Ndugu zangu unganeni nami katika kukipa pongezi Chama cha Mapinduzi kwa utawala wake wa miaka thelathini. Kabla hamjaanza kunirukia na kunishangaa imekuwaje tena mzee wa kijiji aipe pongezi CCM niwaambie mapema kuwa pongezi zangu ni za dhati na zina sababu maalum. Sababu nitakazozianisha nina uhakika na ninyi mtakubaliana nazo.
Nafasi hii ya kutoa pongezi kwa chama cha Mapinduzi inawezekana kuwa ndiyo nafasi yenu pekee mtakayoipata katika maisha yenu ya kuweza kukishukuru Chama hiki kwa kushika hatamu na utamu wa uongozi wa nchi yetu kwa miaka yote hii thelathini. (sasa msiniulize miaka ile kumi na tano ya mwanzo walikuwa wakiongoza kina nani) Kwani baada ya hapa, CCM mliyoijua na kuizoea inaelekea kule ambako jua huzama na mawingu huangukia!
Miaka thelathini si kidogo. Kwa muda wa miaka thelathini serikali ya CCM imeweza kushikilia fikra, mawazo, na mwelekeo wa Taifa kiasi cha kwamba kuifikiria Tanzania bila CCM ni kama kuisaliti nchi. Mikono mirefu ya utawala wa CCM na kucha zisizokatwa za serikali yake zimeweza kuzunguka kila kona Tanzania na kuikumbatia nchi bila ya kuipa mahali pa kupumulia.
Ndani ya miaka hii thelathini ilifikia mahali mtu kula na kupumua ni hewa ya CCM. Chama kilikuwa "kinadumu"! Haukuweza kupata kazi serikalini bila kadi ya chama hicho, hukuweza kujiunga na sekondari bila kuonesha kadi ya chama hicho (angalau kujaza kwenye fomu kuwa ulikuwa mwanachama) na kwa namna fulani maisha ya Watanzania yalikuwa yamefungamana na maisha ya Chama hicho. Hili nalo limeanza kujitokeza tena kwani baadhi ya wafanyakazi, wanafunzi na watu wa kawaida wameanza kuona kuwa ili mambo yawanyokee hawana budi kupiga magoti kwenye altare ya CCM. Kwa hili CCM Hongera!
Miaka thelathini ya kuweza kusimamia utendaji mbovu wa viongozi, kuzoea uzembe na kuacha rushwa iote kama mitete itetemeyo ambayo ncha zake huchoma kama miiba ya michongoma katika maisha ya watu, si miaka michache. Miaka thelathini ya kuweza kuwafanya watanzania wakubali mikataba mibovu na yenye harufu ya rushwa bila ya hata kujisikia hatia, si jambo la kutopongeza! Kuthubutu kwa baadhi ya viongozi wa chama hicho na mashabiki wao kuifanya Tanzania kuwa ni CCM na CCM kuwa ni Tanzania na mtu yeyote ambaye si mwana CCM kama nusu Mtanzania, ni kitu kinachohitaji pongezi za pekee kwani ! CCM hongera!
Miaka thelathini ya kuja na kila aina ya mikakati, maazimio, matamko na kila aina ya kauli mbinu huku wakibadilisha maandishi nje ya chupa bila kubadilisha kilichomo ndani hatuna budi kuwapongeza. Matangazo ya Madaraka Mikoani, Azimio la Iringa, Azimio la Arusha, Azimio la Musoma, Azimio la Zanzibar Siasa ni Kilimo n.k vyote vilikuwa ni vitu vya kukumbukwa na vilivyoleta hamasa kwa wananchi. Kauli kama "Fagio la Chuma", "Kuwajibika", "Uwazi na Ukweli", na "Ari Mpya, Kasi Mpya, na Nguvu Mpya" ni maneno yenye mvuto wa kisiasa lakini yenye maana kiduchu katika maisha halisi ya Watanzania. Jinsi watu waliunga mkono maneno ya chama hicho na vyama asisi vyake leo hii watu hao bila shaka huko waliko wanashika tama, nyuso zao zikiwa zimegubikwa na huzuni.
Watu kama kina Marehemu Seth Benjamin wanaweza kuiangalia Tanzania na kutotambua ni kitu kilichowafanya watembee maili zote kuunga mkono. Kwa kitendo cha kuja na maneno matamu ya kizalendo, yenye mvuto wa ujasiri na kuchochea mapenzi kwa nchi, CCM inastahili pongezi za pekee! CCM hongera!
Miaka thelathini ya kubadilishana na kuzungushana kwenye mfumo wa uongozi kiasi cha kwamba viongozi wapya wanashindwa kupasua anga la chama hicho kwa hakika CCM inastahili pongezi za pekee. Leo chama hicho bado kimejawa maneno matamu na yasiyo na mantiki huku kinaendelea kuwakumbatia viongozi waliofeli huko nyuma lakini leo ati viongozi hao bado wanapewa nafasi ya kufanya jambo jipya.
Viongozi walioshindwa katika kilimo leo wanapewa elimu na kuanza kutumia ubavu wa serikali kulazimisha watu wakubaliane nao. Mawazo yao hayo hayakuanza mwaka jana, walikuwa nayo miaka thelathini iliyopita. Kuwazungusha viongozi kama taka, kuwahamisha kutoka hapa kwenda kule na kuendelea kuwalinda viongozi wazembe, waharibifu na wala rushwa kwa kisingizio cha kukosa ushahidi, CCM lazima ipewe pongezi za dhati. CCM Hongera!
Miaka thelathini ya kuweza kuwafanya Watanzania waamini kabisa kuwa wao ni masikini na hali yao duni ya maisha ni mapenzi ya Mungu huku wabarikiwa wachache wa chama hicho wakiendelea kuishi katika Paradiso ya Bongo hatuna budi kutoa pongezi kwa chama hicho.
Inawezekanaje watu wachache wakaweza kuwalaghai watu wengi kwa maneno matamu na ahadi lukuki na watu hao wengi kwa muda wa miaka thelathini wakaendelea kuwaamini watu wale wale wakitumaini siku moja watawaambia ukweli?
Kufanya hivyo kunahitaji kipaji cha pekee na ufundi wa pekee na pia kinaonesha ni jinsi gani CCM imewiva kisiasa na imekomaa kimikakati.
Watanzania kila baada ya miaka mitano mitano wameendelea kukichagua chama hicho huku wakijua wazi kuwa hakuna mabadiliko yoyote isipokuwa yale ya asili yanayoletwa na muda yatakayowafikia. Hilo ni jambo ambalo hatuna budi kukipongeza chama hicho. CCM Hongera!
Miaka thelathini ya kuweza kumegeana na kugawiana uongozi kama njugu na kuendelea kuangaliana na kupangiana ulaji kama kuandaa mzunguko wa masinia ya pilau kwa hakika inastahili pongezi.
Kwa vile CCM imeweza kila mara kujenga hoja na kuvutia wananchi wengi kwa maneno yake, kwa mbwembwe na vifijo na kiasi kufanya chama hicho kiendelee kukubalika bila ya shaka ni ufundi wa hali ya juu.
Ni uzoefu wa miaka thelathini unaoweza kuwafanya watu wakizoee chama kiasi cha kukubali kila kisemwacho na viongozi wa chama hicho na huku wakitiririka jasho, wamejaa vumbi, na watoto wao wakilala njaa kuandamana kukiimbia nyimbo za "CCM Nambari One". Ndiyo, ni kweli CCM ni nambari wani katika ufundi wa hadaa na uoneshaji wa mazingaombwe yaliyokubuhu! CCM Hongera!
Hata hivyo kama nilivyosema, ni bora uungane nami kutoa pongezi hizo sasa na leo kwani kuanzia wiki ijayo, miaka mingine thelathini inaanza, miaka ambayo itakuwa ni tofauti. Anayedhania kuwa miaka thelathini ijayo itakuwa ni ya hadaa na utawala wa CCM mtu huyo hajui kusoma ishara za nyakati.
Kuna wakati unaweza kumgeresha mtoto na kumnyamazisha kulia kwa kumrushia pipi, lakini kuna siku hata umpe peremende za tofa mtoto hataki ataendelea kulia!!
Mbwa asiyefunzwa vizuri huweza kuhadaiwa kwa kurushiwa vipande vya nyama, lakini yule anayejua ni nani anayemfukuza hata umtupie minofu ya namna gani mdomo haufunguki kwani amefungwa gidamu ya lengo, na moyo wake unajua nini unachofukuzia!
Miaka hii thelathini ya CCM ni miaka ambayo CCM imefanya mambo mengi mazuri kwa jamii kama nilivyosema katika makala nyingine, kusimamia umoja wa Kitaifa, kutuongoza kumng'oa nduli Amin, kusimamia mabadiliko ya kisiasa kwa njia ya Amani kiasi na sasa kuanza kushughulikia tatizo la Zanzibar.
Ni kweli CCM imeweza kuonesha njia kwenye mambo machache ambayo hayajazi kiganja! Lakini ukweli wa mambo ni kuwa miaka thelathini iliyopita ya utawala wa CCM siku moja itaangaliwa kama miaka tuliyopoteza na vizazi vijavyo vya Watanzania watatushangaa ilikuwaje hatukuweza kuona upotovu na ubovu wa chama kilicholewa ugimbi wa madaraka na kubweteka kwa ngoma za sifa! Miaka thelathini iliyopita tunasema hongera CCM, kwani si kidogo, lakini inatosha!

Reply With Quote
Follow Us Here