BAP: Msimamo Mkali Wa Vijana Wa UDSM

Sumaku

Member
Feb 17, 2009
53
1
Na Born Again Pagan

Bado tunajenga muktadha wa matukio ya ki-mataifa, ki-ukanda (regional) na ki-taifa (Tanzania) uliozalisha msimamo mkali kwa baadhi ya wanafunzi wa Mlimani miaka ya 1960 hadi 1970.

Thelathini, Tanzania Bara: Kushindwa kwa siasa na sera za ki-Bepari, chini ya Mpango wa Taifa ya Maendeleo wa Miaka Mitatu-Mitatu (ulioishia mwaka 1965) uliozingatia sana “Tanganyika” (na baadaye Tanzania Bara) kukua ki-viwanda. Mipango hii ilizalisha matabaka ya akina “ma-naiza” na “ma-kabwela” (mithili ya hali ilivyo sasa nchini kwetu tunapozungumzia ya “walalaheri” na “walalahoi”).

Kwa kushirikiana na serikali ya wakati huo, mfumo wa mipango hiyo ya maendeleo ulisimamiwa na Mashirika ya Kimataifa ya Fedha (Benki Kuu ya Dunia na Mfuko wa Fedha) pamoja na wafadhili wengine, kwa mfano, Uingereza na Amerika, kwa minajili ya kujenga ma-Bepari wa tabaka la kati (middle-class) - walaji wa viwandani.

Kujengeka kwa matabaka hayo ya “ma-naiza” na “ma-kabwela” kulichangia kikamilifu kuchachua wimbi la Ujamaa wa ki-Afrika katika nchi zetu za kusini mwa Sahara. Wimbi hili lilitingisha sana, eti, maslahi ya wakubwa wengine kwa kuogopa kile Waziri Mkuu wa u-China Chou-en-Lai alichokiita “Afrika imeiva tayari kwa mapinduzi” (Africa is ripe for a revolution) – kufuatia ziara yake katika nchi kadhaa za ki-Afrika, zikiwemo Zambia na Tanzania.

Thelathini na moja, kupanuliwa kwa elimu ya sekondari ili kuharakisha kujitosheleza kuwapata wataalamu wetu: Kuongeza mitaala (streams) miwili kwa darasa la tisa; kuondoa kikwazo cha Mtihani wa Territorial Standard Ten ili kila mwanafunzi wa darasa la 9 aweze kumaliza darasa la 12; na kuondoa karo katika masomo ya sekondari na chuo kikuu.

Ikumbukwe, kuwa miaka ya nyuma ya 1960 mtihani wa darasa la nane – Territorial Standard Eight – nao ulitolewa, ikiwa ni pamoja na kufupisha miaka ya elimu ya msingi kutoka 8 kuwa 7 na wanafunzi wa darasa la 7 kukubaliwa kujaribu mtihani wa Territorial Standard Eight.

Zaidi, majaribio ya wanafunzi wa darasa la 11 kuruhusiwa kujaribu Mtihani wa darasa la 12 (Cambridge University Overseas School Certificate Examination – Ordinary Level) ili washindapo waingie darasa la 13; kuanza uratatibu wa pre-selection kwa wanafunzi wa darasa la 12 wenye uwezo kuingia na kuanza masomo ya darasa la 13 kabla ya matokeo ya (Cambridge University Overseas School Certificate Examination – Ordinary Level); na wanafunzi wa darasa la 14 kuweza kuingia chuo kikuu kwa kushinda somo moja (principal) na “subsidiary” moja.

Zaidi, ili kujitosheleza kwa mahitaji ya walimu wenye digrii wanafunzi wote wa-Tanzania waliokuwa wakichukua masomo ya sayansi iliwabidi kuchukua pia somo la Elimu/Ualimu (Education Option). Ajabu ni kwamba watoto wa “vigogo” au waliokuwa karibu na “vigogo”, hawakuchukua Elimu/Ualimu (Education Option). Na hata wale wa mwaka wa kwanza 1966 waliporudishwa (baada ya mgomo), waliacha kozi hiyo ya ualimu na kuchukua B.A. General – ili wasipelekwe eti ‘mikoani’ kufundisha!

Hayo ya kudharau elimu yalianza zamani! Watoto wa “vigogo”, kwa kuelekezwa na wazazi wao, walitamani kubakia Dar es Salaam wakifanyakazi Wizara ya Nchi za Nje, Fedha na Mipango au Benki Kuu! Mwaka wetu kulikuwa na wanafunzi wawili tu, watoto wa ma-Waziri – walichukua Elimu/Ualimu (Education Option): Mvulana wa Muhaji (Waziri Mdogo – Elimu) na Blandina Mhando (Steven Mhando - Wizara ya Nchi za Nje).

Tanzania ilikabiliwa na uhaba wa walimu katika mashule yake. Walimu wa-Uingereza walikuwa wananza kutoka mmoja mmoja. Nakumbuka mwalimu wangu wa Fisikia alikataa kutufundisha akidai, “I am going to teach in Kenya because you are now independent!” Ombwe la walimu lilizibwa na walimu wa-Amerika wa mpango wa Peace Corps – toka shule za msingi hadi sekondari…wengine mliopita shule za msingi za wakati huo mnaweza kukumbuka uji wa ki-Amerika, “oatmeal”!

Thelathini na mbili, kuanza kufifia kwa vyama vya upinzani hadi kuanzishwa kwa siasa ya chama kimoja mwaka 1965. Kwa upande wa Tanzania Bara vyama hivyo ni: African National Congress cha Zuberi A. Mtemvu; Peoples Democratic Party (PDP) cha Christopher Kasanga Tumbo; Peoples Convention Party (PCP) cha Samson Mshala; Nationalist Enterprise Party (NEP); na hapo baadaye (PCP) iliungana na NEP kuunda African Independence Movement (AIM).

Kulikuwepo pia na vyama vya Bwana Masalu huko Mwanza na All Muslim National Union of Tanganyika (AMNUT), chini ya mnajimu mashuhuri Sheikh Yahya Hussein. Lakini AMNUT kiliishiwa mafuta ya ki-siasa. Wengine walikiona kuwa ni chama cha ki-dini, eti kwa sababu wa-Islamu walikuwa wakisahauliwa. Lakini ukweli ni kwamba hata kabla ya uhuru Tanganyika chini ya TANU ilikuwa imeishatoa ubaguzi wa rangi na dini mashuleni!

Na huko Tanzania Visiwa (napenda kuiita hivyo kwa sababu Tanzania Bara haiitwi Tanzania Barani) kulikuwepo na vyama vingi hadi Mapinduzi: Zanzibar Nationalist Party (ZNP) cha Sultan na Zanzibar and Pemba People’s Party (ZPPP) kilichomegeka kutoka ZNP, Umma Party cha mkono wa kushoto cha Abdulrahman Muhammad Babu, na Afro-Shirazi Party cha Abed Karume.

Thelathini na tatu, kupinduliwa kwa Rais wa Ghana Osagefo Kwame Nkrumah, ikiwa ni pamoja na baadhi ya Nchi za Magharibi (zikiongozwa na Amerika, Ufaransa na Uingereza) kuunga mkono, na kusaidia askari wa kukodiwa (mercenaries).

Hao “mbwa-wa-vita” waliranda-randa na kutamba-tamba katika nchi changa za Ukanda wa Joto wa Afrika na kutumiwa katika kupindua serikali zake, na kuweka viongozi vibaraka - wengi wakiwa ni wana-jeshi. walidai eti walikilinda maslahi ya wakubwa!

Thelathini na nne, kuzinduliwa kwa East African Community (kuchukua nafasi ya East African Common Organisation) na kujenga makao makuu yake mjini Arusha.

Thelathini na tano, kuzaliwa kwa Chuo Kikuu cha Afrika Mashariki: Makerere (Udaktari na Kilimo), Nairobi (Uhandisi na Biashara), na Dar es Salaam (Sheria na Elimu) na kuvunja uhusiano wa ki-taaluma na London University. Tukawa na digirii zetu za Chuo Kikuu cha Afrika Mashariki badala ya za London University. Chuo Kikuu cha Afrika Mashariki kiliwakutanisha vijana wengi – kwa wakati huo, mbegu nzuri za Umoja wa Nchi za Afrika Mashariki.

Thelathini na sita, matembezi ya aliyekuwa Waziri Mkuu Chou-en-Lai wa u-China katika baadhi ya nchi za Afrika: Ziara hiyo ilileta mafua na kukuna vichwa kwa wivu kwa Nchi za Magharibi, kufuatia kauli yake, “Africa is Ready for Revolution” (Afrika Imeiva Tayari kwa Mapinduzi). Nchi hizo zilijiami kwa mbinu za kulinda eti maslahi yao katika Bara la Afrika.

Thelathini na saba, zikiongozwa na Amerika, Ufaransa na Uingereza katika kulinda maslahi yao, serikali za Nchi za Magharibi zilianza kuzidisha mikakati yake ya kuzisetri tawala za kibaguzi za wa-Ulaya walowezi wachache na wabaguzi huko kusini mwa Afrika (Rhodesia, Msumbiji, Afrika Kusini, South West Africa/Namibia na Angola).

Thelathini na nane, nchi moja kati ya tawala za kibaguzi za wa-Ulaya walowezi wachache na wabaguzi huko kusini mwa Afrika, Rhodesia, ikawa ni “mtoto mbaya”, kwa Uingereza na muasi kwa Afrika. Utawala wake, chini ya kiongozi wao, haini Ian Smith, ulijitangazia uhuru wa mabavu (Unilateral Decralation of Independence - UDI) na kuendelea kuwatesa ndugu zetu zaidi.

Ma-Profesa wengine wa Rhodesia, wenye asili ya Ulaya, walikimbia na kujisetri nchini kwetu wakifundisha hapo Mlimani: Terrence Ranger, John Illife na John Mcracken (Historia) na Roger Woods (Sosiolojia).

Uingereza iliendelea na msimamo wake wa NIBMAR (No Independence Before Majority African Rule). Lakini wananchi vibaraka wa humo nchini na chama chao cha United African National Council (UANC) cha Bishop Abel Tendekayi Muzorewa, kwa kushirikiana na mhaini Ian Smith, waliunda serikali ya muda Rhodesia/Zimbabwe, chini ya Waziri Mkuu Bishop Abel Muzorewa. Serikali hiyo ililaani vita ya ukombozi.

Afrika ilikataa kuitambua serikali hiyo na ilizingatia kuwa Rhodesia lilikuwa bado ni koloni la m-Uingereza. Kwahiyo, jukumu la kuikomboa lilikuwa chini ya uwezo wa Uingereza.


Makala yajayo yataendelea ma matukio mengine.
mwandishi anapatikana kwa barua pepe: romuinja@yahoo.com)

CHANZO: kwanzajamii.com
 
Magnet, hongera kwa makala ndefu, isiyokuwa na mvuto wa aina yoyote na ambayo imeshindwa kutuelekeza wasomaji kule unakotaka kuelekea!?!
 
Last edited:
Wow! The heading is very catchy! The rest is crap. At least to me.
 
Hii article imepitwa na wakati. 100% ya watu aliotataja walishakufa. Halafu hii ni 2009! Terminologies kama ukoloni, haini, Rhodesia etc. na watu kama Bishop Abel Muzorewa, Ian Smith, Chou-en-Lai ktk era hii!

Good text for history book chapter though.
 
Hii article imepitwa na wakati. 100% ya watu aliotataja walishakufa. Halafu hii ni 2009! Terminologies kama ukoloni, haini, Rhodesia etc. na watu kama Bishop Abel Muzorewa, Ian Smith China, Chou-en-Lai ktk era hii!

Good text for history book chapter though.

I think this was intended as a history. What made you think otherwise?
 
Hivi msiposoma historia mtaelewa vipi tulikotoka, tulipo na twendako? Bila shaka kwa vijana wa sasa hii ni carp lakini kwa vijana wa enzi hizo ni kumbukumbu nzuri ya yaliyojiri.

Asante kwa kutuletea. At least sisi tuliointerested umetupatia hiyo link ya kwanzajamii tutaifuatilia.

Usife moyo!
 
Back
Top Bottom