Athuman Mlegeza: Wanaume msiogope kutahiriwa, ndoa zenu zi salama!

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,316
33,125
00000000000000000000000000000000000001aaaamzee.jpg
Athumani Mlegeza​
Na Festo Polea

WASWAHILI husema kazi ni kazi! Wengine husema kazi nzuri ni ile iliyouwezesha mkono kwenda kinywani.
Lakini, kwa bahati mbaya, baadhi ya wanajamii hasa wa siku hizi wamekuwa wakichagua kazi huku wengine zaidi vijana, wakidai kuwa hakuna ajira.Lakini, kwa upande wake, Mzee Athuman Mlegeza, mkazi wa Homboza, Kisarawe, Mkoani Pwani hachagui kazi.

Kutokana na kutochagua kazi, ndiyo maana akiwa na umri wa miaka 64, ameishi kwa kazi ambayo ni nadra kwa wengi kuitangaza hadharani.


Mzee Mlegeza kama anavyofahamika kwa wengi, anaeleza kuwa ameishi kwa kazi hiyo ya kuwatahiri watoto wa kiume na baadhi ya wanaume watu wazima ambao hawakufanya hivyo wakati wa utoto wao.

Anaeleza kuwa amekuwa akifanya hivi bila kificho huku akiunga mkono wito wa mashirika mbalimbali duniani likiwamo la Umoja wa

Mataifa la Kuhudumia Watoto (Unicef) na lile la kupambana na Ukimwi (UN-Aids), ambayo yamekuwa yakihiza tohara kwa wanaume katika nchi mbalimbali ikiwamo Tanzania kama juhudi za kupunguza maambukizi ya Ukimwi.

Lakini, anaeleza kuwa kazi ya kuwashawishi wanaume watu wazima kwenda kutahiriwa, imekuwa mtihani.

Mzee huyu anaeleza kuwa ameanzisha kampeni binafsi ya kuwataka wanaume hao kutoogopa kujitokeza ili kutahiriwa na kuweza kuepuka maambukizi ya magonjwa kwa urahisi.


Mzee huyo anasema mwanaume asipotahiriwa, kwanza ni aibu kwake mwenyewe, pili hatokuwa na uwezo wa kujiamini katika masuala ya mapenzi, pia hupata kirahisi magonjwa ya maambukizi.

Kitaalam, magonjwa mengi hujificha kirahisi katika ngozi ile inayotakiwa kukatwa na pia kubaki bila kutahiriwa ni uchafu kwa mwanaume.

Mzee Mlegeza ambaye ana umri wa miaka 64 anasema ameifanya kazi hiyo kwa takribani miaka 35 hadi sasa na tangu aianze amekumbana na changamoto nyingi, hasa za wanaume wengi kuhofia kutahiriwa kutokana na kutokuwa na elimu inayohusu faida ya kutahiriwa.


Anaeleza kuwa wengi wanahofia kuwa baada ya kufanyiwa kitendo hiki hasa katika umri mkubwa watashindwa kutumikia ndoa zao, jambo ambalo anasema si kweli.


"Tatizo kubwa ni ndoa watu wengi wenye umri mkubwa wanaogopa kutahiriwa tu kwa hofu kuwa hawataweza kushiriki tendo la ndoa kwa wake zao na pia hata kama wakiweza watadharaulika.


“Wengine wamekuwa na hofu kuwa wanapotahiriwa wanapunguzwa uume wao jambo ambalo pia si kweli na hii inatokana na kutokuwa na elimu kuhusu suala hili,'' anasema Mzee Mlegeza.


Anaongeza kuwa kutokana na kutokuwa na mwamko kuhusiana na faida za kutahiriwa kwa mwanaume kila mwaka idadi ndogo ya watu wazima wamekuwa wakijitokeza kutaka kutahiriwa naye.

Anasema idadi yao kwa mwaka mzima hufikia watano, lakini kwa vijana wa miaka saba hadi tisa hujitokeza kwa wingi kuanzia 15 hadi 20 kila mwaka.

Mzee Mlegeza anasema kwa watu wazima wanapotaka kutahiriwa hufika kwake kwa kuhoji namna wanavyofanyiwa huku yeye akieleza kuwa na ndugu yake anayehitaji kufanyiwa hivyo, lakini ana umri kama na baada ya kumweleza mambo mengi naye kuridhika na

kujikuta akijieleza kuwa yeye ndiye anayetaka huduma hiyo na baada ya makubaliano hupanga mahali pa kufanyia shughuli hiyo.

Anasema kwa watu kuna madhara kwa mtu mzima kutotahiriwa anaweza kutengwa akibainika na kukosa mwenza kwa kuwa wengi wao hawapendi wanaume wasiotahiriwa kwa kuwa wanaonekana ni wachafu katika maumbile yao.

Pia, ni rahisi kwao kupata maambukizi ya magonjwa nyemelezi kutokana na kuwa na ngozi inayoficha uchafu.

Anafafanua mzee huyo kuwa mwanaume anapotakiwa kutahiriwa hapunguzwi chochote kwenye maumbile yake ya uume, bali anakatwa ngozi ya mbele yenye kutunza uchafu na kuwa chanzo cha kuleta maambukizi ya magonjwa mbalimbali na kwa watoto hupona kwa muda wa wiki tu huku watu wazima wakitumia wiki mbili hadi tatu.

"Kazi zangu ni za kiasili hivyo nataka kuwahakikishia watu wazima wasiogope kutahiriwa kwani kwa muda wa wiki mbili kama watakuwa wameweza kujituliza bila kuwa na mihangaiko ya hapa na pale wataweza kupona kabisa na kufurahia tendo la ndoa tofauti na wanavyokuwa kabla kwani wakati mwingine wakiwa hawajatairiwa hukosa uhuru wa kufanya mapenzi na wenzi wao na wengi huhitaji giza ili kuficha aibu yao,'' anasema.


Anaongeza: "Kazi hii naifanya kwa siri sana kwa watu wazima hivyo wasihofu kuvuja kwa kuwa utaratibu wangu kwa anayehitaji kufanyiwa suna (tohara) ananipigia simu ama anakuja kwangu tunazungumza na baada ya kukubaliana nampa hifadhi ya maficho, ama naweza kwenda nyumbani kwake nikamtahiri huko huko na kwa muda wa wiki mbili anaweza kuomba ruhusa hata kazini mwake.''


"Nimeshawahudumia watu maarufu na wenye nyadhifa kubwa, lakini hadi leo ni siri yangu na wao na hakuna yeyote aliyesumbuliwa kwa kuwa kazi hii naifanya kwa nidhamu na siri kubwa kati yangu na mteja wangu hivyo wengine wasiogope kwa kuwa kufanya hivyo ni bora kwa afya zao na kuwafanya wajiamini zaidi wawapo katika tendo la ndoa na wenzi wao," anasema


Kwa upande wa hospitali, Mlegeza anaongeza kuwa huko huwa vigumu kwa watu wazima kujitokeza kwa kuwa tendo lenyewe ni la aibu, lakini na nafasi ni finyu ambapo kwa siku moja wanaweza wakatahiriwa watoto wachache, lakini yeye kwa kuwa anatumia vifaa vya asili na kwa uzoefu wa muda mrefu, hutumia mfumo wa kukusanya watoto katika vijiji na wanapofikia idadi kubwa huwaweka katika kambi na huko huwatahiri kwa pamoja.


Anasema kwa siku moja anaweza kutahiri watoto zaidi ya watatu na wote wanakuwa salama, anasema licha ya kufanya shughuli hiyo faida nyingine baada ya kuwafanyia tohara watoto hao huwafundisha stadi za maisha, hivyo wanapotoka hapo wanakuwa na mbinu ya kupambana na maisha.


Mzee Mlegeza anasema kazi yake ni kama urithi katika ukoo wao kutokana na kuanzia katika ukoo uliomtangulia ambapo yeye alifundishwa na kaka yake ambaye naye alifundishwa na baba yao mzazi, lakini naye aliwahi kushiriki mafunzo kwa kuongozana na baba yake kwa muda wa miaka 12 katika kazi hiyo hadi alipoanza kuifanya mwenyewe.

Hata hivyo, anafikiria kuikabidhi mikoba yake kwa mtu mwingine kuwa ameanza kupoteza uwezo wa kuona vizuri.

"Ni shughuli ngumu kama kwa kweli na yenye kutaka ujasiri, mtoto wangu anayeitwa Hamis Mlegeza haitaki kazi hii kwa kuwa ni mwoga, lakini mimi nimeizoea na ndiyo maisha yangu inaniingizia kipato napata chakula hivyo ni kazi nzuri kwangu kwa kuwa sijakumbana na matatizo yoyote tangu nimeianza hadi leo ninapoelekea uzeeni.


Kwa kweli binafsi nimefanikiwa katika kazi yangu hii kwani watu wazima hurudi baada ya kupona na kuniletea zawadi mbalimbali, ambazo hata hivyo anasita kuzitaja, mbali ya kueleza kuwa ameweza kujenga nyumba ya kisasa ya kuishi.

Athuman Mlegeza: Wanaume msiogope kutahiriwa, ndoa zenu zi salama!
 
Back
Top Bottom