Support JamiiForums and Become a 'JF Premium Member' | Click HERE for Details
    Show/Hide This

    Topic: Rais awapiga fullstop mawaziri

    Report Post
    Results 1 to 3 of 3
    1. BAK
      #1
      BAK's Avatar
      JF Senior Expert Member Array
      Join Date : 11th February 2007
      Location : Mfaranyaki
      Posts : 26,537
      Rep Power : 44951
      Likes Received
      8277
      Likes Given
      8280

      Default Rais awapiga fullstop mawaziri

      Rais awapiga fullstop mawaziri wababaishaji bungeni

      Joseph Rusufi

      UBABAISHAJI wa mawaziri wakiwa bungeni ni jambo linalomkasirisha sana Rais Kalete. Tabia hii imekuwa ikiendelea kwa miaka kadhaa sasa tangu yeye mwenyewe alipokuwa waziri katika awamu iliyopita na hata hapo pia tabia hii ilimchukiza. Hakuamini kuwa wasaidizi wake hawa ambao hata wino katika hati zao za uteuzi haujakauka wameanza kutetereka.

      Shughuli za serikali bungeni kwa ujumla haziridhishi na Waziri Mkuu akiwa kama mkuu wa shughuli za serikali bungeni, ameonyesha udhaifu wa kushindwa kumudu ipasavyo majukumu yake.

      Amekuwa akifuatilia shughuli za Bunge kwenye luninga takriban kila siku na kushuhudia jinsi baadhi ya mawaziri walivyokuwa wakipwaya. Majibu yao mepesi ya kitoto kwa maswali magumu yangemuudhi yeyote anayesikiliza.

      Ni kweli kuwa angalau watatu kati yao ni mawaziri waandamizi ambao uzoefu wao ulirudi nyuma awamu zote tatu na kutokana na mazoea ya kubweteka ya siku za nyuma, haikumstaajabisha sana.

      Lakini hawa wengine wote ni wapya, na alidhani amefanikiwa kuwafinyanga atakavyo. Alipata fursa ya kuzungumza nao mmoja mmoja baada ya kuwaapisha kule Dodoma angalau kwa muda mfupi, muda ambao aliutumia kuwatathmini wale ambao hakuwafahamu kwa karibu.

      Mawazo yake yalikatishwa na ujio wa Waziri Mkuu.

      Rais: Oooh, PM karibu, karibu uketi. Nimekuita nipate brief ya mwenendo wa timu yetu bungeni kabla ya kikao cha baraza. Lakini kwanza hebu nieleze taarifa za mikoani, mambo shwari?

      WM: Ahsante mheshimiwa, habari za leo na pole na majukumu. Kwa hakika ripoti zilizonifikia zinaridhisha. Ila ripoti moja ya usalama kutoka Mkoa wa Magharibi, inaonyesha wapinzani wanajizatiti na pengine watakwenda mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi ya majimbo yasiyopungua manane kati ya ishirini na mbili. Matatu walishinda wao na wala sisi hatukupinga. Sasa sijui hata wanachotafuta. Eti wanadai tuliwaibia kura.

      Rais: Lakini Mkoa wa Magharibi tulijitahidi sana, mimi mwenyewe nimekaa wiki nzima pale wakati wa kampeni. Lakini palikuwa pagumu kwa hiyo matokeo yake sikuyashangaa.

      WM: Mheshimiwa, wapinzani hata uwape haluwa na tende hawatoridhika. Kulalama imekuwa ni jadi yao.

      Rais: Enhe… nipe habari, kuna nini tena kinaendelea pale bungeni, mbona mnajigongagonga mno? Nilitegemea tija bora zaidi. Hivi kwa nini mawaziri wanadiriki kutoa majibu ya kipuuzi kwa maswali muhimu yenye maslahi ya kitaifa? Infact nilitarajia wewe binafsi utasimamia mabadiliko hayo.

      WM: Mheshimiwa rais, bahati mbaya mabadiliko yatachukua muda, watu wamezoea hulka za zamani. Lakini ninajitahidi sana.

      Rais: Come on Tony, juhudi ipi unayozungumzia? Juzi naona umeitisha kikao cha Kamati ya Chama ya Wabunge wetu kumjadili Mbunge wa Tinga eti tu kwa sababu amembana Waziri wa Maliasili kuhusu miradi ya makaa ya mawe na chuma. Lakini PM hiki ni kikao cha tatu ndani ya wiki moja. Utaitisha vingapi kuwaokoa mawaziri wako?

      WM: Unajua Mheshimiwa, hivi vitu vingine ni wivu tu, yule mbunge wa Tinga alitupiga vita wakati wa mchakato, si alikuwa yuko upande wa Profesa Mwakilasa akafikiri watapita. Sasa anatumia kila mbinu kutu-frustrate. Basi nikaitisha kikao cha chama nikamuweka mahali pake. Nikamkomesha kisawasawa.

      Rais: Sikiliza PM, kwanza mimi hapa nimeshapata security briefing ya suala la miradi hii miwili. Haya masuala hayahusiani na wivu wala mambo ya mchakato, yale yamepita na kama nilivyosema pale Chimwaga baada ya kushinda, ukurasa ule tumeufunga na sasa sote tushirikiane kujenga urembo mpya kwa faida ya warembo. Hatuwezi kila kukicha tukaendeleza uhasama na wanachama wenzetu.

      WM: Sawa rais, lakini sisi tupo pale, kuna maudhi fulani tunayapata, wanatulenga hawa. Na nikisema hawa simaanishi wapinzani, la hasha, namaanisha wale wenzetu nje ya mchanuo. Hawajatusamehe kwa kuwashinda.

      Rais: Ok nimekusikia, lakini unfortunately sikubaliani nawe. Lazima ujue hivi sasa tupo madarakani na warembo watatupima kwa vitendo vyetu na tija itokanayo. Kama waziri ananuka rushwa tutamshughulikia kwa nguvu zote, hatutomtetea.

      “Kama aliunda kamati ya kitaalamu ya kupitia zabuni zote halafu matokeo halali hayakumridhisha ikabidi awatishe wanakamati ili wabadilishe maamuzi ili yamfurahishe, hilo ni kosa kubwa. Kama Bwana Patel amempa rushwa au yule rafiki yetu ameshirikiana naye, pia huwezi kumtetea. Tony, lazima utofautishe baina ya mchanuo na utawala wa nchi.

      WM: Kweli rafiki yetu Chotamali yuko karibu sana na waziri huyo, lakini tusisahau msaada mkubwa aliotupa wakati wa mchakato.

      Rais: Nimesema na narudia, hii nchi itaendeshwa na utawala wa sheria na sio nani alitoa nini wakati wa mchakato. Ikibidi tutamrudishia fedha zake, lakini nchi hii haiuzwi na mimi sikugombea ili niwe dalali wa kuiuza. Tony, hivi Chotamali kakulisha nini?

      Mbona kila kitu anachosema wewe unaingia kichwakichwa? Turudi kwa Waziri, kama Patel kampa rushwa tutamchunguza na kumuwajibisha. Mstari wa tuhuma za rushwa nilikwisha uchora kwenye kikao cha Baraza la Mawaziri. Kama hafai na aende kunywa chai na Patel. Sisi tuna kazi ya kufanya hapa na hii miradi ina umuhimu mkubwa kwa Taifa hili.

      WM: Sawa rais.

      Rais: PM hii tabia yako ya kukurupuka itatupeleka pabaya, usijidanganye bwana huwezi kuwadhibiti wabunge. Na kwanini uwadhibiti? Hawa ni wawakilishi wa wananchi wamechaguliwa nao ili walinde na kuhoji maslahi yao.

      Hivi vikao vya chama visivyokuwa na idadi unavyoitisha wewe na Katibu Mkuu Mhe. Juma Maropu havistahili. Tena mnaingilia na kukiuka misingi ya demokrasia inayohimiza uhuru wa kujieleza. Wacha hiyo. Hebu niambie kuna tatizo gani wabunge kuhoji ufanisi wa serikali? Au matumizi ya hovyo ya fedha za umma? Kwani huo sio wajibu wa Bunge kufanya hivyo?

      WM: Actually mkuu, suala la ufanisi wa mawaziri wetu ni muhimu, hilo halina shaka. Lakini wabunge na hususan wapinzani wame-specialise kutukandia tu. Eti Mhe. Funga Kazi wa Demokrasia Halisi akauliza kwanini Serikali inaogopa kuwasilisha majina ya wala rushwa wote ambao hivi sasa wanachunguzwa na Takuru (PCB). Waziri akamjibu, unayataka majina kwani wewe polisi au prosecuter? Akatulia. Yaani ni maswali ya kifedhuli tu.

      Rais: Well… PM nakumbuka miaka kadhaa pale bungeni serikali ilikuwa inataka kulazimisha kupitishwa mswada wa ‘kudhibiti rushwa’ na wabunge wakapiga sana kelele namna serikali ilivyozembea katika kushughulikia rushwa. Baada ya kuburuzana sana Mhe. Simaindi Pyua alisimama na kutuambia ‘hivi Serikali kwanini inatuburuza namna hii? Serikali inataka kuoga au kuogelea? Maana iko tofauti kubwa baina ya hayo mawili. Kama ni kuoga basi mnataka kujisafisha tu, kama ni kuogelea basi mnataka kuvuka kwa maana ya kupitisha mswada huu hapa bungeni.’ Mie nadhani kuna mantiki kubwa katika maneno hayo. Kwa hiyo sidhani kama majibu ya mkato yatakujengea murua wa kuheshimika pale bungeni.

      WM: Mheshimiwa, namkumbuka sana Mhe. Simaindi Pyua, alikuwa matata sana. Hata sijui maneno mengine alikuwa anafikiri saa ngapi. Lakini kwa hili letu la sasa ni jepesi tu. Ninaamini wengi wa wabunge wananilinganisha na Waziri Mkuu aliyepita. Nimesikia tetesi kuwa oooh…afadhali awamu iliyopita na maneno kama hayo. Nimefikiri na naamini ni strategy yao tu kutaka nijihisi mnyonge pale bungeni. Yaani ni-develop ka-inferiority complex fulani hivi. Sasa hiyo mimi nimekataa kabisa.

      Rais: No, no, no Tony, attitude hiyo ndio tatizo lako. Heshima haijengwi kwa kutisha watu. Wewe umeshakaa kwenye siasa kwa zaidi ya miongo miwili, kwanini hujajifunza basics za utawala bwana? Na ikiendelea hii tabia ya ubabe watu wataanza kunihusisha na mimi kwenye mwenendo mzima wa Bunge. Hilo ninakataa. Aidha, mawaziri nao lazima wawe makini, hebu chukulia vituko vya juzi tu pale bungeni. Ukisikiliza mijadala bungeni, hususani wakati wa kipindi cha ‘maswali na majibu’ utapata picha kuwa mawaziri hujiona kama wao wanajua kila kitu na kwamba wabunge ni watu wasiojua lolote. Hakika utafikiri wabunge si wawakilishi wa watu! Soma hii hansard:

      “Mhe. Mike Loliondo: Kwa nini serikali inatoa kipaumbele kutenga sehemu nzuri kwa ajili ya mbuga za wanyama wakati wenyeji wa jimbo lake hawana sehemu inayofaa kwa ajili ya kilimo na malisho ya mifugo yao?

      Mhe. Chedi Mgaya, Waziri Mdogo wa Maliasili: Mhe. Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili napenda kujibu swali la nyongeza la Mhe. Mike Kasyaraesi Loliondo Mbunge wa Ngerengere Mashariki kama ifuatavyo. Kama nilivyosema wakati wa kujibu swali la msingi, serikali ilitenga maeneo maalum kwa ajili ya mbuga za wanyama ambao kama Bunge lako tukufu linavyojua wanaliingizia taifa hili mabilioni ya mapato kutokana na utalii na uwindaji. Sehemu ya pesa hizo huchangia maendeleo ya wananchi waliozunguka mbuga hizo kwa njia ya kuwapelekea maji, umeme na shule. Kwa hiyo ni dhahir fedha lazima zipewe kipaumbele, hivyo si sahihi kwa Mheshimiwa Mbunge kudai kuwa serikali inajali wanyama kuliko warembo au eti tumekiuka misingi ya kibinaadamu.

      “Mhe Spika, Bunge lako tukufu litakumbuka hotuba aliyotoa Mhe. Rais wakati wa kuzindua Bunge hili. Alisema na nakuu: ‘Serikali inawajibika kuvuna na kuendeleza rasilimali za taifa letu kwa faida na maslahi ya umma wa Jamhuri ya Urembo. Hapa ningependa kusisitiza jambo moja nalo ni kwamba katika uteuzi wangu wa viongozi wa kitaifa, nitakuwa makini katika kutafuta kiongozi nyota wa kusimamia rasilimali ya taifa kwa maana ya madini, misitu, samaki, maji n.k’, mwisho wa kunukuu. Namuomba Mhe. Mbunge atuachie tufanye kazi na aje atuhukumu baada ya mwaka mmoja.”

      “Spika: Mhe. Loliondo naona hujaridhika. Unalo swali la mwisho la nyongeza?”

      “Mhe. Loliondo: Ndiyo Mhe. Spika. Hapo Naibu Waziri ameboronga na kujitapa tu. Nataka ajibu swali. Aidha Naibu Waziri amenukuu kipande kinachomfurahisha yeye tu cha hotuba ya Mhe. Rais. Nataka anukuu pia kipande hiki; ‘kusimamisha uvunaji wa miti kwa miaka mitano ili kuokoa mazingira; kujali makazi ya watu zaidi badala ya mbuga za wanyama’.

      “Spika: Naona muda umeisha na taratibu hazituruhusu. Mhe. Mbunge itabidi alete swali lingine upya baadaye.”

      WM: Mheshimiwa Rais nimeisoma. Hii ilikuwa kali maana kama Spika angesinzia tu lingekuwa bao la kisigino.

      Rais: Hapana PM, ninachojaribu kusema hapa ni kuwa, mawaziri wako hawajitayarishi ipasavyo. Matokeo yake wanaishia kutoa majibu ya kipuuzi. Utasikia… mipango ipo mbioni, tutatafakari maoni ya mheshimiwa, utekelezaji wa mradi fulani utaanza pindi tu fedha zitakapopatikana, nk. Maswali ya wabunge yanataka majibu sahihi, kama waziri hajui aseme hajui, kama kazembea muwajibishe. Kila mmoja wetu atimize majukumu yake. Tusisahau, Warembo wanatutazama na kutusikiliza. Sitaki mbwembwe zisizokuwa na mpango za mawaziri, nataka hoja. Hata upande wa upinzani kama wana hoja za maana tuzisikilize. Kuwepo kwetu madarakani si kigezo kuwa tunajua kila kitu.

      WM: Sawa Mkuu.

      Rais: Tony, unakumbuka Mwalimu aliwahi kusema: ‘There is a devil in Africa’. Na mimi sasa nafikiri there is a devil in our parliament!! Nataka kujua, kuna shetani gani huko bungeni? Mbona mawaziri wanaboronga kiasi hicho? Sikutegemea kuwa vijana wetu wamekosa majibu sahihi kwa maswali mepesi. Wala wewe sikukusikia ukiingilia na kunyoosha mambo. Hivi mmesahau kuwa tumechaguliwa na wananchi kwa kura nyingi? Tunayo mandate ya kutoa kauli na maamuzi endelevu badala ya kusimama pale pekee na kubishana na wabunge ambao ni wawakilishi wa Warembo au tuseme tayari mmesahahu ahadi zetu kwa wapiga kura? Je, hivyo ndivyo tutakavyoendesha serikali yetu? Kweli tutafika?

      Waziri Mkuu alipoanza kusema “sasa mzee, unajua”, Rais alimkatisha na kusema: “Hapana, usinizeeshe hata kabla sijaanza kazi.” Waziri Mkuu aliendelea: “Hapana samahani, nilichotaka kusema ni kwamba tusipokuwa makini wapinzani wataanza kutuendesha kama gari bovu. Ndiyo maana unaona vijana wanapambana nao vilivyo ili wasitudhalilishe mbele ya wananchi. Naomba utuachie kidogo kwanza tutegue mitego na mabomu ya wapinzani.”

      Rais: Hapana, hapana, hapana. Sitaki mchezo huo. Kwanza mimi sizungumzii wabunge wetu; nazungumzia mawaziri wetu. Wanatuaibisha bungeni. Bunge ni baraza la kutunga sheria na muhimili mkubwa wa utawala. Bunge si kikao cha chama. Wabunge wanayo haki kamili ya kuhoji mwenendo mzima wa serikali. Nataka mawaziri walielewe hilo. PM nitumie lugha gani ili muweze kuelewa azma na dhamira yangu ya kuikwamua Urembo.

      WM: Lakini Rais, azma ni kitu kimoja na siasa ni kitu kingine. Kinachoendelea pale bungeni ni siasa tupu. Tukichezea shilingi chooni, tutapata shida katika Uchanguzi Mkuu ufuatao.

      Rais: Sikiliza PM, nimepanga kulitumia Bunge kama ubao wa kuandikia mafanikio yetu, mahala ambapo tutaweza kujiona tunavyo-perform ili tujisahihishe na si mahala pa kupigania vita za kisiasa. Pale si mahala pa kutangazia itikadi za chama chetu. Tena itikadi za chama naona sasa zinataka kutumika kuficha uzembe na ubadhirifu wa viongozi. Nimezungumza na Spika na nimemuomba aendelee kuimarisha Bunge ili liweze kuwa muhimili wa mageuzi ya nchi yetu. Lipate nguvu za kutuwajibisha sisi tuliopo serikalini. Nimalize tu kwa kukuonya PM, acha hii tabia ya kukurupuka, tumia busara zaidi. Unakumbuka wakati ule katika awamu iliyopita ulipowafurusha Wazungu wa kampuni ya maji? Sasa tuna kesi Uingereza ambayo tukishindwa itatugharimu mabilioni ya fedha za Warembo.


      Hebu twende kikaoni, naona mawaziri wote wameshaingia. Muhimu nikawasisitizie suala la ubabaishaji bungeni lazima likome.

      Ngwe ijayo: Zimwi la ukame laikumba Urembo

    2. Study Abroad

    3. #2
      Jasusi's Avatar
      JF Senior Expert Member Array
      Join Date : 5th May 2006
      Posts : 10,607
      Rep Power : 2889
      Likes Received
      3822
      Likes Given
      12195

      Default

      Brilliant, a masterpiece!

    4. #3
      Kichuguu's Avatar
      JF Senior Expert Member Array
      Join Date : 11th October 2006
      Location : Popote Porini
      Posts : 6,828
      Rep Power : 3269
      Likes Received
      1299
      Likes Given
      913

      Default

      ............fiction?
      Kichuguuu: Nyumba inayohifadhi mchwa na nguchiro kwa pamoja bila mkwaruzo

    5. Miaka 50

    Similar Topics

    1. Replies: 13
      Last Post: 29th November 2011, 17:32
    2. Replies: 0
      Last Post: 1st December 2010, 00:34
    3. Baraza la mawaziri la Rais Dr. Slaa
      By kipipili in forum Tanzania 2010-2015
      Replies: 12
      Last Post: 20th September 2010, 16:27
    4. Rais awapiga kijembe TANROADS awatuhumu kuwa WABAGUZI!
      By Phillemon Mikael in forum Jukwaa la Siasa
      Replies: 51
      Last Post: 25th June 2008, 13:36
    5. Rais asiingiliwe uteuzi wa Mawaziri-Ikulu
      By BAK in forum Jukwaa la Siasa
      Replies: 7
      Last Post: 14th May 2008, 19:00

    User Tag List

    Posting Permissions

    • You may not post new threads
    • You may not post replies
    • You may not post attachments
    • You may not edit your posts
    •  

    Who are WE?

    JamiiForums is a 'User Generated Content' site; anyone can register (MUST) and comment or start a new topic.

    You are always welcome! Read more...

    Where are we?

    We have our offices in Dar es Salaam but we still work virtually.

    For anything related to this site please Contact us.

    Contact us now...

    DISCLAIMER

    JamiiForums, its partners, affiliates and advertisers are not responsible for the content of threads/topics that are submitted by users..

    Read more...

    Forum Rules

    JamiiForums is moderated under the rules set by users and moderators to safeguard you.

    You MUST read them and comply accordingly. Read more...

    Privacy Policy

    We are committed to respecting your privacy rights when visiting any JamiiForums.com page, such as this one.

    Read our Privacy Policy. Proceed here...