Support JamiiForums and Become a 'JF Premium Member' | Click HERE for Details
    Show/Hide This

    Topic: HOTUBA ya Upinzani Bungeni ambayo akina Werema. Lukuvi na wenzao, hawataki wananchi wajue,HII HAPA

    Report Post
    Page 1 of 3 123 LastLast
    Results 1 to 20 of 59
    1. #1
      cvchumvi2012's Avatar
      Member Array
      Join Date : 7th May 2012
      Posts : 12
      Rep Power : 356
      Likes Received
      1
      Likes Given
      0

      Default Re: LUKUVI NA SPIKA WAVURUGA HOTUBA YA KAMBI YA UPINZANI sasa hivi

      Siku zaja hakutakuwa na mahakama wala mahakimu, kwani yaliyofanyika uvunguni yatawekwa juu ya paa mchana kweupe na kila mtu ataona.

      Ndiyo maana sasa hivi polisi wameagizwa baada ya Rais kukaa na baraza la usalama mwezi uliopita kwamba polisi kila jambo wapeleke mahakamani ili kuzipba watu kulizungumzia!!!

    2. Miaka 50

    3. #2
      Chief Isike's Avatar
      Senior Member Array
      Join Date : 17th January 2010
      Posts : 231
      Rep Power : 521
      Likes Received
      207
      Likes Given
      106

      Default HOTUBA ya Upinzani Bungeni ambayo akina Werema. Lukuvi na wenzao, hawataki wananchi wajue,HII HAPA

      HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI MHESHIMIWA VINCENT JOSEPHAT NYERERE (MB), KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA WA FEDHA 2012/2013 WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI


      (Kanuni ya 99(7) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, 2007)








      UTANGULIZI

      Mheshimiwa Spika,

      Kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, napenda kuchukua fursa hii kuwasilisha maoni yake kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi kwa mwaka wa fedha 2012/2013. Aidha, napenda kuwashukuru askari wa Jeshi la Polisi na Jeshi la Magereza wanaoishi Kambi iliyoko katika Kata ya Mkendo kwa kunichagua kuwa Diwani wao. Vile vile, nawashukuru wananchi wote wa vyama vyote na dini zote Jimbo la Musoma Mjini kwa kunichagua kuwa Mbunge na mtetezi wao.

      Pia napenda kumshukuru Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa imani yake kubwa kwangu kwa kuniteua kuwa Msemaji Mkuu wa Kambi katika Wizara hii. Kwa upekee kabisa, Mheshimiwa Spika, kwa wanaoeneza propaganda kwamba CHADEMA inachukia au kudharau askari polisi wetu, naomba nitoe shukrani zangu kwa mke wangu Helen V. Nyerere ambaye pia ni askari wa Jeshi la Polisi.


      UTEKELEZAJI WA AHADI ZA SERIKALI


      Mheshimiwa Spika,

      Katika mwaka uliopita wa fedha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilihoji matukio mbali mbali ya mauaji ya raia yaliyowahusisha askari wa Jeshi la Polisi pamoja na wa vyombo vingine vya dola.

      Aidha, tulihoji matukio mengi ya ukiukwaji wa haki za binadamu za wananchi wetu hasa katika maeneo yenye migodi mikubwa ya dhahabu kama vile Nyamongo, Arusha na kwingineko katika nchi yetu. Vile vile, tulihoji sababu za Serikali kushindwa kuwachukulia hatua za kisheria na za kiutendaji watuhumiwa wa makosa haya makubwa.


      Mheshimiwa Spika
      ,
      Wakati anatoa hoja yake ya kuahirisha Mkutano wa Bunge la Bajeti la mwaka jana, Waziri Mkuu aliahidi kwamba Serikali ingefanya uchunguzi wa matukio yote ya mauaji kwa mujibu wa Sheria ya Uchunguzi wa Vifo (The Inquests Act), Sura ya 24 ya Sheria za Tanzania. Kwa maneno yake mwenyewe, Mheshimiwa Waziri Mkuu alisema: “vifo ... ambavyo vimetokea katika mazingira ya kutatanisha chini ya mikono ya Vyombo vya Dola, ni lazima vichunguzwe.”

      Hata hivyo, Mheshimiwa Spika, hadi wakati tunaandika maoni haya, hakuna Mahakama ya Korona hata moja ambayo imeitishwa kwa lengo la kuchunguza vifo vilivyotokana na matumizi ya nguvu ya vyombo vya dola. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutoa kauli rasmi mbele ya Bunge hili tukufu kama kauli ya Waziri Mkuu ilitolewa kwa lengo la kuwahadaa Watanzania. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali itamke ni lini Serikali itaunda Mahakama za Korona ili kuchunguza matukio yote ya mauaji ya wananchi katika maeneo yote tuliyoyataja mwaka jana.


      Mheshimiwa Spika
      ,
      Kwa sababu ya Serikali kutotimiza ahadi yake ya kuchunguza matukio ya mauaji kwa mujibu wa Sheria tajwa, vitendo vya mauaji na ukiukwaji wa haki za binadamu vimeendelea kutokea katika nchi yetu. Kwa mfano, katika taarifa yake ya Haki za Binadamu kwa Mwaka 2011, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kinaripoti kwamba “mwenendo wa matukio ya ukatili wa polisi na mauaji yanayofanywa kinyume cha sheria na vyombo vya dola umeendelea kuongezeka katika nchi yetu. Kati ya Januari na Desemba 2011 tayari watu 25 wamekwisharipotiwa kuuawa wakiwa mikononi mwa polisi na maafisa wengine wa usalama, wakati ambapo watu wengine 50 walijeruhiwa.”

      Taarifa hii inaungwa mkono na taarifa ya Hali ya Haki za Binadamu kuhusu Tanzania iliyotolewa mwaka huu na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani (State Department) inayoonyesha kuwa bado yapo mauaji yanayotokea mikononi mwa vyombo vya dola ikiwemo jeshi la polisi, utesaji na wananchi wanaotuhumiwa kujikuta wakipata vipigo kinyume na mikataba ya kimataifa ambayo Tanzania imeiridhia.


      MAUAJI YENYE SURA YA KISIASA


      Mheshimiwa Spika,

      Kutokana na Serikali kutochukua hatua kukabiliana na matukio ya mauaji yanayohusishwa na vyombo vya dola, sasa limezuka wimbi la mauaji na matukio ya majaribio ya mauji yenye sura ya kisiasa katika maeneo mbalimbali nchini.

      Matukio hayo ni pamoja na mauji ya kada wa CHADEMA Mbwana Masudi yaliyotokea wakati wa Uchaguzi Mdogo wa Ubunge katika Jimbo la Igunga, na aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Kata ya Usa River, Marehemu Msafiri Mbwambo, mara baada ya Uchaguzi Mdogo wa Ubunge katika Jimbo la Arumeru Mashariki.


      Aidha, Mheshimiwa Spika, kumekuwa na majaribio ya mauaji ambapo wabunge wa CHADEMA Mheshimiwa Highness Kiwia wa Jimbo la Ilemela na Mheshimiwa Salvatory Machemli wa Jimbo la Ukerewe, walioshambuliwa kwa mapanga mbele ya maafisa polisi na watu wanaosadikiwa kutumwa na makada wa CCM mkoani Mwanza. Vile vile, Mheshimiwa Mchungaji Peter Msigwa, Mbunge wa Iringa Mjini (CHADEMA) alivamiwa na wafuasi wa CCM wanaodaiwa kutumwa na Iddi Chonanga, Diwani wa Kata ya Nduli (CCM) katika Halmashauri ya Manispaa ya Iringa.


      Mheshimiwa Spika,

      Matukio ya mauaji au majaribio ya mauaji yenye sura ya kisiasa yamewahusu pia watu ambao sio wanachama au viongozi wa vyama vya siasa lakini wanaonekana kupinga matakwa ya watawala.

      Haya yamemkuta Mwenyekiti wa Jumuia ya Madaktari Dr. Steven Ulimboka ambaye alitekwa nyara na kuteswa kwa kikatili na watu ambao taarifa za vyombo vya habari zimewataja kuwa maafisa wa vyombo vya dola. Kwa mara nyingine tena, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) iamuru kukamatwa kwa watuhumiwa wote ambao wametajwa kuhusika na utekaji nyara na jaribio la kumuua Dr. Ulimboka ili kufuta dhana kwamba vyombo vya dola viko juu ya sheria na vinaweza kuua au kutesa wananchi bila mkono mrefu wa sheria kuwaangukia.


      Mheshimiwa Spika,

      Tarehe 14 Julai 2012, mtu anayesemekana kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM katika Kata Ndago, Jimbo la Iramba Magharibi, Yohana Mpinga, ambaye pia ni mtoto wa Mwenyekiti wa CHADEMA katika Kata ya Urughu alifariki dunia kufuatia vurugu zilizotokea baada ya kumalizika kwa mkutano wa hadhara uliohutubiwa na viongozi wa CHADEMA katika Kata ya Ndago.

      Kwa vile, tayari baadhi ya Wabunge na viongozi wa Serikali ndani ya Bunge hili tukufu wanaelekea kuwa wameshapitisha hukumu kwamba CHADEMA inahusika na kifo cha Marehemu Yohana Mpinga, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ina haya ya kueleza kuhusiana na tukio hili.


      Kwanza, mkutano wa hadhara wa CHADEMA ulihudhuriwa pia na maafisa polisi waliokuwepo wakati wote wa mkutano huo. Pili, licha ya kuwepo kwa maafisa polisi hao, kundi la wahuni wanaodaiwa kukodiwa na makada wa CCM wa Jimbo la Iramba Magharibi walivuruga mkutano huo kwa kupiga mawe watu waliohudhuria mara mbili lakini mara zote polisi waliokuwepo hawakuchukua hatua zozote dhidi ya kundi hilo la wahuni.

      Aidha, mara ya wahuni hao kuvuruga mkutano mara ya pili, viongozi wa CHADEMA walitoa taarifa rasmi katika Kituo cha Polisi cha Ndago na kufunguliwa jalada namba NDG/RB/190/2012.


      Tatu, mara baada ya kutoa taarifa hiyo kwa polisi, mkutano wa hadhara uliendelea bila fujo yoyote hadi ulipomalizika na msafara wa viongozi wa CHADEMA kuondoka eneo la Ndago na kuelekea Kinampanda ambako kulikuwa na mkutano mwingine wa hadhara. Wakati huo, kundi la askari polisi wa Kikosi cha Kuzuia Ghasia (FFU) kutoka Kiomboi walishafika katika eneo la mkutano na kukuta mkutano umemalizika.

      Nne, kwa vile mkutano wa hadhara wa CHADEMA ulimalizika kwa amani mbali na matukio ya kihuni yaliyoripotiwa kwa Jeshi la Polisi, na kwa vile kulikuwa na kikosi cha FFU na askari polisi wengine katika eneo la mkutano baada ya msafara wa CHADEMA kuondoka, ni wazi kwamba watu wanaotakiwa kutoa maelezo ya jinsi Marehemu Yohana Mpinga alivyofikwa na mauti ni Jeshi la Polisi lenyewe.


      Aidha, Mheshimiwa Spika, ni Jeshi la Polisi pekee linaloweza kuwaeleza Watanzania kwa nini kikundi cha wahuni waliowarushia mawe viongozi wa CHADEMA na wananchi waliohudhuria mkutano huo wa hadhara hawakuchukuliwa hatua zozote na polisi waliokuwepo kwa muda wote wa mkutano huo au askari wa FFU waliofika baada ya msafara wa CHADEMA kuondoka.

      Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inasikitishwa sana na mauaji ya kijana huyo na inatuma salamu za pole na rambi rambi kwa familia, ndugu na jamaa wa marehemu. Hata hivyo, Kambi yetu inasikitishwa na kushangazwa sana na ushabiki wa kisiasa ambao umejitokeza humu Bungeni na kauli za kutoa hukumu ambazo zimetolewa na baadhi ya Wabunge na viongozi wa Serikali bila hata kusubiri uchunguzi kamili juu ya jambo hili.


      MASLAHI YA POLISI NA MAGEREZA


      Mheshimiwa Spika,

      Katika maoni yake ya mwaka jana Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ililalamikia utamaduni wa Serikali kupuuza maslahi ya askari polisi na wale wa Jeshi la Magereza. Utamaduni huu ni wa muda mrefu sana. Kwa mfano, katika hotuba ya bajeti ya Waziri wa Mambo ya Ndani kwa mwaka wa fedha 2006/2007, aliyekuwa Waziri wakati huo alikiri kwamba “... kutokana na kipato kidogo cha askari polisi, inawawia vigumu kukopa katika mabenki nchini kutokana na riba kuwa kubwa na kukosa dhamana za uhakika. Hivyo, askari polisi hawana mahali popote wanapoweza kupata fedha za kujiendeleza kiuchumi. Aidha, mishahara na posho wanayolipwa askari bado haikidhi hali halisi ya mahitaji yao na familia zao.”

      Mheshimiwa Spika
      ,
      Toka wakati huo hadi sasa, maslahi ya askari polisi yamekuwa mabaya zaidi kutokana na kushuka kwa thamani ya shilingi na mfumuko wa bei hasa za vyakula kupanda wakati ambapo mishahara yao haijaongezeka sambamba na ongezeko la gharama halisi za maisha.

      Aidha, katika hali inayoonyesha kutokujali kabisa maslahi na hali za maisha za askari wetu, Serikali imeshindwa kutekeleza ahadi yake iliyotolewa
      tarehe 17 Novemba, 2011 na aliyekuwa Naibu Waziri wa Mambo ya ndani Mheshimiwa Khamis Sued Kagasheki, aliyeliambia Bunge hili tukufu kwamba “... posho ya askari imepandishwa na ... kwamba (inatakiwa) itoke kwenye shilingi laki moja mpaka shilingi laki moja na hamsini.... Ni jambo ambalo tunalo na tumelifanyia kazi na tuna uhakika kwamba, litaweza kutimia….”

      Mheshimiwa Spika,

      Ni ukweli usio na mjadala kwamba askari polisi na magereza bado wanapokea posho ya kujikimu ya shilingi laki moja badala ya shilingi laki moja na elfu hamsini iliyoahidiwa na Serikali mbele ya Bunge hili tukufu. Aidha, katika mazingira ya kushangaza kabisa, mara baada ya Serikali kutoa ahadi Bungeni juu ya posho hiyo, uongozi wa juu wa Jeshi la Polisi ulituma maelekezo kwa Makamanda wa Polisi wa Mikoa kufanya uchunguzi ili kubaini askari wote waliokuwa wanadai walipwe posho ya shilingi laki moja na nusu kama ilivyoahidiwa ili askari hao wafukuzwe kazi.

      Mheshimiwa Spika
      ,
      Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali ilieleze Bunge lako tukufu ni lini italipa malimbikizo ya baki ya shilingi elfu hamsini kwa mwezi kwa kila askari polisi na magereza ambayo haijawalipa askari hao hadi hivi sasa. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali ianze kuwalipa askari polisi na magereza posho ya kujikimu ya shilingi laki moja na nusu kwa mwezi kuanzia mwaka huu wa fedha, kwa vile ahadi ya Serikali iliyotolewa na aliyekuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani haijawahi kukanushwa, kubatilishwa au kubadilishwa na Serikali.

      Mheshimiwa Spika,

      Sio tu kwamba Serikali haitekelezi ahadi inazotoa Bungeni juu ya malipo ya askari polisi na magereza. Serikali pia imekuwa inawakopa watumishi hao bila ridhaa yao. Kwa mfano, randama ya fungu la 29 inaonyesha kuwa Jeshi la magereza linadaiwa jumla ya shilingi bilioni 23.65. Kati ya fedha hizo, watumishi wa Jeshi la Magereza wanaidai Serikali jumla ya shilingi bilioni10.34 ambazo ni malipo ya stahili zao mbali mbali kama vile fedha za likizo, uhamisho, mafunzo, n.k.

      Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali itoe kauli mbele ya Bunge hili kama, na lini, italipa madeni haya ya askari magereza wetu wanaokesha magerezani usiku na kushinda juani mchana wakiwalinda wafungwa na mahabusu waliojaa katika magereza ya nchi yetu.


      Mheshimiwa Spika,

      Kuna hatari kwa askari wa Jeshi la Magereza kufanya kazi katika mazingira magumu ambayo tumeyaeleza katika maoni haya. Mfano ni katika Jimbo langu la Musoma Mjini. Mbali na makazi duni ya askari magereza, vile vile kuna umbali mrefu kati ya kambi ya askari magereza ya Nyasho na Gereza la Mkoa lililopo Kata ya Mkendo na askari magereza wamekuwa wakitembea kwa miguu usiku wanapokuwa zamu gerezani.

      Hii inahatarisha usalama wao kwani wanaweza kuvamiwa na kudhuriwa na wafungwa au mahabusu waliokwisha kumaliza adhabu zao lakini wakawa na visasi na askari hao. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali iwapatie gari askari wa kambi ya Nyasho na makazi mengine ya askari magereza yaliyoko mbali na magereza wanakofanyia kazi ili kunusuru maisha ya askari magereza wetu.


      Mheshimiwa Spika,

      Katika maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ya mwaka jana, tulipendekeza kwamba “... utaratibu wa sasa wa polisi wa ngazi za chini kukatwa shilingi 5,000 kila mwezi kwenye mishahara yao, kwa ajili kugharamia mazishi yao na wategemezi wao, ufutwe mara moja, kwani unawanyonya kwa sababu vipato vyao ni vidogo. Badala yake ... serikali ibebe jukumu hilo.”

      Hata hivyo, hadi tunaandika maoni haya, Serikali imeendelea kupuuza mapendekezo haya kwa kisingizio kwamba ‘mfuko wa kufa na kuzikana’ ni wa hiari ilhali askari polisi wanaendelea kukatwa mishahara yao kwa lazima.

      Kwa mara nyingine tena Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inatamka kwamba kukata mshahara wa mfanyakazi bila ridhaa yake wakati hadaiwi chochote na mwajiri wake ni kinyume cha sheria husika za nchi yetu na kitendo cha jeshi la Polisi kuendelea kukata mishahara ya askari polisi kwa ajili ya ‘mfuko wa kufa na kuzikana’ bila ridhaa ya askari polisi wenyewe kikome mara moja.


      Mheshimiwa Spika,

      Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inafahamu kwamba askari polisi wanaofanya kazi za lindo katika mabenki yote ya biashara hapa nchini hulipwa posho ya shilingi elfu kumi kwa siku.

      Hata hivyo, Serikali haijawahi kutamka hadharani kiasi ambacho mabenki hayo hulipa serikalini kwa ajili ya kazi hiyo ya kulinda mabenki binafsi. Kwa sababu hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikli kulieleza Bunge lako tukufu kiasi ambacho mabenki ya biashara hulipa serikalini kwa ajili ya huduma ya ulinzi inayotolewa na askari polisi ili Bunge lako lifahamu kama askari polisi wanaofanya kazi hiyo wanalipwa inavyostahili.


      VITENDEA KAZI VYA POLISI


      Mheshimiwa Spika,

      Kwa mujibu wa ripoti ya Hali ya Uchumi wa Taifa, makosa ya jinai yaliyoripotiwa katika vituo mbalimbali vya polisi hapa nchini yalikuwa 62,133. Ripoti inasema kwamba kwa mwaka 2011 makosa 63,703 ya jinai yaliripotiwa katika vituo vya polisi nchini.Kwa kiasi kikubwa, ongezeko hili la uhalifu linasababishwa na askari wa doria kushindwa kufika kwenye maeneo ya matukio ya uhalifu kwa haraka pindi wapatapo taarifa kwa kisingizio cha kukosa mafuta kwa ajili ya magari ya doria.

      Hata hivyo, Mheshimiwa Spika, nyaraka za Serikali zinaonyesha kwamba Bunge lako tukufu limekuwa likiidhinisha fedha nyingi kwa ajili ya mafuta ya magari ya Jeshi la Polisi. Kwa mfano, kwa mujibu wa randama ya Fungu la 28 kwa mwaka huu wa fedha, matumizi halisi ya mafuta kwa ajili ya Jeshi la Polisi kwa mwaka wa fedha 2010/2011 yalikuwa shilingi bilioni 2.81. Aidha, katika mwaka wa fedha uliopita Bunge lako tukufu liliidhinisha shilingi bilioni 2.61 kwa ajili ya mafuta, wakati ambapo kwa mwaka huu wa fedha Serikali inaomba Bunge liidhinishe shilingi bilioni 2.56 kwa ajili ya mafuta ya magari ya Jeshi la Polisi.


      Wakati Bunge limekuwa lkiidhinisha mafungu haya makubwa ya fedha kwa ajili ya mafuta, askari polisi wamekuwa wakilalamika kwamba hawapewi fedha za mafuta kwa ajili ya magari ya doria hivyo kusababisha askari polisi kushindwa kufanya kazi zao hizo ipasavyo. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali ieleze zinakopelekwa fedha za mafuta kwa ajili ya Jeshi la Polisi kama gari moja la doria linapatiwa lita 5 za mafuta kwa kutwa na/au usiku.


      IDARA YA UHAMIAJI NA PAKACHA LA MIPAKA


      Mheshimiwa Spika
      ,
      Mipaka yetu na nchi jirani zinazotuzunguka imekuwa pakacha linalovuja. Ndio maana katika hotuba yetu ya mwaka janatuliliambia Bunge lako tukufu kwamba “... kumekuwa na ongezeko la wageni wengi kutoka nchi za nje ... kiasi cha kujiuliza kama nchi hii ina utaratibu wowote wa kuratibu na kudhibiti uingiaji wa wageni hapa nchini.”

      Tulionyesha jinsi ambavyo kumekuwa na ongezeko la wageni haramu kutoka nchi za Somalia, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Burundi, Rwanda, Kenya, Uganda, Pakistan, Nigeria, China, India na Bangladesh “ambao wanaishi Tanzania kwa mfumo usio rasmi, bila ya kuwa na hati zinazowaruhusu kufanya hivyo.”

      Tulitahadharisha kwamba “utaratibu wa kuachia kila mgeni kuingia Tanzania na kuishi atakavyo bila ya vyombo husika kujua kuwepo kwake ni hatari kiusalama, hasa katika zama hizi za kusambaa kwa ... ugaidi na uharamia wa kimataifa katika masuala ya fedha, biashara za binadamu ...” n.k.


      Mheshimiwa Spika,

      Maneno na tahadhari zetu ziliangukia kwenye masikio ya Serikali kiziwi. Na sasa yale tuliyoyasema yameanza kutimia kwani ni mwezi mmoja tu umepita tangu wahamiaji haramu zaidi ya arobaini kutoka Ethiopia kukutwa wamekufa ndani ya lori la mizigo ambalo kwa vyovyote vile lilitokea nchi jirani. Watu hawa waliingiaje nchini na kusafiri hadi katikati ya nchi yetu bila kujulikana na maafisa wa Uhamiaji, polisi wa usalama barabarani na usalama wa taifa kama kweli nchi yetu iko salama?

      Ni afisa gani wa Idara ya Uhamiaji aliyewapitisha katika mpaka wetu wa Namanga au Horohoro au Sirari au Kogaja au Borogonja? Na ni askari polisi gani aliyewasindikiza hadi Kongwa? Aidha, ni afisa mizani gani wa TanRoads aliyepitisha lori walimokuwa watu hao bila kulikagua na kujua kilichokuwamo?


      Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilitegemea – kwa kuzingatia ukubwa na uzito wa kashfa hii – viongozi waadilifu katika Wizara, Idara ya Uhamiaji na Jeshi la Polisi wangewajibika kutokana na uchafu huu.

      Hata hivyo, hakuna hata mmoja ambaye amefanya hivyo. Kwa vile uwajibikaji wa hiari unaelekea kushindikana, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inamtaka Rais Kikwete kutumia mamlaka yake ya kikatiba kuwawajibisha wale wote waliohusika kuanzia viongozi wa Wizara walioko humu Bungeni na uongozi wa juu wa Idara ya Uhamiaji na Jeshi la Polisi ili kuondokana na aibu hii ya nchi yetu kuwa transit route ya biashara ya kusafirisha binadamu katika sehemu hii ya Bara la Afrika.


      Mheshimiwa Spika
      ,
      Matatizo ya ongezeko la wahamiaji haramu katika nchi yetu linatokana na Idara ya Uhamiaji kuendekeza vitendo vya kifisadi katika kuajiri, kupandisha madaraja au vyeo wa maafisa wa Idara hiyo. Kwa mujibu wa taarifa tulizo nazo, ajira katika Idara ya Uhamiaji haizingatii tena elimu, uwezo na weledi wa maafisa husika.

      Bali, kwa mujibu Taarifa ya Utafiti wa Mpango Mkakati wa Mageuzi Katika Utumishi wa Uhamiaji (Immigration Service Reform Programme Strategic Plan Research Report) iliyochapishwa na Wizara ya Mambo ya Ndani tarehe 27 Novemba, 2011, “mara nyingi mgawanyo ya kazi (katika Idara) hautegemei sifa bali unategemea upendeleo, rushwa, kujuana na urafiki vitu ambavyo viko kinyume na maana halisi ya mgawanyo wa kazi.” (“Most of the time placement is not based on merits but depends on nepotism, bribery and technical know-who, friendship and favouritism that have been contrary to the whole meaning of placement.”)


      Mheshimiwa Spika,

      Ushahidi wa kauli hii unapatikana katika Taarifa hiyo ya Utafiti inayoonyesha kwamba maafisa wengi wa ngazi za juu katika Idara ya Uhamiaji ni watu wenye uwezo mdogo kielimu kulinganisha na maafisa wa ngazi za chini wa Idara hiyo. Kwa mfano, katika ngazi ya Kamishna Msaidizi wa Uhamiaji kwenda juu hadi kwa Kamishna Mkuu, kuna maafisa kumi wenye shahada ya uzamili (masters degree), wawili wenye post-graduate diploma (PGD), ishirini na nne wenye shahada ya kwanza, tisa wenye stashahada, saba wenye diploma, kumi na moja wenye kidato cha sita na 248 wenye elimu ya kidato cha nne.

      Katika maafisa hawa wa ngazi za juu, kuna Kamishna mmoja mwenye elimu ya kidato cha nne wakati kuna Makaimu Kamishna 216 wenye elimu hiyo ya kidato cha nne na Kamishna Wasaidizi Wakuu 31.

      Kwa upande mwingine,

      Mheshimiwa Spika, kuanzia ngazi ya Mrakibu Mwandamizi (Senior Superintendent) kwenda chini mpaka koplo kuna maafisa wenye shahada ya uzamili 36, wenye post-graduate diploma wako saba, wenye shahada ya kwanza wako 340, wenye stashahada wako 78, diploma wako kumi wenye cheti (certificate) wako 52, waliomaliza kidato cha sita wako 585 wakati waliohitimu kidato cha nne wako 337.

      Katika mazingira ambayo maafisa wenye uwezo mkubwa wa elimu hawapewi nafasi za juu katika Idara badala yake uongozi wa juu umejazwa na wenye elimu za mashaka kama inavyoonyeshwa katika Taarifa ya Utafiti ya Wizara, ni wazi kwamba matukio kama ya maafa ya wahamiaji waliokutwa wamekufa Jimboni kwa Naibu Spika wa Bunge hili tukufu hayawezi kuepukika!


      Aidha, Mheshimiwa Spika, katika mazingira ya upendeleo na rushwa katika ajira ya Idara ya Uhamiaji ya aina hii, maafisa uhamiaji hawawezi kuacha kutumiwa na wanasiasa wa chama tawala kuwatuhumu washindani wao kisiasa kuwa sio raia wa Tanzania ili kuwaondoa katika kinyang’anyiro cha chaguzi zetu.

      Hivi ndivyo ilivyotokea kwa Mheshimiwa Ali Mohamed Keissy alipotaka kugombea Ubunge kwa tiketi ya CHADEMA na kuzushiwa tuhuma kuwa siyo raia. Hata hivyo, alipojiunga na CCM bila ridhaa yake tuhuma za kutokuwa raia ziliyeyuka na sasa ni Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Nkasi Kaskazini katika Mkoa anakotokea Waziri Mkuu!


      Mheshimiwa Spika
      ,
      Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutoa kauli rasmi mbele ya Bunge hili tukufu juu ya mambo haya ambayo yamethibitishwa na Ripoti ya Utafiti ya Wizara ya Mambo ya Ndani. Aidha, Kambi inaitaka Serikali itoe kauli kama kuna haja yoyote ya kutumia mamilioni ya fedha za wananchi kusomesha maafisa wa Idara ya Uhamiaji ambao baada ya kufuzu hawapatiwi vyeo na majukumu yanayolingana na uwezo wao wa kielimu.
      JESHI LA ZIMA MOTO NA UOKOAJI
      Mheshimiwa Spika,
      Ni dhahiri kuwa umuhimu wa Jeshi hili unaonekana pale yanapotokea majanga ya moto, mafuriko au maafa mengine kama vile tetemeko la ardhi ambapo athari za matukio haya ni makubwa sana na mara nyingi hupelekea wananchi kupoteza maisha. Malalamiko ya wananchi katika maeneo mbalimbali juu ya Jeshi la Zimamoto kuchelewa kufika katika maeneo ya tukio yamekuwepo kwa miaka mingi na yamepigiwa kelele sana hapa Bungeni.

      Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inarudia ushauri wake kuwa Serikali iboreshe mfumo mzima wa zimamoto katika nchi yetu ili kukabiliana na majanga ya moto yanayoongezeka kutokana na kupanuka na kukua kwa miji yetu.


      Mheshimiwa Spika,

      Baada ya maelezo na kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ninaomba kuwasilisha.


      .....................……………………… ……………..


      VINCENT JOSEPHAT NYERERE


      MSEMAJI MKUU WA


      KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI


      WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI


      17/07/2012


    4. #3
      WA-UKENYENGE's Avatar
      JF Senior Expert Member Array
      Join Date : 1st October 2011
      Location : Inside a Smart Grid
      Posts : 2,410
      Rep Power : 5037
      Likes Received
      780
      Likes Given
      1780

      Default Re: HOTUBA ya Upinzani Bungeni ambayo akina Werema. Lukuvi na wenzao, hawataki wananchi wajue,HII HA

      Duh, nimesoma mwanzo mwisho bila kupumzika! imetulia na imekaa vizuri sana!! Ahsante kwa taarifa hii mkuu.
      "The usual conclusion is that you can't put a price on a human life. But you can if you must".

    5. #4
      Ruttashobolwa's Avatar
      JF Senior Expert Member Array
      Join Date : 22nd February 2012
      Posts : 13,444
      Rep Power : 19776
      Likes Received
      4282
      Likes Given
      1187

      Default Re: HOTUBA ya Upinzani Bungeni ambayo akina Werema. Lukuvi na wenzao, hawataki wananchi wajue,HII HA

      Daaaaaah lazima lukuvi apanic
      mu-unguja likes this.

    6. #5
      Mkulima wa Kuku's Avatar
      JF Senior Expert Member Array
      Join Date : 13th January 2011
      Posts : 706
      Rep Power : 564
      Likes Received
      240
      Likes Given
      207

      Default Re: HOTUBA ya Upinzani Bungeni ambayo akina Werema. Lukuvi na wenzao, hawataki wananchi wajue,HII HA

      well done Nyerere!

    7. Study Abroad

    8. #6
      mizambwa's Avatar
      JF Senior Expert Member Array
      Join Date : 8th October 2008
      Posts : 1,435
      Rep Power : 974
      Likes Received
      366
      Likes Given
      1804

      Default Re: HOTUBA ya Upinzani Bungeni ambayo akina Werema. Lukuvi na wenzao, hawataki wananchi wajue,HII HA

      Quote By 2MINE
      [CENTER]
      HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI MHESHIMIWA VINCENT JOSEPHAT NYERERE (MB), KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI KWA MWAKA WA FEDHA 2012/2013 WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
      Mheshimiwa Spika, [/FONT][/B]
      Kwa mfano, katika hotuba ya bajeti ya Waziri wa Mambo ya Ndani kwa mwaka wa fedha 2006/2007, aliyekuwa Waziri wakati huo alikiri kwamba “... kutokana na kipato kidogo cha askari polisi, inawawia vigumu kukopa katika mabenki nchini kutokana na riba kuwa kubwa na kukosa dhamana za uhakika. Hivyo, askari polisi hawana mahali popote wanapoweza kupata fedha za kujiendeleza kiuchumi. Aidha, mishahara na posho wanayolipwa askari bado haikidhi hali halisi ya mahitaji yao na familia zao.”

      Wananikera hawa Askali Polisi wa Tanzania; Wanaharakati na vyama vya upinzani wanawapigania ili wapate haki zao, lakini kwa kukosa kufikiria na kujipendekeza kwa Serikali wanaamua kuwapiga mabomu, kuwakamata na hata kuwaua Wanaharakati na Wapinzani eti kuitetea Serikali.

      Sasa haya waliyosema upande wa upinzani endapo wakipewa haki hizi si watanufaika wao!!!!!!

      Lakini utashangaa kesho wnawatendea maovu viongozi wa upinzani na wanaharakati.

      WAKATI wa KUJIPENDEKEZA UMEPITA, WATANZANIA wote TUAMKE NA KUSHIKAMANA TUMUONDOE HUYU NDULI SERIKALI KANDAMIZI.



      MIZAMBWA
      NABII MTARAJIWA!!!
      Last edited by mizambwa; 17th July 2012 at 15:09.
      kibogo likes this.
      SASA NIMEAMINI KUWA TANZANIA BILA CCM INAWEZEKANA!!!!, TUANDAE KABURI LA KUIZIKA MWAKA 2015

    9. #7
      PakaJimmy's Avatar
      JF Senior Expert Member Array
      Join Date : 29th April 2009
      Posts : 14,680
      Rep Power : 22519
      Likes Received
      6338
      Likes Given
      2831

      Default Re: HOTUBA ya Upinzani Bungeni ambayo akina Werema. Lukuvi na wenzao, hawataki wananchi wajue,HII HA

      Kweli hawa Askari polisi ni kama gunia la misumari!
      Wanatetewa namna hii lakini ndo kwanza hawaelewi kinachoendelea kuhusu wapinzani!
      "The only thing that walks back from the tomb with the mourners and refuses to be buried is the character of a man.
      What a man is, survives him... it can never be buried"
      (GENEKAI-Jamiiforums, 4th November 2010 07:32PM).
      [email protected]

    10. #8
      JF mteule's Avatar
      Member Array
      Join Date : 23rd May 2011
      Posts : 33
      Rep Power : 410
      Likes Received
      6
      Likes Given
      2

      Default Re: HOTUBA ya Upinzani Bungeni ambayo akina Werema. Lukuvi na wenzao, hawataki wananchi wajue,HII HA

      hii imetulia sana, hivi haiwezi kuchapwa kwenye magazeti ili wale wasio na access na mitandao nao waisome? Wadau hawa polisi wana matatizo mengi sana ndo maana wanaganga njaa kuomba rushwa ndogo ndogo.

    11. #9
      POMPO's Avatar
      Banned Array
      Join Date : 12th March 2011
      Posts : 2,955
      Rep Power : 0
      Likes Received
      1090
      Likes Given
      625

      Default Re: HOTUBA ya Upinzani Bungeni ambayo akina Werema. Lukuvi na wenzao, hawataki wananchi wajue,HII HA

      Imetulia kamanda Nyerere. Good Job

    12. #10
      mtotowamjini's Avatar
      JF Senior Expert Member Array
      Join Date : 23rd April 2012
      Location : None of Your Business
      Posts : 4,531
      Rep Power : 1262
      Likes Received
      1109
      Likes Given
      28

      Default Re: HOTUBA ya Upinzani Bungeni ambayo akina Werema. Lukuvi na wenzao, hawataki wananchi wajue,HII HA

      Quote By mizambwa
      Wananikera hawa Askali Polisi aw Tanzania; Wanaharakati na vyma vya upinzani wanawapigania ili wapate haki zao, lakini kwa kukosa kufikiria na kujipendekeza wanaamua kuwapiga mabomu, kuwakamata na hata kuwaua Wanaharakati na Wapizani eti kuitetea Serikali.

      Sasa haya waliyosema upande wa upinzania endapo wakipewa haki hizi si watanufaika wao!!!!!!

      Lakini utashangaa kesho wnawatendea maovu viongozi wa upinzania na wanaharakati.

      WAKATI wa KUJIPENDEKEZA UMEPITA, WATANZANIA wote TUAMKE NA KUSHIKAMANA TUMUONDOE HUYU NDULI SERIKALI KANDAMIZI.



      MIZAMBWA
      NABII MTARAJIWA!!!
      unajua kua polisi sio kama kua daktari...daktari akiamua kutofanya kazi ni haki yake lakini polisi hana hiyo haki..polisi wako pale kufuata amri. Boss mwema akitoa amri wakawapige cdm hata kama wanawatetea hawana jinsi bali kwenda kuwafanyizia...ndio kiapo hicho walikula
      mizambwa likes this.
      Every saint has a past, every sinner has a future' ...Oscar Wilde

      One man's good fortune is another man's misfortune


    13. #11
      Inno laka's Avatar
      Senior Member Array
      Join Date : 24th March 2012
      Location : Nyamikoma,Mwanza.
      Posts : 242
      Rep Power : 409
      Likes Received
      15
      Likes Given
      1

      Default Re: HOTUBA ya Upinzani Bungeni ambayo akina Werema. Lukuvi na wenzao, hawataki wananchi wajue,HII HA

      Hapo mmesema chadema.,.',lakn co raia 2 wanaokufa hata polic nao wanakufa..

    14. #12
      Mwanaweja's Avatar
      JF Senior Expert Member Array
      Join Date : 8th February 2011
      Posts : 3,446
      Rep Power : 1108
      Likes Received
      457
      Likes Given
      923

      Default Re: HOTUBA ya Upinzani Bungeni ambayo akina Werema. Lukuvi na wenzao, hawataki wananchi wajue,HII HA

      hii hotuba ni ukweli mtupu ndio maana vibaraka wa ccm wanahaha kuzui au kupotosha umma ukweli ulivyo

    15. #13
      Bisek's Avatar
      Member Array
      Join Date : 2nd April 2012
      Posts : 65
      Rep Power : 372
      Likes Received
      8
      Likes Given
      3

      Default Re: HOTUBA ya Upinzani Bungeni ambayo akina Werema. Lukuvi na wenzao, hawataki wananchi wajue,HII HA

      Ukweli jamen idara ya uhamiaji inanuka kabisa.....haifai

    16. #14
      slufay's Avatar
      JF Senior Expert Member Array
      Join Date : 2nd April 2012
      Posts : 397
      Rep Power : 438
      Likes Received
      37
      Likes Given
      1

      Default Re: HOTUBA ya Upinzani Bungeni ambayo akina Werema. Lukuvi na wenzao, hawataki wananchi wajue,HII HA

      Polisi wako kwa maslahi ya nani,?

