Support JamiiForums and Become a 'JF Premium Member' | Click HERE for Details
    Show/Hide This

    Topic: Kupita bila kupingwa - this too is democracy?

    Report Post
    Page 3 of 8 FirstFirst 12345 ... LastLast
    Results 41 to 60 of 156
    1. #1
      Mzee Mwanakijiji's Avatar
      JF Senior Expert Member Array
      Join Date : 10th March 2006
      Location : Kijijini
      Posts : 29,513
      Rep Power : 46713
      Likes Received
      16404
      Likes Given
      8461

      Default Kupita bila kupingwa - this too is democracy?

      BARUA YA WAZI KWA MWENYEKITI WA TUME YA UCHAGUZI YA TAIFA


      WALIOPITISHWA BILA KUPINGWA HAWASTAHILI KUWA WABUNGE BILA YA KUCHAGULIWA


      Kuna kundi la wagombea ambao hadi hivi wanaamini kuwa wao ni wabunge halali wa Jamhuri ya Muungano na hivyo wanasubiri siku ya kuapishwa ili wachukue nafasi zao Bungeni. Wagombea hawa hadi hivi wanajiona ni wabunge wateule kwa sababu katika majimbo yao hakukuwa na upinzani na hivyo wao “wamepita bila kupinga”. Jambo hili limerudiwa na vyombo vingi vya habari na hadi hivi sasa karibu majimbo 20 yanao watu wanaojulikana kuwa “wamepita bila kupingwa”.

      Jambo hili ni kinyume na Katiba, linatishia demokrasia, linanyang’anya wananchi haki ya kujichagulia viongozi wao na ni msingi wa kuendeleza utaratibu wa watu kutumia ujanja, ulaghai na hata vitisho na unyanyasaji ili wapite “bila kupingwa”. Mheshimiwa Mwenyekiti ninaandika barua hii kuelezea kuwa watu hawa wote bila kujali majina yao, sifa zao, au vyama vyao hawana haki yoyote ya kuingia katiba Bunge la muungano kama “wawakilishi”.

      Kwanza, Katiba yetu haitambue Ubunge wa “kupita bila kupingwa”. Ibara ya 66 ya Katiba yetu iko wazi juu ya aina ya wabunge ambao wanapaswa kuwepo Bungeni. Naomba niinukuu jinsi ilivyo (msisitizo mweusi sehemu zote ni wangu):

      66.-(1) Bila ya kuathiri masharti mengine ya ibara hii, kutakuwa na aina zifuatazo za Wabunge, yaani-
      (a) Wabunge waliochaguliwa kuwakilisha majimbo ya uchaguzi;
      (b) Wabunge wanawake wa idadi inayoongezeka, kuanzia asilimia ishirini ya Wabunge waliotajwa katika aya ya (a), (c ) na (d), itakayotajwa mara kwa mara na Tume ya Uchaguzi kwa taarifa iliyochapishwa katika Gazeti la Serikali baada ya kupata kibali cha Rais, watakaochaguliwa na vyama vya siasa vinavyowakilishwa Bungeni, kwa mujibu wa ibara ya78, na kwa kuzingatia masharti ya uwiano wa uwakilishi baina ya vyama hivyo;
      (c) Wabunge watano waliochaguliwa na Baraza la Wawakilishi kutoka miongoni mwa wajumbe wake;
      (d) Mwanasheria Mkuu;
      (e) Wabunge wasiozidi kumi walioteuliwa na Rais kutoka miongoni mwa watu wenye sifa kwa mujibu wa ibara ya 67, isipokuwa sifa iliyotajwa katika ibara ya 67(1)(b).

      Mheshimiwa Mwenyekiti, Katiba yetu inatambua Ubunge wa aina tatu tu: Ubunge wa kuchaguliwa, Ubunge wa kuteuliwa na Ubunge wa Mwanasheria Mkuu. Wale wa kuchaguliwa wanaangukia katika makundi makubwa matatu: Waliochaguliwa majimboni, waliochaguliwa kwa uwiano wa uwakilishi wa vyama (katika viti maalum) na wanaochaguliwa na baraza la wawakilishi. Wabunge wa kuteuliwa ni wale kumi tu ambao Rais anaweza kuwateua. Na yupo Mbunge mmoja (Mwanasheria Mkuu) ambaye anaingia kutokana na wadhifa wake huo.

      Hivyo, hakuna mtu anayeweza kuingia Bungeni bila ya kuchaguliwa au kuteuliwa kwa namna fulani.

      Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na ukweli huo kuwa Katiba ambayo ni sheria mama ya nchi yetu kutambua kuwa wabunge ni wa aina hizo tu na kwa vile wengi zaidi kati yao ni wale wa kuchaguliwa katika majimbo basi tuna budi kuhoji wale ambao wamepitishwa kama wagombea pekee ambao wanasubiri “kuapishwa” kuwa wabunge katika majimbo yao wanaweza kudai kweli kuwa “wamechaguliwa” kuwa wawakilishi wa majimbo hayo kama hawajapigiwa kura ya aina yoyote? Je kweli tunaweza kusema kuwa “wamepita bila kupingwa” wakati wananchi wote wa majimbo hayo hawakupewa nafasi ya kupinga au kuwaunga mkono kwa namna yoyote ile? Jibu la maswali yote hayo ni “hapana” yenye kupiga kelele kwa sababu Katiba yetu haitambui ubunge wa “kupita bila kupingwa”

      Naomba kwa heshima na taadhima uniruhusu nielezee kwanini wananchi wenzetu hawa hawaruhusiwi, hawapaswi na hawatakiwi kukubalika kuwa wabunge bila ya kuchaguliwa na wananchi wao kwa namna moja au nyingine.

      Kwanza, walichofanya hadi hivi sasa wagombea hawa ni kupitishwa kuwa wagombea pekee katika majimbo yao na siyo kuchaguliwa. Kupitishwa kuwa mgombea pekee si sawa na kuchaguliwa kwa asilimia 100. Kukosekana kuwepo mpiznani haina maana hata kidogo kuwa huyo mgombea mmoja anakubalika na amechaguliwa na wananchi wote. Hivyo, hadi pale wananchi watakapomchagua kwa asilimia mia moja au zaidi ya asilimia ya wale wanaomkataa mgombea huyo hajachaguliwa na hivyo hatimizi sharti la “kuchaguliwa” katika Ibara ya 66:1(a).

      Pili, kwa mujibu wa Ibara ya 63:2 ya Katiba yetu “Sehemu ya pili ya Bunge itakuwa ndicho chombo kikuu cha Jamhuri ya Muungano ambacho kitakuwa na madaraka, kwa
      niaba ya wananchi, kuisimamia na kuishauri Serikali ya Jamhuri ya Muungano na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa Katiba hii.” Kama ni kweli kuwa Bunge ndicho chombo kikuu cha Jamhuri yetu “kwa niaba” ya wananchi itaweza vipi kuwa hivyo endapo baadhi ya wajumbe wake wanaingia Bungeni bila ya kuchaguliwa na “wananchi” hao isipokuwa kutokana na “utaratibu wa kiufundi”? Hivi hawa watakapoenda huko Bungeni wataenda kweli kwa “niaba ya wananchi” bila ya kuchaguliwa kwa namna moja au nyingine?

      Tatu, kwa mujibu wa Ibara ya 21 ya Katiba yetu wananchi wanayo haki ya kushiriki katika utawala wa nchi yao kwa moja kwa moja au “kwa kupitia wawakilishi
      waliochaguliwa na wananchi kwa hiari yao, kwa kuzingatia utaratibu uliowekwa na sheria au kwa mujibu wa sheria.” Ni wazi kwamba kwa kukubali watu waliosimama peke yao kuwa ndio wawe “wawakilishi” wa wananchi bila ya “kuchaguliwa” kwa namna yoyote ni uvunjaji mkubwa wa haki hiyo na ni kufungulia mtindo wa watu kujiingiza katika madaraka makubwa bila ya kuchaguliwa. Katiba hairuhusu wawakilishi wa wananachi wawe wale wa “kupitiba bila kuchaguliwa”. Ni lazima kwa namna moja au nyingine wachaguliwe.

      Nne, kwa kuruhusu baadhi ya watu wapate ubunge kwa njia ya mkato (yaani bila ya kuchaguliwa) ati kwa sababu hakuna mgombea mwingine wa chama “kingine” tunaingiza na kuendeleza utaratibu mbovu kabisa katika demokrasia ambapo watu wenye uwezo au wajanja wanaweza kusababisha wagombea wengine wasijitokeze ili wabakie “peke yao” wakiamini kuwa kwa kufanya hivyo wataweza kuupata Ubunge bila kupigiwa kura na wananchi wao. Hii ni hatari kwa demokrasia.

      Tano, kwa kuingia Bungeni bila kuchaguliwa kwa namna yoyote watu hao watakuwa wamekosa uhalali wa kuitwa “wawakilishi” na hivyo yote watakayoyafanya hata kama yana uzuri wa aina zote yanakosa msingi wa uhalali kwa sababu hakuna mwananchi hata mmoja wa majimbo hayo aliyewachagua. Kwa kuwaruhusu kuingia Bungeni tunaruhusu utawala wa kujipachika na siyo wa kuchagulika. Kama hawakuchaguliwa na wananchi wa majimbo yao, watu hao wanamuwakilisha nani zaidi ya maslahi yao na ya vyama vyao tu? Ni lazima wachaguliwe.

      Sita, uchaguzi wa namna yoyote ile unawapa watu nafasi ya kukataa. Demokrasia hujengwa pale ambapo nafasi ya kukataa inakuwepo na inaweza kutumika. Kwa kuruhusu baadhi ya watu “wapite bila kupingwa” tunaondoa haki ya kidemokrasia ya wananchi wa majimbo ya watu hawa kuweza kukataa. Si lazima wawakatae kabisa lakini ni lazima nafasi ya kukataa (dissent) itolewe. Kwa kuwapitisha ndugu zetu hawa kuwa ni wabunge wanaosubiri kuapishwa tu, tunaondoa utaratibu wa demokrasia wa wananchi kutoa sauti yao. Hili ni jambo kubwa zaidi kwangu kwani nchi kama ya kwetu inayojaribu kujenga demokrasia ikikubali kuwa sauti ya mamilioni ya wananchi isisikike iwe kwa kukubali au kwa kukataa tunakaribisha ubabe wa watu wachache.

      Saba, toka zamani hata katika mfumo wa chama kimoja tuliwapa nafasi wananchi kuchagua wabunge wake aidha kwa kuwashindanisha na mgombea mwingine ndani ya chama hicho au kwa kuruhusu ipigwe kura ya ndio au hapana. Iweje leo tukubali tu kuwa katika demokrasia tunaruhusu watu wapite tu “bila kupingwa”. Hata Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere angeweza kabisa kuwa rais bila kuchaguliwa wakati alisimamishwa kuwa mgombea pekee, lakini katika udhaifu wetu wa demokrasia wananchi bado walipewa nafasi ya kumkataa. Hakuna wakati wowote ambapo Nyerere aliweza kushinda urais kwa kupata kura za asilimia 100. Kama katika mfumo wa chama kimoja tuliruhusu watu hata wapigie kura jogoo na jembe, iweje letu hata uchaguzi huu muhimu tuwanyime wananchi wetu?

      Nane, hawa wanaotajwa kuwa wamepita bila kupingwa ni kwamba hawakuwa na mpinzani wa kushindana naye kwenye kugombea nafasi hiyo na siyo kwamba wamepita kuwa wabunge. Mchakato ambao umewaacha wao kuwa peke yao haukuwa na lengo la kutoa wabunge bali 'wagombea ubunge'. Hivyo, kwa usahihi hawa wanatakiwa kuwa ni "wagombea pekee" na siyo "waliopita bila kupingwa". Kwa vile ni wagombea pekee basi wananchi lazima wapate haki ya kuwakubali au kuwakataa kwa kuwapigia kura.

      Tisa, kinachotokea sasa hivi ni kutafsiri kura za maoni za CCM kuwa ni kura za uchaguzi. Kwamba, kwa vile mtu kashinda kura za maoni na sasa hana mpinzani wa kugombea naye kwenye kura za wananchi wote (uchaguzi mkuu) basi mtu huyo amechaguliwa kuwa mbunge. Hii si kweli. Kura za maoni za watu wa chama kimoja hata kidogo hazipaswi na hazitakiwa kuchukuliwa kama ni kura za wananchi wote. Wana CCM walipopiga kura walikuwa hawachagui Mbunge na si haki kuwapa watu wa chama kimoja tu uamuzi wa mwisho wa nani anakuwa mbunge wa jimbo fulani. Hivyo, ni lazima hao wagombea waletwe kwa wananchi wote ili wao wananchi - wale wasio wana CCM na wale wana CCM waliomkataa kwenye kura za maoni- wapate nafasi ya kusikika uamuzi wao.

      Kumi, kwa makusudi sijagusia suala la sheria ya uchaguzi au hata taratibu ambazo zimeruhusu hali hii kuendelea. Sababu kubwa ni kwamba Ibara hiyo ya 66 ya Katiba haitoi mwanya au nafasi hata chembe ya kupitisha sheria itakayosababisha watu waingie Bungeni bila kuchaguliwa kwani maneno yake yako wazi kabisa kuwa ni lazima wabunge wanaotoka majimboni wawe ni "wa kuchaguliwa" tena kama inavyosema katika sehemu nyingine kuwa "kwa hiari". Waliopita bila kupingwa wakiwa wabunge watakuwa hawajachaguliwa na wananchi hawakupewa hiari yao kutumia kuwachagua. Hivyo, utaratibu au sheria yoyote yenye kuruhusu hilo haina msingi katika Katiba, Mantiki na haki za wananchi.

      Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wazi kuwa bila ya kuchaguliwa au kuteuliwa mtu hawezi kuwa Mbunge. Kwa vile kuna kundi la watu ambao wamepitia na kuwa wagombea pekee katika majimbo yao baada ya vyama vingine kwa sababu mbalimbali kushindwa kusimamisha wapinzani basi ni lazima Tume yako iweke utaratibu ili watu hawa wapigiwe kura na kuchaguliwa ili wapate uhalali wa kuingia Bungeni. Ni lazima wananchi hawa wanaotaka kuwawakilisha wananchi walazimishwe kurudi kwenye majibo yao wauze sera zao wa kwa wananchi na kutoa nafasi kwa wananchi kuwahoji na kuwapinga. Lakini zaidi vile vile ni muhimu sauti tofauti nayo ipewe nafasi ya kusikilizwa kwani kama kuna watu ambao wangependa kuelezea kwanini watu hao wasichaguliwe au chama hicho kisichaguliwe basi ni lazima sauti hizo zipewe nafasi hiyo kwa njia ya kawaida ya kampeni.

      Hivyo basi, naomba kutoa pendekezo jepesi kabisa kuwa wagombea wote waliopitishwa kuwa wagombea pekee katika majimbo yanayokaribia ishirini wapigiwe kura ya “ndio” au “hapana” katika majimbo hayo. Kwa kufanya hivyo wananchi wa majimbo hayo watatumia nafasi yao ya kuwachagua wawakilishi wao na siyo wagombea hao wajipeleke vifua mbele huko Dodoma ili waapishwe kuwa wabunge wakati hakuna kura hata moja iliyopigwa kuwachagua. Endapo watapata kura zaidi za “ndiyo” basi watu hao watakuwa wamepata uhalali wa kuwa Bungeni na watatimiza masharti ya Ibara ya 66 yaani “wamechaguliwa” na endapo watapata kura nyingi za hapana basi watashindwa kuwa wabunge na viti hivyo vitakuwa wazi na hatimaye uchaguzi mdogo mwingine utatakiwa kufanyika kwa mujibu wa sheria.

      Na kwa vile baadhi yao (kama siyo wote) wanaamini kuwa wanakubalika na kupendwa katika majimbo yao kiasi cha kukosa wapinzani ni matumaini yangu watakuwa tayari na watakumbatia kwa furaha wazo hili la kupigiwa kura ya “ndio” au “hapana” ili waweze kusema kuwa na wao wamechaguliwa. Na endapo Ofisi yake itashindwa kuweka utaratibu wa ndugu zetu hawa kupigiwa kura na baadaye kuwatambua kuwa ni “wabunge halali” hata kama hawana uhalali basi wasipewe nafasi nyingine yoyote ya juu katika serikali (kama Uwaziri au Unaibu) kwa sababu ya kukosa sifa muhimu ya kuwawakilisha wananchi kwani ni ukweli wa wazi kuwa hawakuchaguliwa na mtu yeyote kwenye uchaguzi huru na wa haki kuwa wawakilishi wake.

      Na endapo Tume yako itawatambua watu hawa ambao hawajachaguliwa kuwa ni “wabunge” kinyume na matakwa ya Katiba yetu ya Muungano ambayo uliapa kuilinda, mimi kama Mtanzania nikitumia haki yangu ya Kikatiba ya kudumisha hifadhi ya Katiba yetu natangaza katika dhamira safi na mapema kabisa kutowatambua watu hao ambao wataingizwa bungeni bila ya kuchaguliwa na mwananchi mmoja au kuteuliwa Rais; kwamba ninawakataa kuwatambua kama Wabunge halali wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hadi pale watakapopigiwa kura na kuchaguliwa kwa namna moja au nyingine ili wapate uhalali kwa mujibu wa Katiba.

      Ni matumaini msimamo wangu huo utalazimisha Watanzania, taasisi, na vyama mbalimbali kuchukua msimamo kama huo wa kutowatambua kuwa ni wabunge halali wale wote watakaoingia Bungeni aidha bila ya kuchaguliwa na wananchi au kuteuliwa kama ilivyo katika Ibara ya 66.

      Katika ulinzi wa Katiba Yetu na Udumishaji wa Demokrasia

      M. M. Mwanakijiji

      Ushirikiano wa Kimataifa wa Watanzania Wanaojali – Consortium of Concerned Tanzania Intl.
      “Katika Ulinzi wa Demokrasia”
      mwanakijijI - AT - amiiforums.com

      WAKATI vuguvugu la uchaguzi likizidi kupamba moto, wasomi wametaka sheria inayotaka mgombea ambaye hajapata mpinzani, kutotangazwa kuwa mshindi na badala yake apigiwe kura ili ijulikane anayekubalika na wananchi kwa kiwango gani.

      Pia, wasomi hao wamesema utaratibu huo utasaidia kudhibiti hata kupunguza vitendo vya rushwa na ufisadi katika chaguzi.

      Kwa mujibu wa sheria za uchaguzi nchini mgombea yeyote anayekosa mpinzani hutangazwa kuwa mshindi wa kiti hicho bila hata ya kupigiwa kura.

      Kumekuwa na baadhi ya wabunge kutoka chama tawala, na hasa mawaziri ambao wamekuwa wakikosa upinzani kwenye majimbo yao na hivyo kutangazwa washindi mara baada ya kukamilika kwa uandikishaji wagombea, hali inayowafanya wasihangaike kwenye kampeni.

      Miongoni mwa wabunge ambao wamekuwa wakipita bila ya kupingwa ni Waziri John Pombe Magufuli (Biharamulo Mashariki), Mark Mwandosya (Rungwe Mashariki), Edward Lowassa (Monduli), William Ngeleja (Sengerema) na Mizengo Pinda (Mpanda Mashariki).

      Hayo yanatokea wakati vyama vya upinzani vikisita kusimamisha wagombea urais kwenye uchaguzi mkuu ujao huku wenyeviti wake na wanasiasa wa kutegemewa wakitangaza nia ya kugombea ubunge.

      Lakini wasomi waliiambia Mwananchi kwa nyakati tofauti jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki kuwa kumtangaza mshindi bila ya kupigiwa kura ni kuwanyima wananchi haki yao ya kidemokrasia na kwamba ikiwa sheria itabadilishwa vitendo vya rushwa vitapungua.

      Wasomi hao, Dk Benson Bana, wakili Tundu Lissu na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Bashiru Ally walitaka mgombea ambaye hajapata mpinzani apigiwe kura.
      Lissu alisema sheria hiyo ina mapungufu na kwamba umefika wakati sasa wa kumlazimisha mgombea pekee apigiwe kura.

      Wakili Lissu alisema pamoja na mgombea kupigiwa kura pia awekewe masharti ya kwamba ili atangazwe kuwa mshindi ni lazima afikishe nusu ya kura ya watu waliojiandikisha.

      "Mgombea asitangazwe kuwa mshindi... awekewe masharti ya kufikisha nusu ya kura ya watu waliojiandikisha," alisema Lissu.

      Ally, ambaye ni mhadhiri msaidizi wa UDSM, alisema mgombea kukosa mpinzani ni tatizo la kidemokrasia na kutaka sheria hiyo ifanyiwe mabadiliko ili kutoa fursa pana ya kidemokrasia.

      "Kuwepo kwa mgombea mmoja katika nafasi ya urais, ubunge, udiwani na hata katika uwakilishi katika serikali za mitaa ni tatizo la kidemokrasia na inawanyima fursa wananchi kumchagua mtu wamtakaye,"alisema Ally.

      Mhadhiri huyo ambaye ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa nchini na nje ya nchi alifafanua kwamba utafiti uliofanyika katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2000 na 2005, ulibaini kuwa baadhi ya wagombea ubunge walitumia mbinu mbalimbali za kudhibiti vyama vya siasa hasa vya upinzani visiweke wagombea.

      "Ukipeleleza vizuri utagundua kuna wabunge ambao ni mawaziri zaidi ya nane kutoka majimbo tofauti walioshinda bila kupigiwa kura na leo hii wananchi hawawataki na wanawazomea kila wakihutubia katika mikutano mbalimbali," alisema.

      Alisema kuwa utafiti huo ulibaini kuwa viongozi hao walipata nafasi hiyo baada ya kuwarubuni wagombea wa vyama vya upinzani.

      Naye Dk Bana ambaye ni mtaalamu wa sayansi ya siasa alisema sio haki katika nchi inayofuata demokrasia kwa mgombea kutangazwa kuwa mshindi bila ya kupigiwa kura.
      Alisema utaratibu huo hauwatendei haki wananchi na kwamba inadumaza haki na kukua kwa misingi ya demokrasia.

      "Demokrasia maana yake ni upinzani sasa ikitokea mgombea anapita bila kuwa na mpinzani hilo ni tatizo na pia matokeo hayo yanakuwa hayajawatendea haki wananchi,"alisema Dk Bana.

      Kumekuwa na baadhi ya wabunge kutoka chama tawala, na hasa mawaziri ambao wamekuwa wakikosa upinzani kwenye majimbo yao na hivyo kutangazwa washindi mara baada ya kukamilika kwa uandikishaji wagombea, hali inayowafanya wasihangaike kwenye kampeni.

      Miongoni mwa wabunge ambao wamekuwa wakipita bila ya kupingwa ni Waziri John Pombe Magufuli.
      Invisible and Pasco like this.
      [email protected]
      Tunapotaka kubadilisha watawala si kwa sababu tunataka kubadilisha sura; bali kubadilisha utawala! Yaani, tunataka kubadilisha jinsi tunavyotawaliwa siyo tu sura za wanao tutawala M. M. Mwanakijiji

    2. RukaaJuu Final

    3. #41
      Dopas's Avatar
      JF Senior Expert Member Array
      Join Date : 14th August 2010
      Posts : 595
      Rep Power : 564
      Likes Received
      85
      Likes Given
      82

      Default Re: Barua ya wazi kwa mwenyekiti wa tume ya taifa ya uchaguzi

      Mzee Mwanakijiji

      Kwanza nakupongeza barua hii uliyoandika kwa umakini mkubwa.

      Pili, nashauri wakati tume inaendelea kuifanyia kazi, uitume kwa vyombo vya habari- hasa magazeti yenye nia njema kwa nchi yetu yanayowafikia wengi, kama bado hujafanya hivyo. Ili mawazo mazuri haya uliyoibua yawafikie wengi mapema iwezekanavyo.

    4. #42
      Tom Lyimo's Avatar
      Member Array
      Join Date : 5th September 2009
      Posts : 31
      Rep Power : 500
      Likes Received
      1
      Likes Given
      0

      Default Re: Barua ya wazi kwa mwenyekiti wa tume ya taifa ya uchaguzi

      kumbe ndio hvyo sasa ina maana tume hailijui hilo?

    5. #43
      Augustine Moshi's Avatar
      JF Senior Expert Member Array
      Join Date : 22nd April 2006
      Posts : 1,794
      Rep Power : 1841
      Likes Received
      159
      Likes Given
      56

      Default Re: Barua ya wazi kwa mwenyekiti wa tume ya taifa ya uchaguzi

      Pongezi Mzee Mwanakijiji kwa kutoa mawazo muhimu sana.

      1. Mwalimu Nyerere alikuwa mgombea pekee kwenye chaguzi za wakati wake. Hakuna mtu alisema ameshashinda mpaka achaguliwe kwanza. Iweje leo wanaokuwa wagombea pekee waseme tayari ni wabunge?
      2. Unaweza kuwa mgombea pekee na ukashindwa. Kama hupati hata kura moja unakuwa hujashinda.
      3. NEC au Mwanasheria Mkuu wa Serikali alitakiwa awe ameshauri kuwa mgombea pekee bado ni mgombea na sio tayari mbunge. Lakini watu wenyewe ni vilaza.
      4. Kutokuwa na ushindani kwenye kugombania ni ruksa ya kugombania. Sio tayari ushindi.

    6. #44
      Kituko's Avatar
      JF Senior Expert Member Array
      Join Date : 12th January 2009
      Posts : 3,712
      Rep Power : 1287
      Likes Received
      495
      Likes Given
      174

      Default Re: Barua ya wazi kwa mwenyekiti wa tume ya taifa ya uchaguzi

      Quote By Dopas
      Shukrani kwa kufungua macho wengi. Naamini barua hiyo itafungua wengi ufahamu wao kuhusu suala hilo kuliko kuendelea kujipigia makofi. Ni imani yangu kuwa tume ya uchaguzi itaizingatia. Thanks
      hapo ndipo tunapoona upungufu mkubwa katika Wizara mama ya Katiba na Mambo ya sheria, hapo kama sheria itafata mkondo wake kuna uwezekano mkubwa wa hayo majimbo kurudiwa uchaguzi wake,

    7. #45
      Baija Bolobi's Avatar
      JF Senior Expert Member Array
      Join Date : 25th February 2009
      Location : Bosnia
      Posts : 612
      Rep Power : 719
      Likes Received
      325
      Likes Given
      0

      Default Re: Barua ya wazi kwa mwenyekiti wa tume ya taifa ya uchaguzi

      Yaani hapa tungekuwa mahakama huru na tume huru, mambo yangebadilika mara moja. Lakini kwa hali ilivyo watadharau na kuyatupilia mbali. Lakini wakati umefika wa watanzania wenye nia njema kwenda mahakamani hata kama mahakama yenyewe haiko huru.

      Mchezo unaochezwa hapa ni wa mahesabu. Wagombea wa CCM wamechoka kuombwa rushwa na wapiga kura, kwa hiyo mgombea mwenye fedha akimaliza kura za maoni, anawatafuta wagombea na upinzani na kuwakatia chao ili abki peke yake. Ni afadhali kuhonga mtu mmoja kuliko kuhonga makundi mbalimbali. Haiwezekani mtu apite bila kupingwa wakati hata kura za maoni alipitia kwa taabu. Kwani hao wa chama chake waliomkataa hawana haki ya kupiga kura?

      Huu ni mchezo mchafu kuliko yote katika siasa.
      HERI KUFIA MAWAZO YANAYOISHI KULIKO KUISHI KWA MAWAZO YALIYOKUFA.

    8. Miaka 50

    9. #46
      Pasco's Avatar
      JF Premium Member Array
      Join Date : 22nd September 2008
      Posts : 9,839
      Rep Power : 7368
      Likes Received
      6154
      Likes Given
      22277

      Default Re: Barua ya wazi kwa mwenyekiti wa tume ya taifa ya uchaguzi

      Mzee Mwanakijiji, asante kwa hili. Hii ni hoja ya nguvu iliyobeba nguvu ya hoja ambayo kisheria, Tume ya Taifa ya Uchaguzi, haina mahali pa kuipangulia.

      Ila kila sheria huwa inatungiwa regulations za utekelezaji wa sheria husika, sijabahatika kuziona regulations za mwaka huu, ila kwa mwaka 2005, kwenye regulations, zilimpa mamlaka msimamizi wa uchaguzi (RO) kumtangaza mgombea aliyepita bila kupingwa kuwa tayari ni mbunge/diwani mtarajiwa. Kitu ambacho bado sijakijua, hiyo regulation ili derive wapi mamlaka hayo ya kiimla!.

      Regulation hiyo ilisema iwapo hakuna upinzani kwenye nafasi ya urais, mgombea aliyejitokeza, atapigiwa kura za ndiyo au hapana, kama enzi ya chama kimoja, kuweka sura na kivuli., sijui kwa nini utaratibu huu, usitumike, kwa hao wanaodaiwa kupita bila kupingwa.

      Kwa kawaida kabla ya uchaguzi, document ya regulations ndio hutoka kwanza, na vyama vyote lazima visaini hizo rules of the game,ndipo kipenga kipulizwe, kwa vile kipenga kimeshapulizwa, na wakuu wa vyama vyote wameshasaini kanuni za mchezo, nadhani, there is nothing that can be done to rectify this serious anomality ili ni hoja muhimu ya kuishikia bango, katika madai ya tume huru ya uchaguzi.

      Asante tena.

      Pasco.
      Invisible likes this.

    10. #47
      Ramos's Avatar
      JF Senior Expert Member Array
      Join Date : 13th May 2010
      Posts : 485
      Rep Power : 560
      Likes Received
      110
      Likes Given
      85

      Default Re: Barua ya wazi kwa mwenyekiti wa tume ya taifa ya uchaguzi

      Kuipangua hawatashindwa. Kwani sheria ngapi zinakinzana na katiba? Watabez kwenye sheria ya uchaguz. Lakini Ukweli unabakia kuwa sheria hii haitoi haki kwa wananchi, wala sio ya kidemokrasia.

      NYONGEZA: Kwa siku za baadae- hata kama kuna wagombea zaidi ya mmoja, bado kuwe na nafasi ya mtu kuchagua "siridhiki na hata mmoja" ili kama wote waliopitishwa na wananchi wao hawakubaliki basi wapewe nafasi ya kumtafuta mwingine...
      ...kwa ugonjwa huu nitakufa. Watanzania wale watalia sana... mimi nitawaombea kwa Mungu...

    11. #48
      Misterdennis's Avatar
      JF Senior Expert Member Array
      Join Date : 4th June 2007
      Posts : 1,032
      Rep Power : 818
      Likes Received
      66
      Likes Given
      223

      Default Re: Barua ya wazi kwa mwenyekiti wa tume ya taifa ya uchaguzi

      Asante MKJJ, ni kweli wengi tulikuwa hatujaliona hili. Ni matarajio yetu kuwa vyama husika pamoja na wanaharakati wataliona hili suala kama fursa ya kuirudisha demokrasia halisi katika mkondo wake.
      Wakitangazwa tu kama wabunge, kesi zifunguliwe mahakamani. Au ikiwezekana kesi ifunguliwe sasa ktk mahakama ya katiba kupata interpretation ya kisheria

    12. #49
      Mugerezi's Avatar
      JF Senior Expert Member Array
      Join Date : 28th March 2007
      Posts : 433
      Rep Power : 708
      Likes Received
      3
      Likes Given
      19

      Default Re: Barua ya wazi kwa mwenyekiti wa tume ya taifa ya uchaguzi

      Kwanza, nakupongeza Mwanakijiji kwa kutuelimisha thru hii barua yako. Kazi nzuri.

      Pili, hawa jamaa the so called "Wabunge waliopita bila kupingwa" wajiandae kwani kampeni ni hakuna kuchagua chama kilichohasi ukweli na wabunge wasio na vision hivyo kampeni lazima ipigwe na kama hakuna anayechagulika hata kama hana mpinzani watapigia kivuli. Lakini lazima kura ipigwe.

      Tatu, hii tume huwa wanajifanya vitu fulani hawavioni especially vinapowahusu CCM lazima kuwa na fair ground na ni lazima haki itendeke kwa wote siyo watu wanawekewa mapingamizi ya kitoto then jamaa wanakubali tu kisa wapinzani. Mbona CCM watu wana kesi za maadili hawajaondolewa? PIGA CHINI HAWA WABUNGE FEKI.

    13. #50
      MwanaHaki's Avatar
      JF Senior Expert Member Array
      Join Date : 17th October 2006
      Posts : 1,413
      Rep Power : 1003
      Likes Received
      156
      Likes Given
      91

      Default Re: Barua ya wazi kwa mwenyekiti wa tume ya taifa ya uchaguzi

      Elimu daima! Ni muhimu, kwani hao "waliopita bila kupingwa" wengi wao wamepita kwa mizengwe ya chama tawala! Kazi nzuri, endelea kuwapa somo Wadanganyika!

      2010 HATUDANGANYIKI!
      Speaking Openly, without fear!

    14. #51
      MANI's Avatar
      JF Platinum Member Array
      Join Date : 22nd February 2010
      Location : CHINI YA MBUYU
      Posts : 1,915
      Rep Power : 954
      Likes Received
      569
      Likes Given
      632

      Default Re: Barua ya wazi kwa mwenyekiti wa tume ya taifa ya uchaguzi

      Ahsante MM lakini kama alivyoshauri Dopas barua hii isambae.
      " TANZANIA BILA CCM INAWEZEKANA"

    15. #52
      Ndachuwa's Avatar
      JF Senior Expert Member Array
      Join Date : 8th March 2006
      Location : ARUSHA
      Posts : 2,664
      Rep Power : 1213
      Likes Received
      544
      Likes Given
      418

      Default Re: Barua ya wazi kwa mwenyekiti wa tume ya taifa ya uchaguzi

      Hoja hii ni nzito na ina ukweli ndani yake, nashauri nakala ya barua hii itolewe kwa vyama vya siasa na makundi ya wanaharakati yanayotetea demokrasia ya kweli hapa Tanzania

    16. #53
      Mbalinga's Avatar
      JF Senior Expert Member Array
      Join Date : 9th April 2010
      Posts : 654
      Rep Power : 593
      Likes Received
      130
      Likes Given
      0

      Default Re: Barua ya wazi kwa mwenyekiti wa tume ya taifa ya uchaguzi

      Ahsante Mzee Mwanakijji,

      Hapa sasa ndipo anatakiwa mtu kama Mtikilla, kufungua kesi mahakamani, hawa watu wasiingie bungeni mpaka wachaguliwe, huku kwetu watu wamechukia sana huyu mbunge wetu ambaye kwa njama tu ametangazwa kupita bila kupingwa na matokeo yake mabango ya Chagua Kikwete yamechanwa chanwa, na hii inaweza kusababisha uvunjifu wa amani.

    17. #54
      Sn2139's Avatar
      JF Senior Expert Member Array
      Join Date : 9th April 2010
      Location : Dar es Salaam
      Posts : 805
      Rep Power : 2867
      Likes Received
      237
      Likes Given
      1400

      Default Re: Barua ya wazi kwa mwenyekiti wa tume ya taifa ya uchaguzi

      Pongezi MMM kwa wazo lako. Naona kuanzia mwaka huu sheria za Tz zinapata mtihani wa mock na ujanja wa siasa unaanza kupimwa kisheria. Trend hii ni mwelekeo chanya kwa afya ya nchi yetu. Naomba pia wawekewe pingamizi na au yaandaliwe mashtaka dhidi ya wabunge hao baada ya kuapishwa bungeni rasmi

    18. #55
      Ntemi Kazwile's Avatar
      JF Senior Expert Member Array
      Join Date : 14th May 2010
      Location : Bongo salidalam
      Posts : 1,873
      Rep Power : 832
      Likes Received
      135
      Likes Given
      449

      Default Re: Barua ya wazi kwa mwenyekiti wa tume ya taifa ya uchaguzi

      Thumbs up! Keep it up brother. I know your efforts will be rewarded with interest! May God bless you
      “If people are not laughing at your dreams at least once a week, you are aiming too low.” Robin Sharma.

    19. #56
      Kichankuli's Avatar
      JF Senior Expert Member Array
      Join Date : 18th December 2008
      Posts : 440
      Rep Power : 620
      Likes Received
      30
      Likes Given
      19

      Default Re: Barua ya wazi kwa mwenyekiti wa tume ya taifa ya uchaguzi

      Quote By Mzee Mwanakijiji
      Na endapo Tume yako itawatambua watu hawa ambao hawajachaguliwa kuwa ni “wabunge” kinyume na matakwa ya Katiba yetu ya Muungano ambayo uliapa kuilinda, mimi kama Mtanzania nikitumia haki yangu ya Kikatiba ya kudumisha hifadhi ya Katiba yetu natangaza katika dhamira safi na mapema kabisa kutowatambua watu hao ambao wataingizwa bungeni bila ya kuchaguliwa na mwananchi mmoja au kuteuliwa Rais; kwamba ninawakataa kuwatambua kama Wabunge halali wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hadi pale watakapopigiwa kura na kuchaguliwa kwa namna moja au nyingine ili wapate uhalali kwa mujibu wa Katiba.
      Kuna haja ya kufanya utaratibu wa kuwawekea pingamizi la kisheria ili wasiapishwe iwapo hali hiyo itajitokeza

    20. #57
      Njowepo's Avatar
      JF Gold Member Array
      Join Date : 26th February 2008
      Location : Santiago
      Posts : 7,624
      Rep Power : 22060
      Likes Received
      1002
      Likes Given
      793

      Default Re: Barua ya wazi kwa mwenyekiti wa tume ya taifa ya uchaguzi

      Hope tutaiona hii barua via Tz daima,mwanahalisi na Raia mwema ikiwezekana watumie na wahusika
      I strongly believe ipo siku kitaeleweka
      WB Tanzania lead economist Jacques Morisset said the GDP doubled in 10 years, but it has failed to produce any significant decline in poverty levels.

    21. #58
      macho_mdiliko's Avatar
      JF Senior Expert Member Array
      Join Date : 10th March 2008
      Posts : 1,895
      Rep Power : 956
      Likes Received
      404
      Likes Given
      296

      Default Re: Barua ya wazi kwa mwenyekiti wa tume ya taifa ya uchaguzi

      Quote By Ntemi Kazwile
      Thumbs up! Keep it up brother. I know your efforts will be rewarded with interest! May God bless you
      Ohoo dear... Mwanakijiji anazidi kujitofautisha na wengi wetu hapa JF ambao huwa tunafikiri kuandika ''vi-ingereza'' vigumu, ndio usomi na ujanja!! Hii ndio michango inayotakiwa JF. Ahsante sana na Mungu akubariki na akulinde!!

    22. #59
      S.M.P2503's Avatar
      JF Senior Expert Member Array
      Join Date : 25th November 2008
      Posts : 332
      Rep Power : 601
      Likes Received
      88
      Likes Given
      86

      Default Re: Barua ya wazi kwa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi

      Hata kama wataingia Bungeni bila kupingwa bado wanaweza kuwa nulified kutokana na maelekezo yalimo katika katiba kama Mzee Mwanakijiji alivyoyaolodesha... labda huu pia ni mkakati wa wapinzani kuja kuwaengua hao wa kupita bila kupingwa (ingawaje dhana hii ya kupitwa bila kupingwa sijui inatokea wapi.. hata Sadam Hussein alipingwa) baada ya uchaguzi mkuu October hii...

    23. #60
      Mzee Mwanakijiji's Avatar
      JF Senior Expert Member Array
      Join Date : 10th March 2006
      Location : Kijijini
      Posts : 29,513
      Rep Power : 46713
      Likes Received
      16404
      Likes Given
      8461

      Default Re: Barua ya wazi kwa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi

      Asante sana kwa mawazo yenu, nimepitia mawazo na hoja zenu na kutokana nazo nimeongeza sababu nyingine 3 (ya nane, tisa na kumi). Shukrani.
      [email protected]
      Tunapotaka kubadilisha watawala si kwa sababu tunataka kubadilisha sura; bali kubadilisha utawala! Yaani, tunataka kubadilisha jinsi tunavyotawaliwa siyo tu sura za wanao tutawala M. M. Mwanakijiji

    Page 3 of 8 FirstFirst 12345 ... LastLast

    Similar Topics

    1. Ushindi wa Kupita bila Kupingwa Ludewa wapingwa mahakamani
      By Rutashubanyuma in forum Jukwaa la Siasa
      Replies: 36
      Last Post: 1st December 2010, 14:01
    2. Mo Dewji apita bila kupingwa!
      By Invisible in forum Tanzania 2010-2015
      Replies: 32
      Last Post: 23rd August 2010, 12:10

    User Tag List

    Posting Permissions

    • You may not post new threads
    • You may not post replies
    • You may not post attachments
    • You may not edit your posts
    •  

    Who are WE?

    JamiiForums is a 'User Generated Content' site; anyone can register (MUST) and comment or start a new topic.

    You are always welcome! Read more...

    Where are we?

    We have our offices in Dar es Salaam but we still work virtually.

    For anything related to this site please Contact us.

    Contact us now...

    DISCLAIMER

    JamiiForums, its partners, affiliates and advertisers are not responsible for the content of threads/topics that are submitted by users..

    Read more...

    Forum Rules

    JamiiForums is moderated under the rules set by users and moderators to safeguard you.

    You MUST read them and comply accordingly. Read more...

    Privacy Policy

    We are committed to respecting your privacy rights when visiting any JamiiForums.com page, such as this one.

    Read our Privacy Policy. Proceed here...