Bandari waomba kupandisha ada, ushuru

Jul 6, 2012
5
0
Napendekeza Sumatra wasikubali viwango vipya vya bandari!


MAMLAKA ya Bandari Tanzania (TPA), ambayo imeanzishwa kulingana na sheria ya bandari namba 17 ya mwaka 2004 ambayo pamoja na mambo mengine inaitaja mamlaka hiyo kuwa ndio mmiliki wa bandari zote nchini ikitimiza majukumu yake yakiwemo ya kijiografia ambayo yanafanya Tanzania kutambulika kuwa ina bandari.

Kuwa na menejimenti inayowajibika katika utendajikazi wa utoaji na upokeaji wa mizigo katika bandari zake na kuhudumia abiria pia sanjari na hilo ina takiwa kuendeleza, kuhuisha miundombinu na kuhakikisha usalama wa bandari.

Bandari ni lango la maendeleo la Taifa lolote ambalo limepata fursa ya kuwa nayo na kulingana na kasi ya ukuaji wa uchumi wa dunia inahitaji mipango jadidi ya uwekezaji wenye tija ambayo utaiwezesha kushindana na bandari zingine za nchi jirani.

Dira ya TPA kwa miaka 20 kutoka 2008 hadi 2028 pamoja na mambo mengine imekusudia kuziweka bandari zake katika kiwango cha juu cha huduma kwa kutumia mbinu mbalimbai za uwekezaji na mikakati yake hiyo inatajwa kuwa ni kujenga visima zaidi vya kupokelea mafuta na kurekebisha mfumo wa malipo.

Mikakati mingine ni upanuzi wa yadi zake kwa ajili ya kupokelea mizigo yakiwemo makontena na maboresho mengine katika bandari zilizo chini yake ili iweze kutoa huduma bora zaidi kwa nchi ambazo zinategemea zetu ambazo ni Uganda, Zambia, Malawi, Jamhuri ya Congo, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini.

Ili kuweza kufikia lengo hilo hivi karibuni TPA imewasilisha waraka katika Mamlaka ya Udhibiti wa Vyombo vya Majini na Nchi Kavu (Sumatra) ikitaka kupandisha ada na kodi zingine ambazo zinatozwa na mamlaka hiyo kwa watumiaji wa bandari zake.

Mamlaka hiyo ina miliki bandari za Dar es Salaam, Mtwara na Tanga ambazo zipo bahari ya Hindi na zingine zilizopo katika mwambao wa Ziwa Tanganyika, Nyasa na Victoria na sababu za kutakiwa ongezeko hilo inatajwa kuwa ni kutokana na kutokuvifanyia marekebisho kwa kipindi kirefu.

Waraka huo unasema kuwa bandari hawajafanyia marekebisho viwango vyake toka mwaka 1994 na hoja yao ni kuwa kiwango cha shilingi kimeshuka kulinganisna na dola ya Marekani toka wakati huo hadi sasa hali ambayo inaathiri utendaji wa mamlaka.

TPA wanaeleza kuwa wanahitaji pesa kwa ajili ya maboresho ya bandari kulingana na dira ya 2008/2028 na pia kwenda sanjari na kasi ya ukuaji wa uchumi huku wakidai kuwa hawapati ruzuku toka serikalini.

Suala la kuongeza viwango vya ada au tozo zingine zina utaratibu wake na kitendo cha TPA kudai kuwa wanafanya hivyo kutokana na muda mrefu (tokan 1994) hawajafanya marekebisho viwango hivyo sio hoja na haitarajiwi kutolewa na watu ambao tunaamini kuwa wana elimu ya kutosha kuhusiana na masuala ya biashara na hata uendeshaji kwa ujumla wake.

Kushindwa kuongeza viwango wakati wote toka 1994 na kuja kukurupuka mwaka huu 2012 ni sawa na kusema kuwa TPA imelimbikiza bila sababu zozote ufanyaji wa marekebisho ya viwango vyake vya tozo na ada zingine jambo ambalo kimsingi ni uzembe na wao ndio ambao wanawajibika.

Haingilii akilini kutaka kutumia kigezo hicho kuongeza gharama hizo kwa asilimia 134 kutoka kiwango cha awali cha asilimia 17 kwa kutumia kisingizio cha kushuka kwa thamani ya shilingi na kupanda kwa gharama za uendeshaji au maboresho ambayo wanafanya si hoja.

Mbaya zaidi maombi hayo yanaletwa bila mchanganuo ambao unapaswa kuonyesha wanapata nini sasa kulingana na viwango wanavyotaka kuongeza, hasara inayopatikana kutokana na kiwango kidogo cha tozo hizo na matarajio ya kukusanya kiasi gani kutokana na ongezeko hilo.

