Mrisho Mpoto, swali
Kilimo kwanza ni kaulimbiu au mpango Wa kumaliza njaa Tanzania, karne ya 21 bado Chakula ni issue Ndiyo nipo kwenye gate la ukaguzi IKULU kumueleza Mjomba kuwa tuna taka utekelezaji Wa mengi tuliyokubaliana kabla ya kumpa Funguo ya jengo jeupe
Ndimara Tegambwage,jibu
Mpoto ndugu yangu!
Kilimo kwanza ni wao
Na kilichopo ni chao
Si chako, si changu
Hata kaulimbiu ni yao
Wewe na mimi kalagabao!
Yetu yawe makofi - pwa! pwa! pwa!
Ndoto wamepandikiza
Vichwani mwa hohehahe
Eti watakula
Eti watashiba
Hata kuvimbiwa
Eti watasaza
Hata kuuza nje
Eti neema yaja
Yetu yawe makofi - pwa! pwa! pwa!
Si changu si chako
Kilimo Kwanza ni chao
Tunda la mbongo zao
Wenye mipango lukuki
Wenye wenyeji ikulu
Na katika vyake viunga
Wenye "kontakti" nje
Na ndani kusaka manamba
Yetu yawe makofi - pwa! pwa! pwa!
Wamekaa Marekani
Hata nyumanju ya ikulu
Wazawa na wakuja
Kunguru ni kunguru tu!
Wamevikuna vipara
Na kilimo wakatua:
Ndio lango, ndio shibe
Mwafaka wa wanga.
Yetu yawe makofi - pwa! pwa! pwa!
Ili wapate ardhi, wameimba:
Kilimo Kwanza
Ili wapewe mikopo, wameimba:
Kilimo Kwanza
Ili wapewe kipaumbele, wameimba:
Kilimo Kwanza
Ili wale, wanywe ikulu, wameimba
Kilimo Kwanza
Waite unavyotaka:
Wawekezaji au wawekezwaji?
Yetu yawe makofi - pwa! pwa! pwa!
Wanatafuta miliki
Ya ardhi na mazao
Wanahemea mapato
Kwa migongo ya wazawa
Wanatafuta fadhila
Kwa ikulu na kwingineko
Wale, washibe, wasaze
Yetu yawe makofi - pwa! pwa! pwa!
Kilimo Kwanza mpango
Wa wakubwa kuvimbiwa
Kilimo kwao kutaja
Hilo hasa ni kudandia
Waonekane wanajali
Njaa kuikong'ota
Kumbe njaa yao faida, ziada
Nasi yetu makofi: pwa! pwa! pwa!
Sikiliza wa Mpoto
Na umri wako rejea
Kilimo kwanza ije leo
Jana ulikulani?
Mkolezo una jambo
Ni shinikizo babukubwa
Wanasiasa waimbe
Wafike kukushawishi
Wanamipango wanene
Eti huo “ukombozi”
Ili uone sasa utapona:
Kumbe tai anashuka
Chako kitakuwa chao
Na chao kitabaki chao
Nasi yetu makofi: pwa! pwa! pwa!
Wanayo yao madai
Kilimo kikubwa wataleta
Kilimo kikubwa ni ardhi kubwa
Hata yangu na yako kumezwa
Hata ya mkulima wa jembe,
Yule aliyetulisha hadi jana
Hadi leo na hadi kesho wavunapo
Chwai! Itakwenda
Nasi tutabaki na makofi: pwa! pwa! pwa!
Kilimo kikubwa mitambo
Walokuwa wakulima
Sasa wawe manokoa;
Wale wa kurandwa mijeredi
Mithili ya utumwa wa babu.
Kutumika watatumika
Kutumiwa watatumiwa
Kuchakaa watachakaa
Mafao yao ni hapa
Kwani wao watumishi
Kwa soko lile la nje
Lile la wawekezaji
Au sema wawekezwaji
Nasi yetu makofi: pwa! pwa! pwa!
Kilimo kikubwa mbegu
Mbegu nyingi kutumika
Mbegu zao za viwanda
Wanaziita za kisasa.
Za asili zitapotea, pwe!
Sote tule vikakara
Vyenye ladha masimango
Tubaki tukiimba
"Maendeleo, maendeleo!"
Makofi kuwapigia: pwa! pwa! pwa!
Kilimo kikubwa mbolea
Ile ya kwao viwandani
Ardhi hii kunajisi.
Baada ya miaka mitatu, minne
Nayo kuwa kikakara
Hakimei kisichochao
Hakikui wasichotaka
Hakipandwi wasichoruhusu
Sote hatufurukuti
Tunalinda soko la "bwana!"
Tunaendelea: pwa! pwa! pwa!
Kitu gani hatuwezi
Wewe na mimi,
Pale madarakani tukikaa?
Hata hayo tungefanya
Kwa mipango, kwa haki.
Sasa wafanye kunguru
Wasiothamini utu?
Wasiothamini asili yako?
Watumikiao soko la nje
Kwa kutufanya manokoa?
Kwa mwavuli wa Kilimo Kwanza?
Nasi tuendelee kuwapongeza
Kwa makofi: pwa! pwa! pwa!
Kilimo Kwanza ni wao
Wao hawa watafutaji
Kama mipango ni yao
Na kaulimbiu ni yao
Sisi twabaki na njaa yetu
Njaa ya kualika
Njaa ya kusukumiziwa;
Na kwa sauti zilizonyauka
Macho yaliyoenda kengeza;
Kwa uchovu
Miili iliyofinyazwa kwa viboko;
Vile viboko vya watawala
Na wawekezwaji.
Halafu tupige makofi
Pwa! pwa! pwa!
Afadhali "Kilimo Mwisho"
Kuliko Kilimo Kwanza
Kilimo Kwanza si chako
Kilimo Kwanza si changu
Acha watu na dili zao
Wewe na mimi tufumbuke
Tuache kupiga makofi
Mwisho wa pwa! pwa! pwa!
Ndio mwanzo wa kufikiri.
Chanzo. Mabadiliko
Follow Us Here