Bajeti ya Serikali 2008/09 - Exclusive Thread

Usafi wa Lowassa, uchafu wa CCM

ban.maswali.jpg
Ansbert Ngurumo

STAILI ambayo Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimetumia kujisafisha inavutia, inashangaza, inachekesha na kutafakarisha kidogo. Ni staili inayozua maswali yasiyo na majibu au yenye majibu yasiyoridhisha.
Lililo dhahiri ni kwamba, kwa kitendo cha kujisafisha, kwa kutumia kikao cha Halmashauri Kuu (NEC), CCM imekiri kile ilichokuwa inakikataa kwa muda mrefu - kwamba imechafuka.
Lakini staili yake ya kujisafisha inatufanya tuhoji upya: Uchafu ni nini? Umeingiaje CCM? Umeingizwa na akina nani? Umeingia lini? Na unaondolewaje? Labda CCM wangejiuliza maswali haya na kuyatafutia majibu ya kina, wangepiga hatua kidogo.
Majibu ya maswali haya yanatosha kuandika kitabu ambacho kitaandikwa siku moja na kuwa marejeo ya vizazi vijavyo kuhusu historia ya ukombozi wa nchi hii kutoka mikononi mwa wakoloni weusi waliojipa haki ya kutafuna matunda ya uhuru wa Watanzania bila ridhaa yao.
Ikumbukwe kwamba zilipoibuliwa tuhuma dhidi ya CCM, hadi baadhi ya watani wake kisiasa wakakiita Chama Cha Majambazi; Chukua Chako Mapema; Chama Cha Majangili; Chama Cha Mafisadi na kadhalika. Viongozi wakuu wa wanachama walipinga, waling’aka, kuwakebehi na hata wakawatisha waliotoa tuhuma hizo.
Katika hali ya kutapatapa na kukata tamaa, na kama ilivyo kawaida ya CCM kufanya propaganda katika masuala ya msingi, Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, alitamka hadharani kwamba tuhuma dhidi ya CCM ni kelele za mlango zisizoweza kumzuia yeye (akajiita mwenye nyumba) kulala! Wiki hii ni yeye aliyeongoza kikao cha NEC kujaribu kujisafisha, kwa staili aliyochagua yeye na viongozi wenzake. Viongozi wenzake, naye akiwamo, pamoja na wastaafu, wamefunikwa na kashfa nzito mno kichwani hadi miguuni.
Hawaonekani! Hata waliotishia kwenda mahakamani baada ya kuhusishwa na ufisadi wameshindwa kwenda kwa sababu dhamiri zao zinawaeleza ukweli kwamba hizi si kelele za mlango, bali sauti za wanyonge, wenye mali ya nchi hii, ambao hatimaye wamegundua mnyonyaji wao ni nani.
Watuhumiwa hawa wanaogopa yasifumuke mengine wakiwa kule mahakamani. Na licha ya ushahidi wote uliopatikana hata bila kwenda mahakamani, vyombo vya dola vimeshindwa kuchukua hatua dhidi ya watuhumiwa.
Polisi wetu wameamua (bila shaka kwa maagizo ya kisiasa) kufanya kazi ya kisiasa. Wanakimbizana na vibaka na wezi wakuu mitaani; wanawabambikia kesi wananchi maskini wanaotafuta kwa jasho. Wakati mwingine wanawanyonga ili kuwanyang’anya walicho nacho.
Wanashindwa kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria wale wanaotuhimiwa kwa wizi mkubwa unaofilisi hata maisha binafsi ya polisi wenyewe. Maana kama watuhumiwa walishindwa kwenda wenyewe mahakamani kuwashitaki waliowatuhumu, Jeshi la Polisi lingetusaidia kwa kuwakamata watuhumiwa ili haki itendeke.
Kimsingi, hata wanasiasa makini wanaotaka kujisafisha matope ya ufisadi, walio na dhamiri ya kuonyesha kwamba hapa kuna ari mpya, wangepaswa kuchukua hatua za kisheria ili kujisafisha au kuwasafisha watuhumiwa au kuwashughulikia kwa mujibu wa sheria.
Huo ndiyo ungekuwa usafi wa CCM na serikali yake. Hapo ndipo rais angeanzia kuisafisha na kuwasafisha wenzake. Angechanganya hatua hiyo na zile fursa kadhaa zilizojitokeza, akabadilisha sura na mfumo wa utawala; akaondoa wachafu na kuweka wasafi; akafukuza wazembe na kuingiza wachapakazi.
