KIONGOZI wa Kambi ya Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, amelipangua Baraza lake Kivuli la Mawaziri kwa kuunda wizara mpya zinazopunguza ukubwa wa lile la awali.
Mabadiliko hayo pia yamewaacha nje mawaziri kadhaa na kujaza nafasi zilizoachwa wazi na aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, aliyeenguliwa na Mahakama Kuu na marehemu Regia Mtema wa Viti Maalumu.
Hata hivyo, Mbowe hakuwaingiza wabunge wa vyama vingine vinavyounda kambi hiyo vya NCCR-Mageuzi, CUF, TLP na UDP kwa maelezo kuwa bado wanaendelea na mazungumzo yenye kuwafanya waaminiane zaidi.
Wanaounda baraza hilo ni yeye mwenyewe ambaye atakuwa na Wizara ya Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, akisaidiwa na David Silinde, Said Arf anakwenda Miundombinu akisaidiwa na Pauline Gekul, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais atakuwa Profesa Kulikoyela Kahigi, Fedha, Uchumi na Mipango ni Zitto Kabwe akisaidiwa na Christina Mughwai.
Katiba, Sheria na Muungano itaongozwa na Tundu Lissu, Maliasili, Utalii na Mazingira ni Mchungaji Peter Msigwa, Mambo ya ndani ya Nchi, Vincent Nyerere, Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Ezekiah Wenje atakayesaidiana na Raya Ibrahim Khamisi.
Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ni Mchungaji Israel Natse, Maji Mifugo na Uvuvi, Sylvester Kasulumbayi ambaye atasaidiwa na Sabreena Sungura wakati Kazi, Habari, Utamaduni na Michezo ikiongozwa na Joseph Mbilinyi akisaidiwa na Cecilia Pareso.
Nishati na Madini anaendelea kubaki John Mnyika, Viwanda na Biashara, Highness Kiwia na Afya, Jinsia na Jamii ni Dk. Gervas Mbassa, akisaidiana na Conchester Rwamlaza, Elimu, Sayansi na Teknolojia, Suzan Lyimo atasaidiwa na Joshua Nassari.
Wizara ya Kilimo na Ushirika itaongozwa na Rose Kamili wakati Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi inabakia kwa Halima Mdee.
Pia, Mbowe alifafanua sababu za kuendelea kutumia gari la serikali ambalo alikuwa amelikataa, akisema kuwa amelazimika kufanya hivyo kutokana na maelekezo ya serikali iliyopo madarakani.
Alisema kuwa alikuwa amelikataa ili kuishinikiza serikali kupunguza matumizi ya magari na kutaka apewe gari dogo lakini kutokana na kutosikilizwa alilazimika kuendelea kulitumia.
“Mimi nilikataa gari kwa kipindi cha miezi sita na nikawa natumia langu kwa shughuli zote za vikao vya Bunge, lakini nataka umma uelewe kuwa kwa nafasi yangu natakiwa kulipwa posho ya madaraka sh 200,000 kila mwezi, kupewa nyumba ya kuishi ikiwa na samani zake.
Ila mpaka sasa sina nyumba ya serikali wala mlinzi, kulipwa fedha za mawasiliano, vyote natumia fedha zangu….kama ningetaka ningedai mambo mengi ambayo natakiwa kupata lakini kulingana na hali ya uchumi wa nchi ni lazima nitumie fedha zangu ili kunusuru uchumi,” alisema.
Source: Tanzania Daima Ijumaa, 22 juni 2012
|
|
Follow Us Here