Mtambuzi
Platinum Member
- Oct 29, 2008
- 8,810
- 15,398
Leo nimeamua kuwaandikia barua dada zangu ambao wanatamani sana kuwa na mahusiano na wanaume lakini kwa bahati mbaya hawajabahatika kumpata anayewafaa. Kwa wale ambao wanaona kama muda unayoyoma na wanahisi kama wanaume wanawakwepa, kwa wale walio katika hatua ya mwisho ya kuvunja uhusiano, kwa wale ambao wanaona kwamba wao siku zote wanaishia kuwa wapambe wa maharusi na kamwe si mabibi harusi, kwa wale ambao mpaka sasa bado wanapewa mitoko (dating) lakini haizai matunda, kwa wale ambao wamejiondoa katika mahusiano yenye vurugu na wamefanikiwa kusonga mbele na maisha, kwa wale wenye hofu ya kuishi peke yao bila kuwa na mahusiano, kwa wale walioachwa na kukataa kufungua mioyo yao, na mwisho kwa wale ambao wamepoteza upendo na kuhisi kama kwamba kamwe hawataweza kupenda tena……………..
Nawaandikia barua hii ya wazi dada zangu wapendwa mlio single au mnaoelekea kuwa single nikiwaambia kwamba, huo sio mwisho wa dunia, na maisha bado ni zawadi kubwa kwenu na yenye thamani. Zawadi hii haipaswi tuichukulie kirahisi, kwani hutupa fursa ya kujitambua kuwa sisi ni nani na nini madhumuni ya kuwepo kwetu hapa duniani. Pale tunapopatwa na hali ya kujihisi upweke ni vyema tukawa na subira kwani mara nyingi subira hutuweka katika nafasi nzuri ya kujua kile kinachoingia na kutoka akilini mwetu.
Mara nyingi jamii yetu imekuwa ikiwatisha kwamba kutokuwa katika uhusiano au kutokuwa katika nafasi nzuri ya kuelekea kujenga mahusiano au kuchumbiwa au kuolewa iwapo utakuwa umefikisha umri fulani basi ni lazima utakuwa na matatizo ya kiakili, kimwili au kihisia na thamani zenu zinapungua……Ni bahati mbaya kwamba jamii mpaka sasa haimtendei haki mwanamke. Hata hivyo, kile ambacho watu wengi hushindwa kutambua ni kwamba, kuwa single ni sehemu ya maisha na inapaswa kusherehekea na kuiheshimu hali hiyo kama ilivyo pale inapotokea kuolewa. Hali hii ni lazima isherehekewe kwa sababu huu ndio wakati ambapo maarifa ya kujitambua kwamba wewe ni nani hukufanya ukue kifikra kila siku, na kuishi maisha uyapendayo na si vile watu wapendavyo uwe.
Najua wakati mwingine ni vigumu kukubaliana na hali hiyo, hasa pale muwaonapo wanandoa wanaopendana wakiwa na mtoko (dates) wakitembea huku wameshikana mikono, na ninajua ni vigumu kukubaliana na hali hiyo pale mtakapoalikwa na marafiki zenu mshiriki kwenye sherehe zao za kuvishana pete za uchumba. Pia ninajua kwamba itakuwa ni vigumu sana kwenu kukubaliana na hali hiyo, pale ambapo rafiki unayemfahamu mwenye tabia zisizofaa anapokutambulisha kwa mchumba wake unayemuona dhahiri kwamba ni mwenye tabia nzuri na mwadilifu lakini akiwa ameangukia mikononi mwa mwanamke unayemuaona dhahiri hamfai. Lakini pia utajisikia vibaya zaidi pale ambapo kila ufunguapo mitandao ya kijamii kama vile facebook na twitter unakutana na taarifa kutoka kwa baadhi ya marafiki zako wakitoa taarifa kwamba wamefunga ndoa au wamevishwa pete za uchumba…………….
Lakini hali hiyo isiwatishe kwani ni sehemu ya maisha, na hampaswi kuishi kwa kuangalia wenzenu wamepata nini bali lililo muhimu kwenu ni kuyafurahia maisha kwa sababu nyie ni binadamu kamili na mnazo sifa zote anazostahili kuwa nazo mwanamke na hampaswi kusubiri mkamilishwe na mtu yeyote………………..