 
Hapo Umenena mkuu, Tunahitaji Jeshi la Wananchi wa Tanzania kwa Watanzania!! Naamini Mwamunyange ataisoma hii!
 
Safi sana Mwanakijiji...nadhani Jeshi letu linaanza kusahau majukumu yake ya msingi. Endelea kuwakumbusha
 
Kila taaisisi tanzania zinataka utukufu utuka, kuthaminiwa kuheshimika wakati zinasahu kuwa ziko kwa ajili ya wanachi


  • Jeshi
  • Polisi
  • Serikali
  • Bunge.
 
Hakuna paragraph wala topic sentence, kitu kilichoandikwa na mtu kakaa kama hakwenda shule huwa siwezi kukisoma.
 
Ujumbe mzuri sana huu Mzee. unakila sababu ya kufikiriwa mara mbili mbili na jeshi letu maana ni kweli kabisa mambo hayako kama vile yalivyokuwa zamani. Ni aibu kubwa sana kama itatokea jeshi linakuwa sehemu ya matatizo ya rushwa na uadilifu tuliyonayo. Wananchi wataliheshimu jeshi na kuwapenda wanajeshi kama wataona wao sio sehemu ya matatizo tuliyonayo.
 
Ndaga fijo Mwanakijiji hapo umenena!!

Bahati mbaya jeshi letu loyalty yake ni kwa Rais na Sirikali yake ya CCM basi!!!!
 
Hakuna paragraph wala topic sentence, kitu kilichoandikwa na mtu kakaa kama hakwenda shule huwa siwezi kukisoma.
na kabla hujashutuka unakuwa umeshakisoma tayari labda useme huwezi kirudia kukisoma

teh teh teh teh teh
 
Many thanks for your continued support and co-operation. With joined hands we shall win the mêlée.
 
Nimeikubali Barua hii Mwanakijiji, naamini kuwa Watanzania wengi wataisoma na kuuelewa hii Barua ya wazi ya Mkuu wa JWTZ, Ni binafsi nimeukubali na umetulia. Kama kuna watu hapa wapo karibu na mkubwa huyo basi naomba afikishiwe ili ajue nini maana ya jeshi sio kukimbilia siasa au tumeshazoea kuona wakuu wa mikoa na wilaya kutoka jeshini
 
Naona MwanaKJJ tatizo bado ni kubwa sana ktk watendaji wetu ambalo ni upuuzaji wa kila kitu, na nakomea hapo maana yapo Mengi sana ila hili ni Tatizo kubwa sana likipambwa sana na kujawa na uchu na kujikuta wanasahau their responsibilities! Masikio yao kutwa yanawaza rushwa na dodgy deals! we can not go anywhere!
 
Kama Mwinyi na Mwamunyange wataisoma kwa kutulia hii dossier naamini wata'reconsider legitimacy yao kuendelea kuwepo kwenye nafasi wanazong'ang'ania!
Kikawaida Jeshi letu limekuwa ni la msaada sana kwa wananchi, lakini kwa kulitazama kwasasa linaanza kumezwa taratibu na Wanasiasa wenye uchu...na hatimaye raia kuanza kulirushia maswali mazito jeshi hili, kinyume na miaka michache iliyopita!
 
Inabidi tuangalie upya hili jina JWTZ (linalotambulika sasa kama jeshi la wananchi) kama kweli linakidhi mahitaji ya wananchi wazalendo wa Tanzania. Kwa sasa Tz imejaa mafisadi.
Kuna kila dalili tukawa na watu wasiokuwa waadilifu wanaojificha nyuma ya pazia la JWTZ ili kufanikisha maovu yao.
Tumeumwa na nyoka jamani, tukiona ujani tu inabidi tushtuke..
 
Asnte sana mzee mwanakijiji, taifa linakuhitaji sana na pia endelea kua na moyo huo huo wa kizalendo naamini muda si mrefu tutaijenga nchi yetu.

Hasta la victoria siempre
 
[I said:
Mzee Mwanakijiji;1659025]Jen. Mwamunyange, kwanza salamu![/I]
................

Gongo la Mboto mwenye kutakiwa kuwajibika ni waziri.

Nimesema hapo juu nakubaliana na uongozi wa jeshi kuwa hakuna ofisa wa jeshi anayepaswa kujiuzulu na Brig. Jen. Meela alisema kweli kabisa kuwa jeshi haliongozwi kisiasa na kuwa linaongozwa na sheria ya Ulinzi ya mwaka 1966 (na mabadiliko yake ya baadaye).

Matukio yote mawili (lile la Mbagala na la Gongo la Mboto) yote yanatokana kwa kiasi kikubwa na kukosekana kwa uongozi wa kisiasa wa kuweza kuangalia mahitaji ya jeshi na kuyashughulikia mapema iwezekanavyo.

Kwa mujibu wa sheria hiyo hapo juu, waziri ndiye mwenyewe kuwajibika na masuala yote ya udhibiti na utawala wa shughuli za jeshi ukiondoa mambo yale ambayo yameachwa mikononi mwa rais kwa mujibu wa Katiba na sheria hiyo.

Waziri tunaambiwa ndiye mwenye wajibu wa kusimamia ujenzi na ukarabati wa mambo yote yanayohusiana na jeshi na ulinzi wa nchi (Ibara ya 5). Ni yeye pekee basi ndiye kutokana na sheria anatakiwa kuwajibika kwani baada ya tukio la Mbagala alitakiwa kuonyesha uongozi kwa kusimamia lengo la kuhakikisha kuwa jeshi haliwezi kujikuta kwenye tukio kama hilo tena.

Ni kwa sababu hiyo Jen. Mwamunyange nashangazwa na ujasiri wa Dk. Hussein Mwinyi kuweza kutangaza kuwa ati yeye hawezi kuwajibika kwa yaliyotukia na ninashangazwa zaidi na uongozi wa juu yake kumuacha aendelee kuwa madarakani.

Wasalaam!

Mkuu MMKJJ pamoja na analysis yako na comparison na majeshi mengine yenye ufadhili wa serikali ya Marekani, I beg to differ with you as a matter of principle.
Jeshi letu linaongozwa na serikali ya kiraia na siyo kama ilivyo majeshi kama ya Misri na kwingineko.Si jambo la kusha ngaza kuwa hata Mubarak hakuwa na ubavu kkuliagiza jeshi kuzima maandamanano ya ya wa misri.Hii ni pamoja na jeshi letu kutawaliwa na sheria tofauti za utumishi wa umma kijeshi.
Nashangazwa vilevile kumuaddress Gen Mwamunyange kwa suala la Dr Mwinyi!
Muwajibishaji wa Dr Mwinyi ni Rais wa Jamhuri ambaye ndiye Amiri Jeshi Mkuu,barua yako MMKJJ ingeelekezwa huko ungeeleweka.
Nawapongeza sana Jeshi kwa kutoingia katika malumbano kwa yaliyotokea ili hatimaye mchele na mpunga vijitenganishe na wananchi wajue ukweli wa mambo yaliyojiri.
Pamoja na yote kwa tatizo liliotokea kwa nini tusisubiri huo uchunguzi ili hatimaye mambo yote yajulikane.
Sifa ya Jeshi letu bado ni imara pamoja na haya yaliyotokea, you may differ, but the track recordspeaks for itself.
Milipuko katika army munitions si jambo geni duniani.Suala hili geni Tanzania? ,ndiyo, na halipendezi? , ndiyo.
Refer kwa the Halifax Explosion,December 6 , 1917.Hapa mji mzima uliteketea kwa mabomu kulipuka , na leo 2011 jeshi la Marekani bado ndilo the mightiest.
Jambo la msingi ni kujifunza kutokana na mambo haya.
 
Safi Mwanakijiji... Hao JWTZ wasijisahau sana, umma wa watanzania unaona kinachoendelea LIBYA, Wanajeshi wanajiunga na wananchi kuikomboa nchi yao... Jamaa anatoa amri lipueni, marubani wanakataa.. Inauma kuona unawauwa wasio na hatia (km ilivyotokea GOMS). Narudia tena JWTZ najua mnawatu wenu humu JF, wanapaswa kuwaletea haya maoni yetu....Msijisahau... Badilikeni hilo ni jeshi la wananchi... Huyo Waziri wa ulinzi hiyo nafasi si ya maisha yako yote, jiuzulu uwaachie watakaoiweza!!!!! Shauri yako tutakutana mtaani siku moja utashindwa kujua upite upande gani kwa aibu!!!! Mbona baba yako alijiuzulu wewe unaona shida gani?
 
Back
Top Bottom