
By
Mwanagenzi
What is the optimal size for the cabinet for Tanzania?
Kumekuwa na mjadala kuhusu ukubwa wa baraza la mawaziri la serikali ya awamu ya nne. Kwa sasa baraza lina wizara 22. Kuna manaibu waziri 30. Pia kuna mawaziri wa nchi 7 (chini ya ofisi ya rais, makamu wa rais na waziri mkuu). Kwa ujumla, baraza la mawaziri lina watu zaidi ya 60, ukiongeza na makamu wa rais, rais wa Zanzibar, rais mwenyewe na mwanasheria mkuu wa serikali.
Je, tuna wizara nyingi mno bila sababu?
Je, kuna haja ya kuwa na manaibu waziri?
Inawezekana kuwa na wasaidizi wa mawaziri lakini wasio na ngazi au hadhi ya waziri, hivyo kupunguza gharama?
Rais anatumia vigezo vya changamoto na mahitaji ya taifa kama msingi mkuu wa uundwaji wa baraza au anatumia hoja ya uwakilishi wa watu (jinsi (sex-as opposed to jinsia ambayo ni gender), kanda (geographical coverage and tribal balance), na dini (uislam vs ukristo)? Au pengine ukada, urafiki na kulipa fadhila?
Je, inawezekana suala la wizara zipi ziwepo katika serikali likawekwa kama suala la kudumu angalau kwa miaka 10 hivi likiendana na dira ya taifa, badala ya rais kuongozwa na visheni binafsi au ilani ya chama chake (wakati mwingine hizi mbili zaweza kutofautiana!) bila ya kujali rais atatoka kwenye chama kipi?
Nadhani hii itasaidia hata wananchi wote kujua nini kipaumbele cha taifa! Na pia itapunguza uwezekano wa rais kujiundia baraza kwa matakwa yake binafsi badala ya taifa, kadhalika malalamiko kutoka kwa wadau na wananchi kwa ujumla.
Binafsi, naona kuwa mtu au nchi maskini zinakuwa na matatizo mengi kiasi kwamba kila kitu kina kuwa "priority" na hii inachangia kuwa na serikali kubwa kwa matarajio kuwa kwa kufanya hivyo serikali itaweza kuwafikia na kuwahudumia wananchi wake kwa ufanisi zaidi. Ndiyo maana unakuta karibu kila suala lina wizara yake badala ya kusema wizara moja ishughulikie masuala kadhaa kwa wakati mmoja. Hii ni changamoto. Tusipoangalia tutakuta siku moja tuna wizara ya ukimwi, wizara ya ukame, wizara ya kuzuia rushwa, wizara ya kero za wanafunzi (mimba na usafiri), wizara ya kushughulikia migogoro nk.
Angalia baadhi ya nchi na wizara zao (idadi):
Marekani 15 (mwaka 1901 walikuwa na wizara 9 tu pamoja na AG),
Uingereza 22 (Blair alikuwa na 23),
Ujerumani 14,
Kanada 27 (wakati wa Waziri Mkuu Brian Mulroney walikuwa na 40),
Ufaransa 15 (Chirac alikuwa na 30)
Israel 27 (mawaziri kutoka vyama vitano vya siasa)
Japan 17 (mawaziri - wakiwemo mawaziri wa nchi)
China - mawaziri 28 - wakiwemo mawaziri wa nchi
India - mawaziri 23 na mawaziri wa nchi 32, kwenye serikali kuu. Hata hivyo kila jimbo lina wizara zake na jimbo kama Utar Pradesh linaongoza kwa wingi wa mawaziri (105) wakati jimbo la Pondicherry lina wachache kabisa (5). Wenye sera ya majimbo mpo!!
Naijeria - mawaziri 23 na mawaziri wa nchi 45 (rais mwenyewe anaongoza wizara 2)
Misri 30
Aljeria mawaziri 38 (wakiwemo mawaziri kamili 29)
Ghana wizara 12
Zambia wizara 23 (lakini Zambia pia kuna mawaziri wa majimbo na mawaziri wa wilaya!)
Kenya wizara 25, mawaziri wa nchi 8
Afrika Kusini wizara 28 (manaibu 21)
Uganda - licha ya makamu na waziri mkuu, waziri mkuu ana manaibu 3, kuna wizara kamili 22, na mawaziri wa nchi 43. Hivyo baraza zima na rais wake wako 72 (bila Mwanasheria Mkuu)
Follow Us Here