|
Ile kesi ya mauaji ya wafanyabiashara watatu na dereva teksi mmoja inayomkabili aliyekuwa Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Abdallah Zombe na wenzake 11 imetinga katika Mahakama Kuu ya Tanzania leo asubuhi.
Zombe na wenzake isipokuwa mtuhumiwa mwanamke, walitinga katika mahakama hiyo saa 3.00 asubuhi huku wakiwa chini ya ulinzi mkali wa askari wa kikosi cha kutuliza ghasia, FFU waliokuwa na mabomu ya kutoa machozi. Mtuhumiwa huyo wa kike aliwasili kortini hapo kama saa nne na nusu hivi.
Kesi hiyo ambayo imepewa namba 26/2006, iko mbele ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Laurian Karegeya.
Awali, shauri hilo kabla ya kufikishwa Mahakama Kuu lilikuwa likisikilizwa na Hakimu Mkuu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Sivangilwa Mwangesi.
Agosti 11 mwaka huu, mahakama hiyo ilihitimisha wajibu wake wa kisheria wa kusikiliza maelezo ya awali na kuikabidhi Mahakama Kuu ambayo ndiyo yenye mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.
Katika maelezo ya awali yaliyotolewa na wakili wa Serikali William Magoma katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ilidaiwa kuwa marehemu hao kabla ya kuuawa na kushindwa kutambuliwa na wafanyakazi wa Kampuni ya Bidco, walichukuliwa katika gari wakiwa wazima wakiongozwa na Mrakibu Msaidizi wa Polisi, Ahamed Makelle na wakaelekea Ubungo.
Ilielezwa kuwa walipofika Ubungo walichukuwa barabara ya Morogoro kwenda Mbezi Louis kisha wakaelekea kwenye msitu wa Pande ambako marehemu hao walianza kushushwa mmoja mmoja kutoka kwenye gari na Koplo Allawi akaanza kuwamiminia risasi za kisogoni.
Katika maelezo yake, askari Rashid Lema alidai kuwa Zombe alitaka marehemu hao wachinjwe, lakini yeye akajaribu kumsihi asifanye hivyo kwa vile watu hao hawakuwa wanahusika na wizi.
Akasema baadaye mtuhumiwa SP Christopher Bageni alimwamuru Afande Saada awaue mmoja baada ya mwingine na akawaamuru watu hao walale chini, ndipo akaanza kuwamiminia risasi mgongoni na kisogoni.
’’Baada ya Koplo Saada kumaliza zoezi la kuwapiga risasi, niliamuriwa kupanda katika gari kwa ajili ya kupokea miili ya marehemu hao na baada ya hapo baadhi ya askari walichaguliwa kupeleka miili yao katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili,’’ ulidai ushahidi huo.
Baada ya mauaji hayo, ikadaiwa kuwa Zombe aliwaambia wenzake kuwa polisi inajipanga namna ya kuzungumzia tukio hilo na akawatisha polisi wengine kuwa atakayekiuka ndiye atakayebebeshwa mzigo kwamba ndiye aliyefanya mauaji hayo.
Ushahidi wa daktari wa Muhimbili, Dk. Martin Mbonde, aliyewafanyia uchunguzi marehemu hao pia ulibaini kuwa vifo vya marehemu wote wanne vilisababishwa na risasi ambazo walipigwa mgongoni na kisogoni.
Katika ushahidi huo, Dk. Mbonde ameandika kuwa marehemu wawili walikutwa na majeraha ya risasi mbili kila mmoja na marehemu wengine wawili walikutwa na majeraha ya risasi nne kila mmoja.
Wakati ushahidi huo unasomwa mahakamani siku hiyo, watuhumiwa watatu waliiomba mahakama kuwa wakati kesi hiyo itakapoanza kusikilizwa, yatumike maelezo ya pili ambayo waliyaandika kwa hiari yao kwani maelezo ya awali waliyaandika kutokana na shinikizo la baadhi ya viongozi wa Jeshi la Polisi.
Mbali na Zombe, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mrakibu wa Polisi Christopher Bageni, Mrakibu Ahmed Makelle, Konstebo Noel na Koplo Jane Andrew.
Wengine ni Koplo Nyangelera E 6712 Felix Cedrick, Konstebo Michael, Koplo Rashid Lema, D2300 Abeneth, Koplo Rajabu na Koplo Emmanuel Mabula.
Washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kuwa mnamo Januari 14 mwaka huu, katika msitu wa Pande huko Mbezi Luis, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, walimuua Ephraim Chigumbi.
Katika shitaka la pili ilidaiwa kuwa siku ya tukio la kwanza huko kwenye msitu wa Pande, Mbezi Luis, washtakiwa walimuua Sabinus Chigumbi maarufu kwa jina la Jongo.
Katika shitaka la tatu, ilidaiwa kuwa siku ya tukio la kwanza na la pili, kwenye eneo la tukio la kwanza na la pili, washtakiwa walimuua Juma Ndugu.
Pia katika shitaka la nne, ilidaiwa kuwa siku ya tukio la kwanza, la pili na la tatu, katika msitu huo wa Pande huko Mbezi Luis, washitakiwa walimuua Mathias Lukombe.
Hadi tunakwenda mitamboni, kesi hiyo ilikuwa bado haijaanza.
Kesi hiyo ya madai itatajwa tena Oktoba 17 mwaka huu. |
|