Abiria wateketea ndani ya basi

mdau wetu

JF-Expert Member
Apr 20, 2011
548
58
ABIRIA WATEKETEA NDANI YA BASI

VILIO, majonzi na mayowe jana vilitawala eneo lote la Misugusugu katika Barabara Kuu ya Dar es Salaam - Morogoro wilayani Kibaha mkoani Pwani, pale basi la Kampuni ya Deluxe lilipopinduka kisha kuwaka moto na kusababisha abiria zaidi ya 25 kuungua.Ajali hiyo ni mbaya zaidi ya zilizotokea hivi karibuni katika barabara hiyo kwani baadhi ya abiria waliteketea kabisa na kubaki majivu huku wenzao wachache waliowahi kutoka ndani ya gari hilo wakishuhudia, lakini hawakuweza kusaidia kuwaokoa.

Ajali hiyo lilitokea saa 9:00 alasiri na basi lililohusika na tukio hilo ni aina ya Volvo mali ya kampuni Diluxe, likitokea Dar es Salaam kwenda Dodoma.

Polisi wathibitisha
Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Ernest Mangu alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo ambayo alisema ni abiria 17 tu ndio walionusurika na kwamba kumi kati yao walipata majeraha ya kawaida wakati wengine saba walipata majeraha ya moto.

Kamanda Mangu alisema majeruhi wote walikimbizwa kupelekwa katika hospitali teule ya Tumbi, Kibaha .

Mangu alisema chanzo cha ajali hiyo ni kupasuka kwa gurudumu la mbele kulia la gari hilo ambalo baadaye lilipinduka na kutumbukia korongoroni na kuwaka moto ambao kila baada ya dakika chache ulionekana kuongezeka kuwa mkubwa kutokana na upepo mkali uliokuwa ukivuma muda huo wa alasiri.

"Kwa kweli hii ajali naweza kusema ni mbaya na inasikitisha sana maana ni abiria wachache tu ndio walioweza kuokolewa na wenzao zaidi ya 25 tunakadiria waliungua na kuteketea kabisa hadi kuwa majivu kutokana na moto uliokuwepo kuwa mkubwa sana,"alisema Mangu.

Alisema ajali hiyo kama ikilinganishwa na zilizotokea hivi karibuni mkoani humo, wao kama polisi wanakiri hiyo ya jana ni mbaya zaidi na inayosikitisha kwani idadi halisi ya abiria walioteketea haijajulikana na kwamba ofisi yake inafuatilia zaidi kujua idadi halisi ya abiria waliosajiliwa kwenye ofisi za basi hilo Ubungo Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa kituo cha televisheni cha Channel Ten, basi hilo lilikuwa limebeba abiria 42 kutoka Ubungo, lakini kukawa na taarifa kwamba huenda idadi hiyo ikawa imeongezeka kutokana na abiria wengine waliopandia njiani.

Kamanda wa Kikosi cha Usalama barabani, Mohamed Mpinga, alipoulizwa jana jioni alisema bado haikuweza kuthibitika mara moja idadi halisi ya waliofariki na majeruhi.
Mpinga ambaye alikuwa eneo la tukio alisema uchunguzi na juhudi za kufahamu idadi halisi ya vifo na majeruhi ilikuwa ikifanyika.



Mashuhusa wa ajali
Hata hivyo, taarifa zisizo rasmi zinaeleza awali, basi hilo liliondoka katika kituo kikuu cha mabasi Ubungo kikiwa na abiria 45, lakini walikuwepo wengine baadhi ambao walipandia njiani katika eneo la Kimara, Mbezi na Maili Moja Kibaha.

Kwa upande wao mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo alisema basi hilo lilikua kwenye mwendo kasi na lilipofika eneo hilo walisikia kishindo kikubwa na walipofuatilia waliona basi hilo likitumbukia kwenye mtaro mkubwa pembezoni mwa barabara huku moshi mkubwa ukifuka kutoka ndani ya gari hilo.

''Sisi kama kawaida yetu tulikua kijiweni na hili basi lilitupita kwa kasi hapa, lakini muda mfupi tulisikia kishindo na tukatoka na kufatilia, tukagundua ni ajali, tulianza kukimbilia kuokoa watu, lakini masikini tulifanikiwa kuwatoa 10, moto ukawa umetuzidi nguvu. Wengi wakawa wanalia kuomba msaada,”alisema Ramadhani Hussein na kuongeza:,

Shuhuda mwingine, Adam Sultan alisema chanzo cha ajli hiyo ni uzembe wa dereva ambaye alikuwa akijaribu kulipita gari lililokuwa mbele yake hali eneo hilo halistahili kufanya hivyo kwa kuwa lina mlima.

Kwa upande wa shuhuda Abdallaha Kijukuu alisema kuna uwezekano mkubwa kwamba ajali hiyo imesababishwa na mtarimbo unaoshika matairi ya nyuma (diff), kwamba ilikuwa imepata moto kisha kusababisha gari hilo kupinduka.Mashuhuda hao walisema baada ya ajali hiyo kutokea, waliamua kusogelea gari kwa ajili ya kuokoa watu, lakini walikuta vioo vyote vimefungwa hivyo walianza jitihada za kuvipasua ili kuokoa watu hao.

Alisema walifanikiwa kuokoa majeruhi 8 na wengine walitoka wenyewe na kukimbia eneo la tukio wakati gari likifuka moshi.

Majeruhi anena
Mmoja wa majeruhi wa ajali, Danda Juju alisema kwamba huenda kukawa na zaidi ya abiria tisa waliungua ndani ya basi hilo. ,” Nilitokea dirishani na nikaanza kuokoa baadhi ya watu kupitia madrisha mawili tu, moto ulipozidi sikuweza kuendelea, lakini kwa haraka nadhani kama watu tisa watakuwa wameteketea ndani kwa moto,” alisema Juju ambaye ni kada wa NCCR-Mageuzi
Kwa upande wake, Juju alisema ameumia kwenye mguu na mkonono, lakini hali yake haikuwa mbaya sana hivyo aliweza kurejea nyumbani kwake Dar es Salaam.
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom