Kama wabunge watafanya kweli labda tunaweza kupiga hatua kweli...Lakini sijui kama ni kweli!
Mwandishi Wetu
HabariLeo; Tuesday,February 13, 2007
RAIS Jakaya Kikwete amewaeleza wabunge wa CCM wawe huru kuikosoa serikali mradi wawe na ushahidi na hoja zao. Katika semina ya siku moja iliyofanyika Dar es Salaam juzi, rais aliwaambia wabunge hao kuwa hayuko tayari kulinda watu wachafu ndani ya serikali yake, hivyo akatoa mwito kwa wabunge kufichua mambo yanayoenda kinyume na maadili ya uongozi.
“Rais alichotueleza anataka tuwe wasafi kuanzia kwenye chama na serikalini,” kilisema chanzo kimoja cha habari kilichohudhuria semina hiyo. Katika kile kinachoonekana ni kuelekezwa juu ya majukumu yao wakiwa kama wabunge wa chama tawala, Rais Kikwete katika kikao hicho aliwataka wabunge hao kuisaidia serikali katika kutekeleza majukumu yake kwa kuikosoa wanapoona mambo hayaendi.
Chanzo hicho kilidokeza kuwa rais amewapa meno wabunge hao kuhakikisha wanatimiza jukumu lao la kuisaidia serikali lakini pia na kuwa huru kuikosoa. “Siyo kwamba hataki tuikosoe serikali, lakini anataka tuwe na ushahidi wa kile tunachokosoa,” kilisema chanzo hicho cha habari.
Habari hizo zilieleza kuwa Rais Kikwete aliwapa meno wabunge hao lakini pia akawatahadharisha kuwa siyo vizuri kupinga kila kitu wakati hawana ushahidi. Rais pia aliwaeleza kuwa hayuko tayari kulinda watu wachafu ndani ya serikali yake hivyo akatoa mwito kwa wabunge kufichua mambo yanayoenda kinyume na maadili ya uongozi.
Mtoa taarifa mwingine alilidokeza gazeti hili kuwa Rais Kikwete baada ya mada ya Spika wa zamani wa Bunge, Pius Msekwa, aliwashauri wabunge hao wawe wazi lakini pia wasitoe hoja za kubuni na kutunga ambazo haziwezi kuisaidia serikali. “Alitushauri tusikurupuke lakini akataka tuwe wawazi na wakweli tunapoona kuna upungufu…lakini pia amesisitiza mwenye ushahidi asiogope kusema,” alisema mtoa habari.
Awali taarifa iliyotolewa na Ikulu ilisema semina hiyo ilikuwa na mada moja tu kuhusu Kanuni na Majukumu ya Msingi ya Wabunge na Wawakilishi wa Chama Tawala (CCM) katika mfumo wa vyama vingi vya siasa.
Katika mada yake hiyo, Msekwa kutokana na uzoefu wake wa utumishi ndani ya chama na katika Bunge alielezea na kufafanua kwa kina maudhui ya kanuni za kamati za wabunge na wawakilishi wa CCM.
Semina hiyo iliwahusisha Wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar. Walishiriki semina hiyo kama wajumbe wa kamati ya wabunge na wawakilishi wa CCM kwa ajili ya kupigwa msasa. Ilifanyika katika ukumbi wa mikutano wa jengo la Ubungo Plaza.
Ilielezwa kuwa washiriki hao waliijadili kwa kina mada hiyo na kutoa michango ya mawazo yao kwa uwazi na ukweli, na kueleza kuwa semina hiyo ilikuja wakati mwafaka na imekuwa ni elimu tosha kwao kuhusu jinsi ya kutekeleza majukumu yao.
Rais Kikwete aliahidi kuwa semina kama hiyo zitakuwa zinafanyika mara kwa mara ili kupata fursa ya kubadilishana mawazo na kukumbushana mambo mbalimbali.

Reply With Quote



Follow Us Here