Nakumbuka ilikuwa ni mwaka 1976 wakati nilipokuwa JKT, tuliambiwa tuchague jina la chama kipya kitakachotokana na muungano kati ya ASP na TANU. Vikao kama vile vilifanyika na baada ya hapo tukaambiwa kuwa jina la chama litakuwa Chama Cha Mapinduzi, na mboni zake ni jembe na nyundo kuashiria kinawakilisha wakulima na wafanyakazi. Tuliamini sana chama hicho na wengine tulikuwa tayari kufa kupigania sera na maadili ya chama hicho, maadili ambayo tulikuzwa nayo na yalitekelezwa kwa vitendo.
Kwa bahati mbaya sana, nasikitika kusema, kile chama ambacho kilitulea, ambacho kilikuza na kuumba fikra zetu (ambazo ndizo zinazonifanya niandike haya,) chama hicho kimegeuzwa na watu wachache wapendao uchu wa madaraka, wanaojilimbikizia mali na kukuza usultani. Chama hicho kimegeuka kuwa jini subiani ambalo limeenda kinyume na muelekeo wa kile chama tulichokuwa tunakijua na kuanza kunyonya damu ya Watanzania. ccm (sikukosea spelling), imekuwa kama cancer itokanayo na chembechembe nzuri za mwili wa binadamu, na kugeuka chembechembe mbaya ambayo inakula mwili huo huo. Matokeo yake ni cancer ambayo tusipoiondoa mapema, hakika itatuangamiza sote.
Najua kuwa wote ambao mnaotetea cancer hii mnafaidika nayo kwa njia moja au nyingine, hamna uchungu na mamilioni ya wananchi wanaosota na kutokuwa na matumaini ya siku za mbele, kwani wao wanaishi tu bora siku ipite...wanaishi maisha kama ya wanyama. Lakini wananchi wa Tanzania sio wanyama, ni binadamu wenye akili. Kuna siku, na siku hiyo inakuja, watatwaambua wabaya wao na kuwatoa madarakani. Wabaya hao sio tu kwamba watatolewa madatakani, bali pia watawajibishwa kwa matendo yao maovu waliyowafanyia Watanzania kwa kisingizio cha CHAMA CHA MAPINDUZI kilichoanzishwa mwaka 1977.
Sijui unaishi kwa hisia za rangi, lakini kila mtu ana rangi aipendayo, au katika jamii yake, rangi hiyo inaashiria nini. Binafsi, baada ya kuona unafiki unaofanywa na ccm dhidi ya Watanzania, kila nikiona hiyo rangi ya kijani nasikia kichefuchefu. Nikifungua tovuti nikiziona hizo rangi walizovaa wakinadi uongo kwenye majukwaa, nafunga tovuto hizo haraka.
Kama una hata chembe moja ya utu, utaacha kuishabikia ccm na kuiondoa madarakani, kabla haijakuangamiza hata wewe mwenyewe!
Follow Us Here