'AIDS' siyo 'UKIMWI' Tutafute neno Mbadala ( Kwa hisani ya Facebook)

IsangulaKG

JF-Expert Member
Oct 14, 2010
706
386
Habari hii ni kwa Hisani ya Facebook page ya Dr.Isangula Ni vema wana JF Tujadili mawazo ya Daktari huyu. Inapatikana katika http://www.facebook.com/note.php?created&&note_id=117205398345042

Nilibahatika kutembelea kituo cha wanaoishi na VVU hapo Dar,ambacho kinajishughulisha na utoaji wa huduma kwa waathirika wa Ukimwi,na nilifurahishwa sana na mfumo wao ambao unaruhusu waathirika kuunda vikundi na kukutana aghalabu kila jumamosi na kujadiliana kuhusu maendeleo ya afya zao,kupata chakula cha pamoja na kujifunza mambo mapya ili mradi tu waendelee kuwa na afya bora kwa manufaa yao wenyewe,familia zao na taifa kwa ujumla.
Nasema nilifurahishwa na mfumo huu kwa sababu watu wenye tatizo la aina moja japo wanaweza kuwa katika hatua tofauti za uzito wa tatizo husika,wanakutana pamoja na kuongelea afya zao na kushauriana hasa pale mmojawao anapokuwa na tatizo.Kwa kawaida nilielezwa kuwa mara nyingi wanakuwa na mada mbalimbali kila siku,japo majadiliano yao wakati mwingine yanahusisha mabishano lakini baadaye atasimama mwenyekiti wa kikundi na kutoa tamko kwamba kama kuna mawazo tofauti ni vema wamtafute mtaalamu kuhusu tatizo husika ili aje afafanue jambo lililowafanya wapishane kimawazo na hapo wote watakubali na mtaalamu atatafutwa.
Kwa siku hiyo mada kubwa ilikuwa ni kuhusu neno la kiingereza yaani ‘AIDS' na neno la Kiswahili ‘UKIMWI'.Hoja mbalimbali zilitolewa huku wengine wakisema AIDS inamaanisha Ukimwi kwa Kiswahili wakati wengine wakipinga kuwa AIDS haimaanishi Ukimwi bali ni ugonjwa mmojawapo kati ya magonjwa mengi tu yanayoweza kusababisha Ukimwi.Najua hata wewe msomaji kwa aina moja au nyingine unaweza kushindwa kugundua nini msingi wa mabishano hayo.Ukweli ni kwamba majadiliano haya ni ya msingi sana kwani yanawakilisha kile ambacho watu wengi wanaamini kuwa ndicho sahihi.
Kwa kuwa muda mwingi nilikuwa kimya nikisikiliza hoja na si kwamba sikuwa na uwezo wa kushiriki katika mjadala huu bali nilitoa nafasi kwa wenye mjadala waendelee kwani kwa kiasi Fulani waliweza kunifunua akili yangu kuhusu nilichokuwa naamini hapo awali kwa sababu mfumo wenyewe ulinifanya niamini hivyo ,wakati huo wote mawazo yangu yalirudi miaka kadhaa huko nyuma ambapo raisi wa nchi ya Afrika ya Kusini ,mheshimiwa Thabo Mbeki alitoa kauli kuwa virusi vya ukimwi (HIV) havisababishi AIDS,watu wengi sana walimlaumu mheshimiwa huyu kwa kufikiria kuwa umeupotosha umma na dunia hasa ukifikiria cheo na heshima yake,lakini yeye aliendelea na msimamo wake na kama kawaida ya binadamu ,mmoja wetu anapokuwa na msimamo Fulani na akagoma kuubadili tunamuacha na hatimaye jambo hilo husahaulika.
Nikakumbuka tena wakati wa msiba wa Baba wa Taifa,mchungaji mmoja maarufu sana ambaye yuko makini sana katika kuhakikisha kuwa kila jambo linafuata sheria Bw.Christopher Mtikila alitoa kauli kuwa Baba wa Taifa alikufa kwa kuwa alikuwa na Ukimwi,kweli watu wengi sana walimlaumu sana mheshimiwa huyu kwa kuwa alifikiriwa kuwa kauli yake ni ya aibu na kashfa na swali hapa ni kwamba je ni kweli alistahili kulaumiwa kiasi hicho?
Mambo hayo yote yamenifanya niandike waraka au makala hii ambayo nimejitahidi kuchunguza kwa makini kile nitakachokiongelea.Labda sasa nianze kufafanua baadhi ya mambo.AIDS ni neno la kiingereza ambalo linamaanisha (Acquired Immuno-Deficiency Syndrome) na neno UKIMWI ni neno la Kiswahili linalomaanisha Upungufu wa Kinga Mwilini japo wengine wanahimiza kutumia neno Ukosefu badala ya Upungufu,japo ukweli ni kwamba ukikosa kinga mwilini hatima yako ni kifo kwa haraka sana hivyo ni neno upungufu lina maana zaidi.
Kwa ufafanuzi zaidi ,neno Acquired katika lugha ya kiafya linamaanisha tatizo au ugonjwa ambao umepatikana baada ya kuwa mtu amezaliwa yaani hakuzaliwa nao,kwani kuna tatizo ambalo mtu huzaliwa nalo na huitwa 'Congenital'.Hata hivyo neno hili hutumika hapa kuonyesha kuwa AIDS ni ugonjwa ambao mtu anaweza kuupata kutoka kwa mtu Fulani ambaye tayari ana virusi kwa njia yoyote itakayoruhusu damu ya mtu mwenye virusi kuifikia ile ya yule asiyekuwa navyo .Neno Immuno-Deficiency ni muunganiko wa maneno mawili yaani Immunity ambayo humaanisha kinga ya mwili dhidi ya magonjwa yanayoweza kuushambulia na Deficiency yaani upungufu,kwa hiyo neno immuno-deficiency ndilo lenye maana sawa na neno la Kiswahili la upungufu wa kinga mwilini (UKIMWI).Neno syndrome humaanisha mkusanyiko wa dalili zaidi ya moja au magonjwa zaidi ya moja,na hapa wataalamu walikuwa na nia ya kueleza kuwa unapokuwa na upungufu wa kinga mwilini ni rahisi kupata magonjwa mengine mengi ambayo sisi tunayaita nyemelezi.Kutokana na maneno yote haya neno AIDS kwa ujumla wake linamaanisha 'Upungufu wa Kinga Mwilini(UKIMWI) ambao mtu anakuwa hajazaliwa nao na ambao unahusisha magonjwa au dalili zaidi ya moja'
Kihistoria,Upungufu wa kinga mwilini(UKIMWI) umekuwepo muda mrefu sana hata kabla ya kugundulika kwa virusi vya AIDS.Mwanadamu amekuwa akikumbwa na aina nyingi sana za matatizo ambayo yamekuwa yakimsababishia upungufu wa kinga mwilini.Wataalamu wengi sana wamekuwa wakifikilia kuwa zipo aina nyingi sana za chembechembe za mwili ambazo huusika na kupigana na magonjwa yanayomshambulia binadamu,Kwa ujumla chembechembe nyeupe za damu (White blood cell) pamoja na chembe chembe nyingine kama lymphocytes,Neutrophils,Killer cells,Macrophages,Antibody,CD4,CD8,Helper T cells na chembechembe nyingine nyingi tu zilizo katika mwili wa binadamu zote zinafanya kazi ya kuukinga mwili wa binadamu dhidi ya magonjwa mbalimbali na iwapo kwa aina moja au nyingine chembechembe mojawapo itapungua inasababisha upungufu wa kinga ya mwili dhidi ya ugonjwa ambao chembechembe hiyo ilikuwa inaukinga.Kwa hiyo inaaminika kuwa mtu anapokuwa na ugonjwa kama kansa,Kisukari,Ugonjwa wa muda mrefu (chronic disease),na Virusi hasa virusi vya AIDS,Kifua kikuu,lishe duni(Malnutrition),Anaemia,Dawa za kansa (cytotoxic drugs),Dawa za allergy au za kupunguza kinga ya mwili (Steroids) kama vile Prednisolone,au kama atatumia dawa za antibiotics kwa muda mrefu sana zikaua normal flora na kutoa nafasi kwa vimelea wengine kukua kama vile fangasi ,yot haya yanasababisha upungufu wa kinga mwilini (UKIMWI).Kwa ujumla neno Ukimwi linawakilisha maneno mawili tu katika neno AIDS yaani immuno-deficiency huku likiyaacha maneno mawili yaani acquired na syndrome kuwa hayamo katika tafsiri yake.Kwa kiasi Fulani naweza sasa kukubaliana na hoja kwamba neno AIDS siyo Ukimwi bali ni mojawapo tu ya magonjwa yanayoweza kusababisha UKIMWI yaani upungufu wa kinga mwilini .
Tatizo lilopo hapa,hasa baada ya mhesimiwa yule kusema baba wa Taifa alikufa kwa Ukimwi ni kwamba kwa muda mrefu sana neno la kiingereza la Immunity Deficiency limetumika zaidi hasa katika Elimu ya afya na neno Ukimwi lilikuwa halijapata nguvu kubwa na hata kama lilikuwa likitumika pengine lilikuwa halipewi uzito sana kwa kuwa matatizo yaliyokuwa yakisababisha Ukimwi wakati huo yalikuwa yakionekana ya kawaida tu masikioni mwa watu.Neno hili Ukimwi limepata nguvu sana na kuonekana kutisha zaidi hasa miaka ya tisini baada ya AIDS kugunduliwa na kwa kuwa hakukuwa na muda pengine wataalamu wenyewe wa Kiswahili hawakuona umuhimu wa kutafuta neno lenye tafsiri sahihi ya AIDS kwa Kiswahili,wakaamua kutumia neno Ukimwi ambalo kwa mtizamo wangu si tafsiri sahihi ya neno ukimwi.Hii ndiyo maana matatizo yanajitokeza pale mtu mwenye kisukali au kansa anapoambiwa ana upungufu wa kinga mwilini yaani Ukimwi.
Najua jamii imeshalizoea sana neno ukimwi kama tafsiri ya AIDS,najua leo nikimwambia mgonjwa wa kifuakikuu kuwa ana upungufu wa kinga mwilini moja kwa moja atajua nimemaanisha AIDS,labda sasa nitoe wito kwa wataalamu wa Kiswahili wa baraza la Kiswahili la Taifa kututafutia tafsiri halisi ya neno AIDS ili kuondoa kutokueleweka kutakakojitokeza pale mtu anapokuwa na tatizo jingine linalosababisha upungufu wa kinga mwilini kama vile kisukali,Kansa,antibiotics kwa muda mrefu n.k napoambiwa ana upungufu wa kinga mwilini,Nina imani hii ni changamoto kwa wataalamu na wanazuoni waliobobea katika masuala haya ya AIDS kuwa na mjadala wa pamoja kuhusu suala hili.
Suala jingine ni kuhusu virusi vya Ukimwi (VVU) na neno HIV,kwa ujumla neno Human Inmmuno-deficiency Virus linamaanisha Virusi vinavyosababisha upungufu wa kinga katika mwili wa binadamu.Kwa harakaharaka naweza kusema bado neno hili pia lina matatizo kidogo japo si makubwa sana ukilinganisha na neno mama la AIDS na Ukimwi.Kama nilivyosema hapo awali virusi pia ni mojawapo ya vitu vinavyoweza kusababisha upungufu wa kinga mwilini mwa binadamu.Kwa mfano inafikiriwa kuwa virusi vinavyofanana sana na HIV yaani Retrovirus viliwahi kugunduliwa katika mnyama jamii ya Nyani katika maabara Fulani huko Ulaya,kwa hiyo ili kutoa tofauti kati ya virusi vya aina hii ya Retro virus inayopatikana kwa wanyama wengine na hii inayomwathiri binadamu ndiyo maana wataalamu wakaona ni vema kutumia neno HIV ili kuonyesha kuwa hivi ni virusi vinavyosababisha upungufu wa kinga mwilini wa binadamu.Kwa mantiki hiyo badala ya kusema tu Virusi vya Ukimwi basi ni vema tungesema virusi vya ukimwi katika mwili wa Binadamu.Hii nayo ni changamoto kwa wataalamu wanaohusika.Hata hivyo labda niongelee kidogo suala la Thabo Mbeki kuwa HIV haisababishi AIDS japo suala hili ni la kisayansi sana,hata hivyo unaweza kuona kuwa AIDS inaambatana na magonjwa au dalili nyingi ambazo hazisababishwi na HIV moja kwa moja.Kinachofanywa na virusi hivi ni kupunguza tu kinga ya mwili na kuruhusu mwili kushambuliwa na magonjwa mengine kama fangasi,bacteria n.k ambayo magonjwa hayo ndiyo yanayoweza kumuua mgonjwa na siyo AIDS yenyewe.
Mwisho,wale waliosoma na kukubaliana na mtazamo huu wanaweza kuwa chachu ya kuwafafanulia wenzetu kile nilichooleza.Hata hivyo ni wazi kuwa kwa suala hili lugha yetu ya Kiswahili imeonekana kuwa na mapungufu,hata hivyo bado tunayo nafasi ya kuweka mambo sawa japo itachukua muda mrefu.Tujikinge na HIV tusijekupata AIDS ili tusife kwa magonjwa nyemelezi.
MUNGU AWABARIKI
 
Mimi nakuchaguwa wewe uwe wa kwanza kulibadilisha hilo jina la (UKIMWI) tutafutie jina lingine litakalo owana na jina la Kiingereza yaani ('AIDS' ) haya Mkuu tusaide kubadilisha jina hilo la (UKIMWI) kazi kwako.
 
Upungufu wa Kinga Mwilini (UKIMWI) Kwa Kuambukizwa (Acquired) Uambatanao na Magojwa nyemelezi Synrdomes) Tafuta kifupisho chake
 
ni kweli kabisa kwani upungufu wa kinga mwilini unaweza ukasababishwa na sababu nyingi tu zikiwemo za kuzaliwa nazo(inheritated diseases), Autoimmunie diseases au za Kuambukizwa(Aquired) ambayo ndio mantiki mhimu kwa AIDS
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom