Barack OBAMA

Choveki

JF-Expert Member
Apr 16, 2006
458
170
Obama

Barack mwana Obama, ushindi nakutakia
Na pia uwe salama, hilo nasisitizia
Najua si lelemama, kwa Mungu nakuombea
Ushindi twakutakia, Barack mwana Obama

Ushinde hiyo Novemba, wabaki wakishangaa
Uingie kwenye nyumba, nyeupe ukipepea
Najua utaukumba, ushindi kuunyakua
Ushindi twakutakia, Barack mwana Obama

Walianza kukuponda, pia kukupakazia
Wajua utawaponda, novemba ikifikia
Utayaona matunda, ya uungwana sikia
Ushindi twakutakia, Barack mwana Obama

Tunajua mwana kwetu, novemba ni kidedea
Wakati huu ni wetu, ni nani wakubishia?
Twaomba hata kikwetu, kilugha kukuombea
Ushindi twakutakia, Barack mwana Obama

Ni kheri pia fanaka, ambayo nakutakia
Neema kuongezeka, Ikulu ukihamia
Ukuu ni kutukuka, ongoza kinadharia
Ushindi twakutakia, Barack mwana Obama

Chini waanguke puu!, udenda kuwatokea
Wajue wewe ni juu, ushindi kuunyakua
Wakati wako ni huu, wa kwako kujishindia
Ushindi twakutakia, Barack mwana Obama

Ngoma tutacheza sana, huku tuki chekelea
Pia tutashimakana, hatamu ukishikia
Cheo wasema dhamana, nawe uje kumbukia
Ushindi twakutakia, Barack mwana Obama

Mcheza kwao hutuzwa, nami nakukumbushia
Kweli huwezi puuzwa, dunia yakupendea
Kura zisije kuuzwa, macho uje fungulia
Ushindi twakutakia, Barack mwana Obama

Obama sasa kwaheri, mwisho ninapoishia
Ngunguru sema ngangari!, toto wakijatishia
Uwaondoe kiburi, pia wanavyoringia!
Ushindi twakutakia, Barack mwana Obama


Choveki.
 


Mpendwa Barack,


Narudi tena Obama, ushindi kukutakia
Ingawa kuna lawama, kwa mengi sijaridhia

Nakutakia salama, ushindi kukufikia

Ushindi nakutakia, nasema bwana Obama


Ningali natumaini, ukweli umejulia

Umejua akilini, ambapo ulipotea

Moyoni pia kichwani, ni wapi umekosea

Ushindi nakutakia, nasema bwana Obama


Umechemsha kwa mengi, na hilo nakumbushia

Ukasahau misingi, iliyo jenga Dunia

Kujifanya bwana bigi, ubabe ukitumia

Ushindi nakutakia, nasema bwana Obama


Ongeza pia busara, sikia kaka sikia

Punguza zalo hasira, busara zitakujia
Hasira pia hasara, wahenga weshasemea

Ushindi nakutakia, nasema bwana Obama


Ushinde hiki kimbembe, ni mimi nakuombea

Vishinde vyao vijembe, wabaki wakishangaa

Uvunje pia na pembe, za tembo na yake pua

Ushindi nakutakia, nasema bwana Obama


Wakate vyao viburi, wabaki wakiduwaa

Wajue nawe ngangari, halafu hujachokea

Ushinde tena vizuri, wabaki wakiumia

Ushindi nakutakia, Barack mwana Obama


Hapa nasema tamati, kwa heri ndugu sikia

Naaga pia umati, tuzidi kumuombea

Ushindi uwe thabiti, na tena uso na doa

Ushindi nakutakia, Barack mwana Obama



Wakatabahu waraka,

Choveki,

Mtaani,
Jamii Forum. Octoba, 2012
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom