Ahadi Hewa Kwa Wafanyakazi Wa Umma

Ngekewa

JF-Expert Member
Jul 8, 2008
7,705
1,288
Bila mishahara, malimbikizo tutagoma-Wafanyakazi

Habari Zinazoshabihiana
• Madaktari Zanzibar wagomea mishahara 22.12.2007 [Soma]
• Reli ya Kati kumekucha, mgomo wanukia 11.03.2008 [Soma]
• Wafanyakazi Chuo Kikuu wacharuka 25.08.2006 [Soma]

Na Rabia Bakari

SHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) limewataka wafanyakazi na watumishi wa umma kugomea mishahara itakayolipwa bila malimbikizo na kuipa Serikali siku 14 kuhakikisha imelipa mishahara na malimbikizo hayo.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa TUCTA, Bw. Nestory Ngulla, alisema watumishi wote wa umma walitakiwa kuanza kulipwa mishahara mipya Januari mwaka huu, lakini kutokana na makubaliano yaliyofikiwa kati ya Serikali na TUCTA, ilikubaliwa ianze kulipwa Julai pamoja na malimbikizo ya kuanzia Januari.

"Tangu kima kipya kianze kulipwa, watumishi wa umma wameendelea kupokea mishahara ya zamani kwa makubaliano ya kuja kulipwa mishahara mipya pamoja na makato yao.

"Lakini inavyoonekana, Serikali haitalipa malimbikizo hayo, hivyo tunaona imeamua kwa makusudi kukiuka makubaliano. Tunawataka wafanyakazi wasipokee mishahara itakayolipwa bila malimbikizo, badala yake waende likizo," alisema na kuongeza:

"Tunaipa Serikali siku 14 kuhakikisha imelipa wafanyakazi mishahara yote na malimbikizo yake, vinginevyo tutachukua hatua za kisheria na tunaomba watumishi wa umma waunge mkono hatua hizo," alisema Bw. Ngulla.

Aliongeza kuwa Serikali mara kadhaa imekuwa ikikiuka makubaliano, kuvunja sheria kwa kufahamu kuwa ina nguvu, lakini baada ya kuchoshwa na vitendo hivyo, wafanyakazi wameamua kuchukua hatua kali.

"Serikali imekiuka makubaliano tuliyoyafanya, na inadhulumu haki za wafanyakazi, ukidhulumiwa unachukua hatua, nasi tutachukua hatua.

"Jeshi la wafanyakazi sasa litaonekana na kama lilisahaulika na kuonekana si lolote, sasa kwenye uwanja wa vita ndio tutaonekana, kwani tumechoka manyanyaso na tutatumia silaha moja tu, ni kuacha kufanya kazi, migomo na maandamano makubwa," alisema.

Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Bw. Gratian Mkoba, alisema sababu ilizotoa Serikali kwa kushindwa kulipa malimbikizo hawazikubali, hawazipokei na wala hawazitaki na kitakachofuata ni walimu kuacha kufundisha, manesi kuacha kutoa huduma na wafanyakazi wote wa umma kusitisha majukumu yao mpaka malimbikizo yatakapolipwa.

Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (TALGWU), Bw. Jackson Makongwa alisema kinachotakiwa ni viongozi kusema ukweli, kwani wamezidi kuudanganya umma kwa ahadi hewa ambazo hazitekelezeki.
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom