Ardhi wagoma

Facts1

JF-Expert Member
Dec 23, 2009
307
28
Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Ardhi (Aru), jijini Dar es Salaam, jana walianza mgomo wa kuingia madarasani, huku jitihada za serikali Wilaya ya Kinondoni na utawala wa chuo hicho zikishindwa kuuzima.

Mgomo huo ambao haijulikani lini utaisha, unalenga kuishinikiza serikali kusikiliza kilio cha wanafunzi hao na kuweka sawa mambo matano, likiwamo la kutopata fedha za mkopo kwa ajili ya mwaka ujao wa masomo.

Mgomo huo ulianza saa 3:00 asubuhi, baada ya wanafunzi hao kugoma kuingia madarasani, badala yake walijikusanya ndani ya viwanja vya na kufanya maandamano mafupi hadi katika jengo la utawala wa chuo.

Maandamano hayo yaliyoongozwa na viongozi wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo hicho (Aruso), yalitawaliwa zaidi na matamshi yaliyokuwa yakitolewa na wanafunzi hao kupitia nyimbo, mabango na sauti za kawaida, yanayomuomba Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kwenda chuoni hapo kujionea matatizo na kusikiliza kilio chao.

Mbali na kumuomba Pinda suala hilo, matamshi mengine yaliyotolewa na wanafunzi hao, yalijikita katika kudai haki, kuwakataa baadhi ya viongozi wa idara za chuo, kukataa kuingia madarasani na kusifu juhudi za Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere.

Viongozi wa idara za chuo, ambao wanafunzi hao walisikika wakitamka hadharani kuwakataa, ni Dk. Evarist Liwa (Masomo ya Shahada ya Kwanza) na Dk. Acenati Chagu (Mshauri wa Wanafunzi).

Baadhi ya mabango yaliyobebwa na wanafunzi hao yalikuwa na ujumbe uliosomeka: “Pinda ondoa uozo Aru”, “No Dr. Liwa”, “Dk. Liwa hatumtaki”, “Say no to Dr. Liwa and Dr. Chagu”, “Ooh!! Mwl Nyerere umetuachia msalaba Aruso”.

Pia walisikika wakiimba: “Tumechoka na tunataka kuongozwa”, “Haki zetu tunataka”, “Tufunge milango”, “Hatuingii darasani mpaka kieleweke”, “Kama siyo juhudi zako Nyerere na Dk. Liwa angesoma wapi?”, Tunamtaka Mizengo Pinda”.

Wanafunzi hao walifika karibu na jengo la utawala na kuendelea kuimba nyimbo hizo, hali ambayo ilizua hofu kubwa miongoni mwa watu waliokuwa ndani. Hali hiyo iliwafanya baadhi ya watu waliokuwa ndani ya jengo hilo kuanza kutoka nje, kitendo, ambacho kiliwafanya wanafunzi hao kubadili matamshi na kuanza kuwazomea huku wakitamka: “Wanakimbia! Wanakimbia! Wanakimbia”, “Tufunge milango”.

Wakiwa katika eneo hilo, viongozi wao waliwaamuru kuketi chini ili kusikiliza nini wanachotaka kuwaelekeza muda huo, ambapo wote kwa pamoja walitii.

Baada ya kuketi na kutulia, Rais wa Aruso, Tegemeo Sambili, aliwaeleza kuwa kilichowafanya kufika eneo hilo, ni matatizo yao kushindwa kupatiwa ufumbuzi kwa wakati.

Hivyo, akawadokeza kuwa muda mfupi baada ya kufika eneo hilo, alipokea ujumbe kutoka kwa Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa Idris Mshoro kwamba, anataka kuzungumza na viongozi wa Aruso.

Hata hivyo, taarifa hiyo ilipingwa vikali na wanafunzi hao, ambao kwa pamoja walipaza sauti: “Hatutakiiiii!” na kuzua zogo kubwa eneo hilo.

Sambili hakuishia hapo, kwani baada ya zogo hilo kutulia, aliwadokeza jambo la pili kwamba, katika ujumbe aliopokea kutoka kwa Profesa Mshoro ulieleza pia kwamba, baadhi ya mambo wanayodai wataanza kutekelezewa Jumatano ya wiki ijayo.

Taarifa hiyo pia ilipingwa vikali na wanafunzi hao, ambao kwa mara nyingine kwa pamoja, walipaza sauti: “Tunamhitaji aje azungumze mbele yetu”.

Licha ya wanafunzi hao kutaka hivyo, viongozi wa Aruso walikubali wito wa Makamu Mkuu huyo wa Chuo na kwenda ofisini kwake, huku wakiongozana na timu ya waandishi wa habari. Hata hivyo, matumaini ya waandishi wa habari ya kushiriki kikao hicho, yalizimwa na Makamu Mkuu huyo wa Chuo, baada ya kueleza kwamba, hayuko tayari kuzungumza na viongozi wa Aruso kama waandishi watashiriki.

Waandishi walitoka nje ya kikao hicho, ambacho hata hivyo mwafaka baina ya Makamu Mkuu huyo wa Chuo pamoja na viongozi wa Aruso haukuweza kufikiwa.

Kwa mujibu wa Rais wa Aruso, Sambili, mwafaka baina yao ulishindikana, baada ya Makamu Mkuu huyo wa Chuo kukataa ushauri wao, uliomtaka atoke nje akazungumze na wanafunzi, badala ya kujifungia ndani na viongozi wao.

Sambili alisema walilazimika kumweleza hivyo kwa vile tayari walishawahi kuzungumza naye mara nyingi kuhusu matatizo yao, lakini hakuna lililotekelezwa.

Makamu Mkuu huyo wa Chuo aliendelea kugoma kutoka nje, kitendo ambacho kilichochea zaidi hasira za wanafunzi hao, ambao walivamia lango kuu la kuingia na kutoka katika jengo la utawala na kulifunga.

Mbali na hilo, pia walibandika mabango katika lango hilo yenye picha zinazoonyesha hali mbaya ya vyoo, bafu na maeneo mengine yakiwa machafu, huku yakiwa na ujumbe unaomuomba Pinda aende chuoni hapo.

Hali hiyo ilidumu hadi saa 7.00 mchana, ambapo Mkuu wa Wilaya (DC) ya Kinondoni, Jordan Rugimbana akiongozana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Kamishna Msaidizi (ACP), Charles Kenyela, kufika chuoni hapo.

Kamanda Kenyela alifika chuoni hapo akiwa ameongozana na askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) waliokuwa kwenye Land Rover ya polisi namba PT 1146, waliobeba silaha mbalimbali, zikiwamo bunduki za risasi za moto na mabomu ya kutoa machozi.

DC Rugimbana pamoja na Kamanda Kenyela, walifika katika jengo la utawala wa chuo na wanafunzi hao walikubali kuwafungulia mlango na baada ya kufunguliwa, waliingia na kwenda hadi katika ofisi ya Makamu Mkuu wa Chuo na kumshawishi kutoka nje kuzungumza na wanafunzi.

Saa chache baadaye, Rugimbana, Kamanda Kenyela pamoja na baadhi ya viongozi wa idara za chuo, walitoka nje huku wakiongozana na Makamu Mkuu huyo wa chuo na kusimama mbele ya wanafunzi walikokuwa wameketi.

Rais wa Aruso, Sambili, aliwaambia wanafunzi hao kuwa msimamo wao bado uko palepale, lakini akawaomba watulie na wawasikilize viongozi hao.

Wanafunzi walitii amri hiyo na Profesa Mshoro alisimama na kuwauliza: “Habari za mchana”, kauli ambayo iliwafanya wanafunzi hao kuanza kumzomea kiasi ambacho eneo zima likashindwa kusikilizana kutokana na mvumo mkali wa sauti za kuzomea.

Hali hiyo ilimfanya DC Rugimbana kwa kushirikiana na Sambili, kufanya kazi ya ziada kuwatuliza wanafunzi hao na kuwaomba wamsikilize Profesa Mshoro anachotaka kuwaeleza.

Profesa Mshoro alijaribu kuwafafanulia madai yao, huku akikatishwa mara kwa mara na sauti za ama kumpinga, au kumzomea au kurushiwa vijembe.

Hadi anahitimisha, wanafunzi hao walitoa matamshi yaliyoashiria kutoridhishwa na ufafanuzi wa madai yao.

DC Rugimbana aliingilia kati na kuwaahidi wanafunzi hao kwamba, atakwenda chuoni hapo leo na kisha atawachukua viongozi wa Aruso na kwenda nao kwenye mamlaka za nje ya chuo zinazoweza kushughulikia madai yao. Hata hivyo, wanafunzi hao walipinga suala hilo na kumweleza DC huyo, kuwa hawakubali aongozane na viongozi wa Aruso peke yao, bali kama ni kwenda kwenye mamlaka hizo, aende na wanafunzi wote.
 
Back
Top Bottom