Sitaki kuamini kuwa kipengere hicho kimeachwa kwa bahati mbaya au kutokana na ufahamu finyu wa wahusika katika masuala ya fedha na biashara isipokuwa mamlaka hiyo inachokifanya sasa ni hujuma dhidi ya bandari zetu ambazo zinatajwa kuwa na huduma mbovu kuliko zingine zote ukanda huu.

Mamlaka hiyo inachukua jukumu la kuomba kuongeza viwango hivyo huku ikikabiliwa na malalamiko lukuki kutoka kwa wadau wa bandari kutokana na huduma na ucheleweshaji ambao unawaingiza wateja wao katika gharama bila sababu za msingi.

Pia kauni za biashara zinapingana na ongezeko la kadiri hiyo na iwapo Sumatra watakubali ombi hilo ambalo wadau wamelikataa ni wazi kuwa itakuwa safari ya kaburini ya bandari zetu kutokana na ushindani uliopo katika bandari za nchi jirani.

Pia viwango hivyo vilivyopendekezwa vinatajwa kuwa ni vikubwa kuliko vinavyotozwa katika bandari zaa Cape Town (Afrika Kusini) na Beira (Msumbiji), Mombasa (Kenya) na hata Kismayu (Somalia) ambazo ukiondoa ile ya Somalia zingine zote huduma zao ni bora na za haraka kuliko ilivyo kwetu hali ambayo ni wazi kuwa tutawafukuza wateja.

Kiburi kuwa nchi za Uganda, Rwanda, Burundi, Zambia, Jamhuri ya Kongo, Malawi na zingine lazima ikitarajiwa pia Sudan Kusini lazima watumie bandari ya Dar es Salaam au Mtwara ni upuuzi na majidai yasiyo na tija ambayo yanaweza kufanywa na mtu ambaye hajui kuwa dunia ya leo sio ya jana.

Kimantiki bandari walipaswa kuboresha huduma kwanza kisha ndio waombe kuongeza viwango hali ambayo ninaamini ingepata uungwaji mkono hata kutoka kwa wadau ambao wangekuwa wameridhishwa na huduma zao na sio kama ilivyo sasa.

Kupandisha kwa kutegemea kuwa ni lazima wateja watakuja kwa kuwa hawana namna nyingine ni mawazo mgfando ambayo hayaendani na ulimwengu wa sasa ambao umejaa ubunifu na kila namna ya njia za kutafuta nafuu.

Kupanda kwa viwango hivyo kitu ambacho kitatokea tena haraka sana ni kupanda kwa bei za bidhaa mbalimbali zinazopita bandarini hapo jambo ambalo litawaumiza zaidi walaji kuliko waagizaji ambao watalazimika kupandisha bei ili kuweza kwenda sawa na ongezeko hilo la tozo na ada mbalimbali ambalo si la kitaalam.

Kimsingi bandari wanapaswa kujipanga upya na kukokotoa tena viwango hivyo ili waje na hoja yenye mizania ya kibiashara ambayo itajibu maswali lukuki ambayo yamejitokeza ikiwa na vyovyote iwavyo viwango hivyo ni vikubwa na visivyokubalika labda wapendekeze vingine.

Kinyume cha hivyo ni kuziua bandari zetu kwani taarifa zilizopo ni kuwa ile ya Mtwara ipo taaban licha ya ukweli kuwa ina vifaa si haba kwa ajili ya upakiaji na upakuaji wa mizigo hivyo ni wazi kuwa TPA inatakiwa ijitazame upya na sio kukimbilia kuongeza viwango wakati huduma hazikidhi.

Maoni ya wadau yanapaswa kufanyiwakazi ili kunusuru hali hiyo na isifike wakati watumiaji wakajuta kuzijua bandari zetu hivyo kutafuta njia mbadala kwani daima shule ufundisha hivyo kitendo cha kuwaumiza kwa kuwatoza bei za ajabu kutawafanya watafute njia mbadala.

Hilo likitokea ni wazi kuwa utakuwa msiba kwetu kiuchumi kwani bandari ni eneo ambalo serikali haijalitumia kikamilifu kiunua uchumi kutokana na urasimu, miundmbinu na hata uchukuzi baada ya mizigo kutoka bandarini.

Kama reli imeuawa chonde chonde tusiue na bandari kisha tukaja na mikakati ya kuifufua wakati sababu za kufa zinatengenezwa na sote tunazijua na tunaziona sasa ndio maana tuna taadharisha kuwa kupandisha viwango kwa mujibu wa matakwa ya TPA ni kuifanya bandari kuwa kama Kampuni ya Reli Tanzania (TRL).

Si ajabu kabisa wanaopendekeza viwango hivyo sasa ndio ambao watakuwa wa kwanza kutaka bandari ibinafsishwe au kutafutwa mwekezaji kwa madai kuwa inaendeshwa kwa hasara na huo ndio utakuwa mwisho wa kila kitu kwa maana kwamba kama wenyewe tunashindwa hakuna awezaye kuja kutufanyia.
 
Back
Top Bottom