Afutiwa shitaka na kupewa la kuua mke

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
268
MKAZI wa Vingunguti, Rajab Paulo (35) aliyekuwa akishitakiwa kwa kosa la kuendesha gari kwa uzembe, amefutiwa mashitaka hayo na kufunguliwa shitaka la kumuua mkewe katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala.

Mahakama ilifuta shitaka hilo chini ya Kifungu cha Sheria Namba 98 cha Mwenendo wa Makosa ya Jinai, baada ya kupitia maelezo ya awali ya malalamikaji kabla hajafariki dunia na mashahidi wa tukio hilo.

Paulo, ambaye ni maarufu kwa jina la Magongo alifikishwa mahakamani hapo Desemba 20, mwaka huu akikabiliwa na shitaka la kuendesha gari kwa uzembe na kusababisha kifo cha mkewe, Asha Abdalah.

Awali, shauri hilo lilikuwa likisomwa na Hakimu Tarsila Kisoka na Mwendesha Mashitaka Naima Mwanga ambaye baada ya kupitia maelezo ya awali ya mlalamikaji kabla hajafariki na mashahidi walioshuhudia tukio hilo aliona lina mapungufu.

Mwanga alidai kuwa kutokana na maelezo inaonesha wazi kuwa mshitakiwa hakutakiwa kusomewa mashitaka ya kuendesha gari kwa uzembe, bali ni la mauaji kwa kuwa ushahidi unaonesha kuwa alidhamiria kufanya kitendo hicho.

Aliiomba mahakama kurudisha jalada hilo kwa Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Charles Mkumbo, ili lifanyiwe uchunguzi ndipo liliporudishwa na jana mshitakiwa
kusomewa shitaka la mauaji.

Akisoma mashitaka mbele ya Hakimu Tarsila Kisoka, Mwendesha Mashitaka Musa Gumbo alidai kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo Desemba 10, mwaka huu saa 2 usiku katika eneo la Vingunguti Faru.

Kwa mujibu wa Gumbo, kwa makusudi huku akijua kuwa kufanya hivyo ni kinyume cha sheria, mshitakiwa alimuua mke wake.

Mshitakiwa hakutakiwa kujibu shitaka kwa kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi za mauaji isipokuwa Mahakama Kuu.

Mshitakiwa alirudishwa rumande hadi Januari 10, mwakani kesi hiyo itakapotajwa tena.
 
Back
Top Bottom