re: Kashfa mpya Nishati na Madini; Kikwete na Pinda wajiuzulu au wawajibishwe!
MZOZO NISHATI NA MADINI: Pinda amuokoa JK
• Mbatia adai kuna wabunge wamehongwa
na Mwandishi wetu | Tanzania Daima
WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda juzi jioni alifanya kazi ya ziada kuzima hasira za wabunge waliokuwa wakitaka kuona Waziri wa Nishati na Madini, Pofesa Sospeter Muhongo, na Katibu Mkuu wake, Eliakim Maswi, wakiwajibika kwa kujiuzulu nyadhifa zao vinginevyo wangekwamisha bajeti ya wizara hiyo.
Habari ambazo Tanzania Daima, imezipata zinadai kuwa wabunge hao walidhamiria kukwamisha bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka 2012/2013 inayotarajiwa kusomwa bungeni leo.
Chanzo cha habari hizo kilidai wabunge walifikia hatua hiyo baada ya vigogo hao kuripotiwa kuwa waliruhusu ukiukwaji wa sheria ya manunuzi ya umma kwa kuipa zabuni kampuni ya Puma Energy (T) Ltd zamani BP.
Kampuni hiyo ilipewa zabuni ya kununua mafuta ya kuendesha mitambo ya kuzalisha umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) na kuziweka kando kampuni zilizokuwa zimechaguliwa kupitia mchakato halali wa zabuni ya TANESCO.
Suala hilo linahusishwa na kusimamishwa kwa Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO, William Mhando, kwamba alichukuliwa hatua baada ya kukataa kutii maelekezo ya wizara.
Katika kikao cha juzi usiku cha wabunge wa CCM, kilichoongozwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, wabunge hao walikuwa na msimamo wa kumuwajibisha Muhongo na Maswi. Wakati wabunge wakiwa na msimamo huo, Pinda aliingia akiwa na lengo la kuilinda serikali na chama kinachotawala (CCM).
Pinda alidai kuwa kumshinikiza Rais Kikwete amuwajibishe waziri aliyemteua miezi mitatu iliyopita ni kutomtendea haki na kuuonyesha umma kuwa hakufanya chaguo sahihi.
Tanzania Daima, ilidokezwa kuwa wajumbe wote walikubaliana kwamba Katibu Mkuu wa Nishati na Madini alifanya makosa na alivunja sheria.
Wabunge wa CCM walitaka Maswi na Muhongo watoswe ili kujenga heshima ya serikali na kusimika utawala wa sheria.
Inadaiwa kuwa kulikuwa na wabunge waliopangwa kimkakati kushawishi wenzao wasiisulubu serikali kwa kukwamisha Bajeti ya Nishati na Madini leo.
Miongoni mwa wabunge wanaotajwa ni Waziri Mkuu Pinda, William Lukuvi, Jenista Mhagama na Mbunge wa Muleba Kaskazini, Charles Mwijage. Inadaiwa kuwa Mwijage ana maslahi katika Puma Energy iliyopewa zabuni ya kuiuzia mafuta IPTL na Maswi.
Mbunge wa Simanjiro Christopher Ole Sendeka, anadaiwa kutaka iundwe kamati teule ya Bunge kuchunguza uozo ulio ndani ya wizara na TANESCO.
Baadhi ya wabunge wakasema wazo lake ni sawa, lakini katika mazingira ya sasa ya kisiasa ya CCM, tume itaibua uchafu mwingi ambao utaimaliza serikali mbele ya umma.
Sendeka alisema: “Mbona katika sakata la Richmond iliundwa kamati iweje hivi sasa isiundwe wakati kosa la Maswi linafanana na la Lowassa?”
Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango, inasemekana alijenga hoja kuwa CCM na serikali walifanya makosa kwenye sakata la Richmond ambalo lilimfanya aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa, kuachia ngazi.
“Tulimtosa Lowassa, baadaye ukweli umejulikana, na sasa makosa yetu yanaigharimu serikali na CCM. Tusirudie makosa yale yale, tuwaache hawa kwa maslahi ya CCM,” alisema.(Dah! kwa Maslahi ya CCM eeh! na siyo ya nchi!!!)
Hata hivyo baadhi ya wajumbe walishikilia msimamo wa kuwajibishwa kwa Muhongo na Maswi kwa madai kuwa endapo wataachwa, wataimaliza serikali ya CCM.
Walisema kuwaacha ni sawa na kulitangazia taifa kwamba wao ni wavunjaji wa sheria walizozitunga wenyewe.
Tanzania Daima imeelezwa kuwa hata hivyo hatimaye wabunge hao walikubaliana kwa shingo upande kuwa msimamo wa wabunge wa CCM ni kulinda chama na serikali.
Mbatia alonga
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, ameibua ufisadi mzito unaofanywa na TANESCO na kuwaomba wabunge wasimame kidete ili watuhumiwa wachuliwe hatua.
Mbatia ambaye pia ni mbunge wa kuteuliwa na Rais Kikwete, alifichua ufisadi huo mbele ya waandishi wa habari mjini hapa, akisema kuwa serikali imekuwa ikipoteza mabilioni ya fedha kulisaidia shirika hilo wakati zinaishia mikononi mwa wajanja ambao ni menejimenti na Bodi ya Wakurugenzi.
Tuhuma za Mbatia zinakuja ikiwa ni wiki mbili tangu Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO iwasimamishe kazi, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo, William Mhando, na wenzake watatu kwa tuhuma za ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka.
Mhando na Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Robert Shemhilu, Ofisa Mkuu wa Fedha, Lusekelo Kassanga, na Meneja Mwandamizi Ununuzi, Harun Matambo, walisimamishwa na bodi hiyo chini ya Mwenyekiti wake, Jenerali mstaafu, Robert Mboma, ili kupisha uchunguzi wa tuhuma dhidi yao.
Kwa mujibu wa Mbatia, wabunge wamekuwa wakifuatwa ndani na nje ya Bunge na hata kwenye mahoteli walikofikia wakishawishiwa kuiunga mkono TANESCO, jambo alilodai limewaingiza baadhi ya wenzao kwenye ufisadi.
Akifafanua kwa undani, Mbatia ambaye aliongozana na wabunge wote wa chama chake, alisema kuwa mpaka sasa hawana imani na Kamati ya Nishati na Madini kwa kuwa baadhi ya wajumbe wake vile vile ni wajumbe kwenye bodi ya TANESCO na wamekuwa wakitumika kuwarubuni wabunge wakingie kifua ufisadi.
“Tulipokwenda Ikulu kuonana na Rais Kikwete kama chama kuzungumzia mchakato wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Januari 21 mwaka huu… tuligusia pia hali mbaya iliyokuwa ikiikabili TANESCO lakini Rais alitueleza kuwa serikali imeipa ruzuku ya sh bilioni 136 ili kuliwezesha,” alisema Mbatia.
Aliongeza kuwa kwenye bajeti ya mwaka jana, iliafikiwa kuwa TANESCO itafutiwe mkopo wa sh bilioni 408 na serikali pia ikalipa deni lake la sh bilioni 68 kwa shirika hilo pamoja na kulipatia mafuta ya sh bilioni 17.
Alisema kuwa mgogoro wa TANESCO ulianza kuibuka baada ya kuzushwa uongo kuwa nchi inaweza kuingia gizani wakati wowote kutokana na hali mbaya ya shirika, madai ambayo Mbatia alisema si ya kweli kwani ulikuwa ni ujanja wa mafisadi kuzima kwa makusudi mitambo.
“Kisha TANESCO iliingia kwenye mchakato wa kutafuta wazabuni wa kuiuzia mafuta mazito ya kuendesha mitambo yake ambapo ilifanya mazungumzo na kampuni tatu zilizoonyesha kuwa tayari kuiuzia mafuta hayo kwa sh 1,800 kwa lita,” alisema.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi, naye alifanya mazungumzo na Kampuni ya Puma ambako serikali ina hisa za asilimia 50 na kuafikiana kuwa inaweza kusambaza mafuta hayo kwa gharama ya sh 1,460 kwa lita, bei iliyoonekana kuwa na unafuu zaidi.
Mbatia alifafanua kuwa pamoja na kampuni ya Puma kutokuwa kwenye orodha ya zile zilizoomba zabuni hiyo, Maswi alitumia kanuni ya 42 (1) ya mamunuzi ya umma inayompa mamlaka ya kuamua vinginevyo kwenye masuala yenye maslahi ya umma kuipa zabuni hiyo hiyo.
“Kosa na kelele zote zimetoka hapo, mianya ya mafisadi imezibwa kwani walitaka kuzipa zabuni kampuni za bei kubwa ili wavune sh bilioni tatu ambazo zinaokolewa kila baada ya wiki mbili. Sasa kama kwa mwezi TANESCO inaokoa sh bilioni sita kwa nini tumnyime zabuni huyu?” alihoji.
Mbatia alisema kwa mwezi Mei pekee TANESCO ilikusanya sh bilioni 85 na matumizi yake kwa mwezi ni sh bilioni 11 ambapo kwa wastani wanapata zaidi ya sh bilioni 60 wakiwa na ziada ya sh bilioni 50 kila mwezi.
Let your graceful words fly out into the World, carried on winds of courage, imagination and joy. Let them inspire others to step into action
Follow Us Here