TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Isambazwe Mara Moja
Alhamis, Julai 21, 2011
KUITISHWA KWA MAANDAMANO YA AMANI NA MKUTANO WA WAZI
Mahali: Uwanja wa Mwembeyanga, Temeke, Dar es Salaam
Tarehe: 1 Agosti 2011
Nikiwa kama Mtanzania, mpenda amani, raia wa KUZALIWA, Mzalendo Halisi mwenye kuipenda nchi yake, na kiongozi wa asasi-huru ya X Foundation yenye makazi yake Jijini Dar es Salaam, napenda kutoa taarifa kwamba, X Foundation inawaalika Watanzania wote waishio Dar es Salaam na kwingineko, kwamba, kutakuwa na Maandamano ya Amani na Mkutano wa Wazi, siku ya Jumatatu, Agosti Mosi, 2011, kuanzia Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Temeke hadi Uwanja wa Mwembeyanga, Temeke, Dar es Salaam. Watanzania mnaombwa kukusanyika KWA AMANI, kwenye eneo la wazi, nje ya Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Dar es Salaam, kuanzia saa 2 asubuhi. Maandamano yataanza rasmi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Temeke, takriban saa 4 kamili hadi Uwanja wa Mwembeyanga, Temeke, na yanatarajiwa kupokelewa na Mhe. Beatrice Matumbo Shellukindo (MB, Kilindi, CCM), akishirikiana na viongozi wa vyama mbali mbali vya kisiasa na kijamii, ambao watakuwa wamealikwa kuhudhuria.
Dhumuni la Maandamano ya Amani na Mkutano wa Wazi, tukio ambalo litafanyika kwa amani, linachagizwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, toleo la mwaka 1977, kama ifuatavyo:
- Msingi na Mustakabali: Serikali na Watu, Sheria ya 1984, Na. 15, ib. 6, kama ifuatavyo:
8.-(1) Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Nchi inayofuata misingi ya demokrasia na haki ya kijamii, na kwa hiyo -
(a) wananchi ndio msingi wa mamlaka yote, na Serikali itapata madaraka na mamlaka yake yote kutoka kwa wananchi kwa mujibu wa Katiba hii;
(b) lengo kuu la serikali litakuwa ni ustawi wa wananchi;
(c) Serikali itawajibika kwa wananchi;
(d) wananchi watashiriki katika shughuli za Serikali yao kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii.
- Uhuru wa Mawazo: Uhuru wa Maoni, Sheria ya 1984, Na. 15, ib. 6, kama ifuatavyo:
18.-(1) Bila ya kuathiri sheria za nchi, kila mtu yuko huru kuwa na maoni yoyote na kutoa nje mawazo yake, na kutafuta, kupokea na kutoa habari na dhana zozote kupitia chombo chochote bila ya kujali mipaka ya nchi, na pia ana uhuru wa mawasiliano yake kutoingiliwa kati.
- Uhuru wa Kushirikiana na Wengine: Sheria ya 1984, Na. 15, ib. 6, kama ifuatavyo:
20.-(1) Kila mtu anastahili kuwa huru, bila ya kuathiri sheria za nchi, kukutana na watu wengine kwa hiari yake na kwa amani, kuchanganyika na kushirikiana na watu wengine, kutoa mawazo hadharani, na hasa zaidi kuanzisha au kujiunga na vyama au mashirika yaliyoanzishwa kwa madhumuni ya kuhifadhi au kuendeleza imani au maslahi yake au maslahi mengineyo.
- Kila raia anayo haki na uhuru wa kushiriki kwa ukamilifu katika kufikia uamuzi juu ya mambo yanayomhusu yeye, maisha yake au yanayolihusu Taifa.
- Ulinzi wa Mali ya Umma: Sheria ya 1984, Na. 15, ib. 6, kama ifuatavyo:
27.-(1) Kila mtu ana wajibu wa kulinda mali asilia ya Jamhuri ya Muungano, mali ya Mamlaka ya Nchi na mali yote inayomilikiwa kwa pamoja na wananchi, na pia kuiheshimu mali ya mtu mwingine.
- Watu wote watatakiwa na sheria kutunza vizuri mali ya mamlaka ya nchi na ya pamoja, kupiga vita aina zote za uharibifu na ubadhilifu, na kuendesha uchumi wa taifa kwa makini kama watu ambao ndio waamuzi wa hali ya baadaye ya taifa lao.
Kutokana na mustakabali huu, mimi, nikiwa Raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ninao uhuru, haki na wajibu wa kuzingatia masharti haya yaliyotajwa hapa juu, kama ifuatavyo:
- Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania imekuwa katika hali ya jumla ya kuyumba kwa uchumi wake, kuanzia mnamo mwaka 1994, wakati janga la nakisi ya nishati ya umeme lilipoikumba Jamhuri kwa mara ya kwanza, na kusababisha athari mbaya za kiuchumi
- Wizara ya Nishati na Madini ndiyo taasisi kuu ya Serikali ya Tanzania, ambayo, kwa mujibu wa Ibara ya 8-(1) ya Katiba, ibara ndogo ya (b), inatamkwa kwamba “wananchi ndio msingi wa mamlaka yote, na Serikali itapata madaraka na mamlaka yake yote kutoka kwa wananchi kwa mujibu wa Katiba hii”, kwa hiyo, Wananchi ndio wenye mamlaka ya mwisho ya kuamua mustakabali wa utendaji wa viongozi wa Wizara hiyo, ambayo ni taasisi yao, wao wakiwa wenye kutoa “madaraka na mamlaka” kwa Serikali.
Kwa msingi huo mkuu, pamoja na misingi mingine iliyotajwa hapo juu, ninao uhuru, haki na wajibu wa kuitisha Maandamano ya Amani na Mkutano wa Wazi, kwa lengo la kuwashinikiza viongozi watendaji wakuu wa Wizara ya Nishati na Madini, yaani, Waziri, Naibu Waziri na Katibu Mkuu, kujiuzulu mara moja, ili kuwezesha utendaji wa Wizara hiyo kutendeka kwa ufanisi zaidi, kwani imeonekana dhahiri kwamba, katika kipindi cha uongozi wao wa Wizara hiyo, kipindi cha kwanza kikiwa cha 2005-2010, na cha pili kikiwa 2010-2015, hali ya ugavi wa nishati ya umeme imezidi kuwa mbaya kiasi cha sio tu kuathiri uchumi wa nchi, lakini pia, kuathiri vibaya zaidi maisha na mustakabali wa Watanzania kwa ujumla.
Kutokana na usimamiaji mbovu wa utendaji wa Wizara, pamoja na mipango mizuri iliyowekwa hapo awali, na pia, kutosikiliza maoni ya Wabunge, hususan maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya inayohusika na sekta ya nishati, viongozi hawa walioteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, wamepuuza kabisa ushauri wa wataalam na wabunge, na katika utendaji wao mbovu, wameitia hasara kubwa Jamhuri hii, hivyo kusababisha upotevu wa mabilioni ya Shilingi, sio tu kutokana na Serikali kukosa kukusanya mapato kutokana na shughuli mbali mbali za uzalishaji kutoka kwenye viwanda, vingi ambavyo sasa vimefungwa, lakini pia, Serikali kukosa kukusanya mapato kutoka kwa wajasiriamali wadogo na wakati, hivyo kushindwa kujiendesha kwa ufanisi mzuri zaidi.
Kwa kuzingatia Masharti yaliyowekwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 27-(1) na (2), ninao uhuru, haki na wajibu wa kulinda mali ya umma, ikiwa ni pamoja na uchumi wa Jamhuri, lakini pia, kwa kuzingatia Ibara ya 18-(1) na 20-(1) na (2), ninao uhuru, haki na wajibu wa kutoa maoni yangu, na pia kushirikiana na watu wengine katika kutoa maoni hayo, ikiwa ni pamoja na kwenye hadhara, kupitia, kwa mfano, maandamano ya amani na mikusanyiko ya wazi, nikiwa na uhuru wa kutoingiliwa kati kwenye mawasiliano hayo ya amani.
Leo, Alhamis, Julai 21, 2011, ninatamka, kwa faida ya Watanzania wote, kwamba, ifikapo tarehe 1 Agosti 2011, sisi Watanzania, tutakusanyika kwa amani na tutaandamana kwa amani, kama ilivyotajwa hapo juu, na tutafanya mkutano wa wazi na wa amani, ili kuweka bayana maoni na hisia zetu kuhusu janga hili kuu lililoifika nchi yetu.
Tuhuma zinazowakabili watendaji hawa, wa kutaka kutoa hongo ya takriban Shilingi Bilioni Moja za Kitanzania, zitazungumziwa kwa undani na watu wenye taarifa kamili zaidi kwenye mkutano huo utakaofanyika Mwembeyanga, Temeke. Tunatoa maombi ya ushirikiano mwema kwa Watanzania wote katika maandalizi ya maandamano hayo na mkutano huo, ili kuleta ufanisi mzuri zaidi, kwani, penye umoja kuna nguvu, na penye wengi hapakosi mazuri.
Watu wote wenye nia nzuri na nchi yetu wanaombwa kuwasiliana nami kwa njia ya simu na/au barua pepe kama inavyoainishwa hapa chini. Mimi ni mhamasishaji, ninao uhuru, haki na wajibu huo, lakini mustakabali wa nchi yetu ni wetu wote, bila kujali itikadi zetu za kisiasa, au imani zetu za kidini, au rangi za ngozi zetu au makabila yetu, kwani, Tanzania ni moja, ni yetu wote, kila mtu anayeitwa Mtazania ana haki ya kuitetea na kuilinda nchi yake, akishirikiana na wenzake.
Asanteni kwa Ushirikiano wenu.
MwanaHaki
Simu selula: +255-786-019019 na +255-786-019019
Barua pepe: misterx@qi.co.tz



Follow Us Here