Angepata pa kuanzia upya; na tungemsikiliza. Mara zote alizobahatika kufanya mabadiliko madogo na makubwa katika Baraza la Mawaziri zilikuwa fursa muhimu za kutuonyesha nia yake ya kusafisha serikali na CCM. Alishindwa kuzitumia.
Akawahamisha mawaziri kutoka wizara moja hadi nyingine; akawapunguza wachache wasio na tuhuma nyingi; akawabakiza wale wanaotuhumiwa kila siku. Ni sawa na mtu anayefagia nyumba yake halafu akakusanya uchafu wote akaulundika chumbani anakolala; kisha akawatangazia wana familia na majirani kwamba nyumba yake ni safi.
Harufu ya uchafu inayowakera hao, inamburudisha yeye, maana yeye na wao wana tafsiri tofauti ya usafi na uchafu. Tusisahau kuwa kabla aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa kujiuzulu, rais alikuwa ameunda Tume ya Profesa Rwekaza Mukandala kumsaidia kuwachunguza mawaziri wake na kumpa ushauri juu ya nani mbovu, nani ana nafuu, nani aondolewe na nani abaki.
Kwa bahati mbaya, hakuunda tume kabla ya kuwateua, ili kubaini ubovu wao. Lakini wengi wa wateule wake ni wale ambao yeye na wao wamekuwa pamoja serikalini kwa zaidi ya miaka 17. Haiwezekani kwamba hakuwajua. Wala hakuhitaji ushauri wa tume.
Wananchi wenyewe walionyesha wasiwasi juu ya baadhi yao. Iweje wananchi wajue udhaifu wa mawaziri, yule aliyewateua, tena mwenye vyombo vya kiutawala vya kumsaidia kuwajua, ajidai kwamba hawajui hadi aletewe taarifa na tume ya ‘kisomi’! Ajabu ni kwamba, hata tume ilipoleta majibu, hakuyatumia. Akawateua wale wale, tena wengine wakamkejeli kwenye vyombo vya habari. Andrew Chenge ni mfano hai. Alipoteuliwa kuongoza Wizara ya Miundombinu, wanahabari wakamhoji kwanini amerudi akasema “muulize rais aliyeniteua. Ndiye anajua sababu.” Chenge alikuwa sahihi.
Na hata baadaye alipoondoka kwa kashfa za kuficha nje mabilioni ya shilingi ambazo hazijajulikana alivyozipata, alitoa kauli nyingine kwamba ameondoka ili kumwondolea ugumu rais. Maana yake, kama si kwa ajili ya rais, Chenge asingeondoka.
Lakini maana kubwa zaidi inayopatikana kwenye kauli yake ni kwamba kama asingeondoka, rais asingemfukuza! Kauli kama hii ilitolewa pia na Lowassa alipojiuzulu uwaziri mkuu, akasema amefanya hivyo si kwa kuwa ana mkono kwenye Kampuni ya Richmond, bali kwa kuwa alitaka kulinda heshima ya chama na serikali.
Baadhi yetu tuliandika kumsahihisha Lowassa, tukasema alijiuzulu kulinda heshima ya rais kwa kuwa wote walikuwa washiriki wakuu katika mradi wa Richmond. Kuna jambo lilitokea wakati ule ambalo lipo hadi sasa. Ile heshima ya chama na serikali haikurejea.
Kwa hiyo, kujiuzulu kwa Lowassa hakukusaidia kurejesha heshima ya serikali na CCM. Na sababu mojawapo iliyosababisha heshima hiyo isirejee ni kwamba mafisadi wale wale wameendelea kuwa viongozi wa CCM na serikali.
Wao walitaka tuamini kwamba fisadi ni Lowassa; akiondoka serikali inakuwa safi. Wapi! Sasa NEC ya CCM imekaa na kumsafisha rasmi Lowassa kwa kusisitiza kauli yake ya awali.
Maana yake ni kwamba CCM na serikali hii ya Kikwete inamhitaji sana Lowassa. Na imegundua kwamba inahitaji kumlinda. Inajua, kwamba tunavyojua, kwamba alipokuwa waziri mkuu, Lowassa hakutenda jambo lolote zito kwa uamuzi wake pekee.
Yote aliyatenda kwa idhini na ushauri wa rais. Ndiyo maana yalipomtokea yaliyosababisha ajiuzulu, rais alikuwa wa kwanza kumtetea, akasema amepatwa na ajali ya kisiasa; kwa kuwa Lowassa ni kiongozi mchapakazi, mwadilifu na mzalendo wa kweli.
Aliyasema hayo huku akijua kuwa umma wa Watanzania unamzomea Lowassa na kumwona fisadi wa kutupwa, maana katika sakata hili la Richmond, jina la Lowassa limetajwa mno kuliko hata la wamiliki halisi wa Richmond.
Hili ndilo ambalo CCM imejaribu kupambana nalo. Na kitendo cha NEC kumsafisha Lowassa sasa, ni uthibitisho kwamba CCM imesisitiza kauli ya Rais Kikwete juu ya ‘uadilifu na uzalendo’ wa Lowassa. CCM na Serikali ya Kikwete inamuogopa Lowassa. Na haikuanza leo.
Lakini woga huu uliongezeka pale walipoona Lowassa anawekewa zulia jekundu kwao Monduli! Woga ulizidi walipoanza kusikia akijitetea hadharani. Wakajua wasipofanya kitu, atalipuka na kulipua mambo. Wakaamua kumlipua yeye kwa njia mbili.
Kwanza, wakawa wanamtumia wajumbe wa kumpa pole na kumfariji kwa yaliyompata. Pili, walipogundua bado ana kinyongo na kwa hulka yake atazidi kusema mengine wasiyotaka aseme - maana alishaamua kujitetea asife kibudu - wakaingiza nguvu ya dola. Wakamuonya. Akaufyata! Hadi leo najiuliza. Kuna kitu gani serikali inaogopa kwa Lowassa? Kitu gani waliogopa asiseme? Na hapa walipofikia, inawezekana hatasema tena; maana wamemsafisha. Wamemziba mdomo.
Lakini usafi huu wa Lowassa una maana gani pana? Wamemsafisha Lowassa kumlinda mwingine. Na ulinzi huu ndiyo sababu ya NEC kuwatisha wabunge na kuwawekea ‘gundi’ mdomoni wasijadili masuala ya ufisadi wa EPA bungeni.
Huu ni uchafu ambao wakubwa hawataki kuondokana nao. Uchafu huu ndiyo asili ya nyadhifa zao. Uchafu huu ndiyo ulaji wao. Ukizungumzwa kwa uwazi, ukaanikwa, hakuna mmoja wao atakayebaki. Hakuna atakayemfukuza mwingine. Na ndiyo maana wamekuwa wakilindana na kuogopana hata mambo yanapokuwa yameharibika waziwazi.
Na ndiyo maana wengine tunatilia shaka hizi harakati za CCM na serikali kujisafisha kwa kuwatoa kafara wachache na kuwakumbatia wengi. Wanataka kutumia ‘usafi’ wa Lowassa kuisafisha CCM na serikali. Lakini wanashindwa kuchukua hatua za dhati kwa mafisadi wa EPA.
Hakuna atakayewaelewa. Hata Richmond (sasa Dowans) bado inaendelea kulipwa mamilioni wasiyostahili (sh 152,000,000 kila siku). Matendo haya ya NEC huku serikali ikishindwa kuchukua hatua dhidi ya mafisadi, ni sawa na CCM kujisafisha kwa kunawa matope. Sote tunajua matokeo yake.
Inavutia kufuatilia mchakato wa namna hii; inashangaza CCM wasivyojua maswali ya msingi yanayowakabili; inachekesha kwamba watawala wameamua kufanya maigizo mbele yetu; na inatafakarisha kwamba vita dhidi ya ufisadi inahitaji watawala mbadala na vyombo mbadala. Si hawa tulio nao.

ansbertn@yahoo.com
www.ngurumo.blogspot.com
+447853850425
 
Azimio Jipya hongera kwa kulitoa dukuduku lako. Ni kweli kabisa wanatunyanyasa kwa hii misaada yao. Ni wajanja hawa nanatafuta maeneo yale ambayo yanawagusa moj akwa moja ndio wanajidai tuyarekebishe kwanza kabla ya kutupa misaada yao. Wanajitia hawatoi mpaka turekebishe au tuwe na good governance je huko nyuma walipokuwa wanatusaidia tulikuwa na good governance? au wameona nasi tumecharuka tunawadai rushwa mpaka wao na wanaumia ndo maana wanataka tujirekebishe ili wavune ipasavyo?

Mimi hata siku moja simwamini Mzungu na misaada yake, they always come with strings attached ...... si umasikini tena unaotufanya tudhalilishwa na vimisaada vyao bali ni uroho wa baadhi ya viongozi wetu ndo maana tunajikuta tunaingia katika mikataba uchi na hawa mafisadi... hakika wanastahili kuitwa mafisadi weupe shwaiiin
 
Back
Top Bottom