NA MWANDISHI WETU
CCM imesema imesikitishwa na iliouita usanii mkubwa unaofanywa na Chadema, kuwahadaa Watanzania kwa kufanya harambee kwa lengo la kuhalalisha mabilioni ya chama hicho yanayodaiwa kutolewa na wafadhali kutoka mataifa tajiri duniani.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye aliyasema hayo leo, Agosti 12, 2012, wakati akizungumza na waandishi wa habari, kwenye Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, mtaa wa Lumumba jijijni Dar es salaam.
“Itakumbukwa mara kadhaa Chadema wamekuwa wakiitisha harambee za kisanii kwa kujaribu kuwahadaa baadhi ya Watanzania kwa kuwaomba wakichangie chama hicho huku viongozi wa chama hicho wakijua kuwa tayari wameshapata mabilioni toka kwa wafadhili wao. Mfano mzuri wa usanii huu ni juzi siku ya Jumamosi, Agosti 10, 2012, kwenye hoteli ya Serena ambapo walifanyika kiini macho cha harambee na kurushwa moja kwa moja na kituo kimoja cha televisheni." alisema Nape.
Alisema ,umekuwa ni utamaduni wa Chadema kuhadaa watu kwa kuitisha harambee za kisanii kina wanapokuwa wameshapewa mabilioni ya fedha na wafadhili wao, ili mradi wahalalishe kuwa fedha wanazotumia zimetokana na michango ya watanzania wakati si kweli.
Nape alisisitiza kuwa CCM wanao ushahidi kuhusu zinakotoka fedha na mikataba wanayoingia Chadema na wafadhili hao na kudai kuwa kama hawatasema wenyewe basi yeye (Nape) ipo siku atawasaidia kwa kutaja wafadhili hao na kuanika hadarani mikataba hiyo.
“Tunao ushahidi wa kutosha unaoonyesha mabilioni waliyopewa Chadema juzi na wafadhili kutoka nje ya nchi kwa lengo la kuendeleza operesheni zao mbalimbali nchini. Cha kushangaza badala ya kuwaambia wanachama wao na Watanzania kwa jumla mikataba na wanakoyapata mabilioni haya, wanawahadaa kwa kuwachangisha na kugeuza mapato hayo mtaji wa baadhi ya watu binafsi ndani ya chama”, Alisema Nape
Nape alidai kwamba, siri kubwa inayofichwa kuhusu mikataba na mabilioni wanayopewa Chadema ni kwa sababu wanaotoa fedha hizo wana ajenda ya kunyemelea rasilimali za nchi hii zinazoanza kuonyesha matumaini ya kuwepo kwa wingi ili wapate kizikwapua kwa urahisi kupitia mgongo wa chama hicho.
"Kwanini mabilioni hayo yanatolewa kwa Chadema wakati huu ambapo sasa Tanzania imo katika kufanya utafiti na ugunduzi wa rasilimali mbalimbali zikiwamo gesi na mafuta? Na Je ufadhili huu kwa Chadema licha ya kufichwa sana na kufanywa siri, una nia njema kwa nchi yetu na rasilimali za nchi yetu? Kwanini ufadhili huu wa mabilioni unafanywa siri ya watu wachache hata ndani ya chama chenyewe?", Nape alihoji.
Alisema, hatua hiyo ya Chadema itaitumbukiza Tanzania katika machafuko yasiyoisha, kama ambavyo inashuhudiwa katika baadhi ya nchi zenye rasilimali kama madini ambako nchi zenye utajiri wa fedha zilijipenyeza kupitia walioitwa wapambanaji wa uhuru na haki katika nchi hizo na hadi sasa hakuna amani.
"Migogoro mingi tunayoshuhudia hasa katika nchi zinazoendelea pamoja na kuwepo sababu zingine lakini moja ya chanzo kikubwa ni uwepo wa utajiri wa rasilimali mbalimbali ambapo mataifa makubwa huzitamani na njia pekee ya kuzipata kwa urahisi ni kuchochea migogoro ya ndani na hivyo kuwa rahisi kupora rasilimali hizo wakati wenye nchi wanahangaika katika migogoro na kuachwa wakiwa masikini wa kutupwa huku waadhirika wakubwa wa migogoro na vita hivi vikiwanufaisha wakubwa.” Alisema Nape.
Nape alitoa mwito kwa Watanzania kuwa ni muhimu macho na ulaghai huo wa Chadema na wafadhili wao na kukitaka chama hicho na wafadhili wao kama kweli wana nia njema na Tanzania, waweke wazi mashariti ya ufadhili huo wa mabilioni ya fedha ili Watanzania wote wajue kama yana manufaa kwao au la hasa ikizingatiwa kuwa vyama vya siasa hapa nchini vinaendeshwa kwa fedha za walipa kodi, hivyo Watanzania wana haki ya kujua.
Pamoja na kuwataka kuweka wazi mashariti yanayoambatana na mabilioni hayo Nape aliwataka Chadema waseme hadharani wenyewe kwamba wamepewa mabilioni hayo, na kuwataka waache mara moja kuwahadaa Watanzania na kujaribu kujipachika kuwa ni Chama cha wanyonge kinachotegemea kujiendesha kwa michango ya watanzania huku wakiendelea kuchukua mabilioni kwa siri kutoka nje.
“ Wasipowaeleza watanzania ukweli , tutawasidia kuwaeleza watanzania ukweli wa kiasi halisi cha mabilioni haya, walikozitoa na mikataba waliyoingia. Lengo la hili ni kuhakikisha kuwa nchi yetu haiwekwi rehani kwa uroho wa madaraka wa baadhi ya wana siasa.” Nape alisema.
Nape akawaasa wanasiasa, kuendesha siasa za nchi kwa kuzingatia uzalendo na kukwepa kudumbukia kwenye tamaa za madaraka kujisahau na kuwa tayari hata kuweka nchi rehani, hasa kipindi hichi ambapo ugunduzi wa rasilimali mbali mbali hasa madini, gesi na mafuta vikiwa vinashika kasi nchini na kwamba ugunduzi huo uwe baraka kwa nchi badala ya laana na kuwa chanzo cha kuiuza nchi.
By John MnyikaBy John MnyikaDr. Slaa: Nape kakurupuka!
*Aponda hoja zake, adai hazina tija
*Mjumbe NEC naye amshangaa
KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willbrod Slaa, amesema kamwe hawezi kujibizana na hoja za kukurupuka zilizotolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye.
Kauli ya Dk. Slaa, imekuja siku moja tu baada ya Nape kukituhumu Chadema kuwa kimekuwa kikiendesha harambee za kukusanya fedha, jambo ambalo ni sawa na usanii mtupu.
Akizungumza na MTANZANIA mjini Dar es Salaam jana, Dk. Slaa alisema Nape si saizi yake kisiasa na wanachokifanya CCM ni kuweweseka na jinsi chama chake, kinavyozidi kukubalika kwa Watanzania.
Alisema CCM, wamekuwa wakikurupuka kutoa hoja ambazo hazina msingi na badala yake zimekuwa na mrengo wa kuwachanganya Watanzania.
“Kwanza napenda kusema Nape si saizi yangu … hoja zake zote nazipuuza, zimejaa propaganda na uchochezi kwa Watanzania.
“Inashangaza kusikia watu hawa wanatuhumu chama chetu, eti kinapokea fedha chafu, inashangaza kuona wao ndio polisi, usalama wa taifa na Benki Kuu (BoT), sasa inakuwaje wanaacha fedha hizi zinaingia nchini?” Alihoji Dk. Slaa.
Alisema inaonyesha wazi namna ambavyo Nape amekosa hoja za msingi za kuwaambia Watanzania.
Alisema atafurahi kusikia Nape anataja mataifa ambayo yamekuwa yakitoa fedha kuifadhili Chadema, kwani kufanya hivyo kutasaidia kupunguza propaganda.
Alisema kuna sheria ya kudhibiti fedha chafu ambayo imepitishwa na Bunge, sasa inakuwaje utekelezaji wake unakuwa mgumu.
“Nawaomba Watanzani watuelewe tunachofanya, kwani kuendelea kuwasikiliza watu hawa tunapotezea mud wetu.
“Watanzania wanatakiwa kufahamu, kuwa umoja wa utaifa unavurugika kutokana na uchochezi kutoka kwa viongozi au watu waliopewa dhamana ya kusimamia na kulinda amani.
“Nimechoshwa na kujibu hoja za kitoto na hii itakuwa ni mara ya mwisho kwangu kumjibu Nape, kwa sababu hoja zenyewe hazina mashiko kwa wananchi.
“Nasema hivyo, kwa sababu watu hawa wanakurupuka kutoa hoja zisizokuwa na mantiki yoyote…hawana hata makabrasha ya ushahidi wa maneno wanayoyasema …sijui ni aina gani ya viongozi?” alihoji Dk. Slaa.
Juzi Nape alikutana na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam na kudai CCM, imeshtushwa na kasi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kuendesha harambee za kukusanya fedha kila kukicha, kitendo ambacho ni sawa na usanii.
Alisema, CHADEMA kimekuwa kikiendesha usanii huo, licha ya ukweli kuwa, kinapokea mamilioni ya fedha kutoka mataifa ya nje.
Alisema CCM, imesikitishwa na kushangazwa na usanii unofanywa na CHADEMA, kwa kuwahadaa Watanzania, kwa kufanya harambee ili kuhalalisha uwepo wa mabilioni ya fedha wanazopewa na wafadhili wao nje ya nchi.
‘‘Umekuwa utamaduni wa chama hiki kuhadaa watu kwa kuitisha harambee za kisanii, baada ya kupewa mabilioni ya fedha na wafadhili wao, ili mradi wahalalishe fedha wanazotumia zimetokana na michango ya Watanzania, wakati si kweli.
“Tunao ushahidi wa kutosha unaoonyesha fedha walizopewa na wafadhili kutoka nje ya nchi, kwa lengo la kuendeleza operesheni mbalimbali nchini. Cha kushangaza, badala ya kuwaambia wanachama wao na Watanzania ukweli wa haya, wanaanza kuwahadaa kwa kuwachangisha na kugeuza mapato haya, mtaji wa baadhi ya watu binafsi ndani ya chama.
“Hebu tujiulize, kwa nini mabilioni haya yanayotolewa kwa Chadema wakati huu, ambao nchi yetu inaendelea kufanya utafiti na ugunduzi wa rasilimali mbalimbali, zikiwamo mafuta na gesi? Je, ufadhili huu licha ya kufichwa sana na kufanywa kwa siri, una nia njema kwa nchi yetu na rasilimali za nchi yetu?” alihoji Nape.
“Ni muhimu Watanzania tukawa macho na ulaghai huu na tunawataka wafadhili wao kama kweli wana nia njema na nchi yetu, waweke wazi masharti ili Watanzania watambue fedha hizi zina manufaa au la,” alisema Nape.
MJUMBE WA NEC
Katika hatua nyingine, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alisema anashangazwa na kauli za Nape.
“Nimeshangazwa mno na kauli hii, nimeshtushwa kusikia eti kuna mataifa ya nje yanayotoa fedha nje kwa ajili ya kuisaidia Chadema…kumbuka Serikali yetu zaidi ya asilimia 30 tunapewa na wafadhili.
“Naamini kusaidiwa na mataifa si ajabu, kwa sasa hata sisi CCM tunasaidiwa na mataifa ya nje ambayo ni rafiki zetu kifedha na kiutawala.
“Naamini Nape ni kiongozi mkubwa ndani ya chama, hii mikataba anayosema angeitaja ningefurahi sana… huu ni udhaifu mkubwa kwa kiongozi wangu, huu ni mwendelezo wa kujenga majungu na fitina,
…hoja yake ya kusema atawataja ni miujizi, kwa sababu hii si mara ya kwanza kwake, kuibuka na maneno ya aina hii… nadhani kiongozi katika chama kikubwa na tawala wanapaswa kukaa chini na kutafakari kabla ya kuongea,” alisema mjumbe huyo.
CHANZO: Mtanzania - Agosti 14, 2012

Reply With Quote


Follow Us Here