Bajeti ya SMZ hakuna kodi mpya

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,268
33,039
Budget%20Zenzi%281%29.jpg

Waziri wa Fedha na Uchumi Zanzibar, Dk. Mwinyihaji Makame Mwadini, akionyesha mkoba wenye bajeti ya serikali ya mwaka 2010/2011 muda mfupi kabla hajaiwasilisha katika kikao cha Baraza la Wawakilishi jana.(Picha: Martin Kabemba).



Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imewasilisha bajeti yake ya mwaka wa fedha wa 2010/11 bila kupandisha kodi kwa lengo la kuwapunguzia ukali wa maisha wananchi wake.
Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi katika kikao cha Baraza la Wawakilishi jana, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Fedha na Uchumi), Dk. Mwinyihaji Makame Mwadini, alisema serikali imechukua hatua hizo ili kupunguza mfumuko wa bei katika soko la ndani.
Dk. Mwadini alisema bajeti ya mwaka huu imeathiriwa na nakisi kwa Sh. milioni 6,000, lakini alisema pengo hilo litazibwa na mikopo ya ndani kupitia hati fungate.
Alisema kuwa serikali inatarajia kutumia Sh. bilioni 444.637 katika mwaka wa fedha 2010/11 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na utekelezaji mpango wa maendeleo.
Alisema kati ya fedha hizo, Sh. bilioni 193.433 zitatumika kwa kazi za kawaida wakati Sh. bilioni 251.204 zitatumika kwa utekelezaji wa mpango wa maendeleo na Sh. bilioni 82.459 kwa malipo ya mishahara ya watumishi wake.
Waziri Mwadini alisema pato la taifa limeongezeka hadi kufikia Sh. milioni 878.403 kutoka Sh. milioni 748.057 mwaka 2008 sawa na ongezeko la asilimia 17.4.
Alilieleza Baraza la Wawakilishi kwamba uchumi wa Zanzibar umekuwa umeongezeka kwa asilimia 6.7 kutoka asilimia 5.3 kutokana na mageuzi katika sekta ya kilimo pamoja na kuongezeka kwa idadi ya watalii.
Alisema pato la mtu wa kawaida pia limeongezeka kutoka Dola za Marekani milioni 557 hadi 728.364 mwaka 2008 sawa na ongezeko la asilimia 4.3 na kuwataka wananchi kuendelea kudumisha hali ya amani na utulivu wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu.
Hata hivyo, alisema mfumuko wa bei katika soko la ndani la Zanzibar umeongezeka kutoka asilimia 5.1 mwaka 2000 hadi asilimia 9.7 mwaka huu, lakini alisema mwaka 2008 mfumuko wa bei ulikuwa mkubwa baada ya kufikia asilimia 20.6 na kuathiri wananchi wake.
Waziri Mwadini alisema kwamba tayari Serikali imeshaanza kupitia upya muundo wa watumishi wa umma ili iweze kuboresha maslahi yao kwa lengo la kuwapunguzia ukali wa maisha.
“Maslahi ya wafanyakazi yatashughulikiwa vizuri zaidi baada ya kukamilika mapitio ya muundo wa watumishi wa umma,” alisema Waziri huyo.
Watumishi wa umma wamekuwa wakilipwa mshahara wa Sh.100,000 viwango ambavyo vimekuwa vikilalamikiwa na wafanyakazi pamoja na vyama vya wafanyakazi Zanzibar.
Alisema katika mwaka ujao wa fedha, Serikali inatarajia kukusanya Sh. milioni 171,687 kutoka vyanzo vya mapato ya ndani sawa na asilimia 17.9 ya pato la taifa.
Hata hivyo, alisema kwamba katika bajeti hiyo Sh. bilioni 266.950 zinatarajiwa kutoka kwa wafadhili kupitia misaada ya kibajeti kwa ajili ya utekelezaji programu na miradi ya maendeleo katika mwaka wa fedha ujao.
Waziri Mwadini alisema kutokana na wahisani kupunguza misaada ya kibajeti katika mwaka huu wa fedha, bajeti ya Zanzibar itaathiriwa na upungufu wa Sh. bilioni 18, lakini serikali imeshaanza kuchukua hatua mbali mbali kuziba pengo hilo kupitia mikopo.
Aidha alisema kwamba serikali inatarajia kuanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo ili kuharakisha maendeleo katika majimbo 50 ya Zanzibar.
Alisema kwamba serikali inatarajia kuwasilisha muswaada wa sheria wa kuanzisha mfuko huo mwaka huu kama ilivyo kwa serikali ya Muungano ambayo imeshaanza kutoa fedha za maendeleo ya jimbo kwa wabunge wa Tanzania Bara na Zanzibar.




CHANZO: NIPASHE
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom