"Baba yangu, ninazo habari nitakazokuambia, lakini siwezi kusema mbele ya watu wanyonge hawa, maneno yangu ni baina ya mimi na wewe tu. Baba yangu, nitasema haya tu:
Mwanamke alinihaini mautini, akalifunika jina langu kwa aibu, ndiyo, mke wangu mwenyewe, mwanamwali mwenye uso kama mwezi, alinihaini, lakini niliokoka na mauti; ndipo nilipoponyoka katika mikono ya wale waliokuja kuniua. Nilipiga mapigo matatu tu kwa shoka langu hili Inkosikazi - hakika baba yangu atalikumbuka, moja upande wa kuume, moja upande wa kushoto, na moja mbele yangu, na hata hivyo niliwaacha watu watatu wamekufa. Kisha, nilikimbia, na kama baba yangu ajuavyo, ingawa mimi ni mzee, lakini miguu yangu ni myepesi kwenda mbio kama ile ya paa, wala hapana mtu anayeweza kunigusa tena niishapo kutoka mbavuni pake.
Mbele nilikimbia, na matarishi wa mauti walinia ndama nyuma, na sauti zao zilikuwa kama sauti za mbwa wanaowinda. Kutoka nyumbani kwangu nilikimbia; nikampita yule aliyenihaini alikuwa akiteka maji kisimani. Nilimpita upesi kama kivuli cha mauti, na nilipokuwa nikipita nilimpiga dharuba moja kwa shoka langu, tahamaki! kichwa chake kilimtoka, kikaangukia kisimani. Kisha, nilikimbilia kaskazini. Siku baada ya siku nilisafiri; kwa miezi mitatu nilisafiri, nisipumzike, nisisimame, ila nilizidi kukimbilia kwenye usahaulifu, mpaka nilipoonana na safari ya yule mwindaji mweupe aIiyekwisha kufa, nami nimekuja hapa pamoja na watumishi wake.
Wala sikuleta kitu pamoja nami. Mimi niliye mtoto wa watu, ndiyo, wa damu ya mfalme mkuu Chaka, mimi niliye mkuu mwenyewe, jemadari katika kikosi cha Nkomabakosi, sasa mimi ni mgaagaa, mtu asiye na nyumba. Wala sikuleta kitu pamoja nami ila shoka hili langu, kwa nguvu zake ambazo kwazo niliwatawala watu wangu. Wamewagawanya ng'ombe zangu; wamewatwaa wake zangu; na watoto wangu hawautambui uso wangu tena.
Hata hivyo, kwa shoka lili hili nitakata njia nyingine nifike mpaka kwenye usitawi. Nimesema!"
Basi, akalizungusha shoka lake kichwani likalialia lilipokuwa likiikata hewa.
Follow Us Here