Adui si Zitto, hatima ya CHADEMA

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
266
HUWA ninaguswa kwa namna ya pekee na matukio yanayoashiria kuibuka kwa migogoro isiyo na kichwa wala miguu ndani ya vyama vya siasa vya upinzani hapa nchini.
Mguso ninaoupata kutokana na hali hiyo huwa hainifanyi kamwe kusahau wa kupuuza ukweli kwamba, migogoro yenye tija hususan ile inayojengwa katika misingi ya mapambano ya nguvu ya hoja ni jambo la afya ndani ya taasisi yoyote.

Hata hivyo, wakati nikiliamini hilo kwa dhati, bado huwa natambua pia kwamba aina ya migogoro inayojengwa katika uzushi, fitina, majungu, kutojiamini na mambo yanayofanana na hayo ni chanzo kikuu cha kuporomoka kwa taasisi za namna hiyo.

Ni kwa sababu hiyo basi ndiyo maana ushahidi wa kihistoria katika taifa hili umekuwa ni mwalimu mzuri kuthibitisha kwamba, kasi ndogo ya kukua kwa mfumo wa vyama vingi nchini kwa kiwango kikubwa imechangiwa na kuibuka kwa mihemuko ya kisiasa ndani ya vyama vya siasa ambayo mara nyingi imekuwa haina mashiko.

Leo hii, miaka 18 na nusu tangu kuanza kwa mfumo wa kisiasa wa vyama vingi nchini, aina hiyo ya mihemuko ya kisiasa isiyo na msingi imepata kwa nyakati tofauti kuvukumba vyama viwili ya upinzani vya CUF na NCCR Mageuzi ambavyo laiti kama vingeweza kuiepuka hali hiyo, vingeweza vikawa katika ngazi nyingine tofauti na ile vilivyopo leo hii.

Hivi ni mchambuzi gani huru anayeweza akashindwa kutambua kwamba, hatua ya uongozi wa juu wa CUF ya kumtimua kutoka katika chama hicho mwasisi na mwenyekiti wa kwanza wa chama hicho, James Mapalala miaka ya mwanzo ya 1990 ni mzizi wa mkwamo wa chama hicho kwa upande wa Tanzania Bara?

Kwangu mimi, uamuzi ule wa CUF kumtimua Mapalala na viongozi wenzake wa juu wa chama hicho kwa sababu ya kile kilichobatizwa jina la usaliti wa kisiasa si tu uliwakatisha tamaa baadhi ya wapenzi wa mwanzo wa vuguvugu la siasa za vyama vingi, bali ulikwenda mbele zaidi na kukizorotesha chama hicho upande mmoja wa muungano.

Matokeo ya dhambi hiyo ambayo huenda ilifanywa kwa nia njema ndiyo ambayo ilikipa mwanya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na makachero wake kukitungia kila aina ya majina mabaya CUF.

Kosa hilo lilisababisha CUF kipachikwe majina kama vile ‘chama cha Wapemba’, ‘chama cha Waislamu’, ‘chama cha kibaguzi’ na mengine mengi ambayo yumkini hayakuwa yakifanana kwa namna yoyote ile na sera na itikadi zake.

Katika mazingira ya kushangaza na huku kikitumia makosa ya namna hiyo hiyo, CUF kilijiingiza kwa zaidi ya mara mbili katika mizozo ya kipuuzi ya namna hiyo hiyo pale kilipomtimua mmoja wa makada wake maarufu wa zama zile, Naila Jiddawi na miezi kadhaa baadaye kikamfukuza Mkurugenzi wa Habari aliyekuwa kipenzi kikubwa cha wanahabari miaka ya 1990, Ramadhani Mzee.

Matukio hayo yaliyofuatiwa na yale ya kutiwa misukosuko kwa viongozi wengine wa chama hicho kama Tambwe Hizza na baadaye Wilfred Lwakatare ukiyajumlisha pamoja unaweza ukaona namna chama hicho kilivyoshiriki kujiumiza pasipo kuwa na sababu za msingi.

Matokeo ya matukio ya namna hiyo ndiyo ambayo yamekipokonya chama hicho hazina kubwa ya mashabiki na wapenzi wakati katika majimbo ya Bukoba Mjini na Temeke kwa kuyataja maeneo machache tu ya mfano.

Makosa kama hayo ya CUF kwa zaidi ya mara moja yalipata kufanywa pia na NCCR –

Mageuzi ambayo kwa sababu ya mihemuko ya kisiasa isiyo na msingi kilijipalia makaa kwa kuzalisha mgogoro mkubwa wa ndani kilipoamua kumuingia kihuni Augustine Mrema ndani ya chama hicho na kisha kikajaribu kumng’oa kimizengwe shujaa wao huyo ambaye ghafla aligeuka msaliti.

Mhemuko wa kumkumbatia Mrema kishabiki na kumpa madaraka ya juu ya chama na kisha fursa ya kuwa mgombea urais kidikteta kabla ya kupanga njama za kumuangusha kwa hila si tu kwamba ilikitokea puani chama hicho, bali ilitikisa vuguvugu zima la upinzani lililoibuka mwaka 1995.

Hata kabla ya mtikisiko wa Mrema kung’olewa NCCR Mageuzi haujapoa, chama hicho kilijikuta kikilazimika kuendeleza dhambi yake ile ile ya kutafunana pale, James Mbatia alipojijengea mtandao wa siri ndani ya chama hicho na akatumia sanduku la kura za hila kumngoa madarakani aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho, Mabere Marando.

Makosa hayo ya NCCR Mageuzi yalishuhudia chama hicho kikipoteza ushawishi mkubwa kiliojijengea na kaburi la kifo chake likasilibwa vyema katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000 kilipojikuta kikiangushwa vibaya.

Kila wakati ambapo vyama vya CUF na NCCR- Mageuzi vilipofanya makosa hayo ya kisiasa, nyuma yake kulikuwa na ushawishi na ushabiki mkubwa ndani ya vyombo vya habari.

Hali hiyo ilisababisha wanasiasa waliokuwa wakiibua washindi katika kila kosa wajione wao ndiyo mashujaa waliofanikiwa kuwashikisha adabu wasaliti ambao kwa mtazamo wao walikuwa ndiyo wavurugaji wa kasi ya kukua kwa mfumo wa vyama vingi.

Kwa nyakati tofauti wanasiasa wa aina ya Mapalala, Jiddawi, Lwakatare, Tambwe, Mrema, Marando na wengine wengi wakaonekana kuwa ni wasaliti na wanasiasa ambao walipaswa kuadhibiwa.

Leo hii unapogeuka nyuma na kuviangalia vyama hivyo viwili na kutazama namna vilivyopoteza ushawishi wake kwa sababu tu ya mihemuko isiyo na msingi unaweza ukashindwa kupata jibu ni kitu gani hasa kinapita katika vichwa vya wanasiasa wetu hususan wale walio ndani ya vyama vya upinzani.

Lakini pengine mawazo ya namna hii huwa ni makali zaidi kwa watu kama mimi ninaposhuhudia mihemuko ya namna hiyo hiyo ikitokea ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) leo hii.

Kile kinachotokea ndani ya CHADEMA sasa katika sura inayoelezwa kuwa ni kosa la usaliti wa baadhi ya viongozi wa juu wa chama hicho dhidi ya misingi ya uwajibikaji wa pamoja kinaonyesha dhahiri kurejewa kwa historia ya kutafunana ndani ya vyama vya siasa vya upinzani.

Yumkini makosa ya kisiasa yanayoaminika kufanywa na wanasiasa wa kariba ya Zitto Kabwe na wenzake wengine ndani ya chama hicho yanaweza yakafananishwa kwa namna moja au nyingine na yale yaliyofanywa na wanasiasa wa aina ya Mapalala, Jiddawi, Mrema na wengi wengine wa kabla yao.

Pasipo kujali iwapo ni kweli Zitto ana makosa au la, CHADEMA inapaswa kutambua kwamba hatua zozote zitakachochukuliwa dhidi ya mwanasiasa huyo na wenzake wengine zinaweza kwa kiwango kikubwa kuathiri ukuaji wa chama hicho.

CHADEMA inapaswa kutambua kwamba, madhara yatakayotokana na maamuzi yoyote dhidi ya Zitto hayataathiriwa kwa namna yoyote na taswira ya ndani ya chama hicho au nje iwe ni ile inayomsuta au kumbeba mwanasiasa huyo.

Kwa sababu hiyo basi, viongozi wa juu wa chama hicho cha upinzani watapaswa kupima matokeo ya siku zijazo dhidi ya hatua zozote za kinidhamu walizopanga au watakazopanga kuzichukua dhidi ya Zitto leo au kesho.

Ili kuweza kufikia malengo yao, Mbowe, Dk. Slaa na wazee wa chama hicho watalazimika kutambua kwamba japokuwa Zitto anaweza akawa tatizo katika mitizamo yao, adui wanayepaswa kushughulika naye yuko nje ya chama hicho na kimsingi ni hatima ya CHADEMA siku zijazo kwa namna ile ile walipojifikisha CUF na NCCR- Mageuzi.
 
Ahsante sana kaka kwa mchango wako ambao ni chanya katika nyanja zote. Naunga mkono hoja.
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom