Askofu Gamanywa amwalika waziri Pinda kwenye matembezi jumamosi ijayo

[h=2]Kikombe cha Babu chashindwa kutibu ukimwi[/h] Kikombe cha Babu chashindwa kutibu ukimwi

Paul Sarwatt;Arusha;3 Aug 2011; Toleo na 197

MACHI 20 mwaka huu, Mwenyekiti wa Mtandao wa Watu Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (TANOPHA+), Julius Kaaya alikuwa safarini na wenzake 14 wanaoishi na virusi hivyo kwenda kijiji cha Samunge, wilayani Ngorongoro, kupata tiba ya "kikombe" cha Mchungaji Ambilikile Masapila; maarufu kwa jina la Babu wa Loliondo.
Kaaya na wenzake walikuwa na imani kubwa kuwa huenda tiba hiyo ikawa ndiyo mwisho wa mateso na mahangaiko ya muda mrefu yanayotokana na kusumbuliwa na virusi vya ugonjwa huo hatari ambao hadi sasa dunia haijapata tiba yake.
Watu hao walikuwa wamesafirishwa kwa msaada wa shirika la (EACNASO) ambalo pia ni muungano wa mtandao wa mashirika yanayojishughulisha na ugonjwa huo kwa nchi za Afrika ya Mashariki lenye makao yake mjini Arusha.
Imani ya waathirika hao ilijengwa juu ya msingi kuwa dawa ya kikombe cha Babu kwa wakati huo ilikuwa gumzo kubwa nchini na viongozi mbalimbali wa serikali kutoka kada mbalimbali, kama mawaziri wa serikali, majaji wa Mahakama Kuu, wenyeviti wa vyama vya siasa, wakuu wa mjeshi na wananchi, walipigana vikumbo katika kijiji hicho kupata uponyaji wa maradhi yanayowasumbua kupitia tiba hiyo.
Baada ya safari ngumu ya siku moja na nusu kutokana na ubovu wa barabara, Kaaya na wenzake walifika Samunge na kupata tiba ya kikombe cha Babu; huku wakipewa siku 90 kama muda ambao virusi vitakuwa vimetoweka katika miili yao.
Aidha, majibu ya vipimo vya watu hao pia vilikuwa vinasubiriwa kwa hamu na makundi mbalimbali katika jamii kutokana na watu hao kujitangaza kuishi na virusi hivyo na kuwa tayari kuweka hadharani majibu ya vipimo vya hali zao.
Lakini miezi minne sasa tangu muda uliotolewa "kisayansi" na Mchungaji Masapila kuwa virusi vitakuwa vimeisha miilini mwao, Kaaya na wenzake wote waliotumia tiba hiyo wamevunjika moyo baada ya kupimwa upya na kuonekana kuwa bado wana virusi vya ugonjwa huo hatari.
Taarifa za wagonjwa hao kutopona virusi hivyo ilithibitishwa mwishoni mwa wiki na Kaaya mwenyewe alipohojiwa na Raia Mwema ambapo alieleza kusikitishwa kwake na hali hiyo.
"Ni kweli, baada ya siku tisini tumepima virusi mara tatu na majibu yanaonyesha kuwa wote bado tuna virusi vya ugonjwa wa ukimwi, na wala kiasi cha virusi bado hakijapungua mwilini", alieleza Kaaya.
"Matokeo hayo yamewavunja moyo baadhi ya wagonjwa ambao walikuwa na imani kuwa huenda wamepata tiba ya virusi vilivyokuwa vimewasumbua kwa muda mrefu pamoja na magonjwa nyemelezi", aliongeza Mwenyekiti huyo.
Hata hivyo, Kaaya ameitupia lawama serikali kwa kushindwa kuwalinda wananchi na kile alichokiita "uchezewaji wa afya za watu" uliofanywa na Mchungaji huyo mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT).
"Ni jambo la kusikitisha sana. Ilikuwaje Serikali ikaruhusu tiba ya aina hiyo ambayo haikufanyiwa utafiti wowote wa kisayansi na matokeo yake waliotumia hawajapona; huku wakiwa wameingia gharama kubwa sana kuifuata dawa hiyo kutoka maeneo mbalimbali ya nchi", alieleza Kaaya.
"Kilichowashawishi watu wengi wenye matatizo mbalimbali ni ile hatua ya viongozi wa serikali; hasa mawaziri, majaji,wakuu wa majeshi na viongozi wa vyama vya siasa kwenda Samunge kupata kikombe cha Babu.
Alisema kuwa jambo baya zaidi ni kwamba walikubali kupigwa picha na kuonyeshwa katika vyombo mbalimbali vya habari wakipata kikombe cha dawa hiyo. "Hiyo ilikuwa ni sawa na wao kutoa ushuhuda kuwa dawa hiyo inafaa."
Mara baada ya tiba hiyo ya Babu kutangazwa, mawaziri, baadhi ya wakuu wa mikoa, makamanda wa jeshi na wananchi, walifurika kwa mzee huyo wa Loliondo. Aidha, watoa tiba wengine wa vikombe waliibuka huko Tabora, Morogoro, Mbeya na Iringa na watu waliwaendea kupata dawa.
Baadhi ya mawaziri waliokunywa dawa hiyo ya mitishamba ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,Uratibu na Bunge), William Lukuvi, Waziri wa Ujenzi, John Magufuli, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Steven Wassira, Waziri Sophia Simba na Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige.
Viongozi wengine ni mawaziri wakuu wastaafu, Fredrick Sumaye na Edward Lowassa na wabunge ni pamoja na Nimrodi Mkono (Musoma Vijijini), Augustine Mrema (Vunjo), Rose Nyerere, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Yohana Balele na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Abbas Kandoro. Wengine ni IGP Omary Mahita, Mh Edward Hosea (PCCB),Makongoro Mahanga, Mary Chatanda (Arusha).
Aidha, viongozi kadhaa wa madhehebu ya dini kama maaskofu pia walikwenda Samunge kupata kikombe hicho cha Babu hali iliyotia hamasa wananchi wengine kumiminika kwenda Samunge.
"Ilikuwa makosa makubwa kwa viongozi wa serikali kwenda kunywa dawa hiyo wakati haijafanyiwa utafiti wowote wa kisayansi wa kuthibitisha kuwa ilikuwa na nguvu za kuponya", aliongeza Kaaya.
Mwenyekiti huyo wa mtandao wa watu wanaoishi na virusi vya ukimwi aliongeza kusema kuwa, ni ukweli ulio wazi kwamba dawa ya kikombe cha Babu haiponyi, na uthibitisho huo unaonekana kwa wagonjwa wote waliopata tiba hiyo wanaosumbuliwa na magonjwa mengine kama kisukari, shinikizo la damu, pumu na kifafa, na hakuna hata moja aliyepata kupona kabisa.
"Naendelea kutoa wito kwa Watanzania wenzangu wanaosumbuliwa na virusi vya ukimwi, hata kama wamekwenda Samunge kunywa dawa ya kikombe, wasiache kutumia dawa zao za hospitali; kwani wanaweza kupoteza maisha, na hali hiyo imeshawatokea wengi", alionya Kaaya.
Akizungumzia tiba hiyo, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Dk. Salash Toure, alikiri kuwa kisayansi hakuna uthibitisho wowote kuwa dawa hiyo inaponya maradhi yanayotajwa na Mchungaji Masapila.
"Bado taasisi za kiserikali zinazohusika zina fanya utafiti kuchunguza iwapo dawa hiyo inafanya kazi, lakini kwa sasa bado hakuna uthibitisho wa kisayansi kuwa dawa inaponya", alisema Dk.Toure.
Hivi karibuni Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hadji Mponda alikaririwa pia na gazeti moja la wiki akieleza kuwa hakuna utafiti wowote wa kisayansi uliothibitisha kuwa dawa za asili, ikiwemo tiba ya kikombe cha Babu wa Samunge, haina uwezo wa kutibu ukimwi.
Dk. Mponda alitoa kauli hiyo Jijini Dar es Salaam wakati anazindua Kituo cha Matibabu ya Wagonjwa wa Ukimwi na Mafunzo katika Hospitali ya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam wiki mbili zilizopita.
Dk. Mponda alisema wagonjwa wa ukimwi wanatakiwa kutumia dawa za kurefusha maisha (ARVs) na kuwataka waende kwenye vituo vya afya kupewa dawa hizo na kuongeza kuwa vituo vyote vya afya vinatoa dawa za ARVs lengo likiwa ni kuhakikisha kila Mtanzania mwenye tatizo la ukimwi anapata dawa hizo mahali alipo.
Akijibu madai yanayotolewa kuwa dawa yake haina uwezo wa kuponya maradhi yanayotajwa, Mchungajji Masapila akizungumza na Raia Mwema, juzi, kwa njia ya simu kupitia kwa mmoja wa wasaidizi wake, Paulina Lukas, alieleza kuwa wanaolalamika kuwa hawajapona ni wale wasiokuwa na imani.
"Tangu mwanzo Mchungaji alieleza wazi kuwa watakaoponywa ni wale wenye imani na Mungu. Kwa hiyo ambao hawajapona hawana imani, na pia hawakufuata masharti ya dawa; mojawapo ikiwa ni kuacha tabia ya ngono", alieleza msemaji huyo wa Babu.
"Kama hawajapona si makosa yetu. Tuliwaambia kabla kuwa katika tiba hii kigezo cha kwanza ni kuwa na imani, na hapa tuna uthibitisho wa kutosha wa watu walioponywa na maajabu ya dawa hii wakiwemo wagonjwa wenye virusi vya ukimwi", aliongeza.
Alisema watu hao wanaoishi na virusi vya ukimwi si wakweli; kwani kuna uwezekano kuwa wamepona, lakini wanashindwa kuweka wazi hilo kwa malengo ya kukosa fedha wanazopewa na wafadhili wa ndani na nje ya nchi.
"Unajua hawa wengi wanapata misaada ya kifedha kutoka kwa wafadhilimbalimbali wa ndani na nje ya nchi, sasa wakisema ukweli kuwa wamepona watakosa misaada hiyo. Sisi tunajua kuwa ukimwi ni mradi kwa baadhi ya watu", alisema.
Msaidizi huyo wa Mchungaji Masapila aliongeza kuwa kwa sasa wanaendelea kutoa huduma kama kawaida ingawa idadi ya magari imepungua sana tofauti na miezi ya mwanzo ya mwaka huu. "Ni hali inayotokana na sababu mbalimbali ikiwemo baadhi ya watu wabaya kupiga propaganda kuwa dawa hii haiponyi."
"Kwa sasa tunahudumia kati ya gari 30 hadi 50 kwa siku hasa kutoka nchi jirani za Kenya na Uganda na mikoa ya Kanda ya Ziwa tofauti na miezi ya mwanzo wa mwaka ambapo tulikuwa tunapokea wagonjwa kati ya 5,000 na 8,000 kwa siku,"alisema.
Mchungaji Masapila alianza kutoa tiba hiyo kuanzia Agosti mwaka jana baada ya kudai kuwa ameoteshwa na Mungu, na kuwa dawa hiyo inayotokana na mizizi ya mti aina ya "mugamuryaga" kwa lugha ya wa watu wa kabila la Wasonjo ambao ni wenyeji wa Samunge, ilikuwa ina uwezo wa kutibu virusi vya ukimwi.
Dawa hiyo inauzwa kwa kiasi cha Shilingi 500 kwa dozi ya kikombe kimoja ambacho mgonjwa anapaswa kunywa na hairuhusiwi kurudiwa. Wagonjwa wote hulazimika kuhudumiwa na Mchungaji huyo kwa mkono wake mwenyewe.
Baada ya kuonekana kuwa idadi kubwa ya watu wamejitokeza kupata tiba hiyo, Mchungaji Masapila aliwatangazia watu kuwa ameoteshwa tena na Mungu na kuongeza idadi ya magonjwa mengine sugu yanayotibiwa kwa dawa hiyo ambayo ni kisukari, shinikizo la damu, kifafa na pumu.
Hata hivyo, pamoja na umaarufu mkubwa aliopata Mchungaji Masapila na tiba yake ya kikombe, hadi sasa hakuna uthibitisho wowote wa kisayansi uliowahi kutolewa kuwa dawa hiyo ina uwezo wa kutibu maradhi yanayotajwa na Mchungaji huyo.
























Wednesday, 03 August 2011 22:59 0diggsdigg

Leon Bahati
ASILIMIA 78 ya watu waliotibiwa na Mchungaji Mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Ambilikile Masapila, walipona magonjwa yao.
Hiyo ni kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Taasisi ya Synovate kuanzia Mei 2 hadi 19, mwaka huu na kuwahoji watu 1,994 wenye umri zaidi ya miaka 18 maeneo mbalimbali nchini.Utafiti huo uliotolewa na Synovate kwa gazeti hili jana, unaeleza kuwa ni asilimia saba waliosema hawakupona wakati asilimia 15 walisema hawajui.
"Asilimia 78 ya waliotibiwa kwa kikombe cha Babu wa Loliondo, walisema wamepona magonjwa yaliyokuwa yanawakabili," inaeleza sehemu ya ripoti hiyo ya utafiti.
Utafiti wa Synovate umekuja wakati ambapo utafiti wa awali uliofanywa na serikali juu ya dawa hiyo ya Babu kuinyesha kuwa ina uwezo wa kutibu magonjwa sugu kama vile kisukari, saratani, moyo na Ukimwi.
Serikali ilisema bado inaendelea na utafiti zaidi juu ya dawa hiyo, ambao unaweza kuchukua muda wa hadi miaka mitatu ikizingatia kuwachunguza waliotibiwa na kiwango cha dozi, kulingana na aina ya ugonjwa.
Ripoti ya Synovate inaonyesha ingawa ni watu wengi wanaotamani kuponyeshwa dawa ya Babu, ni Watanzania wachache wenye uwezo wa kumudu gharama za kwenda Loliondo.
Asilimia 83 walisema ni vigumu kupata dawa ya mchungaji huyo maarufu kama Kikombe, huku asilimia 17 wakaonyesha hakuna tatizo la kumfikia.Hata hivyo, kati ya waliokwenda asilimia 25 hawakuwa tayari kutaja magonjwa waliyokwenda kutibiwa, wakati asilimia 24 walisema ni kisukari.
Magonjwa mengine na asilimia ya watu walioenda kutibiwa kwenye mabano ni moyo (22), Ukimwi (13), saratani (12), vidonda vya tumbo (7), pumu (5), magonjwa ya ngozi (4), maumivu ya miguu (4), kifua kikuu (3), maumivu ya tumbo (3), maumivu ya uti wa mgongo (2), maumivu ya kifua (2), macho (1) na waliokwenda bila tatizo maalumu (3).
Mchungaji Masapila alijijenga umaarufu mkubwa kuanzia mwanzoni mwa mwaka huu baada ya watu kutoka sehemu mbalimbali nchini na nchi jirani kujitokeza kwa wingi kupata tiba hiyo.
Hali hiyo ilisababisha baadhi ya ndugu kuwachukuwa wagonjwa wao waliolazwa hospitalini kuelekea kwa Babu, yapata kilomita 400 kutoka mjini Arusha.
Misururu mirefu ya magari ilijipanga kwenda kwa babu na kufanya watu kutumia hadi siku saba kupanga foleni ya kupata dawa.
Pia, utafiti wa Synovate ulizingatia kuwa kulikuwa na waganga wa jadi waliojitokeza kutoa tiba sawa na Masapila, lakini licha ya hali hiyo, asilimia 60 walikiamini Kikombe cha Babu.
Wengine waliojitokeza na asilimia za kuaminika kwa watu kwenye mabano ni Dogo Jafferi wa Mbeya (9), Magret maarufu kama Bibi wa Tabora (8), Subira Ali (4), Majimarefu (2), Sinkala wa Mbuyuni (2) na babu wa Moma Mtwara (2).





[h=2]Tiba ya Babu Imeleta Maafa - Chama Cha Madaktari[/h]
Tiba ya Babu Imeleta Maafa - Chama Cha Madaktari

clip_image001.jpg

Mchungaji Mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri
Tanzania (KKKT), Ambilikile Mwasapila
Chama cha Madaktari nchini (MAT) kimesema tiba inayotolewa na Mchungaji Mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Ambilikile Masapila, kwa njia ya "kikombe" kwa ajili ya kutibu magonjwa sugu, imeleta maafa makubwa kwa wagonjwa.

Makamu wa Rais wa MAT, Dk. Primus Saidia, alitoa tamko hilo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana suala zima la magonjwa yasiyoambukiza na tiba mbadala.

Alisema wagonjwa wengi baada ya "kunywa kikombe cha Babu" waliacha kunywa dawa za magonjwa yaliyokuwa yakiwasumbua na kusababisha wengi wao kupooza, kufa na wengine hali zao kuzidi kuwa mbaya, "Ni vyema wananchi walio wagonjwa wa shinikizo la damu, kisukari, anemia na magonjwa mengine wakafuata ushauri wa madaktari badala ya kulaghaiwa na wachache," alisema Dk. Saidia.

Alisema umma wa Watanzania umekuwa ukilaghaiwa kwa tiba mbadala na kuacha kutumia dawa za hospitali hivyo kuongeza ukubwa wa tatizo na wanapokimbilia hospitali tayari hali zao zinakuwa mbaya.

Dk. Saidia alisema ili dawa iweze kutumika hufanyiwa utafiti kwa kati ya miaka 10 hadi 15.

Naye Katibu Mkuu wa MAT, Dk. Richard Kabangira, ambaye ni daktari bingwa ya tiba wa Hospitali ya Rufaa ya Bugando, alisema, "Serikali yetu haisikilizi wana taaluma, mfano Babu wa Loliondo utafiti uliofanyika pale ni wa dawa kutokuwa na madhara kwa binadamu na sio kutibu magonjwa." alisema Dk. Kabangila na kuongeza, "Hospitali ya Rufaa ya Bugando ilipokea wagonjwa wengi wa kisukari baada ya kutoka Loliondo kufuatia wagonjwa hao kuacha kunywa dawa walizopewa hospitalini."

Alisema waliwasiliana na wanachama wao nchini kote kufuatilia hali za wagonjwa waliokuwa wamekwenda "kwa Babu kupata kikombe" na waligundua kwamba waliokuwa wanatumia dawa (ARV) za kufubaza virusi vya UKIMWI, shinikizo la damu, kisukari na hata saratani waliacha dawa baada ya kunywa kikombe cha Babu.

Alisema pamoja na watu kadhaa kutoa ushahidi kuwa wamepona kwa dawa hiyo, utafiti uliofanywa na MAT, umegundua kuwa hakuna hata mtu mmoja aliyepona baada ya kunywa dawa ya Babu.

Alisema watumiaji wa ARV walipungua kama ilivyo kwa hao wengine, lakini baada ya muda hali zao zilikuwa mbaya wengine walikimbilia hospitalini lakini kwa kuwa walikuwa wamevuruga mtiririko wa tiba, walipata madhara makubwa.

Dk. Kabangira alisema MAT ilimwandikia barua Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii juu ya hatari ya tiba ya Babu, na kutoa ushauri wao, lakini ulipuuzwa kwa sababu za kisiasa.

Kufuatia hali hiyo, MAT imetoa wito kwa Serikali na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuwaeleza wananchi ukweli ili wasiangamie huku wakieleza kusikitishwa kwao kutokana na tiba hiyo kutumika kisiasa.

Chama hicho leo kinafanya mkutano wao mjini Mwanza, suala la tiba ya Babu linatarajiwa kuibuka katika mkutano huo unaowakutanisha wanachama wake.

source: ippmedia
"I am the punishment of God... If you had not committed great sins, God would not have sent a punishment like me upon you."
 
Back
Top Bottom