APRILI 7, mwaka huu, baadhi ya wanafunzi kutoka Vyuo Vikuu vya Mzumbe, Sokoine, Tumaini, Dar es Salaam (UDSM) na St. Joseph walishiriki kongamano kuhusu hali ya elimu ya juu nchini, nafasi ya wanataaluma kutetea haki zao na za wanyonge, pamoja na hali ya kisiasa nchini. Kongamano hilo lilifanyika katika Ukumbi wa Shule ya Sekondari Forest Hill, Morogoro. Mwandishi Wetu GODFREY DILUNGA aliyehudhuria kongamano hilo anaeleza zaidi.
ILIKUWA saa nane mchana, katika Ukumbi wa Shule ya Forest Hill, baadhi ya wanafunzi wakiwa na vijitabu vidogo vya kuandikia (note book) kwa ajili ya kuweka katika maandishi kitakachozungumzwa, walionekana kugubikwa na shauki ya kusikia na kujadili kuhusu masuala muhimu yanayohusu taifa lao.
Wanafunzi hao walionekana kuwa na uvumilivu mkubwa, hasa baada ya kubainika kuwa taarifa waliyokuwa nayo awali kuhusu kuanza kwa kongamano hilo haikuwa hivyo. Awali, walielezwa kwamba kongamano litaanza saa tatu asubuhi, lakini kutokana na sababu mbalimbali lilianza saa nane, hata hivyo hawakukata tamaa.
Naam! Muda uliwadia, Dk. Wilbroad Slaa, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ndiye aliyefungua kongamano hilo. Huku hotuba yake ikikatishwa kwa makofi na vifojo kutoka kwa wanafunzi waliokuwa wakimsikiliza.
“Wanafunzi wa vyuo vikuu na wengine siku hizi mnashindwa kufuatilia, kuhoji a kushauri kuhusu mambo ya msingi kwa Taifa lenu. Umakini miongoni mwenu umeteketea. Haupo, mnashindwa kuhoji hata kuhusu MKUKUTA (Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kuondoa Umasikini Tanzania).
“Mnataka nani afanye kazi hiyo? Mnatakiwa kuibana Serikali kuhusu ngonjera hii ya MKUKUTA. Maana ya MKUKUTA haionekani, ninyi wasomi mmebaki kimya. Hamfahamu unapAswa kuwasaidia vipi kuhusu elimu. Hamhoji ni kwa nini pamoja na kuwa na semina nyingi za MKUKUTA, idadi kubwa ya Watanzania hawafahamu chochote.
“Nchi hii inaporomoka, ninyi mmebaki kimya. Baadhi ya wasomi kwa idadi kubwa wanakimbilia CCM kugombea nafasi mbalimbali za uongozi, mjiulize ni kwa nini na nini kinawasukuma kufanya hivyo?
“Hata hivyo, wakishagombea ndani ya CCM na kupata uongozi wanabaki kimya, hawana msaada kwa Taifa. Nitoe mfano? Kuna Mbunge mmoja wa CCM aliwahi kupewa adhabu ya kutochangia hoja bungeni kwa miezi 18, baada ya kuonekana ni tatizo,” alidai Dk. Slaa bila kutaja jina la Mbunge huyo.
“Wapo wabunge ni Maprofesa, lakini hawawezi kutumia akili zao kwa kulinda na kutetea maslahi ya Taifa. Wameligeuza Bunge kuwa kama ‘rubber stamp’. Wanatuliza profession (taaluma) zao kwa sababu ya itikadi, msomi gani anakubali kuuza nchi yake kwa sababu ya itikadi tu. Msomi gani ‘una-compromise principles’ za taaluma yako.
“Hatuna wasomi bungeni bali tuna kundi la watu wenye vyeti tu. Ninavyofahamu msomi wa kweli ni yule anayesimamia misingi ya taaluma yake. Halafu kuna jambo jingine kwa mfano, mishahara ya wabunge na rais ni kwa nini iendelee kuwa siri wakati inatokana na kodi ya wananchi. Mishahara ni lazima iwe wazi ili kuimarisha, kwa nini iwe siri? Nchi kama Mauritius jambo hili linafanyia. Tunaogopa nini?
“Ndani ya Bunge kuna kitu kinaitwa ‘Malt-party Dictatorship’. Bunge linaburuzwa na kufikia uamuzi wa jumla kama Bunge, lakini katika uamuzi huo hakuna ridhaa ya wabunge wa upinzani. Hii yote inatokana na kuwepo kwa idadi ndogo ya wabunge wa upinzani. Ndiyo maana Bunge wakati mwingine linaafiki uamuzi usio na maslahi kwa wengi.
“Nizungumzie suala la vyama vya upinzani kuungana ili kuing’oa madarakani CCM. Kimsingi wingi wa vyama maana yake ni kwamba kunakuwa na utajiri wa mawazo tofauti. Suala la vyama kuungana ili kuing’oa CCM hatuwezi kulikubali moja kwa moja. Mnatakiwa mjiulize baada ya kuing’oa mtafanya nini.
“Tunachokikubali kwa sasa ni kwamba kama tunakubaliana kuungana kwa ajili ya kuondoa sera mbovu zisizo na maslahi kwa Taifa, hatuna tatizo. Ni lazima suala la kuungana lihusishe mtakachofanya baada ya kufanikiwa lengo hilo. Halafu ninyi wenyewe muwe mfano bora wa demokrasia ndani ya vyama vyenu.
“Kwa sasa CHADEMA tuko tayari kuungana katika mambo ya msingi kama vita dhidi ya rushwa. Si suala la kukimbilia Ikulu pekee. Tusiwaze kukimbilia Ikulu kwanza na baadaye mambo mengine yafuate. Tuungane kwanza kudai kuondolewa kwa sheria kandamizi.
“Suala jingine, nizungumzie Shirikisho la Afrika Mashariki. Niwaulize ninyi wasomi, tunalitaka Shirikisho kwa Katiba ipi, kwa mfumo gani wa uongozi, je, ni ‘presidential leadership’ au ‘parliamentary leadership’? Hii Tume ya Kukusanya Maoni imetengewa Sh bilioni 2.3 eti kwa ajili ya kuuliza swali Watanzania kuhusu ‘fast tracking ya federation’, kwa hiyo uamuzi tayari umefikiwa na viongozi.”
Akizungumzia mikopo ya Sh bilioni moja kwa kila mkoa nchini inayotolewa na Serikali, Dk. Slaa alisema, “Serikali makini haikimbilii kutoa fedha bila kuandaa mikakati endelevu. Nadhani na kuna uwezekano mpango huu kutokana na kutokuwa na mikakati endelevu ukafifia na kufa kabisa. Na fedha iliyokwishatolewa ikawa sadaka.”
Kwa upande wake, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zito Kabwe akizungumzia nafasi ya wasomi nchini katika kutetea maslahi yao na ya Taifa, alisema wanafunzi wa vyuo vikuu na wengine wa vyuo vya elimu ya juu wanapaswa kuwa watetezi wa haki zao na za wanyonge, hususan waliopo vijijini.
“Serikali inawajibika kusomesha wanafunzi wake bila masharti. Serikali inayoshindwa kusomesha raia wake haipaswi kukusanya kodi, hivyo haifai kuwepo madarakani. Lakini pia ari ya wasomi kutetea makabwela nchini imeshuka sana.
“Kwa sasa Rais Jakaya Kikwete amepata sifa ya pekee ya kumudu kutuliza mgomo wa wanafunzi bila kutumia virungu vya FFU. Wanafunzi walikuwa na madai yao. Akawaita pale Diamond Jubilee akawaeleza kuwa atashughulikia madai yenu, hadi leo hakuna kitu.
“Ni lazima wanafunzi wawe ‘organized’ kutetea haki zao pamoja na za wadogo zao watakaokuja kusoma katika vyuo vikuu baadaye. Mapinduzi yote huanzia kwa wanafunzi wa vyuo vikuu. Mapinduzi kama yale ya dhidi ya sheria mbovu, na mengineyo.
“Mfano sasa hivi Wizara ya Mipango, Uchumi na Uwezeshaji inaonekana kushindwa kuwa na mipango madhubuti ya kuhakikisha nchi inazalisha. Wanafunzi wa vyuo vikuu mmebaki kimya, hamchambui masuala muhimu ya nchi. Mnashindwa kuhoji. Mnataka nani ahoji, mkulima wa kijijini? Nini faida ya kuwa msomi ndani ya nchi yako.”
Naye Mbunge wa Viti Maalumu (CHADEMA), Suzan Lyimo akiwasilisha mada yake kuhusu elimu ya juu nchini, alisema Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limekuwa likitengewa bajeti nono zaidi kuliko sekta nyingine muhimu kama ya elimu na hata kilimo.
Kwa upande wake, mwanaharakati Ndimara Tegambwage akiwasilisha mada kuhusu hali ya siasa nchini, alisema tatizo la msingi nchini ni wanasiasa. Alisema Serikali inaongozwa na idadi kubwa ya wanasiasa wachafu, wasiokuwa na aibu wakishiriki kuliangamiza Taifa kutokana na ubinafsi walionao.
Baada ya hapo, wanafunzi waliokuwa wakiwasikiliza watoa mada hao walipata nafasi ya kueleza wanachofikiri kwa maslahi ya Taifa lao.
Mwanafunzi aliyeanza kuchangia ni kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), aliyeonyesha kukerwa kwake suala la uchangiaji wa asilimia 40 ya gharama za masomo. Kilichomkera zaidi mwanafunzi huyo ni hatua ya baadhi ya wanafunzi wanaoshindwa kulipa asilimia hiyo 40 kunyimwa matokeo yao.
“Baadhi ya wenzetu wananyanayaswa ndani ya Taifa lao. Wananyimwa matokeo yao kwa sababu ya kushindwa kulipa kwa wakati asilimia 40 ya uchangiaji gharama za masomo. Kwa nini umasikini wetu unatumika kutunyanyasa kiasi hiki?”
Naye, mwanafunzi mwingine kutoka Chuo cha Falsafa cha Salvatorian kilichopo mkoani Morogoro alisema tatizo la msingi nchini si wanafunzi kushindwa kufuatilia au kuhoji masuala ya msingi kuhusu maendeleo ya Taifa lao. Bali tatizo kubwa ni mfumo mzima wa elimu nchini.
Kwa mujibu wa mwanafunzi huyo, mfumo wa elimu nchini unawashurutisha wanafunzi kusoma kwa ajili ya kujibu mitihani yao na kisha kuhitimu masomo yao. Akisisitiza kuwa mfumo huo hautoi fursa kwa wanafunzi kujadili masuala ya msingi ya Taifa lao na ulimwengu kwa ujumla.
Mwanafunzi mwingine, kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine, alizungumzia ukusanyaji wa maoni kuhusu Shirikisho la Afrika Mashariki, akisema tume inayohusika na ukusanyaji wa maoni hayo isiwakimbie wasomi na badala yake ijadiliane nao kwa maslahi ya Taifa.
Katika hatua nyingine, mwanafunzi huyo alimtaka Waziri wa Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Peter Msolla kuchukuliwa hatua kwa kuchunguzwa na tume inayohusika na usimamizi wa maadili ya viongozi, kutokana na waziri huyo kuonekana kuyumba kuhusu suala zima la usimamizi wa mikopo kwa wanafunzi.
Naye mwanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe alisema “Umasikini wetu usitumike kutudharau, hasa katika suala hili la kuchangia asilimia 40 ya mikopo.” Alidai kuwa vyuo takriban vyote vya elimu ya juu nchini vimegeuzwa kuwa taasisi za Chama cha Mapinduzi (CCM).
Alisema kwa kuwa siasa ndiyo sehemu muafaka ya kutafakari na kuamua mustakabali wa Taifa, ni vema wasomi wakaingia katika vyama vingine vya siasa mbali na CCM ili kupata mbadala wa uongozi nchini.
Mwanafunzi mwingine wa Chuo Kikuu Mzumbe, alihoji ni maana ya mtu kuitwa msomi. Akisema hivi msomi maana yake nini, “Je, usomi ni kuwa na ‘degree’ moja? Kama hivyo sivyo ni kwa nini wanafunzi wa ‘masters’ wasipewe mikopo na Serikali?”
Mwanafunzi mwingine wa kutoka SUA alihoji kuhusu mrabaha unaopata Serikali kutoka kwa makampuni makubwa ya madini nchini. Alihoji akisema, “Hivi huu mrabaha wa asilimia tatu umebadilishwa na kuwa asilimia ngapi kwa sasa. Nakumbuka Rais Kikwete aliahidi kurejea mikataba ya madini. Sasa nini kimebadilika?”
Akijaribu kujibu baadhi ya hoja, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zito Kabwe alisema suala la wanafunzi kuchangia asilimia 40 ya mkopo wa elimu ya juu linaweza kufikishwa mahakamani kutokana na suala hilo kuwa na mahusiano na haki zinazobainishwa katika Katiba ya nchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa vijana wa Chadema, John Mnyika alisema kwa sasa CHADEMA inaandaa katiba mbadala ya nchi na kwamba rasimu hiyo itakapokamilika itawasilishwa serikalini kabla ya mwaka 2009. Kabla ya kuanza kwa uchaguzi mkuu wa Serikali za mitaa.
Follow Us Here