Wapendwa
ndugu, jamaa na marafiki;
Hiyo tamaa sikati, ninawajuza wengine
Nimpendaye kwa dhati, ni huyu siyo mwengine
Nitasubiri wakati, miezi hata minane
Mitatu ama minane, nitasubiri kwa dhati!
Nitasubiri kwa dhati, mitatu hata minane
Na bado tampa chati, hata akiwa mjane
Ni huyu huyu binti, sitaki hao wengine
Mitatu ama minane, sitojalia wakati
Nasema kweli sikati, kwa huyu siyo wengine
Ingawa jibu sipati, upite mwezi wa nane
Mwengine simtafuti, na wala sendi pengine
Mitatu ama minane, tamaa miye sikati
Dhamira yangu ya dhati, kutozengea wengine
Sitotumia visheti, wala vitamu vingine!
Mitego ama manoti, kuwinda hao wengine!
Mitatu ama minane, hiyo tamaa sikati
Maneno mengi siteti, bali barua nyengine
Najua ni vizingiti, muvisemavyo wengine
Ni miye mtanashati, ambaye sina mwingine
Mitatu ama minane, kamwe tamaa sikati
Undeni hata kamati, nakadhalika nyingine
Kuwacha kweli siwati, wala silongi mengine
Majibu kwenu ya dhati, ni huyu siyo mwingine
Mitatu ama minane, nitasubiri wakati
Nasema hapa tamati, sitoongeza mengine
Nawajulisha umati, pamoja nanyi wengine
Ingawa kuwa sipati, sitompenda mwengine
Mitatu ama minane, tamaa hiyo sikati!!
Wakatabahu waraka,
Kijana Bin M'bichi
Follow Us Here