Azikwa akiwa hai kwa tuhuma za uchawi

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,299
33,082
Katika hali isiyokuwa ya kawaida wananchi wanaodaiwa kuwa na hasira kali wa kitongoji cha Itezi Magharibi kata ya Itezi katika Halmashauri ya jijini Mbeya, wamechukua uamuzi mgumu kwa kumzika akiwa hai mkazi mwenzao, Nyerere Kombwee, wakimtuhumu kwa uchawi.

Tukio hilo lililitokea jana katika Kitongoji hicho, ambapo wananchi hao walichukua uamuzi huo wakimhusisha Kombwee na kifo cha mtoto wa mdogo wake ambacho kimetokea katika mazingira ya kutatanisha.

Mashuhuda wa tukio hilo wakizungumza na NIPASHE Jumapili walisema wananchi hao walimkamata kwa nguvu marehemu huyo na kumlazimisha kuingia ndani ya kaburi lililoandaliwa kwa ajili ya kumzika mtoto huyo.

Mtoto huyo aliyefariki katika mazingira ya kutatanisha alifahamika kwa jina la Leonard Kombwee ambapo mtuhumiwa (Nyerere Kombwee) alipokubali kuingia ndani ya kaburi walimpiga na jiwe kichwani na hatimaye kumfukia akiwa hai.
Tukio hilo la kinyama la kumzika mtu huyo akiwa hai lilifanyika majira ya saa 3 asubuhi na haikufahamika alidumu kwa muda gani akiwa hai.

Polisi na viongozi hao wa kata walipofika eneo la tukio walianza kuwatawanya wananchi kwa risasi na kuamua kufukua kaburi hilo majira ya saa 8 mchana ambapo hata hivyo mtuhumiwa alikutwa akiwa amekufa.
Diwani wa kata ya Itezi, Frank Maemba, ambaye alikuwa eneo la makaburi kusimamia hali ya amani huku mwili wa marehemu ukiwa ndani ya kaburi hilo, alisema wananchi hawakupaswa kufanya tukio hilo kwa kujichukulia sheria mkononi.

Maemba ambaye pia ni Naibu Meya wa Jiji la Mbeya, alisema hata hivyo watu wote walioshiriki katika tukio hilo lazima watakamatwa na kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.

Askari waliochukua jukumu la kufukua kaburi hilo walilazimika kutupa mabomu ili kuwatawanya wananchi ambao baada ya kumzika mwenzao akiwa hai walibaki eneo hilo kusubiri kama ataweza kutoka ndani ya kaburi.
Askari hao walifika eneo hilo la tukio wakitumia gari aina ya Land Cruiser lenye namba za usajili DFP 474 na kuanza kuwatawanya wananchi kwa kupiga mabomu.

Baadhi ya wakazi wa mtaa wa Itezi walieleza kuwa tukio hilo limesababishwa na ugomvi wa kifamilia ambao umedumu kwa muda mrefu, ambapo inadaiwa marehemu Nyerere alikuwa akituhumiwa kumuua mtoto huyo wa kaka yake na ndipo wananchi wakaamua kulipa kisasi.
Walidai kuwa baada ya marehemu mtoto Leonard kufariki kwa utata siku ya Aprili 27 walimshuku marehemu baba yake mkubwa kwani hakwenda kwenye msiba.

Walisema baada ya kumfuata nyumbani kwake marehemu Nyerere alikutwa amejificha na walipo mbana mama yake alisema kuwa alikuwa amejificha ndani ya moja ya nyumba zake, hali iliyowalazimu kubomoa na kumshushia kipigo kikali wakimlazimisha kwenda kushiriki kuchimba kaburi la marehemu mtoto wa kaka yake.

Inadaiwa akiwa njiani Nyerere alitoa vitisho kwa wananchi hao akiwaonya kuwa kipigo walichompatia na kusababisha amwage damu hakitaenda bure.
Walimlazimisha kuingia ndani ya kaburi hilo na alipoingia tu mmoja wa wananchi hao alimpiga na jiwe zito kichwani huku mwingine akimkandamiza na Chepeo hali iliyosababisha kushindwa kujinasua na kufukiwa kirahisi akiwa mzima.
“Baada ya kuona mchanga unazidi kujaa huku akiwa amekandamizwa na chepeo, aligeuka na kulala kifudifudi hadi mchanga ukajaa kaburi,” alieleza mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo aliyeomba jina lihifadhiwe.

:: IPPMEDIA

CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

 
Unapokuwa na Serikali legelege inayoshindwa kusimamia mambo ya msingi ya kijamii (Elimu, Afya na Ustawi wa Jamii), tukio la aina hii si la ajabu!
 
Back
Top Bottom