    17. #15
      sir.JAPHET's Avatar
      JF Senior Expert Member Array
      Join Date : 18th May 2012
      Posts : 608
      Rep Power : 474
      Likes Received
      90
      Likes Given
      43

      Default Re: HOTUBA ya Upinzani Bungeni ambayo akina Werema. Lukuvi na wenzao, hawataki wananchi wajue,HII HA

      point tupu ! Kweli chadema ni chama cha democracy na maendeleo na kesho.. PEOOPLEE$%%POWER%

    18. #16
      The Invincible's Avatar
      JF Senior Expert Member Array
      Join Date : 6th May 2006
      Location : Online
      Posts : 1,943
      Rep Power : 1056
      Likes Received
      168
      Likes Given
      0

      Default Re: HOTUBA ya Upinzani Bungeni ambayo akina Werema. Lukuvi na wenzao, hawataki wananchi wajue,HII HA

      Duh! Hii inaitwa....za uso au kumkoma nyani giladi.
      Watanzania mbumbumbu wamemchagua raisi dhaifu ajenge taifa la watu wasiojiamini, 2010/2015 - Tafakari

    19. #17
      bemg's Avatar
      JF Senior Expert Member Array
      Join Date : 25th April 2010
      Posts : 1,613
      Rep Power : 782
      Likes Received
      218
      Likes Given
      344

      Default Re: HOTUBA ya Upinzani Bungeni ambayo akina Werema. Lukuvi na wenzao, hawataki wananchi wajue,HII HA

      Well done V N.Ni aibu kuona serikali yetu ni bingwa wakutoa ahadi lakini kutekeleza ni sifuri
      Ni jambo zuri na la kupendeza sana ndugu kuishi pamoja kwa umoja

    20. #18
      Byendangwero's Avatar
      JF Senior Expert Member Array
      Join Date : 24th October 2010
      Posts : 832
      Rep Power : 601
      Likes Received
      28
      Likes Given
      0

      Default Re: HOTUBA ya Upinzani Bungeni ambayo akina Werema. Lukuvi na wenzao, hawataki wananchi wajue,HII HA

      Naona kuna haja kubwa kwa kambi ya upinzani kuiomba mahakama kuu kutolea ufafanuzi dhana hii ya kutozungumzia suala lililoko mahakamani, maana inavyoelekea dhana hiyo imeanza kutumiwa na watawala kama kichaka cha kuficha madhambi yao. Kwa yeyote aliyefuatilia hili sakata la huko Singida atakubaliana na mimi kwamba namna polisi inavyoshughulikia suala hilo ni kuchezea akili ya watanzania. Kwanza tujiulize kama mkutano ulikuwa ni wa CDM huyo kiongozi wa CCM alikuwa akifanya nini kwenye mkutano huo! Pili kama mkutano huo ulikuwa na baraka zote za polisi ilikuwaje polisi hao wakashindwa kudhibiti kundi la vijana wanaosemekana kuwa ni wana CCM wasiingilie mkutano halali wa mahasimu wao? Kwa vyovyote vile , ili kupata ni nini hasa kimetokea huko Singida hapana budi iundwe tume huru ya kuchunguza jambo hilo, polisi wenyewe hawawezi kuchunguza jambo hilo kwakuwa ni watuhumiwa.
      BabaDesi and Borat69 like this.

    21. #19
      mgodi's Avatar
      JF Senior Expert Member Array
      Join Date : 5th November 2010
      Posts : 994
      Rep Power : 631
      Likes Received
      113
      Likes Given
      81

      Default Re: HOTUBA ya Upinzani Bungeni ambayo akina Werema. Lukuvi na wenzao, hawataki wananchi wajue,HII HA

      Hotuba imeenda shule sana.

    22. #20
      magosha's Avatar
      JF Senior Expert Member Array
      Join Date : 25th April 2012
      Posts : 317
      Rep Power : 419
      Likes Received
      34
      Likes Given
      8

      Default Re: HOTUBA ya Upinzani Bungeni ambayo akina Werema. Lukuvi na wenzao, hawataki wananchi wajue,HII HA

      duuu hotuba ya ukweli kinoma. lazima wapaniki

    23. FemaTV & Radio
    Page 1 of 3 123 LastLast

    User Tag List

    Posting Permissions

    • You may not post new threads
    • You may not post replies
    • You may not post attachments
    • You may not edit your posts
    •  

    Who are WE?

    JamiiForums is a 'User Generated Content' site; anyone can register (MUST) and comment or start a new topic.

    You are always welcome! Read more...

    Where are we?

    We have our offices in Dar es Salaam but we still work virtually.

    For anything related to this site please Contact us.

    Contact us now...

    DISCLAIMER

    JamiiForums, its partners, affiliates and advertisers are not responsible for the content of threads/topics that are submitted by users..

    Read more...

    Forum Rules

    JamiiForums is moderated under the rules set by users and moderators to safeguard you.

    You MUST read them and comply accordingly. Read more...

    Privacy Policy

    We are committed to respecting your privacy rights when visiting any JamiiForums.com page, such as this one.

    Read our Privacy Policy. Proceed here...