Babu aomba wagonjwa wasimshangilie

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
268
MCHUNGAJI Ambilikile Mwasapila anayetoa tiba ya magonjwa sugu katika Kijiji cha Samunge, Loliondo amewaomba wagonjwa na watu wengine wanaokwenda kupata huduma yake kuacha kumshangilia kila wanapomwona.

Mchungaji Mwasapila ambaye amekuwa maarufu kwa jina la Babu alisema hayo jana katika mazungumzo yake ya kila siku asubuhi kabla ya kuanza kutoa tiba.Aliwataka wagonjwa na jamaa zao kumshangilia Mungu akisema ndiye anayewatibu na siyo yeye.

"Nawaona nikitokea kuanza kutoa tiba mnashangilia, pia nikiwaeleza kuhusu dawa hii mnashangilia, anayeponya siyo mimi ni Mungu hivyo mnapaswa kumshangilia Mungu wenu mara kwa mara, "alisema Mwasapila.

Katika hatua nyingine, mgogoro wa mapato kati ya Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, Arusha na Serikali ya Kijiji cha Samunge umemalizika baada ya kuamuliwa kwamba kuanzia sasa kijiji hicho kitapata mgawo wa Sh2,000.

Uamuzi huo ulifikiwa juzi jioni katika kikao cha dharura kati ya wajumbe wa Serikali ya Kijiji cha Samunge na Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Elias Wawa Lali.

Kikao hicho kilifanyika siku ya mwisho ambayo ilitolewa na wakazi wa kijiji hicho kupitia mkutano wao mkuu kwa halmashauri hiyo iwe imewaondoa wakusanya ushuru wake kijijini hapo la sivyo watasitisha huduma ya tiba inayotolewa na Mchungaji Ambilikile Mwasapila.

Akizungumza na Mwananchi jana, Lali, alisema kijiji hicho kitakusanya ushuru huo wa Sh 2,000 kwa ajili ya usafi na uboreshaji wa mazingira ya Samunge.

"Kulikuwa na kutoelewana tu, lakini uamuzi wa awali ulikuwa ni Sh2,000 kubaki Samunge kusaidia masuala ya mazingira na afya. Sasa baada ya kuelimishana nadhani limekwisha na watu wao wanashirikiana na halmashauri kukusanya ushuru," alisema Lali.

Alifafanua kwamba, fedha hizo zinazokusanywa ni za Serikali na zitapelekwa benki na baadaye Sh3,000 zitapelekwa kusaidia vituo vya magari na Sh2,000 zitapangiwa utaratibu na kijiji jinsi ya kutumika.
Vituo vya magari vitakavyonufaika na fedha hizo ni Bunda, Arusha, Babati na Longido.

Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Samunge, Michael Lengume alisema kutokana na uamuzi huo, jana wakusanya ushuru wa kijiji walikuwa wakishirikiana na wenzao wa halmashauri.


"Tayari tumeteua watu wetu wanakusanya ushuru. Imekubaliwa kuwa tutachukua pesa yetu Sh2,000 na hizo zao 3,000 watapeleka katika vituo vyao," alisema Lengume.

Mwandishi wa habari hizi alishuhudia wakusanya ushuru wa kijiji hicho Joel Ezekiel, Gadiel Mearo na Charles Kisida wakikusanya ushuru huo pamoja na ofisa wa halmashauri.

Tangu Aprili 6, mwaka huu, halmashauri ilianza kukusanya ushuru wa Sh5,000 kwa magari yanayoingia Samunge.
Awali, kijiji kilikuwa kinakusanya Sh2,000, lakini wakusanya ushuru wake waliondolewa na halmashauri kutokana na uamuzi wa kikao cha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Uratibu na Bunge), William Lukuvi na wakuu wa mikoa inayopakana na Ngorongoro, kwa kutaka kuanzisha mpango wa kuratibu na kutoa vibali vya magari yanayokwenda Samunge.

Vigogo wa Ikulu Kenya
wazidi kumiminika
Maofisa wa Ikulu ya Kenya wakiongozwa na Chifu Morijo Loita na familia zao ambao kwa pamoja ni 81, wamewasili jana kwa Mchungaji Mwasapila kupata kikombe.

Jana, msafara wa maofisa hao ulitua Samunge ukiwa na magari saba na mara baada ya kuwasili walijitambulisha na kuanza kupewa dawa.

Ujio wa maofisa hao unaelezwa kwamba huenda ukasababisha vigogo wengine kadhaa katika nchi za Afrika ya Mashariki na Kati, kufika Samunge kupata kikombe cha dawa kwa Mchungaji Mwasapila.

Juzi, baadhi ya wabunge wa Kenya na wagombea wa Useneta, walikwenda na wapigakura wao kwa mchungaji huyo kupata kikombe cha dawa.


Kwa mujibu wa Ofisa Uhamiaji aliyepo Samunge, Hussein Hamis idadi ya raia wa Kenya waliofika hapo sasa imefikia 2,429 hawa wakiwa ni wale tu waliojitambulisha rasmi.

Mmoja afariki dunia Samunge
Mtu mmoja amefariki dunia jana, kabla ya kupata kikombe cha tiba kutokana na kukaa muda mrefu bila ya huduma yoyote ya afya.

Foleni ya magari jana ilifikia zaidi ya kilometa 10, hali ambayo inatishia tena kutokea kwa vifo hasa kwa wagonjwa ambao hawana dawa za kutosha na chakula.

Kabla ya kuwekwa utaratibu wa kutoa vibali kwa magari yanayokwenda Samunge, watu 78 walifariki kabla ya kupata tiba kutokana na foleni kubwa na hivyo kuchelewa kupata kikombe na wengine kupata baada ya hali zao kuwa mahututi.
 
Back
Top Bottom